16 – Chakula kilichotolewa dhabihu kwa sanamu

Haya ni maneno matakatifu ya Mungu Mwenyezi.
Hatupendi maneno ya wanadamu.
Kwa mtu yeyote anayempenda Mungu... hivi ndivyo Mungu anasema kuhusu: Chakula kilichotolewa dhabihu kwa sanamu.

Mistari 3 Muhimu Zaidi

La hasha! Lakini kafara za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani. Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani. Je, tunataka kuamsha wivu wa Bwana? Je, sisi tuna nguvu kuliko yeye?

Kwa maana kama mtu ye yote mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi huu mkila katika hekalu la sanamu, je, si atatiwa moyo kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu? Kwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, ataangamia kwa sababu ya ujuzi wenu. Mnapotenda dhambi dhidi ya ndugu zenu kwa njia hii na kujeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamkosea Kristo. Kwa hiyo, kama kile ninachokula kitamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi, sitakula nyama kamwe muda nchi idumupo, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke.

“Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu.

Kila Mstari katika Mpangilio wa Biblia - 67 vifungu

Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni ile iliyoko katikati yenu, jitakaseni na mkabadilishe nguo zenu.

Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga katika umbo la kitu cho chote kilicho juu mbinguni, au duniani chini, au ndani ya maji. Usivisujudie au kuviabudu; kwa kuwa Mimi, BWANA Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi ya baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,

“Uzingatie kutenda kila kitu nilichokuambia. Usiombe kwa majina ya miungu mingine, wala usiyaruhusu kusikika kinywani mwako.

Bomoa madhabahu zao, vunja mawe yao ya kuabudia na ukatekate nguzo zao za Ashera. Usiabudu mungu mwingine, kwa kuwa BWANA, ambaye jina lake ni Wivu, ni Mungu mwenye wivu. “Uwe mwangalifu usifanye agano na wale watu wanaoishi katika nchi, kwa maana wakati wanapojifanyia ukahaba kwa miungu yao na kuwatolea kafara, watakualika wewe nawe utakula sadaka za matambiko yao. Unapowachagua baadhi ya binti zao kuwa wake wa wana wenu na binti hao wakajifanyia ukahaba kwa miungu yao, watawaongoza wana wenu kufanya vivyo hivyo.

“ ‘Msiabudu sanamu, wala msijitengenezee miungu ya shaba. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.

Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu cho chote kilicho juu mbinguni au duniani chini au ndani ya maji. Usivisujudie wala kuviabudu; kwa maana Mimi, BWANA Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne cha wale wanichukiao,

pia BWANA Mungu wako atakapowatia mkononi mwako na ukawashinda, basi ni lazima uwaangamize wote kabisa. Usifanye agano nao, usiwahurumie. Usioane nao. Usimtoe binti yako kuolewa na mwanawe, au kumchukua binti yake aolewe na mwanao. Kwa maana watamgeuza mwanao aache kunifuata, ili aitumikia miungu mingine, nayo hasira ya BWANA itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza ghafula. Hili ndilo utakalowafanyia: Vunja madhabahu zao, yabomoe mawe yao yaliyowekwa wakfu, katakata nguzo zao za Ashera na kuchoma sanamu zao kwa moto.

Vinyago vya miungu yao mtavichoma moto. Msitamani fedha wala dhahabu iliyo juu yao, wala msizichukue kwa ajili yenu, la sivyo mtakuwa mmetekwa navyo. Kwa kuwa ni chukizo kwa BWANA Mungu wenu. Msilete vitu vya machukizo katika nyumba zenu kwani ninyi, mtatengwa kama vitu hivyo kwa maangamizo. Ukichukie kabisa kitu hicho kwa kuwa kimetengwa kwa maangamizo.

Ikiwa mtamsahau BWANA Mungu wenu, mkaifuata miungu mingine, mkaiabudu na kuisujudia, ninashuhudia dhidi yenu leo kwamba hakika mtaangamizwa. Kama mataifa BWANA aliyoyaangamiza mbele yenu, ndivyo ninyi mtakavyoangamizwa kwa kutokumtii BWANA Mungu wenu.

Angalieni kwamba mnafanya yote niliyowaamuru; msiongeze kitu wala msipunguze kitu.

Wakamfanya Mungu kuwa na wivu kwa miungu yao migeni, na kumkasirisha kwa sanamu zao za machukizo. Wakatoa dhabihu kwa pepo, ambao si Mungu: miungu wasiyoijua, miungu iliyojitokeza siku za karibuni, miungu ambayo baba zenu hawakuiogopa.

Lakini Samweli akajibu: “Je, BWANA anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu kama vile kuitii sauti ya BWANA? Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu, nako kusikia ni bora kuliko mafuta ya kondoo dume. Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi, nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu. Kwa sababu umelikataa neno la BWANA, naye amekukataa wewe kuendelea kuwa mfalme.”

Wakaileta ile nguzo ya kuabudiwa nje ya hekalu la Baali na wakaichoma moto. Wakabomoa ile nguzo ya kuabudiwa ya Baali pamoja na hekalu la Baali, nao watu wakapafanya kuwa choo hadi leo.

Kwa kuwa BWANA ni mkuu, mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote, yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote. Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini BWANA aliziumba mbingu.

Akatoa kafara kwa miungu ya Dameski, ambao walikuwa wamemshinda, kwa kuwa aliwaza, “Kwa kuwa miungu ya mfalme wa Aramu imewasaidia wao, nitaitolea dhabihu ili inisaidie na mimi.” Lakini haya ndiyo yaliyokuwa maangamizi yake na Israeli wote.

Kwa kuwa BWANA ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote. Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini BWANA aliziumba mbingu.

Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu, zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. Zina vinywa, lakini haziwezi kusema, zina macho, lakini haziwezi kuona; zina masikio, lakini haziwezi kusikia, zina pua, lakini haziwezi kunusa; zina mikono, lakini haziwezi kupapasa, zina miguu, lakini haziwezi kutembea; wala koo zao haziwezi kutoa sauti. Wale wanaozitengeneza watafanana nazo, vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.

Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu, zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. Zina vinywa, lakini haziwezi kusema, zina macho, lakini haziwezi kuona, zina masikio, lakini haziwezi kusikia, wala hakuna pumzi katika vinywa vyao. Wale wanaozitengeneza watafanana nazo, vivyo hivyo wote wanaozitumainia.

Kwa kuwa katika siku ile kila mmoja wenu atazikataa sanamu za fedha na za dhahabu zilizotengenezwa kwa mikono yenu yenye dhambi.

Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiteketeza, kwani haikuwa miungu bali ni miti na mawe tu, iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.

“Mimi ndimi BWANA; hilo ndilo Jina langu! Sitampa mwingine utukufu wangu wala sanamu sifa zangu.

Lakini wale wanaotumaini sanamu, wanaoviambia vinyago, ‘Ninyi ndio miungu yetu,’ watarudishwa nyuma kwa aibu kubwa.

Nitatoa hukumu zangu kwa watu wangu kwa sababu ya uovu wao wa kuniacha mimi, kwa kufukiza uvumba kwa miungu mingine na kuabudu kile ambacho mikono yao imekitengeneza.

Watoto wanakusanya kuni, baba zao wanawasha moto na wanawake wanakanda unga na kuoka mikate kwa ajili ya Malkia wa Mbinguni. Wanamimina sadaka za vinywaji kwa miungu mingine ili kunikasirisha. Lakini je, mimi ndiye wanayenikasirisha? asema BWANA. Je, hawajiumizi wenyewe kwa aibu yao? “ ‘Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenyezi: Hasira yangu na ghadhabu yangu itamwagwa mahali hapa, juu ya mwanadamu na mnyama, juu ya miti ya shambani na juu ya matunda ya ardhini, nayo itaungua pasipo kuzimwa.

Kila mmoja ni mjinga na hana maarifa, kila sonara ameaibishwa na sanamu zake. Vinyago vyake ni madanganyo, wala havina pumzi ndani yake. Havina maana, ni vitu vya mzaha tu, hukumu yao itakapokuja, wataangamia.

nawe useme, ‘Sikieni neno la BWANA, enyi wafalme wa Yuda na watu wa Yerusalemu. Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli asemalo: Sikilizeni! Nitaleta maafa mahali hapa ambayo yatafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yawashe. Kwa kuwa wameniacha na kupafanya mahali hapa kuwa pa miungu ya kigeni, wameiteketezea sadaka miungu ambayo wao wala baba zao wala wafalme wa Yuda kamwe hawakuijua, nao wamelijaza eneo hili kwa damu isiyo na hatia.

Nyumba zilizoko Yerusalemu na zile za wafalme wa Yuda zitatiwa unajisi kama mahali hapa, yaani, Tofethi. Nyumba zote ambazo walifukiza uvumba juu ya mapaa yake kwa jeshi lote la angani na kumimina dhabihu ya kinywaji kwa miungu mingine.’ ”

Kisha wanaume wote ambao walijua kwamba wake zao walikuwa wakifukiza uvumba kwa miungu mingine, pamoja na wanawake wote waliokuweko, yaani, kusanyiko kubwa na watu wote wanaoishi katika nchi ya Misri, katika Pathrosi, wakamwambia Yeremia, “Hatutausikiliza ujumbe uliotuambia katika jina la BWANA! Hakika tutafanya kila kitu tulichosema tutakifanya: Tutafukiza uvumba kwa Malkia wa Mbinguni na tutammiminia sadaka zetu za kinywaji kama vile sisi na baba zetu, wafalme wetu na maafisa wetu walivyofanya katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu. Wakati ule tulikuwa na chakula tele, tulikuwa matajiri wala hatukupata dhara lo lote. Lakini tangu tulipoacha kumfukizia uvumba Malkia wa Mbinguni na kummiminia sadaka za kinywaji, hatukupata cho chote na tumekuwa tukiangamizwa kwa upanga na njaa.” Wanawake wakaongeza kusema, “Wakati tulipomfukizia uvumba Malkia wa Mbingu na kummiminia sadaka zetu za kinywaji, je, waume zetu hawakujua kwamba tulikuwa tukitengeneza maandazi kwa mfano wake na kummiminia yeye sadaka za kinywaji?”

BWANA alipokuwa hawezi kuendelea kuvumilia matendo yenu maovu na mambo ya machukizo mliyoyafanya, nchi yenu ilikuwa kitu cha kulaania na kuachwa ukiwa pasipo wakazi, kama ilivyo leo. Kwa sababu mmefukiza uvumba na kufanya dhambi dhidi ya BWANA nanyi hamkumtii wala kufuata sheria yake au amri zake au maagizo yake, maafa haya yamekuja juu yenu, kama mnavyoona sasa.”

“Kila mtu hana ufahamu na hana maarifa; kila sonara ameaibika kwa sanamu zake. Vinyago vyake ni vya udanganyifu, havina pumzi ndani yake. Hazifai kitu, ni vitu vya kufanyia mzaha, hukumu yao itawadia, zitaangamia.

Badala yake, umejiinua dhidi ya Bwana wa mbingu. Uliletewa vikombe vya Hekalu lake, nawe na wakuu wako, wake zako na masuria wako mlivitumia kwa kunywea mvinyo. Ukaisifu miungu ya fedha, ya dhahabu, ya shaba, ya chuma, ya miti na ya mawe, miungu ambayo haiwezi kuona au kusikia wala kufahamu. Lakini hukumheshimu Mungu ambaye anaushikilia uhai wako na njia zako zote mkononi mwake.

Wanaweka Wafalme bila idhini yangu, wamechagua wakuu bila kibali changu. Kwa fedha zao na dhahabu wamejitengenezea sanamu kwa ajili ya maangamizi yao wenyewe.

Lakini kadiri nilivyomwita Israeli, ndivyo walivyokwenda mbali nami. Walitoa dhabihu kwa Mabaali na kufukiza uvumba kwa vinyago.

“Sanamu ina thamani gani, kwani mwanadamu ndiye aliyechonga? Ama kinyago kinachofundisha uongo? Kwa kuwa yeye aliyekitengeneza hutegemea kazi ya mikono yake mwenyewe; hutengeneza sanamu zisizoweza kuzungumza.

“Msidhani kwamba nimekuja kufuta Torati au Manabii, sikuja kuondoa bali kutimiza. Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yo yote kutoka kwenye Torati mpaka kila kitu kiwe kimetimia. Kwa hiyo, ye yote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini ye yote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni.

Akawajibu, “Hata nanyi hamwelewi? Hamtambui kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi? Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Yesu alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni “safi.”)

“Ye yote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa.

“Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Ama atamchukia mmoja na kumpenda mwingine au atamheshimu mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.”

Kuhani wa Zeu, ambaye hekalu lake lilikuwa nje kidogo tu ya mji, akaleta mafahali na mashada ya maua penye lango la mji kwa sababu yeye pamoja na ule umati wa watu walitaka kuwatolea dhabihu. Lakini mitume Paulo na Barnaba waliposikia na kuona mambo haya waliyotaka kufanya, wakararua nguo zao, wakawaendea wale watu kwa haraka, wakawapigia kelele, wakisema, “Enyi watu, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi ni wanadamu tu kama ninyi! Tunawaletea habari njema, tukiwaambia kwamba mgeuke mtoke katika mambo haya yasiyofaa mmwelekee Mungu aliye hai, aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na kila kitu kilicho ndani yake.

badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe tu na vitu vilivyotiwa unajisi na uasherati na wasile nyama za wanyama walionyongwa au kunywa damu.

Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wo wote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima: Kwamba mjiepushe na kitu cho chote kilichotolewa sadaka kwa sanamu, kunywa damu, nyama ya wanyama walionyongwa na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya mtakuwa mmefanya vyema. Kwaherini.

Wakati Paulo akiwasubiri huko Athene, alisumbuka sana moyoni mwake kuona kwamba mji umejaa sanamu.

“Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa Uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe iliyotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu. Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua, kwake huyo amewahakikishia watu wote kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”

Lakini kuhusu wale watu Mataifa walioamini tumewaandikia uamuzi wetu kwamba wajitenge na kitu cho chote kilichotolewa sadaka kwa sanamu na damu au kula nyama ya mnyama aliyeuawa kwa kunyongwa, tena wajitenge na uasherati.” Ndipo kesho yake Paulo akawachukua wale watu na akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya Hekalu ili akatoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.

Ingawa wakijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.

Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake. Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu.

Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni Hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu na katika roho zenu ambazo ni mali ya Mungu.

Sasa kuhusu chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sisi sote tuna ujuzi.” Lakini ujuzi hujivuna, bali upendo hujenga. Mtu ye yote anayedhani kwamba anajua kitu, hajui kama impasavyo kujua. Lakini mtu ampendaye Mungu, hujulikana naye.

Hivyo basi, kuhusu kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sanamu si kitu cho chote kabisa duniani na kwamba kuna Mungu mmoja tu.” Kwa maana hata kama wapo hao wanaoitwa “miungu” kama ni mbinguni au duniani (kama ilivyo kweli wapo “miungu” wengi na “mabwana” wengi). Lakini kwetu sisi yuko Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vyatoka kwake na kwa ajili yake sisi twaishi na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa yeye vitu vyote vimekuwepo na kwa yeye sisi tunaishi.

Lakini si wote wanaojua jambo hili. Baadhi ya watu bado wamezoea kufikiria kuwa sanamu ni halisi hivyo wanapokula chakula kama hicho wanadhani kimetolewa sadaka kwa sanamu na kwa kuwa dhamiri zao ni dhaifu, kinatiwa unajisi. Lakini chakula hakituleti karibu na Mungu wala hatupotezi cho chote tusipokula, wala hatuongezi cho chote kama tukila. Lakini angalieni jinsi mnavyotumia uhuru wenu usije ukawa kikwazo kwao walio dhaifu katika imani. Kwa maana kama mtu ye yote mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi huu mkila katika hekalu la sanamu, je, si atatiwa moyo kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu? Kwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, ataangamia kwa sababu ya ujuzi wenu. Mnapotenda dhambi dhidi ya ndugu zenu kwa njia hii na kujeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamkosea Kristo. Kwa hiyo, kama kile ninachokula kitamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi, sitakula nyama kamwe muda nchi idumupo, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke.

Kwa hiyo wapenzi wangu, zikimbieni ibada za sanamu. Nasema nanyi kama na watu wenye ufahamu, amueni wenyewe kuhusu haya niyasemayo.

Waangalieni watu wa Israeli: Je, wale wote walao dhabihu si ni wale watendao kazi madhabahuni? Je, nina maana kwamba kafara iliyotolewa kwa sanamu ni kitu chenye maana yo yote? Au kwamba sanamu ni kitu chenye maana yo yote? La hasha! Lakini kafara za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani. Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani. Je, tunataka kuamsha wivu wa Bwana? Je, sisi tuna nguvu kuliko yeye?

“Vitu vyote ni halali,” lakini si vitu vyote vilivyo na faida. “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote vinavyojenga. Mtu ye yote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine. Kuleni cho chote kinachouzwa sokoni, bila kuuliza swali lo lote kwa ajili ya dhamiri. Kwa maana, “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.” Kama ukikaribishwa chakula na mtu asiyeamini nawe ukikubali kwenda, kula kila kitu kitakachowekwa mbele yako bila kuuliza maswali kwa ajili ya dhamiri. Lakini kama mtu ye yote akikuambia, “Hiki kimetolewa kafara kwa sanamu,” basi usikile kwa ajili ya huyo aliyekuambia na kwa ajili ya dhamiri. Nina maana dhamiri ya huyo aliyekuambia, wala si kwa ajili ya dhamiri yako. Lakini kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine? Kama nikila kwa shukrani, kwa nini nashutumiwa kwa kile ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu?

Basi, lo lote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. Msiwe kikwazo kwa mtu ye yote, kwa Wayahudi au kwa Wayunani, au kwa Kanisa la Mungu, kama mimi ninavyojaribu kumpendeza kila mtu kwa kila namna. Kwa maana sitafuti mema kwa ajili yangu mwenyewe bali mema kwa ajili ya faida ya wengi, ili waweze kuokolewa.

Msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa, kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu? Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza? Kuna mapatano gani kati ya Kristo na Beliari? Yeye aaminiye ana sehemu gani na yeye asiyeamini? Kuna mapatano gani kati ya Hekalu la Mungu na sanamu? Kwa kuwa sisi tu Hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu alivyosema: “Nitakaa pamoja nao na kutembea katikati yao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.” “Kwa hiyo tokeni miongoni mwao, mkatengwe nao, asema Bwana. Msiguse kitu cho chote kilicho najisi, nami nitawakaribisha.”

Kwa hiyo mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au Siku ya Sabato. Hizi zilikuwa kivuli cha mambo ambayo yangekuja, lakini ile iliyo halisi imo ndani ya Kristo.

Kwa kuwa mlikufa pamoja na Kristo, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kama vile ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri: “Msishike! Msionje! Msiguse!”? Haya yote mwisho wake ni kuharibika yanapotumiwa, kwa sababu huo msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu. Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hayafai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.

Kwa maana watu wa maeneo hayo wenyewe wanaeleza jinsi mlivyotupokea na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli

Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani. Mafundisho kama hayo huja kwa kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto. Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli. Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu cho chote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani, kwa sababu kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.

Basi iweni watendaji wa Neno wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu. Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na mara husahau jinsi alivyo.

Kila mtu atendaye dhambi afanya uasi, kwa kuwa dhambi ni uasi.

Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu. Amen.

Mtu ye yote asiyedumu katika mafundisho ya Kristo, bali akayaacha, yeye hana Mungu. Ye yote anayedumu katika mafundisho ana Baba na Mwana pia. Msimpokee mtu ye yote anayewajia ambaye hawaletei mafundisho haya, wala msimkaribishe nyumbani mwenu. Ye yote amkaribishaye mtu wa namna hiyo anashiriki katika matendo maovu ya mtu huyo.

“Hata hivyo, nina mambo machache dhidi yako: Unao watu wafuatao mafundisho ya Balaamu, yule aliyemfundisha Balaki kuwashawishi Waisraeli watende dhambi kwa kula vitu vilivyotolewa kafara kwa sanamu na kufanya uasherati.

“Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu. Nimempa muda ili atubie uasherati wake, lakini hataki. Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, nami nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake. Nami nitawaua watoto wake. Nayo makanisa yote yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia za watu na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.

Wanadamu waliosalia, ambao hawakuuawa katika mapigo hayo, bado walikataa kutubia kazi za mikono yao na hawakuacha kuabudu mashetani na sanamu za dhahabu, za fedha, za shaba, za mawe na za miti, ambazo haziwezi kuona, kusikia wala kutembea.

Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

Swahili - Kiswahili - SW

NEN'2014 - Neno Bibilia Takatifu Kiswahili Contemporary Version - 2014

This Bible text is from Biblica Open Kiswahili Contemporary Version Neno 2015
https://open.bible/bibles/swahili-biblica-text-bible/
provided by: Biblica Inc, available by Creative Commons CC-BY-SA-4.0,
and this new compilation is shared as www.creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0.
Languages are made available to you by www.ipedge.net