28 – Malaika

Haya ni maneno matakatifu ya Mungu Mwenyezi.
Hatupendi maneno ya wanadamu.
Kwa mtu yeyote anayempenda Mungu... hivi ndivyo Mungu anasema kuhusu: Malaika.

Mistari 3 Muhimu Zaidi

Malaika wa BWANA hufanya kituo akiwazunguka wale wamchao, naye huwaokoa.

Je, ni kwa malaika yupi ambaye Mungu amepata kumwambia wakati wo wote, “Wewe keti mkono wangu wa kuume mpaka nitakapowaweka adui zako chini ya nyayo zako”? Je, malaika wote si roho watumikao waliotumwa kuwahudumia wale watakaorithi wokovu?

Vivyo hivyo, nawaambia, kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu juu ya mwenye dhambi mmoja atubuye.”

Kila Mstari katika Mpangilio wa Biblia - 183 vifungu

Baada ya kumfukuzia mbali Adamu, Mungu akaweka makerubi mashariki ya Bustani ya Edeni, pamoja na upanga wa moto ukimulika huku na huko kulinda njia ya kuuendea mti wa uzima.

Malaika akaendelea akasema, “Nitazidisha wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi mno wasiohesabika.” Pia malaika wa BWANA akamwambia: “Wewe sasa una mimba nawe utamzaa mwana. Utamwita jina lake Ishmaeli, kwa sababu BWANA amesikia juu ya huzuni yako. Atakuwa punda-mwitu katikati ya wanadamu, mkono wake utakuwa dhidi ya kila mtu na mkono wa kila mtu dhidi yake, naye ataishi kwa uhasama na ndugu zake wote.”

BWANA akamtokea Abrahamu karibu na mialoni ya Mamre wakati alipokuwa ameketi kwenye ingilio la hema lake wakati wa adhuhuri. Abrahamu akainua macho akaona watu watatu wamesimama karibu naye. Alipowaona, aliharakisha kutoka kwenye ingilio la hema lake kuwalaki na kuwasujudia hadi nchi.

Kisha wakawapiga kwa upofu wale watu waliokuwa mlangoni mwa ile nyumba, vijana kwa wazee, hivyo hawakuweza kuupata mlango. Wale watu wawili wakamwambia Loti, “Una mtu mwingine ye yote hapa, wakwe zako, wana au binti, ama ye yote mwingine aliye wako katika mji huu? Waondoe hapa, kwa sababu tunapaangamiza mahali hapa. Kilio kwa BWANA dhidi ya watu wa hapa, ni kikubwa kiasi kwamba ametutuma kupaangamiza.” Kwa hiyo Loti alitoka ili kuzungumza na wakwe zake, waliokuwa wamewaposa binti zake. Akawaambia, “Fanyeni haraka kuondoka mahali hapa, kwa kuwa BWANA yu karibu kuangamiza mji huu!” Lakini wakwe zake walifikiri kwamba alikuwa akitania. Kunako mapambazuko, malaika wakawahimiza Loti, wakamwambia, “Fanya haraka! Mchukue mke wako na binti zako wawili walioko hapa, la sivyo utaangamizwa wakati mji utakapoadhibiwa.”

Lakini malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Abrahamu! Abrahamu!” Akajibu, “Mimi hapa.” Akamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo lo lote. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.”

Basi malaika wa BWANA akamwita Abrahamu kutoka mbinguni mara ya pili, akasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, kwamba kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee, hakika, nitakubariki na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga ulioko pwani. Wazao wako watamiliki miji ya adui zao, na kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”

Akaota ndoto ambayo aliona ngazi imesimamishwa juu ya ardhi, ncha yake ikiwa imefika mbinguni na malaika wa Mungu wakawa wakipanda na kushuka juu yake.

Malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, ‘Yakobo.’ Nikamjibu, ‘Mimi hapa.’

Yakobo pia akaondoka akaenda zake, malaika wa Mungu wakakutana naye. Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali pale Mahanaimu.

Huko malaika wa BWANA akamtokea Mose katika mwali wa moto kutoka katika kichaka. Mose akaona hilo, ingawa kile kichaka kilikuwa kinawaka moto, kilikuwa hakiteketei. Ndipo Mose akawaza, “Nitageuka sasa nione kitu hiki cha ajabu, nami nione ni kwa nini kichaka hiki hakiteketei.”

Ndipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma, ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha.

“Tazama, ninamtuma malaika akutangulie mbele yako akulinde njiani na kukuleta mpaka mahali nilipoandaa.

Malaika wangu atatangulia mbele yako na kukuleta katika nchi ya Waamori, Wahiti, Waperizi, Wakanaani, Wahivi na Wayebusi, nami nitawafutilia mbali.

Tengeneza makerubi wawili kwa dhahabu iliyofuliwa kwenye miisho miwili ya hicho kifuniko. Tengeneza kerubi mmoja kwenye mwisho mmoja, na kerubi mwingine kwenye mwisho mwingine; yatengeneze makerubi yawe kitu kimoja na hicho kifuniko katika miisho hiyo miwili. Makerubi hao watakuwa wametandaza mabawa kuelekea juu, yakitia kivuli hicho kifuniko. Makerubi hao wataelekeana, wakitazama hicho kifuniko. Weka huo Ushuhuda nitakaokupa ndani ya hilo Sanduku la Agano, na uweke hicho kifuniko juu ya hilo Sanduku. Hapo juu ya hicho kifuniko, kati ya hao makerubi wawili walioko juu ya hilo Sanduku la Ushuhuda, hapo ndipo nitakapokutana nawe na kukupa maagizo yangu kwa ajili ya Waisraeli.

Sasa nenda, uongoze hao watu mpaka mahali nilipokuambia, naye malaika wangu atakutangulia. Pamoja na hayo, wakati utakapofika wa mimi kuwaadhibu, nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi yao.”

Nitamtuma malaika mbele yenu, naye atawafukuza Wakanaani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.

Mose alipoingia kwenye Hema la Kukutania kuzungumza na BWANA, alisikia sauti ikisema naye kutoka kati ya wale makerubi wawili waliokuwa juu ya kile kiti cha rehema, juu ya Sanduku la Ushuhuda. Mose akazungumza naye.

lakini tulipomlilia BWANA, alisikia kilio chetu na akamtuma malaika akatutoa Misri. “Sasa tupo hapa Kadeshi, mji ulio mpakani mwa nchi yako.

Lakini Mungu alikasirika sana alipokwenda, naye malaika wa BWANA akasimama barabarani kumpinga. Balaamu alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. Wakati punda alipomwona malaika wa BWANA akiwa amesimama barabarani akiwa na upanga uliofutwa mkononi mwake, punda akageukia upande kuelekea shambani. Balaamu akampiga ili amrudishe barabarani. Ndipo malaika wa BWANA akasimama katika njia nyembamba iliyo kati ya mashamba mawili ya mizabibu, yakiwa na kuta pande zote mbili. Punda alipomwona malaika wa BWANA, alijisukumiza karibu na ukuta, na kugandamiza mguu wa Balaamu ukutani. Ndipo Balaamu akampiga tena punda. Kisha malaika wa BWANA akaendelea mbele na kusimama mahali pembamba ambapo hapakuwepo nafasi ya kugeuka, upande wa kulia wala wa kushoto. Punda alipomwona malaika wa BWANA, alilala chini Balaamu angali amempanda, naye Balaamu akakasirika na kumpiga kwa fimbo yake. Kisha BWANA akakifunua kinywa cha punda, akamwambia Balaamu, “Nimekutendea nini kinachokufanya unipige mara hizi tatu?” Balaamu akamjibu punda, “Umenifanya mjinga! Kama ningelikuwa na upanga mkononi mwangu, ningelikuua sasa hivi.” Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si punda wako mwenyewe, ambaye umenipanda siku zote, hadi leo? Je, nimekuwa na tabia ya kufanya hivi kwako?” Akajibu, “Hapana.”

Kisha BWANA akafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika wa BWANA amesimama barabarani akiwa ameufuta upanga wake. Balaamu akainama, akaanguka kifudifudi. Malaika wa BWANA akamwuliza Balaamu, “Kwa nini umempiga punda wako mara tatu hizi? Nimekuja kukuzuia kwa sababu njia yako imepotoka mbele yangu. Punda aliniona na kunikwepa mara hizi tatu. Kama punda hangenikwepa, hakika ningekuwa nimeshakuua sasa, lakini ningemwacha punda hai.” Balaamu akamwambia malaika wa BWANA, “Nimetenda dhambi. Sikutambua kuwa umesimama barabarani kunizuia. Basi kama haikupendezi, nitarudi.” Malaika wa BWANA akamwambia Balaamu, “Uende na watu hao, lakini useme tu lile nikuambialo.” Kwa hiyo Balaamu akaenda na wale wakuu wa Balaki.

Basi wakati Yoshua alipokaribia Yeriko, akainua macho, akaona mtu aliyesimama mbele yake, akiwa na upanga mkononi uliofutwa kwenye ala. Yoshua akamwendea na kumwuliza, “Je, wewe uko upande wetu au upande wa adui zetu?” Akajibu, “La, siko upande wo wote, lakini mimi nimekujia nikiwa amiri jeshi wa jeshi la BWANA.” Yoshua akaanguka kifudifudi hadi nchi, akasujudu, akamwuliza, “Je, Bwana, una ujumbe gani kwa mtumishi wako?” Amiri jeshi wa jeshi la BWANA akajibu, “Vua viatu vyako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni patakatifu.” Naye Yoshua akafanya hivyo.

Malaika wa BWANA alipomaliza kusema mambo haya kwa Waisraeli wote, watu wakalia kwa sauti kuu.

Kutoka mbinguni nyota zilipigana, nyota kutoka katika njia zake zilipigana na Sisera.

Malaika wa BWANA alipomtokea Gideoni, akamwambia, “BWANA yu pamoja nawe, Ewe shujaa mwenye nguvu.”

Malaika wa BWANA akainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika wa BWANA akatoweka kutoka machoni pake. Gideoni alipotambua kuwa ni malaika wa BWANA, akapiga kelele kwa mshangao, akasema, “Ole wangu, BWANA Mwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika wa BWANA uso kwa uso!”

Ndipo huyo mwanamke akamwendea mumewe na kumweleza kuwa, “Mtu wa Mungu alinijia. Kule kuonekana kwake kulikuwa kama kwa malaika wa Mungu, wa kutisha sana. Sikumwuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake.

Akamjibu, “Kwa nini unauliza Jina langu? Ni Jina la ajabu.” Ndipo Manoa akamchukua mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, naye akamtolea BWANA dhabihu hapo juu ya mwamba. Naye yule malaika wa BWANA akafanya jambo la ajabu wakati Manoa na mkewe wakiwa wanaangalia: Mwali wa moto kutoka hapo madhabahuni ulipowaka kuelekea mbinguni, malaika wa BWANA akapaa ndani ya huo mwali. Manoa na mkewe, kwa kuona jambo hili, wakaanguka chini kifudifudi.

Basi BWANA akaruhusu tauni katika Israeli kuanzia asubuhi mpaka mwisho wa muda ulioamuriwa, wakafa watu 70,000 kuanzia Dani hadi Beer-Sheba. Malaika aliponyoosha mkono wake ili kuangamiza Yerusalemu, BWANA alihuzunika kwa sababu ya maafa akamwambia malaika aliyekuwa anawadhuru watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika alikuwa kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna, Myebusi. Ikawa Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa akiwaua watu, akamwambia BWANA, “Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kufanya kosa. Hawa ni kama kondoo tu. Wamefanya nini? Mkono wako uwe juu yangu na nyumba yangu.”

Kisha akajinyoosha chini ya mti, akalala usingizi. Mara malaika akamgusa na akamwambia, “Inuka na ule.” Akatazama pande zote, napo hapo karibu na kichwa chake palikuwepo mkate uliookwa kwenye makaa ya moto na gudulia la maji. Akala na kunywa, kisha akajinyoosha tena. Yule malaika wa BWANA akaja tena mara ya pili, akamgusa akamwambia, “Inuka na ule, kwa kuwa safari ni ndefu kwako.” Kwa hiyo akainuka, akala na kunywa. Akiwa ametiwa nguvu na kile chakula, akasafiri siku arobaini mchana na usiku mpaka akafika Horebu, mlima wa Mungu.

Mikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la BWANA: Nilimwona BWANA ameketi juu ya kiti chake cha enzi pamoja na jeshi lote la mbinguni wamesimama kumzunguka kulia kwake na kushoto kwake.

Malaika wa BWANA akamwambia Eliya, “Shuka pamoja naye, usimwogope.” Hivyo Eliya akainuka na kushuka pamoja naye kwa mfalme.

Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Eliya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli. Elisha aliona hili akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Elisha hakumwona tena. Kisha akazishika nguo zake mwenyewe na kuzichana.

Kisha Elisha akaomba, “Ee BWANA, mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo BWANA akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya moto yote yamemzunguka Elisha pote.

Naye Hezekia akamwomba BWANA akisema: “Ee BWANA, Mungu wa Israeli, uliyeketi kwenye kiti chako cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako, ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe ndiye uliyeumba mbingu na dunia.

Usiku ule, malaika wa BWANA akatokea na kuwaua watu 185,000 katika kambi ya Waashuru. Askari waliosalia walipoamka asubuhi yake, walikuta maiti kila mahali!

Basi BWANA akapeleka tauni juu ya Israeli, watu 70,000 wa Israeli wakafa. Mungu akapeleka malaika kuangamiza Yerusalemu. Lakini malaika alipokuwa akifanya hivyo, BWANA akaona na akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anaangamiza watu, “Yatosha! Sasa rudisha mkono wako.” Wakati huu huyu malaika wa BWANA alikuwa amesimama katika uwanja wa kupuria nafaka wa Arauna, Myebusi. Daudi akayainua macho yake akamwona huyo malaika wa BWANA akiwa amesimama katikati ya mbingu na dunia, naye ameunyosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuangamiza. Kisha Daudi na wazee, waliokuwa wamevaa nguo za gunia, wakaanguka kifudifudi.

Maskani ya BWANA ambayo Mose aliitengeneza kule jangwani, pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa wakati huo vilikuwa viko mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni. Lakini Daudi hakuthubutu kuisogelea ili kumwuliza Mungu, kwa sababu aliuogopa upanga wa yule malaika wa BWANA.

Katika sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu akafanyiza jozi moja ya makerubi ya kuchongwa na kuyafunika kwa dhahabu. Urefu wa mabawa ya hao makerubi ulikuwa jumla ya dhiraa ishirini. Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano, nalo liligusa ukuta wa Hekalu, bawa lake lingine, lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano, ambalo liligusa bawa la kerubi lingine.

Makerubi walitanda mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kufunika Sanduku na mipiko yake ya kubebea.

Mfalme Hezekia na nabii Isaya mwana wa Amozi wakalilia mbingu katika maombi kuhusu jambo hili. Naye BWANA akamtuma malaika ambaye aliangamiza wanaume wote wenye kupigana na viongozi na maafisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Kwa hiyo, Mfalme wa Ashuru akarudi kwenye nchi yake mwenyewe kwa aibu. Naye alipokwenda katika hekalu la mungu wake, baadhi ya watoto wake walimkata na kumwua kwa upanga.

Wewe peke yako ndiwe BWANA. Uliumba mbingu, hata mbingu za mbingu, nalo jeshi lote la angani, dunia na vyote vilivyo ndani yake, bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.

Siku moja wana wa Mungu walikwenda kujionyesha mbele za BWANA. Shetani naye akaja pamoja nao.

Siku nyingine wana wa Mungu walikuja kujionyesha mbele za BWANA. Shetani naye akaja pamoja nao kujionyesha mbele zake.

wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha?

mwanadamu ni kitu gani hata umkumbuke, binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu, umemvika taji ya utukufu na heshima.

Malaika wa BWANA hufanya kituo akiwazunguka wale wamchao, naye huwaokoa.

Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo, malaika wa BWANA akiwafukuza; njia yao na iwe giza na ya utelezi, malaika wa BWANA akiwafuatilia. Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu, na bila sababu wamenichimbia shimo,

Magari ya Mungu ni makumi ya maelfu, na maelfu ya maelfu; Bwana amekuja kutoka Sinai kuja katika patakatifu pake.

akawanyeshea mana ili watu wale, aliwapa nafaka ya mbinguni. Watu walikula mkate wa malaika, aliwatumia chakula chote ambacho wangeliweza kula.

Aliwafungulia hasira yake kali, ghadhabu yake, hasira na uadui, na kundi la malaika wa kuharibu.

Kwa kuwa atawaagiza malaika zake kwa ajili yako, wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuinua, ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe.

BWANA anatawala, mataifa na yatetemeke; anaketi kwenye kiti cha enzi katikati ya makerubi, dunia na itikisike.

Mhimidini BWANA, enyi malaika zake, ninyi mlio mashujaa mnaozitii amri zake, ninyi mnaotii neno lake. Mhimidini BWANA, ninyi jeshi lake lote la mbinguni, ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake.

Hufanya pepo kuwa wajumbe wake, miali ya moto watumishi wake.

Msifuni, enyi malaika wake wote, msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni.

Katika mwaka ule Mfalme Uzia alipokufa, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu. Juu yake walikuwepo maserafi, kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao na kwa mawili walikuwa wakiruka. Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ni BWANA Mwenye Nguvu Zote; dunia yote imejaa utukufu wake.” Kwa kutoa kwao sauti miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi. Ndipo nikalia, “Ole wangu mimi! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi katikati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA Mwenye Nguvu Zote.” Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni. Akanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa nayo dhambi yako imesamehewa.”

“Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Umeumba mbingu na nchi.

“Nitaulinda mji huu na kuuokoa, kwa ajili yangu mwenyewe na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu!” Ndipo malaika wa BWANA akaondoka na kuwaua watu mia themanini na tano elfu katika kambi ya Waashuru. Watu walipoamka asubuhi yake, wote huko walikuwa maiti!

Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini, wingu kubwa sana pamoja likiwa na umeme wa radi likiwa limezungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama rangi ya manjano ya chuma kinapokuwa ndani ya moto. Katika ule moto kulikuwa na kitu kinachofanana na viumbe vinne vyenye uhai. Katika kuonekana kwake vilikuwa na umbo mfano wa mwanadamu, lakini kila kimoja kilikuwa na nyuso nne na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyooka, nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa, nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja, hawakugeuka walipokuwa wanatembea. Kuonekana kwa nyuso zao kulikuwa hivi: Kila mmoja wa wale wanne alikuwa na uso wa mwanadamu na kwa upande wa kulia kila mmoja alikuwa na uso wa simba, upande wa kushoto alikuwa na uso wa ng'ombe pia kila mmoja alikuwa na uso wa tai. Hivyo ndivyo zilivyokuwa nyuso zao. Mabawa yao yalikunjuliwa kuelekea juu, kila mmoja alikuwa na mabawa mawili ambayo kila moja liligusa bawa la mwenzake kila upande na mabawa mengine mawili yakifunika mwili wake. Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja. Po pote roho alipotaka kwenda, ndipo walipokwenda pasipo kugeuka. Kuonekana kwa vile viumbe hai katikati kulikuwa kama makaa ya mawe yanayowaka au kama mienge. Moto ule ulikuwa ukienda mbele na nyuma katikati ya vile viumbe, ulikuwa na mwangaza mkali na katikati ya ule moto kulitoka kimulimuli kama umeme wa radi. Vile viumbe vilipiga mbio kwenda na kurudi, kama vimulimuli vya umeme wa radi.

Nilipokuwa nikitazama vile viumbe hai, niliona gurudumu moja juu ya ardhi kando ya kila kiumbe kikiwa na nyuso zake nne. Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa hayo magurudumu na muundo wake: yaling'aa kama zabarajadi, nayo yote manne yalifanana. Kila gurudumu lilikuwa na gurudumu jingine ndani yake. Yalipokwenda yalielekea upande wo wote wa pande nne walipoelekea wale viumbe, magurudumu hayakuzunguka wakati viumbe vile vilipokwenda. Kingo zake zilikuwa ndefu kwenda juu na za kutisha, nazo zote nne zilijawa na macho pande zote. Vile viumbe hai vilipokwenda, magurudumu yaliyokuwa kando yao yalisogea na wakati hivyo viumbe hai vilipoinuka kutoka ardhini magurudumu nayo yaliinuka. Mahali po pote roho alipokwenda wale viumbe nao walikwenda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja navyo, kwa sababu roho ya vile viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu. Wakati viumbe vile viliposogea, nayo magurudumu yalisogea, viumbe viliposimama kimya, nayo pia yalisimama kimya, viumbe vilipoinuka juu ya nchi magurudumu yaliinuliwa pamoja navyo kwa kuwa roho ya hivyo viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu.

Juu ya vichwa vya hao viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa eneo lililokuwa wazi, lililokuwa angavu kabisa na lenye kutisha. Chini ya hiyo nafasi mabawa yao yalitanda moja kuelekea jingine, kila mmoja alikuwa na mabawa mengine mawili yaliyofunika mwili wake. Viumbe wale waliposogea nilisikia sauti ya mabawa yao, kama ngurumo ya maji yaendayo kasi, kama sauti ya Mwenyezi, kama makelele ya jeshi. Waliposimama kimya walishusha mabawa yao. Ndipo ikaja sauti toka juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, wakati waliposimama mabawa yao yakiwa yameshushwa.

Ilikuwa ni sauti ya mabawa ya wale viumbe hai yakisuguana moja kwa jingine, sauti kama ya ngurumo.

Nikatazama, nikaona juu ya ile nafasi iliyokuwa juu ya vichwa vya wale makerubi kulikuwa na kitu kilichofanana na kiti cha enzi cha yakuti samawati. BWANA akamwambia mtu yule aliyekuwa amevaa nguo ya kitani, “Ingia katikati ya yale Magurudumu yaliyo chini ya makerubi. Ukaijaze mikono yako makaa ya mawe ya moto kutoka katikati ya makerubi na uyatawanye juu ya mji.” Nilipokuwa nikiangalia, akaingia ndani. Basi wale makerubi walikuwa wamesimama upande wa kusini wa Hekalu wakati yule mtu alipoingia ndani, wingu likaujaza ule ukumbi wa ndani. Kisha utukufu wa BWANA ukainuka kutoka juu ya wale makerubi ukaenda kwenye kizingiti cha Hekalu. Wingu likajaza Hekalu, nao ukumbi ukajawa na mng'ao wa utukufu wa BWANA. Sauti ya mabawa ya wale makerubi ingeweza kusikika mpaka kwenye ukumbi wa nje, kama sauti ya Mungu Mwenyezi wakati anapoongea. BWANA alipomwamuru yule mtu aliyevaa nguo za kitani akisema, “Chukua moto toka katikati ya magurudumu, kutoka katikati ya makerubi,” yule mtu aliingia ndani akasimama pembeni mwa gurudumu. Ndipo mmoja wa wale makerubi akanyoosha mkono wake kwenye moto uliokuwa katikati yao. Akachukua baadhi ya moto na kuutia mikononi mwa yule mtu aliyevaa mavazi ya kitani, naye akaupokea akatoka nje. (Chini ya mabawa ya makerubi paliweza kuonekana kitu kilichofanana na mikono ya mwanadamu.)

Nikatazama, nikaona magurudumu manne pembeni mwa makerubi, moja pembeni mwa kila kerubi. Magurudumu hayo yalimetameta kama jiwe la zabarajadi. Kule kuonekana kwake, yote manne yalifanana kila gurudumu lilikuwa kama linazunguka ndani ya lingine. Yalipozunguka, yalikwenda kokote katika pande nne walikoelekea wale makerubi. Magurudumu hayakugeuka wakati makerubi yalipokwenda. Makerubi walikwenda upande wo wote kichwa kilikoelekea pasipo kugeuka walipokuwa wakienda. Miili yao yote, pamoja na migongo yao, mikono na mabawa yao yote yalikuwa yamejaa macho kabisa kama yalivyokuwa yale magurudumu yao manne. Nikasikia magurudumu yakiitwa, “Magurudumu ya kisulisuli.” Kila mmoja wa wale makerubi alikuwa na nyuso nne: Uso mmoja ulikuwa kama vile wa kerubi, uso wa pili ulikuwa wa mwanadamu, uso wa tatu ulikuwa wa simba na uso wa nne ulikuwa wa tai. Kisha makerubi wakapaa juu. Hawa ndio wale viumbe walio hai niliowaona kando ya Mto Kebari. Wakati makerubi walipokwenda, magurudumu yaliyoko kando yao yalikwenda na wakati makerubi walipotanda mabawa yao wapate kupaa juu kutoka katika ardhi, magurudumu yale hayakuondoka pembeni mwao. Makerubi yaliposimama kimya, nayo pia yalitulia kimya, nao makerubi yalipoinuka juu, magurudumu nayo yaliinuka juu pamoja nao, kwa sababu roho ya vile viumbe hai ilikuwa ndani yake.

Kisha utukufu wa Mungu ukaondoka pale kwenye kizingiti cha Hekalu na kusimama juu ya wale makerubi. Nilipokuwa nikitazama, makerubi yakatanda mabawa yao na kuinuka kutoka ardhini, nao walipokuwa wakienda yale magurudumu yakaenda pamoja nao. Wakasimama kwenye ingilio la lango la mashariki la nyumba ya BWANA, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ukawa juu yao. Hawa walikuwa ndio viumbe hai niliokuwa nimewaona chini ya Mungu wa Israeli kando ya Mto Kebari, nami nikatambua ya kuwa hao walikuwa makerubi. Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, mabawa manne, chini ya mabawa yao kulikuwa na kile kilichoonekana kama mikono ya mwanadamu. Nyuso zao zilifanana kama zile nilizokuwa nimeziona kando ya Mto Kebari. Kila mmoja alikwenda mbele moja kwa moja.

Ndipo wale makerubi, wenye magurudumu pembeni mwao, wakakunjua mabawa yao, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.

Watu hawa watatu, wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana, walianguka ndani ya tanuru iwakayo moto. Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?” Washauri wakajibu, “Hakika, Ee mfalme.” Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembea-tembea ndani ya moto, hawakufungwa na hawakudhurika, naye mtu yule wanne anaonekana kama mwana wa miungu.” Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iwakayo moto na kupaza sauti, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njoni huku!” Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto. Nao maliwali, wasimamizi, watawala na washauri wa kifalme wakakusanyika kuwazunguka. Waliona kwamba moto haukudhuru miili yao, wala unywele wa vichwa vyao haukuungua, majoho yao hayakuungua, wala hapakuwepo na harufu ya moto kwenye miili yao. Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Waliomtumaini na kutoogopa amri ya mfalme nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine ye yote isipokuwa Mungu wao.

“Katika maono niliyoyaona nikiwa nimelala kitandani mwangu, nilitazama, mbele yangu alikuwepo mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni.

“ ‘Uamuzi huu umetangazwa na walinzi, hukumu hii imetangazwa na watakatifu, ili walio hai wajue kuwa Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme zote za wanadamu, naye humpa ye yote amtakaye na kumtawaza juu yake hata yeye aliye mnyonge sana miongoni mwa wanadamu.’

Mungu wangu alimtuma malaika wake, naye akafunga vinywa vya hawa simba. Hawajanidhuru, kwa sababu nilionekana sina hatia mbele zake. Wala kamwe sijafanya jambo lo lote baya mbele yako, Ee mfalme.”

Mto wa moto ulikuwa unatiririka, ukipita mbele yake. Maelfu elfu wakamhudumia, kumi elfu mara kumi elfu wakasimama mbele zake. Mahakama ikakaa ili kuhukumu na vitabu vikafunguliwa.

Kisha nikasikia sauti ya mwanadamu kutoka mto Ulai ikiita, “Gabrieli, mwambie mtu huyu maana ya maono haya.” Alipokuwa akikaribia pale mahali nilipokuwa nimesimama, niliogopa nikaanguka kifudifudi, akaniambia, “Mwana wa mwanadamu, fahamu kuwa maono haya yanahusu siku za mwisho.”

wakati nilipokuwa bado katika maombi, Gabrieli, yule mtu niliyekuwa nimemwona katika maono hapo awali, alinijia kwa kasi karibia na wakati wa kutoa dhabihu ya jioni. Akanielimisha na kuniambia, “Danieli, sasa nimekuja kukupa akili na ufahamu.

Mkono ulinigusa, ukaninyanyua, nikapiga magoti na vitanga vyangu vikiwa vimeshika chini, huku nikiwa ningali bado ninatetemeka. Akasema, “Danieli, wewe mtu upendwaye sana, fikiri kwa makini maneno ninayokwenda kunena nawe sasa, simama wima, kwa maana sasa nimetumwa kwako.” Naye aliposema nami haya, nikasimama nikitetemeka. Ndipo akaendelea kusema, “Danieli usiogope. Tangu siku ya kwanza ulipotia moyo wako ili kupata ufahamu na kujinyenyekeza mbele ya Mungu wako, maneno yako yalisikiwa, nami nimekuja kwa ajili ya kuitikia maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinizuia kwa siku ishirini na moja. Ndipo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu, alikuja kunisaidia, kwa sababu nilikuwa nimezuiliwa huko na mfalme wa Uajemi. Sasa nimekuja kukueleza mambo yatakayowatokea watu wako wakati ujao, kwa maana maono hayo yanahusu wakati ambao haujaja bado.”

Wakati alipokuwa akinieleza haya, nilisujudu uso wangu ukiwa umeelekea chini nikawa bubu. Ndipo mmoja aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa midomo yangu, nami nikafungua kinywa changu, nikaanza kunena. Nikamwambia yule aliyesimama mbele yangu, “Nimepatwa na huzuni kubwa kwa sababu ya maono haya, bwana wangu, nimeishiwa nguvu. Bwana wangu, mimi mtumishi wako nitawezaje kuzungumza na wewe? Nguvu zangu zimeniishia hata ninashindwa kupumua.” Tena yule aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa na kunitia nguvu. Akasema, “Ee mtu upendwaye sana, usiogope. Amani iwe kwako! Uwe na nguvu sasa, uwe na nguvu.” Alipozungumza nami, nilipata nguvu nikasema, “Nena, bwana wangu, kwa kuwa umenipa nguvu.” Kwa hiyo akasema, “Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa hivi nitarudi kupigana dhidi ya mkuu wa Uajemi, nami nikienda, mkuu wa Uyunani atakuja, lakini kwanza nitakuambia kile kilichoandikwa katika Kitabu cha Kweli. (Hakuna hata mmoja anayenisaidia dhidi yao isipokuwa Mikaeli, mkuu wako.

“Katika wakati huo Mikaeli, mtawala mkuu ambaye huwalinda watu wako, atainuka. Kutakuwako wakati wa taabu ambao haujatokea tangu mwanzo wa mataifa hadi wakati huo. Lakini wakati huo, watu wako, kila mmoja ambaye jina lake litakutwa limeandikwa kwenye kitabu, ataokolewa.

Pigeni tarumbeta katika Sayuni; pigeni mbiu katika mlima wangu mtakatifu. Wote waishio katika nchi na watetemeke, kwa kuwa siku ya BWANA inakuja. Iko karibu, siku ya giza na huzuni, siku ya mawingu na utusitusi. Kama mapambazuko yasambaavyo toka upande huu wa milima hata upande mwingine jeshi kubwa na lenye nguvu linakuja. Jambo kama hili halijakuwapo tangu zamani wala halitakuwapo tena kamwe kwa vizazi vijavyo. Mbele yao moto unateketeza, nyuma yao miali ya moto inawaka kwa nguvu. Mbele yao nchi iko kama bustani ya Edeni, nyuma yao ni jangwa lisilofaa: hakuna kitu kinachowaepuka. Wanaonekana kama farasi; wanakwenda mbio kama askari wapanda farasi. Wanatoa sauti kama magari ya vita, wanaporukaruka juu ya vilele vya milima, kama mlio wa miali ya moto ilayo mabua, kama jeshi kubwa lililojipanga kwa ajili ya vita. Wanapoonekana, mataifa yanakuwa katika maumivu makuu; kila uso unabadilika rangi. Wanashambulia kama wapiganaji wa vita; wanapanda kuta kama askari. Wote wanatembea katika safu, hawapotoshi safu zao. Hakuna anayemsukuma mwenzake; kila mmoja anakwenda mbele moja kwa moja. Wanapita katika vizuizi bila kuharibu safu zao. Wanaenda kasi kuingia mjini; wanakimbia ukutani. Wanaingia ndani ya nyumba; kwa kuingilia madirishani kama wevi. Mbele yao dunia inatikisika, anga linatetemeka, jua na mwezi vinatiwa giza, na nyota hazitoi mwanga wake tena. BWANA anatoa mshindo wa ngurumo mbele ya jeshi lake; majeshi yake hayana idadi, ni wenye nguvu nyingi wale ambao hutii agizo lake. Siku ya BWANA ni kuu, ni ya kutisha. Ni nani anayeweza kuistahimili?

Wakati wa usiku nilipata maono, mbele yangu alikuwepo mtu akiendesha farasi mwekundu! Alikuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi kwenye bonde. Nyuma yake walikuwepo farasi wekundu, wa kikahawia na weupe. Nikauliza, “Hivi ni vitu gani bwana wangu?” Malaika aliyekuwa akizungumza na mimi akanijibu, “Nitakuonyesha kuwa ni nini.” Kisha yule mtu aliyesimama katikati ya miti ya mihadasi akaeleza, “Ni wale ambao BWANA amewatuma waende duniani kote.” Nao wakatoa taarifa kwa yule malaika wa BWANA, aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumepita duniani kote na kukuta ulimwengu wote umepumzika kwa amani.” Kisha malaika wa BWANA akasema, “BWANA Mwenye Nguvu Zote, utazuia mpaka lini rehema kutoka Yerusalemu na miji ya Yuda, ambayo umeikasirikia kwa miaka hii sabini?” Kwa hiyo BWANA akazungumza maneno ya upole na ya kufariji kwa malaika aliyezungumza nami. Kisha malaika yule aliyekuwa akizungumza nami akasema, “Tangaza neno hili: Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote asemalo: ‘Nina wivu sana kwa ajili ya Yerusalemu na Sayuni,

Kisha nikatazama juu: pale mbele yangu alikuwepo mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi mwake! Nikamwuliza, “Unakwenda wapi?” Akanijibu, “Kupima Yerusalemu, kupata urefu na upana wake.” Kisha malaika aliyekuwa akizungumza nami akaondoka, malaika mwingine akaja kukutana naye na kumwambia: “Kimbia, umwambie yule kijana, ‘Yerusalemu utakuwa mji usio na kuta kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo. Mimi mwenyewe nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka,’ asema BWANA, ‘nami nitakuwa utukufu wake ndani yake.’

Kisha akanionyesha Yoshua, Kuhani Mkuu akiwa amesimama mbele ya malaika wa BWANA, naye Shetani amesimama upande wake wa kuume ili amshitaki. BWANA akamwambia Shetani, “BWANA akukemee Shetani! BWANA, ambaye ameichagua Yerusalemu, akukemee! Je, mtu huyu siyo kijinga kinachowaka kilichonyakuliwa kwenye moto?” Wakati huu, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu alipokuwa amesimama mbele ya malaika. Malaika akawaambia wale waliokuwa wamesimama mbele yake, “Mvueni hizo nguo zake chafu.” Kisha akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakuvika mavazi ya kitajiri.” Kisha nikasema, “Mvike kilemba kilicho safi kichwani mwake.” Kwa hiyo wakamvika kilemba safi kichwani na kumvika yale mavazi mengine, wakati malaika wa BWANA akiwa amesimama karibu. Malaika wa BWANA akamwamuru Yoshua: “Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: ‘Ikiwa utakwenda katika njia zangu na kushika masharti yangu, basi utaitawala nyumba yangu na kuwa na amri juu ya nyua zangu, nami nitakupa nafasi miongoni mwa hawa wasimamao hapa.

Nikamwuliza malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Hawa ni nani bwana wangu?” Malaika akanijibu, “Hizi ni roho nne za mbinguni zisimamazo mbele ya uwepo wa Bwana wa dunia yote, zinatoka kwenda kufanya kazi yake.

Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao.” Haya yote yametukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema: “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli,” maana yake, “Mungu pamoja nasi.” Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake.

Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akamwambia, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”

Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto huko Misri na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wanatafuta uhai wa mtoto wamekufa.”

akamwambia, “Kama wewe ndiye Mwana wa Mungu jitupe chini, kwa kuwa imeandikwa, “ ‘Atakuagizia malaika zake, nao watakuchukua mikononi mwao ili usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe.’ ”

Ndipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumtumikia.

Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika. “Kama vile magugu yang'olewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.

Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”

Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

“Angalia ili usimdharau mmojawapo wa hawa wadogo, kwa maana nawaambia, malaika wao mbinguni daima wanauona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [

Wakati wa ufufuo watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa Mungu mbinguni.

Naye atawatuma malaika zake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.

“Kwa habari ya siku ile na saa hakuna ajuaye, hata malaika mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake.

“Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake.

Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?

Ghafula pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni akaenda penye kaburi akalivingirisha lile jiwe na kulikalia. Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu. Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama vile alivyosema. Njoni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa. Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye awatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtakakomwona. Sasa nimekwisha kuwaambia.’ ”

naye akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama wa mwituni, nao malaika wakamhudumia.

Mtu ye yote anayenionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na cha dhambi, Mwana wa Adamu, atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”

Wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa, watakuwa kama malaika wa mbinguni.

Naye atawatuma malaika zake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka miisho ya dunia hadi miisho ya mbingu.

“Lakini kwa habari ya siku ile na saa hakuna ye yote ajuaye, hata malaika walioko mbinguni wala Mwana hajui, ila Baba peke yake.

Walipokuwa wakiingia mle kaburini, wakamwona kijana mmoja aliyevaa joho jeupe akiwa ameketi upande wa kuume, nao wakastaajabu. Yule malaika akawaambia, “Msistaajabu. Mnamtafuta Yesu, Mnazareti, aliyesulibiwa. Amefufuka! Hayuko hapa. Tazameni mahali walipomlaza. Lakini nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro, kwamba ‘Anawatangulia kwenda Galilaya, huko ndiko mtakakomwona, kama alivyowaambia.’ ”

Ndipo malaika wa Bwana, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zekaria. Zekaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana akajawa na hofu. Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zekaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji cho chote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake. Naye atawageuza wengi wa wana wa Israeli warudi kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki na kuliweka tayari taifa lililoandaliwa kwa ajili ya Bwana.” Zekaria akamwuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.” Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema. Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.”

Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yosefu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Maria. Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!” Maria akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni, “Salamu hii ni ya namna gani?” Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, umepata kibali kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume na utamwita jina lake Yesu. Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. BWANA Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Maria akamwuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?” Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli, kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu. Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.” Maria akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka akamwacha.

Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. Ghafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawang'aria kotekote, wakaingiwa na hofu. Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote. Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori ya kulia ng'ombe.” Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema, “Atukuzwe Mungu juu mbinguni na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao wakisema, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya ya ajabu yaliyotukia, ambayo Bwana ametuambia habari zake.”

kwa maana imeandikwa: “ ‘Atakuagizia malaika zake ili wakulinde; nao watakuchukua mikononi mwao usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ”

Kama mtu ye yote akinionea aibu mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea aibu mtu huyo atakapokuja katika utukufu wake na katika utukufu wa Baba na wa malaika watakatifu.

“Ninawaambia kwamba, ye yote atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri mbele za malaika wa Mungu. Lakini yeye atakayenikana mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkana mbele ya malaika wa Mungu.

Nawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.”

Vivyo hivyo, nawaambia, kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu juu ya mwenye dhambi mmoja atubuye.”

“Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa.

Hawa hawawezi kufa tena, kwa maana wao ni kama malaika. Wao ni watoto wa Mungu, kwa sababu ni watoto wa ufufuo.

Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu.

Walipokuwa wanashangaa juu ya jambo hili, ghafula watu wawili waliokuwa wamevaa mavazi yanayong'aa kama umeme wa radi, wakasimama karibu nao. Wale wanawake, wakiwa na hofu, wakainamisha nyuso zao mpaka chini. Lakini wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai miongoni mwa wafu? Hayuko hapa, amefufuka! Kumbukeni alivyowaambia alipokuwa bado yuko pamoja nanyi huko Galilaya kwamba: ‘Ilikuwa lazima Mwana wa Adamu atiwe mikononi mwa watu wenye dhambi, waovu, asulibiwe na siku ya tatu afufuke.’ ”

lakini hawakuukuta mwili wake. Walirudi wakasema wameona maono ya malaika ambao waliwaambia kwamba Yesu yu hai.

Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”

Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, palikuwa na bwawa moja lililoitwa kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa limezungukwa na kumbi tano. Hapa palikuwa na idadi kubwa ya wasiojiweza, yaani, vipofu, viwete, na waliopooza, wakingojea maji yatibuliwe [kwa maana malaika alikuwa akishuka wakati fulani, akayatibua maji na yule aliyekuwa wa kwanza kuingia ndani baada ya maji kutibuliwa alipona ugonjwa wo wote aliokuwa nao].

Lakini Maria Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama, kuchungulia mle kaburini, naye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni. Wakamwuliza Maria, “Mwanamke, mbona unalia?” Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu na sijui walikomweka.”

Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena. Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao, wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”

wakawakamata mitume na kuwatia gerezani. Lakini wakati wa usiku malaika wa Bwana akaja akafungua milango ya gereza akawatoa nje akawaambia, “Nendeni, mkasimame Hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uzima huu mpya.”

Ninyi ndio mlipokea sheria zilizoletwa kwenu na malaika, lakini hamkuzitii.”

Basi Malaika wa Bwana akamwambia Filipo, “Nenda upande wa kusini kwenye ile barabara itokayo Yerusalemu kuelekea Gaza ambayo ni jangwa.”

Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!” Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?” Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.

Kwa hiyo Petro akawekwa gerezani, lakini kanisa lilikuwa likimwombea kwa Mungu kwa bidii. Usiku ule kabla ya siku ambayo Herode Agripa alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili, akiwa amefungwa kwa minyororo miwili. Nao walinzi wa zamu walikuwa wakilinda penye lango la gereza. Ghafula malaika wa Bwana akatokea na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro. Yule malaika akamwambia, “Vaa nguo zako na viatu vyako.” Petro akafanya hivyo. Kisha akamwambia, “Jifunge vazi lako na unifuate.” Petro alitoka mle gerezani akiwa amefuatana na yule malaika. Hakujua wakati huo kuwa yaliyokuwa yakitukia yalikuwa kweli. Alidhani kuwa anaona maono. Wakapita lindo la kwanza na la pili, ndipo wakafika kwenye lango la chuma linaloelekea mjini. Lango likawafungukia lenyewe, nao wakapita hapo wakatoka nje. Baada ya kutembea umbali wa mtaa mmoja, ghafula yule malaika akamwacha Petro.

Ndipo Petro akarudiwa na fahamu, akasema, “Sasa ninajua bila shaka yo yote kuwa Bwana amemtuma malaika wake na kuniokoa kutoka katika makucha ya Herode Agripa na kutoka katika matazamio yote ya Wayahudi.” Mara Petro alipotambua hili alikwenda nyumbani kwa Maria, mama yake Yohana aliyeitwa pia Marko, ambako watu wengi walikuwa wamekutana kwa maombi. Petro alipobisha hodi kwenye lango la nje, mtumishi wa kike jina lake Roda, akaja kumfungulia. Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi mno akarudi bila kufungua na kuwaeleza kwamba, “Petro yuko langoni!” Wakamwambia yule mtumishi wa kike, “Umerukwa na akili.” Alipozidi kusisitiza kuwa ni kweli, wakasema, “Lazima awe ni malaika wake.” Lakini Petro aliendelea kugonga langoni, nao walipofungua lango na kumwona Petro, walistaajabu sana.

Katika siku iliyochaguliwa Herode Agripa akavaa mavazi yake ya kifalme, akaketi kwenye kiti chake cha enzi na kuwahutubia watu. Watu waliokuwa wamekusanyika wakapiga kelele, wakisema, “Hii si sauti ya mwanadamu, bali ni ya Mungu.” Ghafula, kwa kuwa Herode Agripa hakumpa Mungu utukufu, malaika akampiga, akaliwa na chango akafa.

(Kwa maana Masadukayo wanasema kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho, lakini Mafarisayo wanaamini haya yote.)

Jana usiku, malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake na ambaye ninamwabudu alisimama karibu nami, naye akasema, ‘Paulo usiogope, kwa kuwa ni lazima usimame mbele ya Kaisari, naye Mungu amewapa usalama wote wanaosafiri pamoja nawe.

Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya?

Kwa sababu hii na kwa sababu ya malaika, inampasa mwanamke awe na ishara ya mamlaka iliyo juu yake.

Hata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo.

Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele!

Mtu ye yote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kumnyenyekea yeye na kuabudu malaika, akidumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu,

Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka toka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu pamoja na sauti ya malaika mkuu na sauti ya tarumbeta ya Mungu, nao wale waliolala mauti wakiwa wanamwamini Kristo watafufuka kwanza.

Kwa maana ni malaika yupi ambaye wakati wo wote Mungu alipata kumwambia, “Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuzaa?” Au tena, “Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu?”

Tena, Mungu amletapo mzaliwa wake wa kwanza ulimwenguni, husema, “Malaika wote wa Mungu na wamsujudu.”

Anenapo kuhusu malaika husema, “Huwafanya malaika zake kuwa upepo, watumishi wake kuwa miali ya moto.”

Je, ni kwa malaika yupi ambaye Mungu amepata kumwambia wakati wo wote, “Wewe keti mkono wangu wa kuume mpaka nitakapowaweka adui zako chini ya nyayo zako”? Je, malaika wote si roho watumikao waliotumwa kuwahudumia wale watakaorithi wokovu?

Mungu hakuuweka ulimwengu ujao ambao tunanena habari zake chini ya malaika. Lakini kuna mahali mtu fulani ameshuhudia akisema: “Mwanadamu ni kitu gani hata umfikirie, mwana wa mwanadamu ni nani hata umjali? Umemfanya kuwa chini kidogo kuliko malaika; umemvika taji ya utukufu na heshima,

Kwa kuwa ni dhahiri kwamba hakuja kusaidia malaika, bali uzao wa Abrahamu.

Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi ya Utukufu yakitilia kivuli kile kifuniko ambacho ndicho kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kueleza vitu hivi kwa undani sasa.

Lakini ninyi mmekuja Mlima Sayuni, Yerusalemu ya mbinguni, mji wa Mungu aliye hai. Mmekuja penye kusanyiko kubwa la malaika maelfu kwa maelfu wasiohesabika wanaoshangilia, kwenye kanisa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mmekuja kwa Mungu, mhukumu wa watu wote, kwenye roho za wenye haki waliokamilishwa,

Msisahau kuwakaribisha wageni, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengine waliwakaribisha malaika pasipo kujua.

Mitume walidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali walihudumu kwa ajili yenu katika mambo hayo ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo ambayo hata malaika wanatamani kuyafahamu.

ambaye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu: pamoja na malaika, mamlaka na nguvu zote vikiwa vimetiishwa chini yake.

lakini hata malaika, ingawa wana nguvu na uwezo zaidi, hawaleti mashtaka dhidi ya viumbe kama hao mbele za Bwana.

Wapenzi, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho mwone kama zimetoka kwa Mungu, kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea ulimwenguni. Hivi ndivyo mnavyoweza kutambua Roho wa Mungu: Kila roho inayokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatoka kwa Mungu.

Lakini hata Malaika Mkuu Mikaeli alipokuwa anashindana na ibilisi juu ya mwili wa Mose, hakuthubutu kumlaumu, bali alimwambia, “Bwana na akukemee!”

Kuhusu siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba, navyo vile vinara saba ni hayo makanisa saba.

Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao, nami sitafuta jina lake kutoka katika kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake.

Pia kukizunguka hicho kiti cha enzi palikuwa na viti ishirini na vinne na juu ya hivyo viti walikuwa wameketi wazee ishirini na wanne, waliovaa majoho meupe, wakiwa na taji za dhahabu vichwani mwao. Kwenye kile kiti cha enzi palikuwa panatoka miali ya umeme wa radi, ngurumo na sauti za radi. Mbele ya hicho kiti cha enzi, palikuwa na taa saba zilizokuwa zinawaka. Hizi ndizo Roho saba za Mungu.

Pia mbele ya hicho kiti cha enzi palikuwa na kile kilichoonekana kama bahari ya kioo, iliyokuwa angavu kama jiwe lisilo na rangi yo yote ling'aalo sana. Katikati, kukizunguka kile kiti cha enzi, kulikuwa na viumbe wanne wenye uhai, wakiwa wamejawa na macho mbele na nyuma. Huyo kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, wa pili alikuwa kama ng'ombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu na wa nne alikuwa kama tai anayeruka. Kila mmoja wa hawa viumbe wenye uhai wanne, alikuwa na mabawa sita na kujawa na macho pande zote, hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawakuacha kusema: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA Mungu Mwenyezi, aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.” Kila mara viumbe hao wenye uhai wanne walipomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele, wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Wao huziweka taji zao mbele ya hicho kiti cha enzi, wakisema: “Bwana wetu na Mungu wetu, wewe umestahili kupokea utukufu na heshima na uweza, kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa mapenzi yako viliumbwa na vimekuwako.”

Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, akisema, “Ni nani anayestahili kuzivunja hizo lakiri na kukifungua hicho kitabu?”

Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne na miongoni mwa wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho saba za Mungu zilizotumwa duniani pote. Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka kwenye mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi. Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu.

Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne, idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. Nao wakiimba kwa sauti kuu, wakisema: “Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa, kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na sifa!” Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba: “Sifa na heshima na utukufu na uweza ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi na kwa Mwana-Kondoo, milele na milele!” Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.

Baada ya hili nikaona malaika wanne wakiwa wamesimama katika pembe nne za dunia, wakizuia hizo pepo nne za dunia, ili kwamba pasiwe na upepo utakaovuma juu ya nchi au juu ya bahari au juu ya mti wo wote. Nikaona malaika mwingine akipanda kutoka maawio ya jua akiwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Akawaita kwa sauti kubwa wale malaika wanne waliokuwa wamepewa mamlaka ya kuidhuru nchi na bahari, akisema, “Msiidhuru nchi wala bahari, wala miti, hadi tuwe tumetia muhuri kwenye vipaji vya nyuso za watumishi wa Mungu wetu.”

Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee ishirini na wanne na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu, wakisema: “Amen! Sifa na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu viwe kwa Mungu wetu milele na milele. Amen!”

Nami nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele za Mungu, nao wakapewa tarumbeta saba. Malaika mwingine aliyekuwa na chetezo cha dhahabu, akaja na kusimama mbele ya madhabahu. Akapewa uvumba mwingi ili autoe pamoja na maombi ya Watakatifu wote, juu ya ile madhabahu ya dhahabu iliyoko mbele ya kile kiti cha enzi. Ule moshi wa uvumba pamoja na yale maombi ya watakatifu, vikapanda juu mbele za Mungu, kutoka mkononi mwa huyo malaika. Kisha yule malaika akachukua kile chetezo, akakijaza moto kutoka kwenye ile madhabahu, akautupa juu ya dunia. Pakatokea sauti za radi, ngurumo, umeme wa radi na tetemeko la nchi. Basi wale malaika saba waliokuwa na zile tarumbeta saba wakajiandaa kuzipiga.

Malaika wa kwanza akaipiga tarumbeta yake, pakatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyika na damu, vikatupwa kwa nguvu juu ya nchi na theluthi ya dunia ikateketea, theluthi ya miti ikateketea na majani yote mabichi yakateketea. Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu, theluthi ya viumbe vyenye uhai viishivyo baharini vikafa na theluthi ya meli zikaharibiwa. Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka toka angani, ikaangukia theluthi ya mito na chemchemi za maji. Nyota hiyo inaitwa Uchungu. Theluthi ya maji yakawa machungu na watu wengi wakafa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu. Kisha malaika wa nne akaipiga tarumbeta yake na theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota, zikapigwa. Kwa hiyo theluthi moja ya mwanga ikawa giza. Theluthi ya mchana ikawa haina mwanga na pia theluthi ya usiku. Nilipokuwa tena nikitazama, nikamsikia tai mmoja akipiga kelele kwa sauti kuu wakati akiruka katikati ya mbingu, akisema, “Ole! Ole! Ole wa watu waishio duniani, kwa sababu ya tarumbeta ambazo malaika hao wengine watatu wanakaribia kuzipiga!”

Malaika wa tano akaipiga tarumbeta yake, nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka toka angani hadi ardhini. Nyota hiyo ilipewa ufunguo wa lile Shimo lisilo na mwisho.

Malaika wa sita akaipiga tarumbeta yake, nami nikasikia sauti ikitoka katika zile pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyoko mbele za Mungu. Ile sauti ikamwambia yule malaika wa sita mwenye tarumbeta, “Wafungulie wale malaika wanne waliofungwa kwenye ule mto mkubwa Eufrati.” Basi wale malaika wanne wakafunguliwa ambao walikuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hiyo na siku hiyo na mwezi huo na mwaka huo ili wawaue theluthi ya wanadamu. Idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa 200,000,000. Nilisikia idadi yao.

Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua juu ya kichwa chake. Uso wake uling'aa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto. Mkononi mwake alikuwa ameshika kitabu kidogo kilichokuwa kimefunguliwa. Akauweka mguu wake wa kuume juu ya bahari na mguu wake wa kushoto akauweka juu ya nchi kavu. Naye akapiga kelele kwa sauti kuu kama simba anayenguruma. Alipopiga kelele, zile radi saba zikatoa ngurumo zake. Nazo zile radi saba zilipotoa ngurumo, nilitaka kuanza kuandika, lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Yatie muhuri hayo yaliyosemwa na hizo radi saba na usiyaandike.” Kisha yule malaika niliyekuwa nimemwona akiwa amesimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni. Naye akaapa kwa Jina la Mungu aishiye milele na milele, aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, dunia na vyote viijazavyo, pamoja na bahari na vyote vilivyomo ndani yake, akasema, “Hakuna kungoja tena! Lakini katika siku zile ambazo huyo malaika wa saba atakapokaribia kuipiga hiyo tarumbeta yake, siri ya Mungu itatimizwa, kama vile alivyowatangazia watumishi wake manabii.”

Ndipo ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni ikasema nami tena ikaniambia, “Nenda, chukua kile kitabu kilichofunguliwa kilichoko mkononi mwa yule malaika aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu.” Basi nikamwendea nikamwomba yule malaika anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, “Chukua na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako, lakini kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali.” Hivyo nikakichukua kile kitabu kidogo kutoka mkononi mwa yule malaika nikakila. Kilikuwa kitamu kama asali kinywani mwangu, lakini baada ya kukila, tumbo langu likatiwa uchungu. Kisha nikaambiwa, “Imekupasa kutoa unabii tena kuhusu makabila mengi, mataifa, lugha na wafalme.”

Yule malaika wa saba akaipiga tarumbeta yake, pakawa na sauti kubwa mbinguni iliyosema: “Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atatawala milele na milele.” Nao wale wazee ishirini na wanne, waliokuwa wameketi mbele za Mungu, kwenye viti vyao vya enzi wakaanguka kifudifudi wakamwabudu Mungu, wakisema: “Tunakushukuru, BWANA Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa kuwa umetwaa uweza wako mkuu na ukaanza kutawala.

Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao. Lakini joka na malaika zake wakashindwa na hapakuwa tena na nafasi kwa ajili yao mbinguni.

Nao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Hakuna mtu ye yote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao 144,000 waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani.

Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale waishio duniani, yaani, kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa. Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.” Malaika wa pili akafuata akisema, “Ameanguka! Ameanguka Babeli aliye mkuu, yeye aliyeyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.” Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu ye yote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye kipaji chake cha uso au kwenye mkono wake, yeye naye, atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo.

Kisha malaika mwingine akaja kutoka Hekaluni naye akamwita kwa sauti kubwa yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akasema, “Chukua mundu wako ukavune kwa kuwa wakati wa mavuno umewadia, kwa maana mavuno ya dunia yamekomaa.” Hivyo yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akauzungusha mundu wake duniani, nayo dunia ikavunwa.

Malaika mwingine akatoka katika Hekalu lililoko mbinguni, naye pia alikuwa na mundu mkali. Kisha malaika mwingine, aliyekuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu, naye akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kubwa, akisema, “Chukua mundu wako mkali ukakusanye vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.” Hivyo yule malaika akauzungusha mundu wake duniani na kukusanya vichala vya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. Lile shinikizo likakanyagwa nje ya mji, nayo damu ikatiririka kama mafuriko kutoka katika hilo shinikizo kufikia kimo cha hatamu za farasi, kwa umbali wa maili 200.

Ndipo nikaona ishara nyingine kubwa ya ajabu mbinguni, malaika saba wenye yale mapigo saba ya mwisho, kwa sababu kwa mapigo hayo ghadhabu ya Mungu ilikuwa imekamilika.

Ndani ya lile Hekalu wakatoka malaika saba wakiwa na mapigo saba. Walikuwa wamevaa nguo safi za kitani ing'aayo na kufungwa mikanda ya dhahabu vifuani mwao. Ndipo mmoja wa wale wenye uhai wanne akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, yeye aishiye milele na milele. Nalo lile Hekalu lilijawa na moshi uliotokana na utukufu wa Mungu na uweza wake, wala hakuna ye yote aliyeweza kuingia mle Hekaluni mpaka yale mapigo saba ya wale malaika saba yalipomalizika.

Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mle Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni, mkayamwage duniani hayo mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu.” Malaika wa kwanza akaenda akalimwaga hilo bakuli lake juu ya nchi. Majipu mabaya yenye maumivu makali yakawapata wale watu wote waliokuwa na chapa ya yule mnyama na walioabudu sanamu yake. Malaika wa pili akalimwaga bakuli lake baharini, nayo ikabadilika kuwa damu kama ya mtu aliyekufa na kila kiumbe hai kilichokuwa ndani ya bahari kikafa. Malaika wa tatu akalimwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, nazo zikawa damu. Ndipo nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema: “Wewe una haki katika hukumu hizi ulizotoa, wewe uliyeko, uliyekuwako, uliye Mtakatifu, kwa sababu umehukumu hivyo; kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu wako na manabii wako, nawe umewapa damu wanywe kama walivyostahili.” Nikasikia madhabahu ikiitikia, “Naam, BWANA Mungu Mwenyezi, hukumu zako ni kweli na haki.” Malaika wa nne akamimina bakuli lake kwenye jua, nalo likapewa nguvu za kuwaunguza watu kwa moto. Watu wakaunguzwa na hilo joto kali, wakalaani Jina la Mungu, aliyekuwa na uwezo juu ya mapigo haya, tena wakakataa kutubu na kumtukuza Mungu. Malaika wa tano akamimina bakuli lake kwenye kiti cha enzi cha yule mnyama, nao ufalme wake ukagubikwa na giza. Watu wakatafuna ndimi zao kwa ajili ya maumivu wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majeraha yao, wala hawakutubu kwa ajili ya matendo yao maovu. Malaika wa sita akamimina bakuli lake kwenye mto mkubwa Eufrati, maji yake yakakauka ili kutayarisha njia kwa ajili ya wafalme watokao Mashariki.

Malaika wa saba akamimina bakuli lake angani na sauti kubwa ikatoka mle Hekaluni katika kile kiti cha enzi, ikisema, “Imekwisha kuwa!”

Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba akaja akaniambia, “Njoo, nitakuonyesha adhabu ya yule kahaba mkuu, aketiye juu ya maji mengi. Yule ambaye wafalme wa dunia walizini naye na watu wakaao duniani walilewa kwa mvinyo wa uzinzi wake.” Kisha yule malaika akanichukua katika Roho akanipeleka nyikani. Huko nikamwona mwanamke mmoja ameketi juu ya mnyama mwekundu aliyejaa majina ya kumkufuru Mungu mwili mzima. Mnyama huyo alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.

Baada ya haya nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka makuu na dunia ikamulikiwa na mng'ao wake.

Kisha malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe kubwa kama la kusagia akalitupa baharini akisema: “Hivyo ndivyo mji mkubwa Babeli utakavyotupwa chini kwa nguvu wala hautaonekana tena.

Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu: “Amen, Haleluya!”

Nami nikamwona malaika amesimama ndani kwenye jua, akaita ndege wote warukao angani kwa sauti kuu, “Njoni, kusanyikeni kwa ajili ya karamu kubwa ya Mungu,

Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa ameshika ufunguo wa lile Shimo lisilo na mwisho na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ndiye ibilisi na Shetani, naye akamfunga kwa muda wa miaka 1,000.

Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba ya hayo mapigo saba ya mwisho akaja akaniambia, “Njoo, nami nitakuonyesha bibi arusi, yaani, mke wa Mwana-Kondoo.” Naye akanichukua katika Roho hadi kwenye mlima mkubwa na mrefu, akanionyesha ule Mji Mtakatifu, Yerusalemu, likishuka kutoka mbinguni kwa Mungu.

Akaupima ukuta wake, ulikuwa na unene wa dhiraa 144 kwa kipimo cha kibinadamu ambacho huyo malaika alikuwa akikitumia.

Mimi, Yohana, ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Nami nilipokwisha kuyasikia na kuyaona, nilianguka chini nikasujudu miguuni pa yule malaika aliyekuwa akinionyesha mambo hayo. Lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi ni mtumishi pamoja nawe na ndugu zako manabii na wote wanaoyashika maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu!”

“Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kushuhudia mambo haya kwa ajili ya makanisa. Mimi ndimi Shina na Mzao wa Daudi, ile Nyota ya Asubuhi ing'aayo.”

Swahili - Kiswahili - SW

NEN'2014 - Neno Bibilia Takatifu Kiswahili Contemporary Version - 2014

This Bible text is from Biblica Open Kiswahili Contemporary Version Neno 2015
https://open.bible/bibles/swahili-biblica-text-bible/
provided by: Biblica Inc, available by Creative Commons CC-BY-SA-4.0,
and this new compilation is shared as www.creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0.
Languages are made available to you by www.ipedge.net