19 – Kanisa

Haya ni maneno matakatifu ya Mungu Mwenyezi.
Hatupendi maneno ya wanadamu.
Kwa mtu yeyote anayempenda Mungu... hivi ndivyo Mungu anasema kuhusu: Kanisa.

Mistari 3 Muhimu Zaidi

Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”

Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, ye yote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, Naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu ni lazima awe mtumwa wenu, kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

Walipokwisha kuomba, mahali pale walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema cho chote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. Wala hapakuwepo mtu ye yote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa wale mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

Kila Mstari katika Mpangilio wa Biblia - 313 vifungu

Kwa hiyo akaogopa, akasema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ndipo nyumba ya Mungu ilipo, hili ni lango la mbinguni.”

nalo jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu na katika yote utakayonipa nitakutolea wewe sehemu ya kumi.”

Wakati wa mchana BWANA aliwatangulia kwa nguzo ya wingu kuwaongoza katika njia yao, na wakati wa usiku aliwatangulia kwa nguzo ya moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana au usiku. Ile nguzo ya wingu wakati wa mchana au ile nguzo ya moto wakati wa usiku haikuondoka mahali pake mbele ya watu.

Sasa kama mkinitii kikamilifu na kutunza Agano langu, basi ninyi mtakuwa mali yangu ya thamani kubwa miongoni mwa mataifa yote. Ijapokuwa dunia yote ni mali yangu, ninyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Haya ndiyo maneno utakayosema kwa wana wa Israeli.”

Hata makuhani, watakaomkaribia BWANA ni lazima wajiweke wakfu, la sivyo BWANA atawaadhibu.”

“Kisha amuru watengeneze mahali patakatifu kwa ajili yangu, nami nitakaa miongoni mwao.

Kila mara Mose alipoingia ndani ya hema, nguzo ya wingu ingeshuka chini na kukaa kwenye ingilio, wakati Mungu akizungumza na Mose. Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake. BWANA angezungumza na Mose uso kwa uso, kama vile mtu azungumzavyo na rafiki yake. Kisha Mose angerudi kambini, lakini msaidizi wake kijana Yoshua mwana wa Nuni hakuondoka mle Hemani.

“Wewe na wanao msinywe mvinyo wala kinywaji kingine kilichochachuka wakati mwingiapo katika Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa. Hili litakuwa Agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Ni lazima mtenganishe kilicho kitakatifu na kile kilicho cha kawaida, kati ya yaliyo najisi na yaliyo safi,

Katika siku hiyo ambayo Maskani, Hema la Ushuhuda, liliposimamishwa, wingu liliifunika. Kuanzia jioni mpaka asubuhi wingu lililokuwa juu ya maskani lilionekana kama moto. Hivyo ndivyo lilivyoendelea kuwa; wingu liliifunika wakati wa mchana, na usiku lilionekana kama moto.

Sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowaleta Waisraeli kutoka Misri hadi leo. Nimekuwa nikitembea kutoka mahali pamoja hadi mahali pengine ndani ya hema kama makao yangu.

“Kwa habari ya Hekalu hili unalojenga, kama ukifuata amri zangu, ukatunza masharti yangu na kushika maagizo yangu yote na kuyatii, kwa kupitia wewe nitatimiza ahadi niliyomwahidi Daudi baba yako. Nami nitakaa miongoni mwa Waisraeli, nami sitawaacha watu wangu Israeli.”

Makuhani walipoondoka katika Mahali Patakatifu, wingu likalijaza Hekalu la BWANA. Nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa BWANA ulilijaza Hekalu lake.

Solomoni alipomaliza kujenga Hekalu la BWANA pamoja na jumba la kifalme, alipokwisha kufanya yote aliyotaka kufanya,

Hilkia kuhani mkuu akamwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Torati ndani ya Hekalu la BWANA.” Akampa Shafani, ambaye alikisoma.

Akabomoa pia nyumba za mahanithi wa mahali pa ibada za miungu, zilizokuwa ndani ya Hekalu la BWANA na mahali wanawake walipofuma kwa ajili ya Ashera.

Sasa itoeni mioyo yenu na nafsi zenu katika kumtafuta BWANA Mungu wenu. Anzeni kujenga Maskani ya BWANA Mungu, ili mweze kulileta Sanduku la Agano la BWANA na vyombo vitakatifu vya Mungu katika Hekalu litakalojengwa kwa ajili ya Jina la BWANA.”

Wapiga tarumbeta na waimbaji wakaungana katika sauti linganifu, ikawa kama vile ni sauti moja, wakimsifu na kumshukuru BWANA, nao alipoinua sauti zao pamoja na tarumbeta na matoazi na vyombo vingine vya uimbaji, wakamsifu BWANA wakisema: “Yeye ni mwema; upendo wake unadumu milele.” Ndipo Hekalu la BWANA likajazwa na wingu, nao makuhani hawakuweza kusimama kufanya huduma yao kwa sababu ya wingu, kwa maana utukufu wa BWANA ulilijaza Hekalu la Mungu.

Baada ya Solomoni kumaliza kuomba, moto ukashuka kutoka mbinguni na kuteketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu, nao utukufu wa BWANA ukalijaza Hekalu. Makuhani hawakuweza kuingia ndani ya Hekalu la BWANA kwa sababu utukufu wa BWANA ulilijaza. Waisraeli wote walipoona moto ukishuka na utukufu wa BWANA ukiwa juu ya Hekalu, wakapiga magoti sakafuni wakasujudu nyuso zao mpaka chini, nao wakamwabudu na kumshukuru BWANA wakisema, “Yeye ni mwema; upendo wake unadumu milele.”

Pia akawaweka mabawabu kwenye malango ya Hekalu la BWANA ili kwamba kwa vyo vyote asije akaingia mtu ye yote aliye najisi.

Msiwe na shingo ngumu, kama baba zenu walivyokuwa, bali nyenyekeeni kwa BWANA. Njoni mahali patakatifu, alipopatakasa milele. Mtumikieni BWANA Mungu wenu, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nanyi.

Akawaagiza watu wanaoishi Yerusalemu watoe sehemu iliyo haki ya makuhani na Walawi ili waweze kujitoa kikamilifu kutimiza wajibu wao katika Sheria ya BWANA.

BWANA, Mungu wa baba zao, akawapelekea neno kupitia wajumbe wake tena na tena, kwa sababu alikuwa anawahurumia watu wake pamoja na mahali pa maskani yake.

Walisoma kutoka katika kile Kitabu cha Sheria ya Mungu, wakiifafanua na kuwapa maelezo ili watu waweze kufahamu kile kilichokuwa kikisomwa.

Watu wa Israeli, pamoja na Walawi itawapasa kuleta michango yao ya nafaka, divai mpya na mafuta katika vyumba vya ghala mahali vifaa vya mahali patakatifu vihifadhiwapo na wanapokaa makuhani wanaohudumu, mabawabu na waimbaji. “Hatutaacha kuijali nyumba ya Mungu wetu.”

Kwa habari ya watakatifu walioko duniani, ndio walio wa fahari ambao ninapendezwa nao.

Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu, katika kusanyiko nitakusifu wewe.

Hakika wema na upendo vitanifuata siku zote za maisha yangu, nami nitakaa nyumbani mwa BWANA milele.

Jambo moja ninamwomba BWANA, hili ndilo ninalolitafuta: niweze kukaa nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa BWANA na kumtafuta hekaluni mwake.

Waokoe watu wako na uubariki urithi wako; uwe mchungaji wao na uwabebe milele.

Mtukuzeni BWANA pamoja nami, naam, na tulitukuze jina lake pamoja.

Vitu hivi ninavikumbuka ninapoimimina nafsi yangu: Jinsi nilivyokuwa nikienda na umati wa watu, nikiongoza maandamano kuelekea kwenye nyumba ya Mungu, kwa kelele za shangwe na za shukrani katikati ya umati wa watu wanaoadhimisha sikukuu.

Heri wale uliowachagua na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako! Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako, mema ya Hekalu lako takatifu.

Mungu huwaweka wapweke katika jamaa, huwaongoza wafungwa wakiimba, bali waasi huishi katika nchi kame.

Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako, tutakusifu milele; toka kizazi hadi kizazi tutasimulia sifa zako.

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Gitithi. Zaburi Ya Wana Wa Kora) Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, makao yako yapendeza kama nini! Nafsi yangu inatamani sana, naam, hata kuona shauku, kwa ajili ya nyua za BWANA; moyo wangu na mwili wangu vinamlilia Mungu Aliye Hai. Hata shomoro amejipatia makao, mbayuwayu amejipatia kiota mahali awezapo kuweka makinda yake: mahali karibu na madhabahu yako, Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mfalme wangu na Mungu wangu. Heri wale wanaokaa nyumbani mwako, wanaokusifu wewe daima.

Siku moja katika nyua zako ni bora kuliko siku elfu mahali pengine; afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu kuliko kukaa katika mahema ya waovu.

Katika kusanyiko la watakatifu Mungu huogopwa sana, anahofiwa kuliko wote wanaomzunguka.

waliopandwa katika nyumba ya BWANA, watastawi katika nyua za Mungu wetu.

Msifuni BWANA. Nitamtukuza BWANA kwa moyo wangu wote, katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko.

(Wimbo Wa Kwenda Juu) Nilishangilia pamoja na wale walioniambia, “Twende katika nyumba ya BWANA.”

(Wimbo Wa Kwenda Juu. Wa Solomoni) BWANA asipoijenga nyumba, wajengao hufanya kazi bure. BWANA asipoulinda mji, walinzi wakesha bure.

(Wimbo Wa Kwenda Juu. Wa Daudi) Tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza wakati ndugu wanapoishi pamoja katika umoja!

Msifuni BWANA. Mwimbieni BWANA wimbo mpya, sifa zake katika kusanyiko la watakatifu.

Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea, naye hataiacha hata akiwa mzee.

Kama vile chuma kinoavyo chuma, ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.

Linda hatua zako uendapo katika nyumba ya Mungu. Karibia usikilize kuliko kutoa dhabihu ya wapumbavu, ambao hawajui kuwa wanafanya kosa.

Katika mwaka ule Mfalme Uzia alipokufa, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu.

Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?” Nami nikasema, “Mimi hapa. Nitume mimi!” Akasema, “Nenda ukawaambie watu hawa: “ ‘Mtaendelea daima kusikia, lakini kamwe hamtafahamu; mtaendelea daima kuona, lakini kamwe hamtatambua.’

Ondokeni, ondokeni, tokeni huko! Msiguse kitu kilicho najisi! Tokeni kati yake mwe safi, ninyi mchukuao vyombo vya BWANA.

Wageni wanaoambatana na BWANA kumtumikia, kulipenda jina la BWANA, na kumwabudu yeye, wote washikao Sabato bila kuinajisi na ambao hushika sana Agano langu hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala. Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao zitakubalika juu ya madhabahu yangu, kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.”

Kisha nitawapeni wachungaji wanipendezao moyo wangu ambao watawaongoza kwa maarifa na ufahamu.

“Ole wa wachungaji wanaoharibu na kutawanya kondoo wa malisho yangu!” Asema BWANA. Kwa hiyo hili ndilo BWANA, Mungu wa Israeli, analowaambia wachungaji wanaowachunga watu wangu: “Kwa sababu mmelitawanya kundi langu, na kuwafukuzia mbali wala hamkuwatunza, basi mimi nitawaadhibu kwa ajili ya uovu mliofanya,” asema BWANA. “Mimi mwenyewe nitayakusanya mabaki ya kundi langu kutoka nchi zote ambazo nimewafukuzia nami nitawarudisha katika malisho yao, mahali ambapo watazaa na kuongezeka idadi yao. Nitaweka wachungaji juu yao ambao watawachunga, nao hawataogopa tena au kutishwa, wala hatapotea hata mmoja,” asema BWANA.

“Nabii na kuhani wote si wacha Mungu; hata hekaluni mwangu ninaona uovu wao,” asema BWANA.

“Mwanadamu, nimekufanya uwe mlinzi wa nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo, ukawape onyo litokalo kwangu. Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ na wewe usipomwonya mtu huyo au kumshauri aache njia zake mbaya ili kuokoa maisha yake, huyo mtu mwovu atakufa katika dhambi yake na damu yake nitaidai mkononi mwako. Lakini ukimwonya mtu mwovu naye akakataa kuacha uovu wake na njia zake mbaya, atakufa katika dhambi yake, lakini wewe utakuwa umejiokoa nafsi yako. “Tena, mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda maovu, nami nikaweka kikwazo mbele yake mtu huyo atakufa. Kwa kuwa hukumwonya, atakufa katika dhambi yake. Mambo ya haki aliyotenda, hayatakumbukwa, damu yake nitaidai mkononi mwako. Lakini ukimwonya mwenye haki asitende dhambi na akaacha kutenda dhambi, hakika ataishi kwa sababu alipokea maonyo na utakuwa umejiokoa nafsi yako.”

Makuhani wake wameihalifu sheria yangu na kunajisi vitu vyangu vitakatifu, hawatofautishi kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida. Wanafundisha kuwa hakuna tofauti kati ya vitu vilivyo najisi na visivyo najisi, nao wanafumba macho yao katika kutunza Sabato zangu, hivyo katikati yao nimetiwa unajisi.

“Mwanadamu, tabiri juu ya wachungaji wa Israeli, tabiri na uwaambie: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ole wa wachungaji wa Israeli ambao hujitunza wenyewe tu! Je, haiwapasi wachungaji kutunza kundi la kondoo? Mnakula mafuta ya wanyama, mnavaa mavazi ya sufu na kuchinja kondoo walionona, lakini hamlitunzi kundi. Hamkuwatia nguvu walio dhaifu wala hamkuwaganga wenye maradhi wala kuwafunga waliojeruhiwa. Hamkuwarudisha waliotangatanga wala kuwatafuta wale waliopotea. Badala yake mmewatawala kwa ukali na kwa ukatili. Hivyo walitawanyika kwa sababu hapakuwepo mchungaji, nao walipotawanyika, wakawa chakula cha wanyama wa mwitu wote. Kondoo wangu walitawanyika, wakatangatanga kwenye milima yote na kwenye kila kilima kirefu. Kondoo wangu walitawanyika juu ya uso wa dunia yote bila kuwa na ye yote wa kuwaulizia wala wa kuwatafuta.

“ ‘Kwa hiyo, ninyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA: Kwa hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, kwa sababu kondoo zangu wamekosa mchungaji na hivyo wametekwa nyara na kuwa chakula cha wanyama wote wa mwituni na kwa sababu wachungaji wangu, hawakuwatafuta kondoo zangu, bali wachungaji wamejitunza wenyewe, nao hawakuwalisha kondoo zangu, kwa hiyo enyi wachungaji, sikieni neno la BWANA: Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mimi ni kinyume na wachungaji nami nitawadai kondoo zangu mikononi mwao. Nitawafukuza kutoka kwenye kuchunga kundi langu, ili wachungaji wasiendelee kujitunza wenyewe. Nitaokoa kondoo zangu kutoka kwenye vinywa vyao, nao kondoo hawatakuwa tena chakula chao.

“ ‘Kwa hiyo, hili ndilo BWANA Mwenyezi awaambialo: Tazama, mimi mwenyewe nitahukumu kati ya kondoo wanono na waliokonda. Kwa sababu mmewapiga kikumbo na kuwapiga kwa pembe zenu kondoo wote walio dhaifu mpaka wakawafukuza, nitaliokoa kundi langu na hawatatekwa nyara tena. Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo.

Nitaweka juu yao mchungaji mmoja, mtumishi wangu Daudi, naye atawachunga, atawachunga na kuwa mchungaji wao.

Maskani yangu yatakuwa pamoja nao, nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.

Kisha yule mtu akanileta kwa njia ya lango la kaskazini mpaka mbele ya Hekalu. Nikatazama nami nikauona utukufu wa BWANA ukilijaza Hekalu la BWANA, nami nikaanguka kifudifudi.

Watawafundisha watu wangu tofauti kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida na kuwaonyesha jinsi ya kupambanua kati ya vitu najisi na vitu safi.

Siku atakapoingia katika ukumbi wa ndani wa mahali patakatifu ili kuhudumu, atatoa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe, asema BWANA Mwenyezi.

Itakuwa sehemu takatifu ya nchi kwa ajili ya makuhani, wale wanaohudumu ndani ya mahali patakatifu na ambao hukaribia ili kuhudumu mbele za BWANA. Patakuwa mahali pa nyumba zao pamoja na sehemu kwa ajili ya mahali patakatifu.

“Hata itakuwa, baada ya hayo, nitamimina Roho yangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono. Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho yangu.

Hakika BWANA Mwenyezi hatafanya neno lo lote bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.

Nitatikisa mataifa yote, nacho kile kinachotamaniwa na mataifa yote kitakuja, nami nitaujaza utukufu katika nyumba hii,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. ‘Fedha ni mali yangu na dhahabu ni mali yangu,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. ‘Utukufu wa nyumba hii ya sasa utakuwa mkubwa kuliko utukufu wa ile nyumba ya mwanzoni,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. ‘Na mahali hapa nitawapa amani,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote.”

“Kwa maana yapasa midomo ya kuhani kuhifadhi maarifa. Tena kutoka kinywani mwake watu wangepaswa kutafuta mafundisho, kwa sababu yeye ni mjumbe wa BWANA Mwenye Nguvu Zote.

Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi mpaka mkose nafasi ya kutosha au la.

Yesu akawaambia, “Njoni, nifuateni, nami nitawafanya muwe wavuvi wa watu.”

Yesu akapita katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu, akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu.

Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao.

Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake na haya yote mtaongezewa.

“Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa mwitu wakali.

Yesu akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme na kuponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu. Alipoona makutano aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache, Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watenda kazi katika shamba lake la mavuno.”

Ndipo Yesu akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa mamlaka juu ya pepo wachafu kuwatoa na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila aina.

Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure.

“Jihadharini na wanadamu, kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kuwapiga kwenye masinagogi yao,

“Mtu ye yote atakayewapokea ninyi atakuwa amenipokea mimi na ye yote atakayenipokea mimi atakuwa amempokea yeye aliyenituma. Mtu ye yote anayempokea nabii kwa kuwa ni nabii, atapokea thawabu ya nabii na mtu anayempokea mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapokea thawabu ya mwenye haki. Kama ye yote akimpa hata kikombe cha maji mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, ninawaambia, hataikosa thawabu yake.”

Alipofika mjini kwao, akawafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza?”

Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, hata malango ya kuzimu hayataweza kulishinda. Nitakupa funguo za Ufalme wa Mbinguni na lo lote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, lo lote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa Mbinguni.”

“Mwaonaje? Ikiwa mtu anao kondoo mia moja na mmoja wao akapotea, hatawaacha wale tisini na tisa vilimani na kwenda kumtafuta huyo mmoja aliyepotea? Naye akisha mpata, amin, nawaambia, hufurahi zaidi kwa ajili ya huyo kondoo mmoja kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea.

“Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako. Lakini kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno lithibitishwe na ushahidi wa mashahidi wawili au watatu. Kama akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa, naye kama akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi mtendeeni mtu huyo kama vile ambavyo mngemtendea asiyeamini.

Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”

Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, ye yote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, Naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu ni lazima awe mtumwa wenu, kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni, akazipindua meza za watu waliokuwa wakibadilisha fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.”

Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya. Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walipoona mambo ya ajabu aliyofanya na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi”, walikasirika.

“Lakini ninyi msiitwe ‘Rabi’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu. Nanyi msimwite mtu ye yote ‘Baba,’ hapa duniani kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni. Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Kristo. Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu. Kwa kuwa ye yote anayejikweza atashushwa na ye yote anayejinyenyekeza atakwezwa.

Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo na kufanya ishara kubwa na miujiza mingi ili kuwapotosha, hata ikiwezekana wale wateule hasa.

nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’

Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka.

Kwa sababu hii, enendeni ulimwenguni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.” Amen.

Kwa hiyo akazunguka Galilaya kote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu. Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.” Yesu akiwa amejawa na huruma, akanyosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka takasika!”

Akawachagua kumi na wawili ambao pia aliwaita mitume, ili wapate kuwa pamoja naye na kuwatuma kwenda kuhubiri na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu.

Ilipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi na wengi waliomsikia wakashangaa. Wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake!

Huniabudu bure, wakifundisha mapokeo ya wanadamu.’ Ninyi mmeziacha amri za Mungu na kushika desturi za watu.” Naye akawaambia, “Ninyi mnayo njia nzuri ya kukataa amri za Mungu ili mpate kuzishika desturi zenu!

Kwa njia hiyo ninyi mnabatilisha neno la Mungu kwa taratibu zenu mlizojiwekea. Nanyi mnafanya mambo mengi ya jinsi hiyo.”

Amin, amin nawaambia, ye yote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Kristo, hakika hataikosa thawabu yake.”

Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia Hekaluni akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wananunua na kuuza humo ndani. Akapindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, wala hakumruhusu mtu ye yote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu. Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa: “ ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote’? Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyang'anyi.’ ”

Ndipo Yesu akajibu akasema, “Je, unayaona majengo haya yalivyo makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, yote yatabomolewa.”

“Lakini ninyi jihadharini. Kwa maana watawapeleka mahakamani na kuwapiga mijeledi katika masinagogi. Mtashtakiwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao.

Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini.

Akawaambia, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Ye yote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini ye yote asiyeamini atahukumiwa. Nazo ishara hizi zitafuatana na wale waaminio: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu, watasema kwa lugha mpya, watashika nyoka kwa mikono yao na hata wakinywa kitu cho chote cha kuua, hakitawadhuru kamwe, wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”

Kisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.

Yesu akaenda Nazareti, hapo alipolelewa na siku ya Sabato alikwenda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome,

Wakashangazwa sana na mafundisho yake, maana maneno yake yalikuwa na mamlaka. Ndani ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, akapiga kelele kwa nguvu akisema, “Tuache! Tuna nini nawe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.” Basi Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akisema, “Nyamaza na umtoke!” Yule pepo mchafu akamwangusha chini yule mtu mbele yao wote, akatoka pasipo kumdhuru. Watu wote wakashangaa wakaambiana, “Mafundisho haya ni ya namna gani? Kwa mamlaka na nguvu, anawaamuru pepo wachafu, nao wanatoka!”

Naye aliendelea kuhubiri katika masinagogi ya Uyahudi.

vivyo hivyo wenzake Simoni, yaani, Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo walishangazwa pia. Ndipo Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.”

Ikawa siku nyingine ya Sabato Yesu aliingia ndani ya sinagogi akawa anafundisha, huko palikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza.

Mwanafunzi hamzidi mwalimu wake, ila yule aliyehitimu aweza kuwa kama mwalimu wake.

Yesu akiisha kuwaita wale kumi na wawili pamoja, aliwapa mamlaka na uwezo wa kutoa pepo wachafu wote na kuponya magonjwa yote, kisha akawatuma waende wakahubiri Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa.

Bali utafuteni Ufalme wa Mungu na vitu hivyo vyote atawapatia pia. “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme.

Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato. Wakati uo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na minane, wala alikuwa hawezi kunyoka wima. Yesu alipomwona, akamwita akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.” Yesu alipomwekea mikono yake, mara akasimama wima akaanza kumtukuza Mungu. Lakini mkuu wa sinagogi, akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Kwa hiyo mkuu wa sinagogi akaendelea kuuambia ule umati wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi, katika siku hizo, njoni mponywe, lakini si kuja kuponywa siku ya Sabato.”

“Ikiwa mmoja wenu ana kondoo mia moja naye akapoteza mmoja wao, je, hawaachi wale tisini na tisa nyikani na kwenda kumtafuta huyo aliyepotea mpaka ampate? Naye akiisha kumpata, kwa furaha humbeba mabegani mwake na kwenda nyumbani. Kisha huwaita rafiki zake na majirani na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami, nimempata kondoo wangu aliyepotea.’ Nawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.”

Kwa hiyo, jilindeni. “Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe.

kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili.

Kisha wakamwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu. Nao wakadumu ndani ya Hekalu wakimtukuza Mungu. Amen.

Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka kwenye eneo la Hekalu pamoja na kondoo na ng'ombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao. Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa biashara?” Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa imeandikwa: “Wivu wa nyumba yako utanila.”

Hivyo Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.

Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.

“Amri mpya nawapa: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi, vivyo hivyo nanyi mpendane. Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.”

Watawatenga na masinagogi. Naam, saa yaja ambayo mtu ye yote atakayewaua atadhani kwa kufanya hivyo anamtumikia Mungu. Nao watawatenda haya kwa sababu hawamjui Baba wala mimi.

Mimi sasa simo tena ulimwenguni, lakini wao bado wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba Mtakatifu, uwalinde kwa uweza wa jina lako ulilonipa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja.

Wao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndilo kweli.

ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiye uliyenituma mimi. Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja.

Walipokwisha kula, Yesu akamwuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?” Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.” Yesu akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.” Yesu akamwambia tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?” Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.” Yesu akamwambia, “Chunga kondoo zangu.” Kwa mara ya tatu Yesu akamwuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?” Petro akahuzunika sana kwa kuwa Yesu alimwuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.” Yesu akamwambia, “Lisha kondoo zangu.

Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”

Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwapo wanawake kadha wa kadha na Maria mama yake Yesu pamoja na ndugu zake Yesu. Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao wote walikuwa watu wapatao 120), akasema,

Ilipowadia siku ya Pentekoste, walikuwa wote mahali pamoja. Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo uliotoka mbinguni, ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.

Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000. Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, wakamgawia kila mtu kwa kadiri alivyokuwa anahitaji. Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa kwa wale watu waliokuwa wakiokolewa.

Walipokwisha kuomba, mahali pale walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema cho chote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. Wala hapakuwepo mtu ye yote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa wale mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

Hofu kuu ikalipata kanisa lote pamoja na watu wote waliosikia juu ya matukio haya. Mitume wakafanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Nao wale wote walioamini walikuwa wakikusanyika katika ukumbi wa Solomoni kwa nia moja. Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. Lakini wengi walioamini idadi kubwa ya wanaume na wanawake wakaongezeka kwa Bwana. Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. Pia watu wakakusanyika kutoka katika miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu, hao wote wakaponywa.

Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema kwamba Yesu ndiye Kristo.

wakati sisi tutatumia muda wetu mrefu kuomba na kulihudumia lile neno.”

Neno la Mungu likazidi kuenea. Idadi ya wanafunzi ikazidi kuongezeka sana katika Yerusalemu hata makuhani wengi wakaitii ile imani. Stefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu. Hata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa Sinagogi la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa), la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano. Lakini hawakuweza kushindana na hekima yake wala huyo Roho ambaye alisema kwake. Ndipo kwa siri wakawashawishi watu fulani waseme, “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kufuru dhidi ya Mose na dhidi ya Mungu.”

“Hata hivyo, Yeye Aliye Juu Sana hakai kwenye nyumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu. Kama nabii alivyosema: “ ‘Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu. Mtanijengea nyumba ya namna gani? asema Bwana. Au mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?

Naye Sauli alikuwepo pale, akiridhia kuuawa kwa Stefano. Siku ile kukatukia mateso makuu dhidi ya kanisa huko Yerusalemu, waumini wote isipokuwa mitume wakatawanyika, wakakimbilia Uyahudi na Samaria.

Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipokwenda. Filipo akatelemkia mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo. Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza aliyofanya, wakasikiliza kwa bidii yale aliyosema. Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.

Wakati ule ule, Sauli alikuwa bado anazidisha vitisho vya kuua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, naye akamwomba Kuhani Mkuu ampe barua ya kwenda kwenye masinagogi huko Dameski, ili akimkuta mtu ye yote wa Njia Ile, akiwa mwanaume au mwanamke, aweze kuwafunga na kuwaleta Yerusalemu.

Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?” Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?” Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu unayemtesa.” “Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.” Watu wale waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila kuwa na la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza. Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu cho chote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza mpaka Dameski. Naye kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu naye hakula wala kunywa cho chote.

Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba “Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu” Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wamefungwa mbele ya viongozi wa makuhani?” Sauli akazidi kuwa uhodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Yesu ndiye Kristo.

Sauli alipofika Yerusalemu akajaribu kujiunga na wanafunzi lakini wote walimwogopa, kwa maana hawakuamini kwamba kweli naye alikuwa mwanafunzi. Lakini Barnaba akamchukua, akampeleka kwa wale mitume. Akawaeleza jinsi Sauli akiwa njiani alivyomwona Bwana, jinsi Bwana alivyosema naye na jinsi alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Yesu huko Dameski. Kwa hiyo Sauli akakaa nao akishirikiana nao na akihubiri waziwazi kwa jina la Yesu kila mahali huko Yerusalemu. Alinena na kuhojiana na Wayahudi wenye asili ya Kiyunani lakini wao walijaribu kumwua.

Ndipo kanisa katika Uyahudi wote, Galilaya na Samaria likafurahia wakati wa amani. Likatiwa nguvu na likaendelea kudumu katika kumcha Bwana na kwa faraja ya Roho Mtakatifu, idadi yake ikazidi kuongezeka.

Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyetiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu.

Mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, nayo idadi kubwa ya watu wakaamini na kumgeukia Bwana.

naye alipompata akamleta Antiokia. Hivyo kwa mwaka mzima Barnaba na Sauli wakakutana na kanisa na kufundisha idadi kubwa ya watu. Ilikuwa ni katika kanisa la Antiokia kwa mara ya kwanza wanafunzi waliitwa Wakristo.

Ilikuwa wakati kama huu Mfalme Herode Agripa aliwakamata baadhi ya watu wa kanisa. Akaamuru Yakobo, ndugu yake Yohana, auawe kwa upanga. Alipoona jambo hilo limewapendeza Wayahudi, akaendelea, akamkamata pia Petro. Hii ilitokea wakati wa Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu.

Kwa hiyo Petro akawekwa gerezani, lakini kanisa lilikuwa likimwombea kwa Mungu kwa bidii. Usiku ule kabla ya siku ambayo Herode Agripa alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili, akiwa amefungwa kwa minyororo miwili. Nao walinzi wa zamu walikuwa wakilinda penye lango la gereza. Ghafula malaika wa Bwana akatokea na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro.

Paulo na Barnaba walipokuwa wakitoka nje ya sinagogi, watu wakawaomba wazungumze tena mambo hayo Sabato nyingine inayofuata. Baada ya kusanyiko la Sinagogi kutawanyika, wengi wa Wayahudi na waongofu wa dini ya Kiyahudi wakawafuata Paulo na Barnaba, wakazungumza nao na kuwahimiza wadumu katika neema ya Mungu. Sabato iliyofuata karibu watu wote wa mji ule walikuja kusikiliza neno la Mungu. Lakini Wayahudi walipoona ule umati mkubwa wa watu walijawa na wivu na kunena maneno ya kashfa kuhusu yale Paulo aliyokuwa akisema. Ndipo Paulo na Barnaba wakawajibu kwa ujasiri, wakisema, “Ilitupasa kunena nanyi neno la Mungu kwanza. Lakini kwa kuwa mmelikataa, mkajihukumu wenyewe kuwa hamstahili uzima wa milele, sasa tunawageukia watu Mataifa.

Huko Ikonio Paulo na Barnaba waliingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi kama kawaida yao. Huko wakahubiri kwa uwezo mkubwa kiasi kwamba Wayahudi pamoja na watu Mataifa wakaamini. Lakini wale Wayahudi waliokataa kuamini, wakawachochea watu Mataifa, wakatia chuki ndani ya mioyo yao dhidi ya wale walioamini. Hivyo Paulo na Barnaba wakakaa huko kwa muda wa kutosha wakihubiri kwa ujasiri juu ya Bwana, ambaye alithibitisha ujumbe wa neema yake kwa kuwawezesha kufanya ishara na miujiza.

Nao baada ya kuwateua wazee katika kila kanisa, kwa kufunga na kuomba wakawakabidhi kwa Bwana waliyemwamini.

Walipowasili Antiokia wakaliita kanisa pamoja na kutoa taarifa ya yale yote Mungu aliyokuwa ametenda kwa kupitia kwao na jinsi alivyokuwa amefungua mlango wa imani kwa ajili ya watu Mataifa.

Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka.

Hawa Wayahudi wa Beroya walikuwa waungwana zaidi kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa waliupokea ule ujumbe kwa shauku kubwa na kuyachunguza Maandiko kila siku ili kuona kama yale Paulo aliyosema yalikuwa kweli. Wayahudi wengi wakaamini pamoja na wanawake na wanaume wa Kiyunani wa tabaka la juu.

Hivyo akahojiana kila siku na Wayahudi pamoja na wacha Mungu kwenye sinagogi na pia sokoni kwa wale waliokutana naye huko.

Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao akijitahidi kuwavuta Wayahudi na Wayunani.

Apolo alianza kunena kwa ujasiri mkubwa katika sinagogi, Lakini Prisila na Akila walipomsikia walimchukua kando na kumweleza njia ya Mungu kwa ufasaha zaidi.

Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akawa na majadiliano ya kuwafanya watu waamini mambo yanayohusu Ufalme wa Mungu. Lakini baadhi yao kwa ukaidi walipokataa kuamini na kukashifu ujumbe wake mbele ya umati wa watu, Paulo aliachana nao, akawachukua wanafunzi na kuhojiana nao kila siku katika darasa la mtu mmoja aitwaye Tirano.

Wakati huo huo pakatokea dhiki kubwa kwa sababu ya Njia ile ya Bwana.

Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lo lote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba. Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.

Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua kwamba baada mimi kuondoka, mbwa mwitu wakali watakuja katikati yenu ambao hawatalihurumia kundi. Hata kutoka miongoni mwenu wenyewe watainuka watu na kuupotosha ukweli ili wawavute wanafunzi wawafuate. Hivyo jilindeni! Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuacha kamwe kuwaonya, kila mmoja kwa machozi usiku na mchana.

Niliwatesa watu wa Njia hii hadi kufa, nikiwakamata, waume kwa wake na kuwatupa gerezani. Kama Kuhani Mkuu na baraza zima la wazee wanavyoweza kushuhudia kuhusu mimi. Hata nilipokea barua kutoka kwao kwenda kwa wale wa Dameski, nami nikaenda huko ili kuwaleta watu hawa Yerusalemu kama wafungwa ili waadhibiwe.

Lakini, ninakubali kwamba mimi namwabudu Mungu wa baba zetu, mfuasi wa Njia, ile ambayo wao wanaiita dhehebu. Ninaamini kila kitu kinachokubaliana na Sheria na kile kilichoandikwa katika Manabii,

Basi Feliksi ambaye alikuwa anafahamu vizuri habari za Njia ile, akaahirisha shauri lile kwa maelezo yake akisema, “Wakati jemadari Lisia atakapotelemka huku, nitaamua shauri lako.”

Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume na kutengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu,

Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu.

Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyaoandikwa, “Ni mizuri mno miguu ya hao wanaohubiri Injili ya amani na kuleta habari ya mema!”

Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.

Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa kindugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine.

ili kuwa mhudumu wa Kristo Yesu kwa watu Mataifa nikiwa na huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.

Napenda kumtambulisha kwenu dada yetu Foibe, mtumishi katika kanisa la Kenkrea. Naomba mpokeeni katika Bwana ipasavyo watakatifu na kumpa msaada wo wote atakaohitaji kutoka kwenu, kwa maana yeye amekuwa msaada kwa watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao. Wasalimuni Prisila na Akila, watumishi wenzangu katika Kristo Yesu. Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu wala si mimi tu ninayewashukuru bali pia makanisa yote ya watu Mataifa. Lisalimuni pia kanisa linalokutana nyumbani mwao. Msalimuni rafiki yangu Epaineto, aliyekuwa mtu wa kwanza kumwamini Kristo huko Asia.

Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo yanawasalimu.

Kwa Kanisa la Mungu lililoko Korintho, kwa wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa kuwa watakatifu, pamoja na wale wote ambao kila mahali wanaliitia Jina la Kristo Yesu Bwana wetu, aliye Bwana wao na wetu pia:

Mungu ni mwaminifu, ambaye mmeitwa naye ili mwe na ushirika na Mwanawe Yesu Kristo, Bwana wetu. Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano katikati yenu na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi. Kwa maana ndugu zangu, nimepata habari kutoka kwa baadhi ya watu wa nyumbani mwa Kloe kwamba kuna magomvi katikati yenu. Maana yangu ni kwamba: Mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo”; mwingine, “Mimi ni wa Apolo”; mwingine, “Mimi ni wa Kefa”; na mwingine, “Mimi ni wa Kristo.” Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye aliyesulibishwa kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?

lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulibiwa, ambaye kwa Wayahudi ni kitu cha kukwaza na kwa Wayunani ni upuzi.

Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu.

Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya kuwashawishi watu, bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho Mtakatifu ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu. Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika. Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika kwa wanadamu, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu. Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati zetu aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangelielewa, wasingemsulibisha Bwana wa utukufu.

Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa wale watu wa kiroho.

Mimi nilipanda mbegu, Apolo akatia maji, lakini Mungu ndiye aliyekuza. Hivyo mwenye kupanda mbegu na mwenye kutia maji si kitu, bali Mungu peke yake ndiye akuzaye. Apandaye mbegu ni sawa na yule atiaye maji. Kila mmoja atalipwa kulingana na kazi yake. Sisi ni watenda kazi pamoja na Mungu, ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu.

Kwa neema Mungu aliyonipa, niliweka msingi kama mjenzi stadi na mtu mwingine anajenga juu ya huo msingi. Lakini kila mmoja inampasa awe mwangalifu jinsi anavyojenga juu yake. Kwa maana hakuna mtu ye yote awezaye kuweka msingi mwingine wo wote isipokuwa ule uliokwisha kuwekwa, ambao ni Yesu Kristo.

Je, hamjui ya kwamba ninyi ni Hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu ye yote akiliharibu Hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza mtu huyo, Kwa maana Hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.

Basi, watu na watuhesabu sisi kuwa tu watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu. Zaidi ya hayo, litakiwalo ni mawakili waonekane kuwa waaminifu.

Lakini sasa nawaandikia kwamba msishirikiane na mtu ye yote anayejiita ndugu, hali akiwa ni mzinzi, au mwenye tamaa mbaya, mwabudu sanamu au msingiziaji, mlevi au mdhalimu. Mtu kama huyo hata msile naye. Yanihusu nini kuwahukumu wale watu walio nje ya kanisa? Je, si mnapaswa kuwahukumu hao walio ndani ya kanisa? Mungu atawahukumu hao walio nje ya kanisa. “Ninyi mwondoeni huyo mtu mwovu miongoni mwenu.”

Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni Hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe,

Je, hamjui kwamba, watu wafanyao kazi Hekaluni hupata chakula chao kutoka Hekaluni, nao wale wahudumiao madhabahuni hushiriki kile kitolewacho madhabahuni? Vivyo hivyo, Bwana ameagiza kwamba wale wanaohubiri injili wapate mahitaji yao kutokana na injili.

Lakini ninapohubiri injili siwezi kujisifu maana ninalazimika kuhubiri. Ole wangu nisipoihubiri Injili!

Basi je, thawabu yangu ni nini? Thawabu yangu ni hii: Ni kwamba katika kuhubiri Injili niitoe bila gharama, nisije nikatumia vibaya ule uwezo wangu nilio nao katika Injili.

la, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha ili nikiisha kuwahubiria wengine, mimi nisiwe mtu wa kukataliwa.

Je, kikombe cha baraka ambacho tunakibariki, si ushirika katika damu ya Kristo? Mkate tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? (Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa wote twashiriki mkate mmoja). Waangalieni watu wa Israeli: Je, wale wote walao dhabihu si ni wale watendao kazi madhabahuni? Je, nina maana kwamba kafara iliyotolewa kwa sanamu ni kitu chenye maana yo yote? Au kwamba sanamu ni kitu chenye maana yo yote? La hasha! Lakini kafara za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani. Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.

Niigeni mimi, kama nami ninavyomwiga Kristo.

Basi katika maagizo yafuatayo, siwezi kuwasifu, kwa sababu mkutanikapo si kwa ajili ya faida bali kwa hasara. Kwanza, mnapokutana kama kanisa, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo. Bila shaka lazima pawe na tofauti miongoni mwenu ili kuonyesha ni nani anayekubaliwa na Mungu.

Maana kila mlapo mkate huu na kunywea kikombe hiki, mnatangaza mauti ya Bwana mpaka ajapo. Kwa hiyo, mtu ye yote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana. Inampasa mtu ajichunguze mwenyewe, kabla ya kula mkate na kukinywea kikombe. Kwa maana mtu ye yote alaye na kunywa pasipo kuutambua mwili wa Bwana, anajiletea hukumu juu yake mwenyewe. Hii ndiyo sababu wengi miongoni mwenu ni wagonjwa na dhaifu na wengine wenu hata wamekufa.

Basi ndugu zangu, kuhusu karama za rohoni, sitaki mkose kufahamu.

Basi kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule. Pia kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana ni yule yule. Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote. Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya. Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, kwa mwingine tafsiri za lugha. Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo mwenyewe.

Kama vile mwili ulivyo mmoja nao una viungo vingi, navyo viungo vyote vya mwili ingawa ni vingi, ni mwili mmoja, vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja wote tulibatizwa katika mwili mmoja, kama ni Wayahudi au Wayunani, kama ni watumwa au watu huru, nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

Basi mwili si kiungo kimoja, bali ni viungo vingi. Kama mguu ungesema, “Kwa kuwa mimi si mkono basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya huo mguu usiwe sehemu ya mwili. Na kama sikio lingesema, “Kwa kuwa mimi si jicho, basi mimi si la mwili,” hiyo isingefanya hilo sikio lisiwe sehemu ya mwili. Kama mwili wote ungelikuwa jicho, kusikia kungekuwa wapi? Au kama mwili wote ungelikuwa sikio, kunusa kungekuwa wapi? Lakini kama ilivyo, Mungu ameweka viungo katika mwili, kila kimoja kama alivyopenda. Kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Kama ulivyo, una viungo vingi, lakini mwili ni mmoja. Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sina haja nawe!” Wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu, “Sina haja na ninyi!” Lakini badala yake, vile viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu, ndivyo ambavyo ni vya muhimu sana. Navyo vile viungo vya mwili tunavyoviona havina heshima, ndivyo tunavipa heshima maalum. Vile viungo vya mwili ambavyo havina uzuri, tunavipa heshima ya pekee. Wakati vile viungo vyenye uzuri havihitaji utunzaji wa pekee. Lakini Mungu ameviweka pamoja viungo vya mwili na akavipa heshima zaidi vile vilivyopungukiwa, ili pasiwe na mafarakano katika mwili, bali viungo vyote vihudumiane kwa usawa kila kimoja na mwenzake. Kama kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia pamoja nacho, kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Sasa ninyi ni mwili wa Kristo na kila mmoja wenu ni kiungo.

Mungu ameweka katika kanisa, kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu, kisha watenda miujiza, pia karama za kuponya, karama za masaidiano, karama za maongozi, aina mbalimbali za lugha. Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote wanafanya miujiza? Je, wote wana karama ya kuponya? Je, wote hunena kwa lugha mpya? Je, wote wanatafsiri?

Lakini anayetoa unabii anasema na watu akiwajenga, kuwatia moyo na kuwafariji. Anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, bali atoaye unabii hulijenga kanisa. Ningependa kila mmoja wenu anene kwa lugha mpya, lakini ningependa zaidi nyote mtoe unabii. Kwa kuwa yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko anenaye kwa lugha, isipokuwa kama kuna mtu wa kutafsiri, ili kanisa zima lipate kujengwa.

Lakini ndani ya kanisa ni afadhali niseme maneno matano ya kueleweka kwa akili ili niwafundishe wengine kuliko kusema maneno 10,000 kwa lugha.

Basi kunena kwa lugha mpya ni ishara, si kwa watu waaminio, bali kwa ajili ya wasioamini, wakati unabii si kwa ajili ya wasioamini, bali kwa ajili ya waaminio. Kwa hiyo kama kanisa lote likikutana na kila mmoja akanena kwa lugha, kisha wakaingia wageni wasioamini, je, hawatasema kwamba wote mna wazimu? Lakini kama mtu asiyeamini au asiyeelewa akiingia wakati kila mtu anatoa unabii, ataaminishwa na watu wote kuwa yeye ni mwenye dhambi na kuhukumiwa na wote, nazo siri za moyo wake zitawekwa wazi. Kwa hiyo ataanguka chini na kumwabudu Mungu akikiri, “Kweli Mungu yuko katikati yenu!”

Basi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, mmoja ana wimbo, mwingine neno la mafundisho, mwingine ufunuo kutoka kwa Mungu, mwingine ataongea lugha mpya na mwingine atatafsiri hiyo lugha. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kujenga kanisa. Kama mtu ye yote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu si zaidi, mmoja baada ya mwingine na lazima awepo mtu wa kutafsiri. Lakini kama hakuna mtu ye yote wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya kanisani na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu. Manabii wawili au watatu wanene na wengine wapime yale yasemwayo. Kama mtu ye yote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze. Kwa maana wote mnaweza kutoa unabii, mmoja baada ya mwingine, ili kila mtu apate kufundishwa na kutiwa moyo. Roho za manabii huwatii manabii. Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani. Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu,

wanawake wanapaswa kuwa kimya kanisani. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama sheria isemavyo. Kama wakitaka kuuliza kuhusu jambo lo lote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza kanisani. Je, neno la Mungu lilianzia kwenu? Au ni ninyi tu ambao neno la Mungu limewafikia? Kama mtu ye yote akidhani kwamba yeye ni nabii, au ana karama za rohoni, basi na akubali kwamba haya ninayoandika ni maagizo kutoka kwa Bwana. Kama mtu akipuuza jambo hili yeye mwenyewe atapuuzwa.

Kwa hiyo ndugu zangu, takeni sana kutoa unabii na msikataze watu kusema kwa lugha. Lakini kila kitu kitendeke kwa heshima na kwa utaratibu.

Kwa maana mimi ndiye mdogo kuliko mitume wote, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu.

Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.”

Pia ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.

Tofauti na watu wengine wengi, sisi hatufanyi biashara na Neno la Mungu kwa ajili ya kupata faida. Kinyume chake, katika Kristo tunalisema Neno la Mungu kwa unyofu, kama watu tuliotumwa kutoka kwa Mungu.

Si kwamba sisi tunafikiri kuwa tunaweza kufanya jambo lo lote wenyewe, lakini nguvu yetu inatoka kwa Mungu. Yeye ndiye aliyetuwezesha sisi kuwa wahudumu wa Agano Jipya: si wa andiko, bali wa Roho; kwa kuwa andiko huua bali Roho hutia uzima.

Tumekataa mambo ya siri na ya aibu, wala hatufuati njia za udanganyifu, tukichanganya Neno la Mungu na uongo. Kinyume cha hayo, tunadhihirisha kweli waziwazi na kujitambulisha wenyewe kwenye dhamiri ya kila mtu mbele za Mungu.

Kwa maana hatujihubiri sisi wenyewe ila tunamhubiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.

Kwa maana twajua kwamba kama hema yetu ya dunia tunayoishi ikiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu.

Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kwa kupitia vinywa vyetu, nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu.

Kama watenda kazi pamoja na Mungu, tunawasihi msipokee neema ya Mungu bure.

bali kama watumishi wa Mungu tuonyeshe kwa kila njia saburi nyingi katika dhiki, katika misiba, katika shida,

Kuna mapatano gani kati ya Hekalu la Mungu na sanamu? Kwa kuwa sisi tu Hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu alivyosema: “Nitakaa pamoja nao na kutembea katikati yao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.” “Kwa hiyo tokeni miongoni mwao, mkatengwe nao, asema Bwana. Msiguse kitu cho chote kilicho najisi, nami nitawakaribisha.”

wakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu.

Kwa habari ya Tito, yeye ni mwenzangu na mtenda kazi pamoja nami miongoni mwenu. Kwa habari za ndugu zetu, wao ni wawakilishi wa makanisa, na utukufu kwa Kristo. Kwa hiyo waonyesheni wazi hawa ndugu uthibitisho wa upendo wenu na sababu inayotufanya tujivune kwa ajili yenu, mbele ya makanisa, ili yapate kuona.

Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia. Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo.

Mambo yanayomtambulisha mtume wa kweli, yaani, ishara, miujiza na maajabu, yalifanywa miongoni mwenu kwa saburi nyingi.

Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu. Watakatifu wote wanawasalimu. Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote. Amen.

Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele! Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu ye yote atawahubiria injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele! Je, sasa mimi ninatafuta kukubaliwa na wanadamu au kukubaliwa na Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa bado najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumishi wa Kristo.

Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejezeni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo. Kama mtu ye yote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe.

Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa, ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.

Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena wala wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni. Ndani yake jengo lote limeshikamanishwa pamoja na kusimamishwa ili kuwa Hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa makao ambayo Mungu anaishi ndani yake kwa njia ya Roho wake.

Siri hii haikudhihirishwa kwa wanadamu katika vizazi vingine kama vile sasa ilivyodhihirishwa na Roho kwa mitume na manabii watakatifu wa Mungu. Siri hii ni kwamba, kwa njia ya Injili, watu Mataifa ni warithi pamoja na Israeli, viungo vya mwili mmoja na washiriki pamoja wa ahadi katika Kristo Yesu. Nimekuwa mtumishi wa Injili hii kwa kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa nguvu yake itendayo kazi. Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii ili niwahubirie watu Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Kristo na kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa kwa nyakati zote katika Mungu aliyeumba vitu vyote. Ili sasa kwa njia ya Kanisa, hekima yote ya Mungu ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho,

yeye atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.

Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa. Iweni wanyenyekevu kabisa na wapole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja. Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja, Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote.

Yeye ndiye aliyeweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo. Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu, siku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kwa heshima kwa ajili ya Kristo.

Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Kristo alivyo kichwa cha Kanisa, ambalo ni mwili wake, naye Kristo ni Mwokozi wake. Basi, kama vile Kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo. Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake, apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lo lote, bali takatifu lisilo na hatia.

Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza Kanisa lake. Sisi tu viungo vya mwili wake. “Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe na hawa wawili watakuwa mwili mmoja.” Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Kristo na Kanisa.

Kama kukiwa na jambo lo lote la kutia moyo, kukiwako faraja yo yote katika upendo, kukiwa na ushirika wo wote katika Roho, kukiwa na wema wo wote na huruma, basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia kama hiyo, mkiwa na upendo huo huo, wenye roho moja na kusudi moja. Msitende jambo lo lote kwa nia ya kujitukuza, bali kwa unyenyekevu, kila mtu akimhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. Kila mmoja wenu asiangalie mambo yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

Ndugu zangu, kwa pamoja fuateni mfano wangu na kuwatazama wale wanaofuata kielelezo tulichowawekea.

Naam, nawasihi ninyi pia, wenzi wangu waaminifu, wasaidieni hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watenda kazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.

Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani, Kanisa, naye ni wa mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote.

Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni Kanisa. Mimi nimekuwa mtumishi wa Kanisa kwa wajibu alionipa Mungu ili kuwaletea ninyi Neno la Mungu kwa ukamilifu.

wala hakishiki kwa uthabiti kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, ambao hukua kwa ukuaji utokao kwa Mungu.

Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu, wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. Vumilianeni na kusameheana. Mtu akiwa na lalamiko lo lote dhidi ya mwenzake, sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu. Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu.

Kinyume chake, tulinena kama watu tuliokubaliwa na Mungu tukakabidhiwa Injili. Sisi hatujaribu kuwapendeza wanadamu bali kumpendeza Mungu, yeye ayachunguzaye mawazo ya ndani sana ya mioyo yetu. Kama mjuavyo na Mungu akiwa shahidi yetu hatukuja kwenu kwa maneno ya kujipendekeza au maneno yasiyo ya kweli kwa ajili ya kuficha tamaa mbaya. Wala hatukuwa tunatafuta sifa kutoka kwa wanadamu, wala kutoka kwenu au kwa mtu mwingine awaye yote. Kama mitume wa Kristo tungaliweza kuwa mzigo kwenu, lakini tulikuwa wapole katikati yenu kama mama anayewatunza watoto wake wadogo. Tuliwapenda sana kiasi kwamba tulifurahia kushirikiana nanyi, si Injili ya Mungu tu, bali hata maisha yetu, kwa sababu mlikuwa wa thamani mno kwetu. Ndugu zetu, mnakumbuka juhudi yetu na taabu yetu. Tulifanya kazi usiku na mchana, ili tusimlemee mtu ye yote wa kwenu wakati tulipokuwa tunawahubiria Injili ya Mungu.

Sasa kuhusu upendano wa ndugu hamna haja mtu ye yote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.

Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa. Sasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana na ambao wanawaonya. Mkawajali sana katika upendo kwa ajili ya kazi yao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi. Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni wale wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na iweni na uvumilivu na kila mtu.

Ndiyo sababu miongoni mwa makanisa ya Mungu, tunajivuna kuhusu saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili. Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili Ufalme wa Mungu, ambao ninyi mnateswa kwa ajili yake.

Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa.

Ikiwa mtu ye yote hayatii maagizo yetu yaliyoko katika barua hii, mwangalieni sana mtu huyo. Msishirikiane naye, ili kwamba apate kuona aibu. Lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.

Watu wengine wamepotoka kutoka katika haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa, wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.

Nami kwa kusudi hili nimewekwa niwe mhubiri na mtume (nasema kweli katika Kristo wala sisemi uongo), mwalimu wa watu Mataifa katika imani na kweli. Nataka kila mahali wanaume wasali wakiinua mikono mitakatifu pasipo hasira wala kugombana.

Vivyo hivyo nataka wanawake wajipambe kwa adabu na kwa heshima katika mavazi yanayostahili, si kwa kusuka nywele, kuvalia dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa, bali kwa matendo mazuri kama iwapasavyo wanawake wanaokiri kuwa wanamcha Mungu. Mwanamke na ajifunze kwa utulivu na kwa utii wote. Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume. Mwanamke inampasa kukaa kimya. Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza, kisha Eva. Wala si Adamu aliyedanganywa, bali ni mwanamke aliyedanganywa akawa mkosaji.

Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kazi ya uangalizi, atamani kazi nzuri. Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?) Asiwe mtu aliyeongoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya Shetani. Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.

Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali. Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi. Ni lazima wapimwe kwanza, kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi. Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasiozungumza maneno ya kuwadhuru wengine, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo. Shemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema. Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Kristo Yesu.

kama nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa kweli.

Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani.

Kama ukiwakumbusha ndugu mambo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, uliyelelewa katika kweli ya imani na yale mafundisho mazuri uliyoyafuata. Usijishughulishe kamwe na hadithi za kipagani na masimulizi ya uongo ya wanawake wazee, badala yake, jizoeze kuwa mtauwa.

Mambo haya yaagize na kuyafundisha. Mtu ye yote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waaminio katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi. Fanya bidii kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. Usiache kutumia kipawa kilicho ndani yako, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee walipokuwekea mikono. Uwe na bidii katika mambo haya, jitolee kwa ajili ya mambo hayo kikamilifu, ili kila mtu aone kuendelea kwako. Jilinde sana nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika hayo, kwa maana kwa kufanya hivyo utajiokoa wewe mwenyewe pamoja na wale wanaokusikia.

Wazee wa kanisa wanaoongoza shughuli za kanisa vizuri wanastahili heshima mara mbili, hasa wale ambao kazi yao ni kuhubiri na kufundisha. Kwa maana Maandiko husema, “Usimfunge ng'ombe kinywa apurapo nafaka,” tena, “Mfanyakazi anastahili mshahara wake.” Usiendekeze mashtaka dhidi ya mzee isipokuwa yawe yameletwa na mashahidi wawili au watatu. Wale wanaodumu katika dhambi uwakemee hadharani, ili wengine wapate kuogopa. Ninakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu na mbele za malaika wateule, shika maagizo haya pasipo ubaguzi wala upendeleo. Usiwe na haraka kumwekea mtu mikono wala usishiriki dhambi za watu wengine. Jilinde nafsi yako uwe safi.

Ikiwa mtu ye yote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa, huyo amejivuna wala hajui kitu cho chote.

Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii. Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile.

Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vile vile. Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Kristo Yesu.

Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtenda kazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli. Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu. Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kuwako na kupotosha baadhi ya watu. Lakini msingi wa Mungu ulio madhubuti umesimama ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Bwana anawajua walio wake” tena, “Kila alitajaye jina la Bwana auache uovu.”

Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.

Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kuwaongoza na kuwafundisha katika haki ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, ili apate kutenda kila kazi njema.

Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake kwamba: Uhubiri Neno, uwe tayari wakati ufaao na wakati usiofaa, karipia, kemea na kuonya kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri. Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima, badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia. Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo. Kwa habari yako wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako.

Sababu ya mimi kukuacha huko Krete ni ili uweke kwenye utaratibu mambo yale yaliyosalia na kuwaweka wazee wa kanisa katika kila mji, kama nilivyokuagiza. Mzee wa kanisa asiwe na lawama, awe mume wa mke mmoja, mtu ambaye watoto wake ni waaminio na wala hawashtakiwi kwa ufisadi. Kwa kuwa mwangalizi, kama wakili wa Mungu, imempasa kuwa mtu asiye na lawama, asiwe mwenye majivuno au mwepesi wa hasira, wala mlevi, wala asiwe mtu mwenye tamaa ya mapato yasiyo ya halali. Bali awe mkarimu, anayependa mema, mwenye kiasi, mwenye haki, mwadilifu, mnyofu, mtakatifu na mwenye kuitawala nafsi yake. Inampasa alishike kwa uthabiti lile neno la imani kama lilivyofundishwa, kusudi aweze kuwafundisha wengine kwa mafundisho manyofu na kuwakanusha wale wanaopingana nayo.

Basi wewe fundisha mambo haya; onya na karipia kwa mamlaka yote. Mtu ye yote asikudharau.

Yeye husema, “Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu; mbele ya kusanyiko nitaimba sifa zako.” Tena, “Nitaweka tumaini langu kwake.” Tena anasema, “Niko hapa, mimi pamoja na watoto Mungu alionipa.” Basi kwa kuwa watoto wana nyama na damu, yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani, Shetani,

Lakini Kristo yeye ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu, sisi ndio nyumba yake, kama tutashikamana sana na ujasiri wetu na katika tumaini tunalojivunia.

Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu iitwapo Leo, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.

Kwa hakika, ingawa mpaka wakati huu ingewapasa kuwa walimu, lakini bado mnahitaji mtu wa kuwafundisha tena hatua za awali za kweli ya Neno la Mungu. Mnahitaji maziwa, wala si chakula kigumu! Kwa maana ye yote aishiye kwa kunywa maziwa bado yeye ni mtoto mchanga, hana ujuzi katika mafundisho kuhusu neno la haki. Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu wazima, ambao kwa kujizoeza wamejifunza kupambanua kati ya mema na mabaya.

basi kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu,

Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi ya kukutana, tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.

Lakini ninyi mmekuja Mlima Sayuni, Yerusalemu ya mbinguni, mji wa Mungu aliye hai. Mmekuja penye kusanyiko kubwa la malaika maelfu kwa maelfu wasiohesabika wanaoshangilia, kwenye kanisa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mmekuja kwa Mungu, mhukumu wa watu wote, kwenye roho za wenye haki waliokamilishwa,

Wakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Angalieni matokeo ya mwenendo wa maisha yao mkaiige imani yao.

Watiini viongozi wenu na kujinyenyekeza chini ya mamlaka yao. Kwa maana wao wanakesha kwa ajili yenu kama watu watakaopaswa kutoa hesabu. Watiini ili kwamba wafanye kazi yao kwa furaha, wala si kama mzigo, maana hiyo haitakuwa na faida kwenu. Tuombeeni. Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia.

Kwa maana kama akija mtu katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, pia akaingia mtu maskini mwenye mavazi yaliyochakaa, nanyi mkampa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,” je, hamjawabagua na kuwa mahakimu mioyoni mwenu mkihukumu kwa mawazo yenu maovu? Ndugu zangu, sikilizeni: Je, Mungu hakuwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi Ufalme aliowaahidi wale wampendao?

Je, kuna ye yote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana. Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua na kama ametenda dhambi, atasamehewa. Kwa hiyo ungamianeni makosa yenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.

Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa kuwa nyumba ya Roho, mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Kwa maana Andiko lasema: “Tazama, naweka katika Sayuni, Jiwe Kuu la pembeni, teule lenye thamani, na kila amwaminiye hataaibika.” Kwenu ninyi mnaoamini, yeye ni wa thamani. Lakini kwao wasioamini, “Jiwe lile walilolikataa waashi limekuwa Jiwe Kuu la pembeni,” tena, “Jiwe lenye kuwafanya watu wajikwae, mwamba wa kuwafanya waanguke.” Wanajikwaa kwa sababu hawakulitii lile neno: kama walivyowekewa tangu zamani. Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu la Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamkupata rehema, lakini sasa mmepata rehema.

Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. Iweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manung'uniko. Kila mmoja na atumie kipawa cho chote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu. Ye yote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Ye yote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile apewazo na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.

Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu. Basi kama ikianza kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje?

Kwa wazee waliomo miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Kristo na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa, lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe, si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika. Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali iweni vielelezo kwa hilo kundi. Naye Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa mtapokea taji ya utukufu isiyoharibika. Vivyo hivyo ninyi mlio vijana hamna budi kuwatii wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu katika kuhudumiana, kila mtu na mwenzake, kwa kuwa, “Mungu huwapinga wenye kiburi bali huwapa wanyenyekevu neema.”

Salimianeni kwa busu la upendo. Amani iwe nanyi nyote mlio katika Kristo. Amen.

Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama vile watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu, ambao kwa siri, wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli hata kumkana Bwana wa pekee aliyewanunua na kujiletea juu yao maangamizi ya haraka. Hata hivyo, wengi watafuata njia zao za ufisadi ambao kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa. Nao katika tamaa zao mbaya, watajipatia faida kwenu kwa maneno ya madanganyo waliyotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, ambayo haikawii wala uangamivu wao haujalala usingizi.

Twawatangazia lile tuliloliona na kulisikia, ili kwamba nanyi mwe na ushirika nasi. Na ushirika wetu hasa ni pamoja na Baba na Mwanawe, Yesu Kristo.

Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake yatusafisha dhambi yote.

Ye yote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.

Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu hasa. Kwa maana kama wangelikuwa wa kwetu, wangelikaa pamoja nasi, lakini kutoka kwao kulionyesha kwamba hakuna hata mmoja wao aliyekuwa wa kwetu.

Ninawaandikia mambo haya kuhusu wale watu ambao wanajaribu kuwapotosha. Kwa habari yenu ninyi, upako ule mlioupata kutoka kwake unakaa ndani yenu, wala ninyi hamna haja ya mtu ye yote kuwafundisha. Lakini kama vile upako wake unavyowafundisha kuhusu mambo yote nayo ni kweli wala si uongo, basi kama ulivyowafundisha kaeni ndani yake.

Ye yote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu. Kwa jinsi hii tunaweza kujua dhahiri watoto wa Mungu na pia watoto wa ibilisi. Ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake. Hili ndilo neno mlilolisikia tangu mwanzo: Kwamba imetupasa tupendane sisi kwa sisi.

Sisi tunajua ya kwamba tumepita kutoka mautini kuingia uzimani, kwa sababu tunawapenda ndugu. Kila asiyempenda ndugu yake akaa mautini.

Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? Watoto wangu wadogo, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na katika kweli.

Wapenzi, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho mwone kama zimetoka kwa Mungu, kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea ulimwenguni.

Mtu ye yote asiyedumu katika mafundisho ya Kristo, bali akayaacha, yeye hana Mungu. Ye yote anayedumu katika mafundisho ana Baba na Mwana pia. Msimpokee mtu ye yote anayewajia ambaye hawaletei mafundisho haya, wala msimkaribishe nyumbani mwenu. Ye yote amkaribishaye mtu wa namna hiyo anashiriki katika matendo maovu ya mtu huyo.

Nililiandikia kanisa, lakini Deotrefe, yeye apendaye kujifanya wa kwanza, hakubali mamlaka yetu. Hivyo kama nikija, nitakumbuka matendo yake atendayo, akitusingizia kwa maneno ya hila. Wala hatosheki na hayo anayotusingizia, bali pia hukataa kuwakaribisha ndugu na hata huwazuia wale walio tayari kufanya hivyo na kuwafukuza watoke kanisani. Mpenzi, usiige lile lililo baya bali lile lililo jema. Ye yote atendaye mema atoka kwa Mungu, atendaye mabaya hakumwona Mungu.

Yohana, kwa makanisa saba yaliyoko Asia: Neema na amani iwe kwenu kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja na kutoka kwa wale Roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi

Kuhusu siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba, navyo vile vinara saba ni hayo makanisa saba.

“Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika: “Haya ndiyo maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea katikati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu. Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo. Nami najua umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka. “Lakini nina neno juu yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza. Kumbuka basi ni wapi ulikoanguka! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake. Lakini una jambo hili kwa upande wako: Unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo nami nayachukia. “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye atakayeshinda, nitampa haki ya kula matunda ya mti wa uzima, ambao uko katika paradiso ya Mungu.

“Kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika: “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa kisha akafufuka. Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, wao ni sinagogi la Shetani. Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia Shetani atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu, hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima. “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatadhuriwa na mauti ya pili.

“Kwa malaika wa Kanisa lililoko Pergamo andika: “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye na upanga wenye makali kuwili. Ninajua unakoishi, ni kule ambako Shetani ana kiti chake cha enzi. Lakini umelishika Jina langu. Wala hukuikana imani yako kwangu hata katika siku za shahidi wangu mwaminifu Antipa, ambaye aliuawa katika mji wenu, ambako ndiko anakokaa Shetani. “Hata hivyo, nina mambo machache dhidi yako: Unao watu wafuatao mafundisho ya Balaamu, yule aliyemfundisha Balaki kuwashawishi Waisraeli watende dhambi kwa kula vitu vilivyotolewa kafara kwa sanamu na kufanya uasherati. Vivyo hivyo unao wale wayashikao mafundisho ya Wanikolai. Basi tubuni! Ama sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga wa kinywa changu. “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa yeye jiwe jeupe ambalo juu yake limeandikwa jina jipya asilolijua mtu, isipokuwa yule anayelipokea.

“Kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika: “Haya ndiyo maneno ya Mwana wa Mungu, ambaye macho yake ni kama mwali wa moto na ambaye miguu yake ni kama shaba iliyosuguliwa sana. Nayajua matendo yako, upendo wako, imani yako, huduma na saburi yako na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza. “Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu. Nimempa muda ili atubie uasherati wake, lakini hataki. Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, nami nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake. Nami nitawaua watoto wake. Nayo makanisa yote yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia za watu na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. Basi nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, ninyi ambao hamyafuati mafundisho ya Yezebeli, wala hamkujifunza hayo wengine wanayoyaita mambo ya ndani sana ya Shetani (sitaweka mzigo mwingine wo wote juu yenu): Lakini shikeni sana mlicho nacho, mpaka nitakapokuja. “Atakayeshinda na kutenda mapenzi yangu mpaka mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa: “ ‘Atawatawala kwa fimbo ya chuma, atawavunja vipande vipande kama chombo cha udongo’: kama vile mimi nilivyopokea mamlaka kutoka kwa Baba yangu. Nami nitampa pia ile nyota ya asubuhi. Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.

“Kwa malaika wa Kanisa lililoko Sardi andika: “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye na zile Roho saba za Mungu na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, kwamba una sifa ya kuwa hai, lakini umekufa. Amka! Nawe uyaimarishe yale yaliyo karibu kufa, kwa maana sikuona kwamba kazi zako zimekamilika machoni pa Mungu wangu. Kumbuka basi yale uliyoyapokea na kuyasikia, yatii na ukatubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwivi wala hutajua saa nitakayokuja kwako. “Lakini bado una watu wachache katika Sardi ambao hawajayachafua mavazi yao. Wao wataenda pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wanastahili. Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao, nami sitafuta jina lake kutoka katika kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake. Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.

“Kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika: “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, yeye aliye na ufunguo wa Daudi. Anachokifungua hakuna awezaye kukifunga, wala anachokifunga hakuna awezaye kukifungua. Nayajua matendo yako. Tazama, nimeweka mbele yako mlango uliofunguliwa, wala hakuna awezaye kuufunga. Ninajua kwamba una nguvu kidogo lakini umelishika neno langu wala hukulikana Jina langu. Nitawafanya wale wa sinagogi la Shetani, wale ambao husema kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali ni waongo, waje wapige magoti miguuni pako, nao watatambua ya kwamba nimekupenda. Kwa kuwa umelishika neno la saburi yangu nitakulinda hata utoke katika saa ya kujaribiwa inayokuja ulimwenguni pote ili kuwajaribu wote wakaao duniani. “Ninakuja upesi. Shika sana ulicho nacho, ili mtu asije akaichukua taji yako. Yeye ashindaye nitamfanya kuwa nguzo katika Hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo kamwe. Nitaandika juu yake Jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu, yaani, Yerusalemu mpya, ambao unashuka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Nami pia nitaandika juu yake Jina langu jipya. Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.

“Kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika: “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye Amen, shahidi mwaminifu na wa kweli, mtawala wa uumbaji wote wa Mungu. Nayajua matendo yako, ya kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungelikuwa baridi au moto. Hivyo kwa kuwa u uvuguvugu, kwamba wewe si baridi wala si moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu. Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu cho chote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi. Kwa hiyo nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto ili upate kuwa tajiri na mavazi meupe ili uyavae, upate kuficha aibu ya uchi wako na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona. “Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu. Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu ye yote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami. “Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi. Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.”

Kwa hiyo, “Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu na kumtumikia usiku na mchana katika Hekalu lake; naye aketiye katika kile kiti cha enzi atakaa pamoja nao na kuwalinda.

Ndipo nikapewa mwanzi wa kupimia ulio kama fimbo, nikaambiwa, “Nenda ukapime Hekalu la Mungu pamoja na madhabahu, nawe uwahesabu wale waabuduo humo.

Ndipo Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa na Sanduku la Agano lake likaonekana humo ndani. Kukatokea mianga ya umeme wa radi, ngurumo, sauti za radi, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.

Hapa ndipo penye subira na uvumilivu wa watakatifu, yaani, wale wanaozishika amri za Mungu na kudumu kuwa waaminifu kwa Yesu.

Nalo lile Hekalu lilijawa na moshi uliotokana na utukufu wa Mungu na uweza wake, wala hakuna ye yote aliyeweza kuingia mle Hekaluni mpaka yale mapigo saba ya wale malaika saba yalipomalizika.

Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema: “Tokeni katikati yake, enyi watu wangu, ili msije mkashiriki dhambi zake, ili msije mkapatwa na pigo lake lo lote;

Furahia kwa ajili yake, Ee mbingu! Furahini watakatifu, mitume na manabii! Kwa kuwa Mungu amemhukumu kwa vile alivyowatendea ninyi.’ ”

Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema: “Msifuni Mungu wetu, ninyi watumishi wake wote, ninyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa!” Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipiga kelele wakisema: “Haleluya! Kwa maana BWANA Mungu wetu Mwenyezi anatawala. Tufurahi, tushangilie na kumpa utukufu! Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia na bibi arusi wake amejiweka tayari. Akapewa kitani safi, nyeupe inayong'aa, ili avae.” (Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.) Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.”

Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe. Nami nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Atafuta kila chozi, kutoka katika macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”

Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba ya hayo mapigo saba ya mwisho akaja akaniambia, “Njoo, nami nitakuonyesha bibi arusi, yaani, mke wa Mwana-Kondoo.” Naye akanichukua katika Roho hadi kwenye mlima mkubwa na mrefu, akanionyesha ule Mji Mtakatifu, Yerusalemu, likishuka kutoka mbinguni kwa Mungu. Ulikuwa uking'aa kwa utukufu wa Mungu kama kito chenye thamani sana, kama yaspi, safi kama kioo. Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mawili, pakiwa na malaika kumi na wawili kwenye hayo malango. Kwenye malango hayo yaliandikwa majina ya yale makabila kumi na mawili ya Israeli. Kulikuwa na malango matatu upande wa mashariki, matatu upande wa kaskazini, matatu upande wa kusini na matatu upande wa magharibi. Ukuta wa huo mji ulikuwa na misingi kumi na miwili na juu yake yaliandikwa majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.

Sikuona Hekalu ndani ya huo mji kwa sababu BWANA Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo ndio Hekalu lake.

“Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kushuhudia mambo haya kwa ajili ya makanisa. Mimi ndimi Shina na Mzao wa Daudi, ile Nyota ya Asubuhi ing'aayo.”

Swahili - Kiswahili - SW

NEN'2014 - Neno Bibilia Takatifu Kiswahili Contemporary Version - 2014

This Bible text is from Biblica Open Kiswahili Contemporary Version Neno 2015
https://open.bible/bibles/swahili-biblica-text-bible/
provided by: Biblica Inc, available by Creative Commons CC-BY-SA-4.0,
and this new compilation is shared as www.creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0.
Languages are made available to you by www.ipedge.net