15 – Ulevi

Haya ni maneno matakatifu ya Mungu Mwenyezi.
Hatupendi maneno ya wanadamu.
Kwa mtu yeyote anayempenda Mungu... hivi ndivyo Mungu anasema kuhusu: Ulevi.

Mistari 3 Muhimu Zaidi

Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

Amkeni, enyi walevi, mlie! Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo, pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya, kwa kuwa mmenyang'anywa kutoka midomoni mwenu.

Lakini sasa nawaandikia kwamba msishirikiane na mtu ye yote anayejiita ndugu, hali akiwa ni mzinzi, au mwenye tamaa mbaya, mwabudu sanamu au msingiziaji, mlevi au mdhalimu. Mtu kama huyo hata msile naye.

Kila Mstari katika Mpangilio wa Biblia - 79 vifungu

Noa akawa mkulima, akawa mtu wa kwanza kupanda mizabibu. Alipokunywa huo mvinyo wake akalewa na akalala uchi kwenye hema lake. Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake na kuwaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.

“Wewe na wanao msinywe mvinyo wala kinywaji kingine kilichochachuka wakati mwingiapo katika Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa. Hili litakuwa Agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Ni lazima mtenganishe kilicho kitakatifu na kile kilicho cha kawaida, kati ya yaliyo najisi na yaliyo safi,

ni lazima ajitenge na mvinyo na kinywaji kingine cho chote chenye chachu, na kamwe asinywe siki itokanayo na mvinyo au itokanayo na kinywaji kingine chenye chachu. Kamwe asinywe maji ya zabibu wala kula zabibu mbichi au kavu.

Watawaambia wazee, “Huyu mwanetu ni mkaidi na mwasi. Hatutii sisi, yeye ni mpotovu na mlevi.”

Mzabibu wao unatoka kwenye mzabibu wa Sodoma, na kutoka kwenye mashamba ya Gomora. Zabibu zake zimejaa sumu, na vishada vyake vimejaa uchungu. Mvinyo wao ni sumu ya nyoka, sumu yenye kufisha ya swila.

Lakini ujihadhari sana usinywe mvinyo wala kileo kingine cho chote, wala usile kitu cho chote kilicho najisi,

Umewaonyesha watu wako nyakati za kukata tamaa; umetunywesha mvinyo unaotufanya tupepesuke.

Mkononi mwa BWANA kuna kikombe kilichojaa mvinyo unaotoka povu uliochanganywa na vikolezo; huumimina, nao waovu wote wa dunia hunywa mpaka tone la mwisho.

Wanakula mkate wa uovu, na kunywa mvinyo wa jeuri.

Mvinyo ni mdhihaki na kileo ni mgomvi; ye yote apotoshwaye navyo hana hekima.

Mtu apendaye anasa atakuwa maskini, ye yote apendaye mvinyo na mafuta kamwe hatakuwa tajiri.

Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo, au wale walao nyama kwa pupa, kwa maana walevi na walafi huwa maskini, nako kusinzia huwavika matambara.

Ni nani mwenye ole? Ni nani mwenye huzuni? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye malalamiko? Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu? Ni nani mwenye macho mekundu? Ni hao wakaao sana kwenye mvinyo, hao waendao kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa. Usiukodolee macho mvinyo wakati ukiwa mwekundu, wakati unapometameta kwenye bilauri, wakati ushukapo taratibu! Mwisho huuma kama nyoka na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu. Macho yako yataona mambo mageni na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka. Utakuwa kama alalaye katikati ya bahari, alalaye juu ya kamba ya merikebu. Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia! Wamenichapa, lakini sisikii! Nitaamka lini ili nikanywe tena?”

“Ee Lemueli, haifai wafalme, haifai wafalme kunywa mvinyo, haifai watawala kutamani sana kileo, wasije wakanywa na kusahau ile sheria inayoamuru na kuwanyima haki zao wote walioonewa. Wape kileo wale wanaoangamia, mvinyo wale walio na uchungu, Wanywe na kusahau umaskini wao na wasikumbuke taabu yao tena.

Heri wewe, Ee nchi ambayo mfalme wako ni wa uzao wenye kuheshimika na ambayo wakuu wako hula chakula kwa wakati unaofaa: ili kupata nguvu na si kwa ajili ya ulevi.

Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema wakikimbilia kunywa vileo, wale wakawiao sana mpaka usiku, mpaka wamewaka kwa mvinyo. Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao, matari, filimbi na mvinyo, lakini hawayajali matendo ya BWANA, wala hawana heshima kwa ajili ya kazi ya mikono yake.

Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo nao walio hodari katika kuchanganya vileo,

BWANA amewamwagia roho ya kizunguzungu; wanaifanya Misri iyumbeyumbe katika yale yote inayoyafanya, kama vile mlevi ayumbayumbavyo katika kutapika kwake.

Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo, kileo ni kichungu kwa wanywaji wake. Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa, mlango wa kila nyumba umefungwa. Barabarani wanalilia kupata mvinyo, furaha yote imegeuka kuwa majonzi, furaha yote imefukuziwa mbali na dunia. Mji umeachwa katika uharibifu, lango lake limepigwapigwa na kuvunjwa vipande vipande.

Dunia inapepesuka kama mlevi, inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo; imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake na ikianguka kamwe haitainuka tena.

Ole wa lile taji la maua, kiburi cha walevi wa Efraimu, kwa ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake, uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba, kwa ule mji, kiburi cha wale walioshushwa na mvinyo!

Lile taji la maua, kiburi cha walevi cha Efraimu, kitakanyagwa chini ya nyayo.

Hawa pia wanapepesuka kwa sababu ya mvinyo, wanayumbayumba kwa sababu ya kileo: Makuhani na manabii wanapepesuka kwa sababu ya kileo, wanachanganyikiwa kwa sababu ya mvinyo; wanapepesuka wanapoona maono, wanajikwaa wanapotoa maamuzi. Meza zote zimejawa na matapishi wala hakuna sehemu hata ndogo isiyokuwa na uchafu.

Duwaa na kushangaa, jifanyeni vipofu wenyewe na msione, leweni, lakini si kwa mvinyo, pepesukeni lakini si kwa kileo.

Kila mmoja hulia, “Njoni, tupate mvinyo! Tunywe kileo sana! Kesho itakuwa kama leo, au hata bora zaidi.”

“Waambie: ‘Hili ndilo BWANA, Mungu wa Israeli asemalo: kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo.’ Kama wao wakikuambia, ‘Kwani hatujui kwamba kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo?’ Kisha uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: nitawajaza ulevi wote waishio katika nchi hii, pamoja na wafalme waketio juu ya kiti cha enzi cha Daudi, makuhani, manabii na wale wote waishio Yerusalemu. Nitawagonganisha kila mmoja na mwenzake, baba na wana wao, asema BWANA. Sitawarehemu wala kuwahurumia ili niache kuwaangamiza.’ ”

Kuhusu manabii: Moyo wangu umevunjika ndani yangu; mifupa yangu yote inatetemeka. Nimekuwa kama mtu aliyelewa, kama mtu aliyelemewa na divai, kwa sababu ya BWANA na maneno yake matakatifu.

Hili ndilo BWANA, Mungu wa Israeli, aliloniambia: “Chukua kutoka mkononi mwangu kikombe hiki kilichojaa mvinyo ya ghadhabu yangu na kuyanywesha mataifa yote ambayo ninakutuma kwao. Watakapoinywa watapepesuka na kukasirika sana kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka katikati yao.”

“Kisha uwaambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli asemalo: Kunyweni, mlewe na mtapike, angukeni wala msiinuke tena kwa sababu ya upanga nitakaotuma miongoni mwenu.’

Kisha nikaweka mabakuli yaliyojaa divai na baadhi ya vikombe mbele ya watu wa jamaa ya Warekabi na kuwaambia, “Kunyweni divai.” Lakini wao wakajibu, “Sisi hatunywi divai, kwa sababu baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu, alitupa agizo hili: ‘Ninyi wala wazao wenu kamwe msinywe divai.

Amenijaza kwa majani machungu na kunishibisha kwa nyongo.

Umeiendea njia ya dada yako, hivyo nitakitia kikombe chake mkononi mwako. “Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “Utakinywea kikombe cha dada yako, kikombe kikubwa na chenye kina kirefu; nitaletea juu yako dharau na dhihaka, kwa kuwa kimejaa sana. Utalewa ulevi na kujawa huzuni, kikombe cha maangamizo na ukiwa, kikombe cha dada yako Samaria. Utakinywa chote na kukimaliza; utakivunja vipande vipande na kuyararua matiti yako. Nimenena haya, asema BWANA Mwenyezi. “Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa tangu uliponisahau mimi na kunitupa nyuma yako, lazima ubebe matokeo ya uasherati wako na ukahaba wako.”

Kuhani ye yote asinywe mvinyo aingiapo katika ukumbi wa ndani.

Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha kifalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa kwa ajili ya kutokujinajisi kwa njia hii.

Hivyo mlinzi wao akaondoa chakula chao na divai yao waliopangiwa kula na kunywa akawapa nafaka na mboga za majani badala yake.

Badala yake, umejiinua dhidi ya Bwana wa mbingu. Uliletewa vikombe vya Hekalu lake, nawe na wakuu wako, wake zako na masuria wako mlivitumia kwa kunywea mvinyo. Ukaisifu miungu ya fedha, ya dhahabu, ya shaba, ya chuma, ya miti na ya mawe, miungu ambayo haiwezi kuona au kusikia wala kufahamu. Lakini hukumheshimu Mungu ambaye anaushikilia uhai wako na njia zako zote mkononi mwake.

katika ukahaba, divai ya zamani na divai mpya, ambavyo huondoa ufahamu

Katika sikukuu ya mfalme wetu wakuu wanawaka kwa mvinyo, naye anawaunga mkono wenye mizaha.

Amkeni, enyi walevi, mlie! Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo, pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya, kwa kuwa mmenyang'anywa kutoka midomoni mwenu.

Watu hulala kando ya kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani. Katika nyumba ya mungu wao hunywa mvinyo ulionunuliwa kwa fedha walizotozwa watu.

“Lakini mliwafanya Wanadhiri kunywa mvinyo na kuwaamuru manabii wasitoe unabii.

Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa na mnajipaka mafuta mazuri, lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yosefu.

Ikiwa mwongo na mdanganyifu atakuja na kusema, ‘Nitawatabiria divai na pombe kwa wingi,’ angekuwa ndiye nabii anayekubalika na watu hawa!

Watasongwa katikati ya miiba na kulewa kwa mvinyo wao. Watateketezwa kama mabua makavu.

“Ole wake yeye ampaye jirani yake kileo, akiimimina kutoka kwenye kiriba cha mvinyo mpaka wamelewa, ili apate kutazama miili yao iliyo uchi. Utajazwa na aibu badala ya utukufu. Sasa ni zamu yako! Kunywa na ujifunue! Kikombe kutoka kwenye mkono wa kuume wa BWANA kinakujia, na aibu itafunika utukufu wako.

Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuja hali wala hanywi, nao wanasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’ Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nao wanasema, ‘Tazama, mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ Lakini hekima huthibitishwa kwa haki ya matendo yake.”

Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’ kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake na kula na kunywa pamoja na walevi, bwana wa mtumishi huyo atakuja siku ambayo mtumishi huyo hamtazamii na saa ile ambayo haijui. Atamkata huyo mtumishi vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.

Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji cho chote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake.

Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuwa hali mkate wala hanywi divai, ninyi mkasema, ‘Ana pepo mchafu,’ Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nanyi mnasema: ‘Mtazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’

Lakini ikiwa yule mtumishi atawaza moyoni mwake, ‘Bwana wangu anakawia kurudi,’ akaanza kuwapiga wale watumishi wa kiume na wa kike na kula na kunywa na kulewa, bwana wake yule mtumwa atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. Huyo bwana wake atamkata vipande vipande na kumwekea fungu lake pamoja na wale wasio waaminifu.

“Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama vile mtego unasavyo.

Yule mkuu wa meza akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilika kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji wao walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando akamwambia, “Watu wote hutoa kwanza divai nzuri, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa vya kutosha, lakini wewe umeiweka ile nzuri kupita zote mpaka sasa.”

Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa mvinyo!” Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na moja, akainua sauti yake na kuhutubia ule umati wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, jueni jambo hili mkanisikilize. Hakika watu hawa hawakulewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi! Hawa hawakulewa, ila jambo hili ni lile lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:

Basi na tuenende kwa adabu kama inavyopasa wakati wa mchana, si kwa kufanya karamu za ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali jivikeni Bwana Yesu Kristo, wala msifikiri jinsi mtakavyotimiza tamaa za miili yenu yenye asili ya dhambi.

Ni afadhali kutokula nyama wala kunywa divai au kufanya jambo lingine lo lote litakalomsababisha ndugu yako ajikwae.

Je, hamjui ya kwamba ninyi ni Hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu ye yote akiliharibu Hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza mtu huyo, Kwa maana Hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.

Lakini sasa nawaandikia kwamba msishirikiane na mtu ye yote anayejiita ndugu, hali akiwa ni mzinzi, au mwenye tamaa mbaya, mwabudu sanamu au msingiziaji, mlevi au mdhalimu. Mtu kama huyo hata msile naye.

Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati hawaurithi Ufalme wa Mungu, wala waombao sanamu, wala wahanithi, wala walawiti, wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walafi, wala wanaodhihaki, wala wanyang'anyi. Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.

Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni Hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu na katika roho zenu ambazo ni mali ya Mungu.

Hakuna jaribu lo lote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu ambaye hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

Kama kwa tumaini la kibinadamu tu nilipigana na wanyama wakali huko Efeso, ningekuwa nimepata faida gani kwa jambo hilo? Kama wafu hawafufuliwi, “Sisi na tule na kunywa, kwa kuwa kesho tutakufa.” Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.” Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.

Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho. Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu,

Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi. Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku. Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo. Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha.

Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali.

Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.

Kwa habari yako wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako. Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia.

Kwa kuwa mwangalizi, kama wakili wa Mungu, imempasa kuwa mtu asiye na lawama, asiwe mwenye majivuno au mwepesi wa hasira, wala mlevi, wala asiwe mtu mwenye tamaa ya mapato yasiyo ya halali. Bali awe mkarimu, anayependa mema, mwenye kiasi, mwenye haki, mwadilifu, mnyofu, mtakatifu na mwenye kuitawala nafsi yake.

Wafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi. Vivyo hivyo wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa unyenyekevu unaostahili utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema,

Vivyo hivyo, sisitiza vijana wawe na kiasi.

Nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya kumcha Mungu, katika ulimwengu huu wa sasa, huku

Kwa hiyo, vifungeni viuno vya nia zenu, mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa, Yesu Kristo atakapodhihirishwa. Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya za kwanza za wakati wa ujinga. Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote, kwa maana imeandikwa: “Mtakuwa watakatifu, kwa kuwa Mimi ni mtakatifu.”

Maana wakati uliopita mmekwisha kutumia muda wa kutosha katika maisha yenu mkifanya yale ambayo watu wasiomjua Mungu hupenda kutenda, wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya na ibada za sanamu ambazo ni chukizo.

Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi, kama simba angurumaye huzungukazunguka akitafuta mtu ili apate kummeza. Mpingeni huyo mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso yayo hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha toka kwenye udhalimu wote.

Malaika wa pili akafuata akisema, “Ameanguka! Ameanguka Babeli aliye mkuu, yeye aliyeyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.”

Yule ambaye wafalme wa dunia walizini naye na watu wakaao duniani walilewa kwa mvinyo wa uzinzi wake.”

Kwa maana mataifa yote yamekunywa mvinyo wa uasherati wake. Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye, nao wafanya biashara wa dunia wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.”

Swahili - Kiswahili - SW

NEN'2014 - Neno Bibilia Takatifu Kiswahili Contemporary Version - 2014

This Bible text is from Biblica Open Kiswahili Contemporary Version Neno 2015
https://open.bible/bibles/swahili-biblica-text-bible/
provided by: Biblica Inc, available by Creative Commons CC-BY-SA-4.0,
and this new compilation is shared as www.creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0.
Languages are made available to you by www.ipedge.net