05 – Mbingu

Haya ni maneno matakatifu ya Mungu Mwenyezi.
Hatupendi maneno ya wanadamu.
Kwa mtu yeyote anayempenda Mungu... hivi ndivyo Mungu anasema kuhusu: Mbingu.

Mistari 3 Muhimu Zaidi

Lakini ni kama ilivyoandikwa: “Lile jambo ambalo jicho halijapata kuona, sikio halijapata kusikia, wala halikuingia moyoni, lile ambalo Mungu aliwaandalia wale wampendao”:

Katika mji huo hakutakuwa tena na kitu cho chote kilicholaaniwa, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia, nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye vipaji vya nyuso zao. Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana BWANA Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.

Watu wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwenye aibu na kudharauliwa milele. Wale wenye hekima watang'aa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watang'aa kama nyota milele na milele.

Kila Mstari katika Mpangilio wa Biblia - 183 vifungu

Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.

BWANA Mungu akafanya aina zote za miti ziote kutoka ardhini, miti yenye kupendeza macho na mizuri kwa chakula. Katikati ya bustani ulikuwepo mti wa uzima na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.

Akaota ndoto ambayo aliona ngazi imesimamishwa juu ya ardhi, ncha yake ikiwa imefika mbinguni na malaika wa Mungu wakawa wakipanda na kushuka juu yake.

Kwa hiyo akaogopa, akasema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ndipo nyumba ya Mungu ilipo, hili ni lango la mbinguni.”

Mbingu, hata mbingu za juu sana, dunia na kila kitu kilichomo ndani yake, ni mali ya BWANA Mungu wako.

Angalia chini kutoka mbinguni, maskani yako matakatifu, uwabariki watu wako Israeli pamoja na nchi uliyotupa kama ulivyoahidi kwa kiapo kwa baba zetu, nchi inayotiririka maziwa na asali.”

“Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga!

Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia kutoka mbinguni, mahali pa makao yako na usikiapo, samehe.

Ukuu na uweza, ni vyako, Ee BWANA, na utukufu na enzi na uzuri, kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani ni chako wewe. Ee BWANA, ufalme ni wako, umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.

Wewe peke yako ndiwe BWANA. Uliumba mbingu, hata mbingu za mbingu, nalo jeshi lote la angani, dunia na vyote vilivyo ndani yake, bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.

BWANA yuko ndani ya Hekalu lake takatifu; BWANA yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni. Huwaangalia wana wa watu, macho yake yanawajaribu.

Umenijulisha njia ya uzima; utanijaza na shangwe katika uwepo wako, pamoja na furaha za milele katika mkono wako wa kuume.

Sasa nafahamu kuwa BWANA humwokoa mpakwa mafuta wake, humjibu kutoka mbingu yake takatifu kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume.

Alikuomba maisha, nawe ukampa, wingi wa siku milele na milele.

ili kwamba aishi milele na asione uharibifu.

Magari ya Mungu ni makumi ya maelfu, na maelfu ya maelfu; Bwana amekuja kutoka Sinai kuja katika patakatifu pake.

Nitaudumisha uzao wake milele, kiti chake cha enzi kama mbingu zinavyodumu.

Kama vile mbingu zilivyo juu sana juu ya dunia, ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;

BWANA ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni, ufalme wake unatawala juu ya vyote.

Ni kama vile umande wa Hermoni unavyoanguka juu ya Mlima Sayuni. Kwa maana huko ndiko BWANA alikoamuru baraka yake, naam, hata uzima milele.

Katika njia ya haki kuna uzima; katika mapito hayo kuna maisha ya milele.

Amefanya kila kitu kiwe kizuri kwa wakati wake. Pia ameiweka hiyo milele katika mioyo ya wanadamu, wala hawawezi kutambua kwa kina yale ambayo Mungu amefanya tangu mwanzo hadi mwisho.

Katika mwaka ule Mfalme Uzia alipokufa, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu. Juu yake walikuwepo maserafi, kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao na kwa mawili walikuwa wakiruka. Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ni BWANA Mwenye Nguvu Zote; dunia yote imejaa utukufu wake.”

Kuongezeka kwa utawala wake na amani hakutakuwa na mwisho. Atatawala katika kiti cha enzi cha Daudi na juu ya ufalme wake, akiuthibitisha na kuutegemeza kwa haki na kwa adili, tangu wakati huo na hata milele. Wivu wa BWANA Mwenye Nguvu Zote utatimiza haya.

Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo, chui atalala pamoja na mbuzi, ndama, mwana simba na ng'ombe aliyenona wa mwaka mmoja watalisha pamoja, naye mtoto mdogo atawaongoza.

yeye atameza mauti milele katika ushindi. BWANA Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote, ataondoa aibu ya watu wake duniani kote. BWANA amesema hili.

Kwa maana hili ndilo asemalo Aliye juu, yeye aliyeinuliwa sana, yeye aishiye milele, ambaye jina lake ni Mtakatifu: “Ninaishi mimi mahali palipoinuka tena palipo patakatifu, tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na mwenye roho ya unyenyekevu, ili kuzihuisha roho za wanyenyekevu na kuihuisha mioyo yao waliotubu.

Jua halitakuwa tena nuru yako mchana, wala mwangaza wa mwezi hautakuangazia, kwa maana BWANA atakuwa nuru yako ya milele, naye Mungu wako atakuwa utukufu wako. Jua lako halitazama tena, nao mwezi wako hautafifia tena; BWANA atakuwa nuru yako milele, nazo siku zako za huzuni zitakoma. Ndipo watu wako wote watakuwa waadilifu nao wataimiliki nchi milele. Wao ni chipukizi nililolipanda, kazi ya mikono yangu, kwa ajili ya kuonyesha utukufu wangu.

“Tazama, nitaumba mbingu mpya na dunia mpya. Mambo ya zamani hayatakumbukwa, wala hayatakuja akilini.

Hili ndilo asemalo BWANA, “Mbingu ni kiti changu cha enzi, nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu. Iko wapi nyumba mtakayojenga kwa ajili yangu? Mahali pangu pa kupumzika patakuwa wapi?

“Kama vile mbingu mpya na nchi mpya ninazozifanya zitakavyodumu mbele zangu,” asema BWANA, “ndivyo jina lenu na wazao wenu watakavyodumu.

Hili ndilo asemalo BWANA: “Ikiwa mbingu zilizo juu zitaweza kupimika na misingi ya dunia chini ikaweza kuchunguzwa, ndipo nitakapowakataa wazao wote wa Israeli kwa sababu ya yote waliyoyatenda,” asema BWANA.

Juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha enzi kuonekana kwake chenye rangi ya yakuti samawi, na juu ya kile kiti cha enzi kulikuwa na umbo mfano wa mwanadamu. Nikaona kwamba kutokana na kile nilichoona kama kiuno chake kuelekea juu alionekana kama chuma inayowaka kana kwamba imejaa moto na kuanzia kiuno kwenda chini alionekana kama moto na mwanga mkali ulimzunguka. Kama vile kuonekana kwa upinde wa mvua mawinguni siku ya mvua, ndivyo ulivyokuwa ule mng'ao uliomzunguka. Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa utukufu wa BWANA. Nilipouona, nikaanguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea.

Miti ya matunda ya kila aina itaota kwenye kingo zote mbili za mto huu. Majani yake hayatanyauka wala haitaacha kuwa na matunda katika matawi yake. Kila mwezi kutakuwa na matunda, kwa sababu maji yatokayo patakatifu yanaitiririkia. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatakuwa dawa.”

“Katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni atauweka ufalme ambao kamwe hautaangamizwa, wala hautaachiwa taifa jingine. Utaziponda zile falme zote na kuzikomesha, bali wenyewe utadumu milele.

“Katika maono yangu ya usiku nilitazama, mbele yangu nikamwona anayefanana na mwanadamu, akija pamoja na mawingu ya mbinguni. Akamkaribia huyo Mzee wa Siku na akaongozwa mbele zake. Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme wenye nguvu, watu, kabila zote za mataifa na watu wa kila lugha wakamwabudu. Utawala wake ni utawala wa milele ambao hautapita, nao ufalme wake ni ule ambao kamwe hautaangamizwa.

Lakini watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana watapokea ufalme na kuumiliki milele, naam, milele na milele.’

Ndipo ufalme, mamlaka na ukuu wa falme chini ya mbingu yote utakabidhiwa kwa watakatifu, watu wa Yeye Aliye Juu Sana. Ufalme wake utakuwa ufalme wa milele, nao watawala wote watamwabudu na kumtii yeye.’

Watu wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwenye aibu na kudharauliwa milele. Wale wenye hekima watang'aa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watang'aa kama nyota milele na milele.

“Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni u karibu.”

Chombo chake cha kupuria kiko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, akiikusanya ngano yake ghalani na kuyachoma makapi kwa moto usiozimika.”

Tangu wakati huo, Yesu alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.”

“Heri walio maskini wa roho, maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao.

Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki, maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao. “Heri ninyi watu watakapowashutumu na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kuu.

Kwa hiyo, ye yote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini ye yote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni. Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya walimu wa sheria na Mafarisayo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

“Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba: “ ‘Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe. Ufalme wako uje. Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni.

Usitutie majaribuni, bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu [kwa kuwa Ufalme ni wako na nguvu na utukufu, hata milele. Amen].’

“Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

“Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo. Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.

“Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

Wakati mnapokwenda, hubirini mkisema, ‘Ufalme wa Mbinguni umekaribia.’

Amin, nawaambia, miongoni mwa watu waliozaliwa na wanawake, hajatokea mtu aliye mkuu zaidi ya Yohana Mbatizaji, lakini aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, ni mkuu kuliko Yohana.

Wanafunzi wake wakamwendea wakamwuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?” Akawajibu, “Ninyi mmepewa kuzifahamu siri za Ufalme wa Mbinguni, lakini wao sivyo.

Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa Mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua akaipanda shambani mwake. Ingawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hata ndege wa angani huja na kutengeneza viota katika matawi yake.”

Ndipo wenye haki watang'aa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.

“Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.”

“Tena, Ufalme wa Mbinguni unafanana na mfanya biashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.”

“Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. Ulipojaa, wavuvi wakavuta pwani, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki.

Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa sheria aliyefundishwa elimu ya Ufalme wa Mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka katika ghala yake mali mpya na mali ya zamani.”

wakamsihi awaruhusu wagonjwa waguse tu pindo la vazi lake, nao wote waliomgusa, wakaponywa.

Nitakupa funguo za Ufalme wa Mbinguni na lo lote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, lo lote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa Mbinguni.”

Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

“Angalia ili usimdharau mmojawapo wa hawa wadogo, kwa maana nawaambia, malaika wao mbinguni daima wanauona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [

“Amin, nawaambia, lo lote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni na lo lote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.

Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mbinguni ni wa wale walio kama hawa.”

Mtu mmoja akamjia Yesu na kumwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?” Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mimi mwema? Hakuna aliye mwema ila Mmoja tu, ndiye Mungu: Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.” Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?” Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako na umpende jirani yako kama nafsi yako.” Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?” Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, amin nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, wakati wa kufanywa upya vitu vyote, wakati Mwana wa Adamu atakapoketi kwenye kiti chake cha utukufu cha enzi, ninyi mliomfuata pia mtaketi katika viti vya enzi kumi na viwili, mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. Kila mmoja aliyeacha nyumba au ndugu zake wa kiume au wa kike au baba au mama au watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo na ataurithi uzima wa milele.

“Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja.

Wakati wa ufufuo watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa Mungu mbinguni. Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia kwamba, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo?’ Yeye si Mungu wa wafu bali ni Mungu wa walio hai.”

“Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu.

Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

“Wakati huo, Ufalme wa Mbinguni utakuwa kama wanawali kumi waliochukua taa zao na kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara. Wale wapumbavu walichukua taa zao lakini hawakuchukua mafuta ya akiba, lakini wale wenye busara walichukua taa zao na mafuta ya akiba kwenye vyombo.

“Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache, nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’

“Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njoni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu, urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

“Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.

Yesu alipoona yaliyokuwa yakitukia akachukizwa, akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa watu kama hawa. Amin, amin nawaambia, mtu ye yote asiyeukubali Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”

Yesu alipokuwa anaondoka, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Yesu akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema isipokuwa Mungu peke yake. Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’ ” Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.” Yesu akamtazama na kumpenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja, nenda ukauze kila kitu ulicho nacho uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” Yule mtu aliposikia hayo, akasikitika sana, akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

Wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa, watakuwa kama malaika wa mbinguni. Basi kuhusu ufufuo wa wafu: Je, hamjasoma katika kitabu cha Mose jinsi Mungu alivyosema na Mose kutoka katika kile kichaka akisema, ‘Mimi, ni Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Isaki na Mungu wa Yakobo?’

Akawatazama wanafunzi wake, akasema: “Mmebarikiwa ninyi mlio maskini, kwa sababu Ufalme wa Mbinguni ni wenu. Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashibishwa. Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa, kwa sababu mtacheka. Mmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia, watakapowatenga na kuwatukana na kulikataa jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. “Furahini na kurukaruka kwa shangwe kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii.

Naye akasema, “Ninyi mmejaliwa kufahamu siri za Ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili, “ ‘ingawa wanaona, wasione; ingawa wanasikia, wasielewe.’

Basi msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Wakati huo mtaalamu mmoja wa sheria alisimama ili kumjaribu Yesu, akamwuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili nipate kurithi uzima wa milele?” Yesu akamjibu, “Imeandikwaje katika Torati? Kwani unasoma nini humo?” Akajibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote, tena mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ ” Yesu akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”

Bali utafuteni Ufalme wa Mungu na vitu hivyo vyote atawapatia pia. “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwivi hakaribii wala nondo haharibu. Kwa maana hazina yako ilipo, ndipo na moyo wako utakapokuwa pia.

Nawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.”

“Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. Zaidi ya hayo kati yetu na ninyi huko, kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu ye yote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’

Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama hawa watoto. Amin, nawaambia, ye yote ambaye hataupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”

Mtawala mmoja akamwuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna mtu ye yote aliye mwema ila Mungu peke yake. Unazifahamu amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’ ” Akajibu, “Amri zote hizi nimezishika tangu ujana wangu.” Yesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi. Yesu akamtazama akasema, “Tazama ni jinsi gani ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu! Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.” Wale waliosikia haya wakauliza, “Kama ni vigumu hivyo, ni nani basi awezaye kuokoka?” Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu kwa Mungu yawezekana.”

Yesu akajibu, “Amin nawaambia, hakuna hata mmoja aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”

Kisha akasema, “Bwana Yesu, unikumbuke utakapokuja katika Ufalme wako.” Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”

Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”

Yesu akamjibu, “Amin, amin nakuambia, mtu hawezi kuuona Ufalme wa Mungu asipozaliwa mara ya pili.” Nikodemo akauliza, “Awezaje mtu kuzaliwa wakati akiwa mzee? Hakika hawezi kuingia mara ya pili kwenye tumbo la mama yake ili azaliwe!” Yesu akamwambia, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu ye yote anayeweza kuingia katika Ufalme wa Mungu isipokuwa amezaliwa kwa maji na kwa Roho. Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho.

Nimewaambia mambo ya duniani, nanyi hamkuniamini, mtaniaminije basi nitakapowaambia mambo ya mbinguni? Hakuna mtu ye yote aliyekwenda mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. Kama vile Mose alivyomwinua yule nyoka kule jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu. Ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Ye yote anayemwamini Mwana ana uzima wa milele, lakini yeye asiyemwamini Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yake.”

Lakini ye yote anywaye maji nitakayompa, hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji yakibubujika uzima wa milele.”

“Amin, amin ninawaambia, ye yote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma, anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini, na kuingia uzimani.

“Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka nje, wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima na wale waliotenda maovu, watafufuka wahukumiwe.

Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele, maandiko haya ndiyo yanayonishuhudia Mimi.

Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba amemtia muhuri.”

Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.”

Amin, amin nawambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele.

Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu ye yote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”

Mtu ye yote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho.

Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tuondoke twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.

nami ninawapa uzima wa milele, hawataangamia kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka katika mikono yangu.

Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi na ye yote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?” Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana, ninaamini ya kuwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yeye ajaye ulimwenguni.”

Mtu ye yote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata uzima wa milele.

Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Nakwenda kuwaandalia makao. Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo.

Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema: “Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe. Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa. Nao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mungu wa pekee, wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma.

Yesu akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini kama ilivyo ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.”

“ ‘Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu. Mtanijengea nyumba ya namna gani? asema Bwana. Au mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?

Watu Mataifa waliposikia haya wakafurahi na kulitukuza neno la Bwana; nao wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.

wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kupitia katika taabu nyingi.”

Akahubiri Ufalme wa Mungu na kufundisha mambo yale yaliyomhusu Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri wote na bila kizuizi cho chote.

Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele.

Ili kwamba kama vile dhambi ilivyotawala kwa njia ya mauti, vivyo hivyo neema iweze kutawala kwa njia ya kuhesabiwa haki hata uzima wa milele katika Yesu Kristo Bwana wetu.

Lakini sasa kwa kuwa mmewekwa huru mbali na dhambi na mmekuwa watumwa wa Mungu, faida mnayopata ni utakatifu, ambao mwisho wake ni uzima wa milele. Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokoka.”

Lakini ni kama ilivyoandikwa: “Lile jambo ambalo jicho halijapata kuona, sikio halijapata kusikia, wala halikuingia moyoni, lile ambalo Mungu aliwaandalia wale wampendao”:

Hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati wa ufufuo wa wafu. Ule mwili wa kuharibika uliopandwa, utafufuliwa usioharibika, unapandwa katika aibu, unafufuliwa katika utukufu, unapandwa katika udhaifu, unafufuliwa katika nguvu, unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa mwili wa kiroho. Kama kuna mwili wa asili, basi kuna mwili wa kiroho pia. Kwa hiyo imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika kiumbe hai”; Adamu wa mwisho, yeye ni roho iletayo uzima. Lakini si ule wa kiroho uliotangulia, bali ni ule wa asili, kisha ule wa kiroho. Mtu wa kwanza aliumbwa kwa mavumbi ya ardhini, mtu wa pili alitoka mbinguni. Kama vile alivyokuwa yule wa ardhini, ndivyo walivyo wale walio wa ardhini; na kwa vile alivyo mtu yule aliyetoka mbinguni, ndivyo walivyo wale walio wa mbinguni. Kama vile tulivyochukua mfano wa yule mtu wa ardhini, ndivyo tutakavyochukua mfano wa yule mtu aliyetoka mbinguni.

Ndugu zangu nisemalo ni hili: nyama na damu haviwezi kuurithi Ufalme wa Mungu, wala kuharibika kurithi kutokuharibika. Sikilizeni, nawaambia siri: Sote hatutalala, lakini sote tutabadilishwa ghafula, kufumba na kufumbua, parapanda ya mwisho itakapolia. Kwa kuwa parapanda italia, nao wafu watafufuliwa na miili isiyoharibika, nasi tutabadilishwa. Kwa maana mwili huu wa kuharibika lazima uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa lazima uvae kutokufa. Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.” “Kuko wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? Uko wapi, Ewe mauti, uchungu wako?” Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria.

Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi kupita kiasi, kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.

Kwa maana twajua kwamba kama hema yetu ya dunia tunayoishi ikiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu. Kwa maana katika hema hii twalia kwa uchungu, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni,

Naam, tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana.

Namjua mtu mmoja katika Kristo ambaye miaka kumi na minne iliyopita alichukuliwa juu hadi mbingu ya tatu. Kama ni katika mwili au nje ya mwili, sijui, Mungu ajua. Nami najua ya kwamba mtu huyu, kwamba ni katika mwili au nje ya mwili mimi sijui, lakini Mungu ajua, alinyakuliwa hadi Paradiso. Huko alisikia mambo yasiyoelezeka, mambo ambayo binadamu hana ruhusa ya kuyasimulia.

Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. Apandaye kwa mwili, katika mwili wake, atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo.

Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena wala wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu.

Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo na kufa ni faida. Kama nitaendelea kuishi katika mwili, kwangu hili ni kwa ajili ya matunda ya kazi. Lakini sijui nichague lipi? Mimi sijui! Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi.

Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani, Bwana Yesu Kristo, atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.

Kwa maana ametuokoa kutoka katika ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa,

Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani.

Tuliwatia moyo, tuliwafariji na kuwahimiza kuishi maisha yampendezayo Mungu, anayewaita katika Ufalme na utukufu wake.

na kuwapa ninyi mnaoteseka raha pamoja na sisi, wakati Bwana Yesu atakapodhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu.

Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili kwamba katika mimi niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini wapate uzima wa milele. Basi, Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.

Kwa maana mazoezi ya mwili yana faida kwa sehemu, lakini utauwa una faida katika mambo yote, yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa na ya ule ujao.

Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu cho chote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu.

Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi.

Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili.

Bwana ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe yeye milele na milele. Amen.

imani na ujuzi ulioko katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu, asiyesema uongo, aliahidi hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu,

ili kwamba, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele.

Lakini kwa habari za Mwana asema, “Kiti chako cha enzi, Ee Mungu, kitadumu milele na milele, nayo haki itakuwa fimbo ya utawala ya ufalme wako.

Kwa hiyo basi, imebaki raha ya Sabato kwa ajili ya watu wa Mungu,

akiisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii,

Kwa hiyo, ilikuwa muhimu kwa nakala za vitu vile vya mbinguni vitakaswe kwa dhabihu hizi, lakini vitu halisi vya mbinguni vilihitaji dhabihu bora kuliko hizi. Kwa maana Kristo hakuingia kwenye patakatifu palipofanywa kwa mikono ya mwanadamu, ambao ni mfano wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni penyewe, ili sasa aonekane mbele za Mungu kwa ajili yetu.

Lakini badala yake wanatamani nchi iliyo bora zaidi, yaani, nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao.

Lakini ninyi mmekuja Mlima Sayuni, Yerusalemu ya mbinguni, mji wa Mungu aliye hai. Mmekuja penye kusanyiko kubwa la malaika maelfu kwa maelfu wasiohesabika wanaoshangilia, kwenye kanisa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mmekuja kwa Mungu, mhukumu wa watu wote, kwenye roho za wenye haki waliokamilishwa,

Kwa kuwa hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule ujao.

ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu,

ambaye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu: pamoja na malaika, mamlaka na nguvu zote vikiwa vimetiishwa chini yake.

Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu, kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe. Kwa njia hii, mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia kwa furaha mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.

Tunawajulisha lile lililokuwako tangu mwanzo, lile tulilosikia, ambalo tumeliona kwa macho yetu, ambalo tumelitazama na kuligusa kwa mikono yetu, kuhusu Neno la uzima. Uzima huo ulidhihirishwa; nasi tumeuona na kuushuhudia, nasi twawatangazia uzima wa milele, ambao ulikuwa pamoja na Baba, nao ukadhihirishwa kwetu.

Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.

Hii ndiyo ahadi yake kwetu, yaani, uzima wa milele.

Wapenzi, sasa tu watoto wa Mungu, lakini bado haijadhihirika tutakavyokuwa, lakini twajua ya kwamba yeye atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo.

Huu ndio ushuhuda: kwamba Mungu ametupa uzima wa milele, nao huo uzima umo katika Mwanawe. Aliye naye Mwana wa Mungu anao uzima, yeye asiye na Mwana wa Mungu hana uzima. Nawaandikia mambo haya ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu ili mpate kujua ya kuwa mnao uzima wa milele.

Nasi pia twajua ya kwamba Mwana wa Mungu amekuja, naye ametupa sisi ufahamu ili tupate kumjua yeye aliye Kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye Kweli, yaani, ndani ya Yesu Kristo Mwanawe. Yeye ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele.

Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele.

“Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye atakayeshinda, nitampa haki ya kula matunda ya mti wa uzima, ambao uko katika paradiso ya Mungu.

Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao, nami sitafuta jina lake kutoka katika kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake.

“Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi.

Baada ya mambo hayo nilitazama, nami nikaona mbele yangu mlango ulio wazi mbinguni. Nayo ile sauti niliyokuwa nimeisikia hapo kwanza ikisema nami kama tarumbeta ikasema, “Njoo panda huku nami nitakuonyesha yale ambayo hayana budi kutokea baada ya haya.” Ghafula nilikuwa katika Roho, hapo mbele yangu kilikuwapo kiti cha enzi mbinguni, kikiwa kimekaliwa na mtu mmoja. Yeye aliyekuwa amekikalia alikuwa anaonekana kama yaspi na akiki. Kukizunguka kile kiti cha enzi palikuwa na upinde wa mvua ulioonekana kama zumaridi. Pia kukizunguka hicho kiti cha enzi palikuwa na viti ishirini na vinne na juu ya hivyo viti walikuwa wameketi wazee ishirini na wanne, waliovaa majoho meupe, wakiwa na taji za dhahabu vichwani mwao.

Kwenye kile kiti cha enzi palikuwa panatoka miali ya umeme wa radi, ngurumo na sauti za radi. Mbele ya hicho kiti cha enzi, palikuwa na taa saba zilizokuwa zinawaka. Hizi ndizo Roho saba za Mungu. Pia mbele ya hicho kiti cha enzi palikuwa na kile kilichoonekana kama bahari ya kioo, iliyokuwa angavu kama jiwe lisilo na rangi yo yote ling'aalo sana. Katikati, kukizunguka kile kiti cha enzi, kulikuwa na viumbe wanne wenye uhai, wakiwa wamejawa na macho mbele na nyuma. Huyo kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, wa pili alikuwa kama ng'ombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu na wa nne alikuwa kama tai anayeruka. Kila mmoja wa hawa viumbe wenye uhai wanne, alikuwa na mabawa sita na kujawa na macho pande zote, hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawakuacha kusema: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA Mungu Mwenyezi, aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.”

Kila mara viumbe hao wenye uhai wanne walipomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele, wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Wao huziweka taji zao mbele ya hicho kiti cha enzi, wakisema: “Bwana wetu na Mungu wetu, wewe umestahili kupokea utukufu na heshima na uweza, kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa mapenzi yako viliumbwa na vimekuwako.”

Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani wa kumtumikia Mungu wetu, nao watatawala duniani.” Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne, idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu.

Baada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna ye yote awezaye kuuhesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. Nao walikuwa wakipiga kelele kwa sauti kubwa wakisema: “Wokovu una Mungu wetu, yeye aketiye kwenye kiti cha enzi na Mwana-Kondoo!” Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee ishirini na wanne na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu, wakisema: “Amen! Sifa na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu viwe kwa Mungu wetu milele na milele. Amen!”

Kwa hiyo, “Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu na kumtumikia usiku na mchana katika Hekalu lake; naye aketiye katika kile kiti cha enzi atakaa pamoja nao na kuwalinda. Kamwe hawataona njaa wala kiu tena. Jua halitawapiga wala joto lo lote liunguzalo. Kwa maana Mwana-Kondoo aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi atakuwa Mchungaji wao; naye atawaongoza kwenda kwenye chemchemi za maji yaliyo hai. Naye Mungu atafuta kila chozi kutoka katika macho yao.”

Ndipo Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa na Sanduku la Agano lake likaonekana humo ndani. Kukatokea mianga ya umeme wa radi, ngurumo, sauti za radi, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.

Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao. Lakini joka na malaika zake wakashindwa na hapakuwa tena na nafasi kwa ajili yao mbinguni.

Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.”

Kisha nikaona kiti kikubwa cheupe cha enzi pamoja na yeye aliyeketi juu yake. Dunia na mbingu zikaukimbia uso wake wala mahali pao hapakuonekana.

Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwepo na bahari tena. Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe. Nami nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Atafuta kila chozi, kutoka katika macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”

Naye yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nayafanya mambo yote kuwa mapya!” Kisha akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika tena ni kweli.” Akaniambia, “Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Yeye aonaye kiu nitampa kunywa kutoka katika chemchemi ya maji ya uzima bila gharama yo yote. Yeye atakayeshinda atayarithi haya yote, Nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.” Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba ya hayo mapigo saba ya mwisho akaja akaniambia, “Njoo, nami nitakuonyesha bibi arusi, yaani, mke wa Mwana-Kondoo.”

Naye akanichukua katika Roho hadi kwenye mlima mkubwa na mrefu, akanionyesha ule Mji Mtakatifu, Yerusalemu, likishuka kutoka mbinguni kwa Mungu. Ulikuwa uking'aa kwa utukufu wa Mungu kama kito chenye thamani sana, kama yaspi, safi kama kioo. Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mawili, pakiwa na malaika kumi na wawili kwenye hayo malango. Kwenye malango hayo yaliandikwa majina ya yale makabila kumi na mawili ya Israeli. Kulikuwa na malango matatu upande wa mashariki, matatu upande wa kaskazini, matatu upande wa kusini na matatu upande wa magharibi. Ukuta wa huo mji ulikuwa na misingi kumi na miwili na juu yake yaliandikwa majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.

Huyo malaika aliyesema nami alikuwa na ufito wa dhahabu wa kupimia huo mji, malango yake na kuta zake. Mji huo ulikuwa mraba, urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Akaupima huo mji kwa huo ufito akakuta una kama kilomita 2,400; urefu wake na upana wake na kwenda juu kwake vilikuwa sawa. Akaupima ukuta wake, ulikuwa na unene wa dhiraa 144 kwa kipimo cha kibinadamu ambacho huyo malaika alikuwa akikitumia. Ukuta huo ulijengwa kwa yaspi hali mji wenyewe ulijengwa kwa dhahabu safi, iking'aa kama kioo. Misingi ya kuta za mji huo zilipambwa kwa kila aina ya kito cha thamani. Msingi wa kwanza ulikuwa wa yaspi, wa pili yakuti samawi, wa tatu kalkedoni, wa nne zumaridi, wa tano sardoniki, wa sita akiki, wa saba krisolitho, wa nane zabarajadi, wa tisa yakuti manjano, wa kumi krisopraso, wa kumi na moja hiakintho, wa kumi na mbili amethisto. Yale malango kumi na mbili yalikuwa ni lulu kumi na mbili, kila lango lilikuwa limetengenezwa kwa lulu moja. Barabara za mji huo zilikuwa za dhahabu safi ing'aayo kama kioo.

Sikuona Hekalu ndani ya huo mji kwa sababu BWANA Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo ndio Hekalu lake. Ule mji hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, kwa sababu utukufu wa Mungu ndio nuru yake na Mwana-Kondoo ndiye taa yake. Mataifa yatatembea yakiangaziwa na nuru yake na wafalme wa duniani wataleta fahari yao ndani yake. Malango yake hayatafungwa kamwe, kwa maana hakutakuwa na usiku humo. Utukufu na heshima za mataifa zitaletwa humo. Lakini kitu kichafu hakitaingia humo kamwe, wala mtu ye yote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali watakaoingia humo ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.

Kisha yule malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, maangavu kama kioo yakitiririka kutoka kwenye kile kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo, kupitia katikati ya barabara kuu ya huo mji. Kwenye kila upande wa huo mto kulikuwa na mti wa uzima utoao matunda ya aina kumi na mbili, ukizaa matunda yake kila mwezi. Nayo majani ya mti huo ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa. Katika mji huo hakutakuwa tena na kitu cho chote kilicholaaniwa, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia, nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye vipaji vya nyuso zao. Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana BWANA Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.

“Wamebarikiwa wale wafuao mavazi yao, ili wapate haki ya kuuendea huo mti wa uzima na kuuingia huo mji kupitia kwenye malango yake.

Roho na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Naye asikiaye na aseme, “Njoo!” Ye yote mwenye kiu na aje na kila anayetaka na anywe maji ya uzima bure.

Swahili - Kiswahili - SW

NEN'2014 - Neno Bibilia Takatifu Kiswahili Contemporary Version - 2014

This Bible text is from Biblica Open Kiswahili Contemporary Version Neno 2015
https://open.bible/bibles/swahili-biblica-text-bible/
provided by: Biblica Inc, available by Creative Commons CC-BY-SA-4.0,
and this new compilation is shared as www.creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0.
Languages are made available to you by www.ipedge.net