06 – Kuzimu

Haya ni maneno matakatifu ya Mungu Mwenyezi.
Hatupendi maneno ya wanadamu.
Kwa mtu yeyote anayempenda Mungu... hivi ndivyo Mungu anasema kuhusu: Kuzimu.

Mistari 3 Muhimu Zaidi

Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake, nayo mauti na kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Kila mtu akahukumiwa kulingana na yale aliyotenda. Kisha Mauti na Kuzimu zikatupwa katika ziwa la moto. Hii ndio Mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto.

Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao utakaowaangamiza adui za Mungu.

Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”

Kila Mstari katika Mpangilio wa Biblia - 123 vifungu

BWANA akamjibu Mose, “Ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta kutoka kwenye kitabu changu. Sasa nenda, uongoze hao watu mpaka mahali nilipokuambia, naye malaika wangu atakutangulia. Pamoja na hayo, wakati utakapofika wa mimi kuwaadhibu, nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi yao.”

BWANA kamwe hatakuwa radhi kumsamehe, ghadhabu na wivu wa Mungu vitawaka dhidi ya mtu huyo. Laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki zitamwangukia na BWANA atafuta jina lake chini ya mbingu.

Kwa maana moto umewashwa kwa hasira yangu, ule uwakao hadi kwenye vina vya mauti. Utateketeza dunia pamoja na mazao yake, na kuwasha moto katika misingi ya milima.

Kama vile wingu liondokavyo na kutoweka, vivyo hivyo yeye ashukaye kaburini harudi tena.

kwamba mtu mwovu huepushwa kutoka katika siku ya maafa, kwamba huokolewa kutoka katika siku ya ghadhabu?

Waovu wataishia kuzimu, naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.

kwa sababu hutanitelekeza kuzimu, wala hutaacha Mtakatifu Wako aone uharibifu.

Kamba za kuzimu zilinizunguka, mitego ya mauti ilinikabili.

Mkono wako utawashika adui zako wote, mkono wako wa kuume utawakamata adui zako. Wakati utakapojitokeza utawafanya kama tanuru ya moto. Katika ghadhabu yake BWANA atawameza, moto wake utawateketeza.

Kifo na kiwajilie adui zangu ghafula, na washuke kuzimu wangali hai, kwa maana ubaya upo ndani yao.

Wafutwe kutoka kitabu cha uzima na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki.

Wale wanaomchukia BWANA wangalinywea mbele zake, na adhabu yao ingedumu milele.

Kwa maana upendo wako ni mkuu kwangu; umeniokoa kutoka kwenye vilindi vya kaburi.

Mjinga hafahamu, mpumbavu haelewi, ingawa waovu huchipua kama majani na wote watendao mabaya wanastawi, wataangamizwa milele.

Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu, wafungwa wakiteseka katika minyororo, kwa sababu walikuwa wameasi dhidi ya maneno ya Mungu na kudharau shauri la Aliye Juu Sana.

BWANA huwalinda wote wampendao, bali waovu wote atawaangamiza.

Lakini hawajui hata kidogo kuwa wafu wako humo, kwamba wageni wake huyo mwanamke wako katika vilindi vya kuzimu.

Mauti na Uharibifu viko wazi mbele za BWANA, je, si zaidi sana mioyo ya wanadamu!

Mapito ya uzima huelekea juu kwa ajili ya wenye hekima kumwepusha asiende chini kaburini.

Usimnyime mtoto adhabu, kwa maana ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa. Mwadhibu kwa fimbo na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini.

Kuzimu na uharibifu havishibi kadhalika macho ya mwanadamu.

Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa: Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au baya.

Nuru ya Israeli itakuwa moto, Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto; katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba na michongoma yake. Fahari ya misitu yake na mashamba yenye rutuba utateketeza kabisa, kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo.

naye atafurahia kumcha BWANA. Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake, wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake, bali kwa adili atahukumu wahitaji, kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia. Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.

Ombolezeni, kwa maana siku ya BWANA i karibu, itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi. Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea, moyo wa kila mtu utayeyuka. Hofu itawakamata, uchungu na maumivu makali yatawashika, watajinyonganyonga kama mwanamke aliye na utungu wa kuzaa. Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake, nyuso zao zikiwa katika hali ya kuwaka kama moto. Tazameni, siku ya BWANA inakuja, siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali, kuifanya nchi kuwa ukiwa na kuwaangamiza wenye dhambi waliomo ndani yake. Nyota za mbinguni na makundi ya nyota havitatoa mwanga wake. Jua linalochomoza litatiwa giza na mwezi hautatoa nuru yake. Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake, waovu kwa ajili ya dhambi zao. Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi Na nitakishusha kiburi cha watu wakatili.

Kwa hiyo nitazifanya mbingu zitetemeke, nayo dunia itatikisika kutoka mahali pake katika ghadhabu ya BWANA Mwenye Nguvu Zote, katika siku ya hasira yake iwakayo.

Huko chini Kuzimu kote kumetaharuki kukulaki unapokuja, inaamsha roho za waliokufa ili kukupokea, wote waliokuwa viongozi katika ulimwengu, inawafanya wainuke kwenye viti vyao vya kifalme, wale wote waliokuwa wafalme juu ya mataifa. Wote wataitika, watakuambia, “Wewe pia umekuwa dhaifu, kama sisi tulivyo; wewe umekuwa kama sisi.” Majivuno yako yote yameshushwa mpaka kuzimu, pamoja na kelele ya vinubi vyako, mafunza yametanda chini yako na minyoo imekufunika.

Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko! Umetupwa chini duniani, wewe uliyepata kuangusha mataifa! Ulisema moyoni mwako, “Nitapanda juu hadi mbinguni, nitakiinua kiti changu cha enzi juu ya nyota za Mungu, nitaketi nimetawazwa juu ya mlima wa kusanyiko, kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu. Nitapaa juu kupita mawingu, nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.” Lakini umeshushwa chini hadi kuzimu, hadi kwenye vina vya shimo.

Wao sasa wamekufa, wala hawako tena hai, roho za waliokufa hazitarudi tena. Uliwaadhibu na kuwaangamiza, umefuta kumbukumbu lao lote.

Tazama, BWANA anakuja kutoka katika makao yake ili kuwaadhibu watu wa dunia kwa ajili ya dhambi zao. Dunia itadhihirisha umwagaji damu juu yake, wala haitaendelea kuwaficha watu wake waliouawa.

Haitazimishwa usiku wala mchana, moshi wake utapaa juu milele. Kutoka kizazi hadi kizazi itakuwa ukiwa, hakuna mtu ye yote atakayepita huko tena.

Kwa maana kaburi haliwezi kukusifu, mauti haiwezi kuimba sifa zako; wale washukao chini shimoni hawawezi kuutarajia uaminifu wako.

Tazama, BWANA anakuja na moto, magari yake ya vita ni kama upepo wa kisulisuli, atatelemsha hasira yake kwa ghadhabu kali na karipio lake pamoja na miali ya moto. Kwa maana kwa moto na kwa upanga wake BWANA atatekeleza hukumu juu ya watu wote, nao wengi watakuwa ni wale waliouawa na BWANA.

“Nao watatoka nje na kuona maiti za wale walioniasi mimi, funza wao hawatakufa, wala moto wao hautazimika, nao watakuwa kitu cha kuchukiza sana kwa wanadamu wote.”

Kwa kuwa kila roho ni mali yangu, kama vile ilivyo roho ya baba, vivyo hivyo roho ya mtoto ni mali yangu. Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa.

“Kisha nikaendelea kutazama kwa sababu ya yale maneno ya majivuno yaliyosemwa na ile pembe. Nikaendelea kuangalia mpaka yule mnyama alipochinjwa na mwili wake ukaharibiwa na kutupwa katika ule moto unaowaka.

Atanena maneno kinyume cha Yeye Aliye Juu Sana na kuwaonea watakatifu wake, huku akijaribu kubadili sikukuu zao takatifu pamoja na sheria. Watakatifu watatiwa chini ya mamlaka yake kwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati. “ ‘Lakini ndipo mahakama itakapokaa kuhukumu, nayo mamlaka yake yataondolewa na kuangamizwa kabisa milele.

Watu wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwenye aibu na kudharauliwa milele.

“Hakika siku inakuja, itawaka kama tanuru. Wote wenye kiburi na kila mtenda mabaya watakuwa mabua makavu na siku ile inayokuja itawawasha moto,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. “Hakuna mzizi wala tawi litakalosalia kwao.

Lakini alipowaona Mafarisayo na Masadukayo wengi wakija ili kubatizwa, aliwaambia, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja?

Hata sasa shoka limekwisha kuwekwa tayari kwenye mizizi ya mti. Kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni.

Chombo chake cha kupuria kiko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, akiikusanya ngano yake ghalani na kuyachoma makapi kwa moto usiozimika.”

“Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue, ye yote atakayeua atapaswa hukumu.’ Lakini mimi nawaambia kwamba, ye yote atakayemkasirikia ndugu yake wa kiume au wa kike, atapaswa hukumu. Tena, ye yote atakayemwambia ndugu yake wa kiume au wa kike, ‘Raca’, yaani kumdharau na kumdhihaki, atapaswa kufanyiwa baraza. Lakini ye yote atakayesema ‘Wewe mpumbavu ulaaniwe!’ Atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.

Jicho lako la kuume likikufanya utende dhambi, ling'oe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu. Kama mkono wako wa kuume ukikufanya utende dhambi, ukate uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.

“Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo. Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.

Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Hivyo kwa matunda yao mtawatambua.

“Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

Lakini warithi wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwa na kulia na kusaga meno.”

Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali, mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu

Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka katika hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake. Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilo maana walilonena. Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki na kwa maneno yako utahukumiwa.”

Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa Ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika. “Kama vile magugu yang'olewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.

Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”

Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, hata malango ya kuzimu hayataweza kulishinda.

Kwa maana itamfaidia nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya maisha yake? Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

Lakini kama mtu ye yote anamsababisha mmojawapo wa hawa wadogo wanaoniamini atende dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake na kutoswa katika kilindi cha bahari.

Ikiwa mkono wako au mguu wako unakusababisha utende dhambi, ukate na uutupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa huna mkono mmoja au mguu mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili na kutupwa katika moto wa milele. Nalo jicho lako kama linakusababisha utende dhambi ling'oe, ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili ukatupwa katika moto wa jehanamu.

“Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi. Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema. “Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu mkamtupe nje, kwenye giza. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’

“Ninyi nyoka, ninyi uzao wa nyoka wenye sumu! Mtaiepukaje hukumu ya jehanamu?

Atamkata huyo mtumishi vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.

“Nao walipokuwa wakienda kununua mafuta, bwana arusi akafika. Wale wanawali waliokuwa tayari, wakaingia ndani pamoja naye kwenye karamu ya arusi na mlango ukafungwa. “Baadaye wale wanawali wengine nao wakaja, wakaita, ‘Bwana! Bwana! Tufungulie mlango!’ “Lakini yeye bwana arusi akawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, siwajui ninyi!’

Nanyi mtupeni huyo mtumishi asiyefaa nje, kwenye giza, mahali ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.’

“Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. Atawaweka kondoo upande wake wa kuume na mbuzi upande wake wa kushoto.

“Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’ “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’ “Naye atawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’ “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

Lakini ye yote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”

Mtu atafaidiwa nini kama akiupata ulimwengu wote lakini akaipoteza nafsi yake? Au mtu atatoa nini apate tena maisha yake?

“Kama mtu ye yote akimsababisha mmojawapo wa wadogo hawa wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa afadhali mtu huyo afungiwe shingoni mwake jiwe kubwa la kusagia na kutoswa baharini. Kama mkono wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja kuliko kuwa na mikono miwili ukaingia jehanamu mahali ambako moto hauzimiki. [Mahali ambako funza wake hawafi wala moto wake hauzimiki]. Kama mguu wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa kilema kuliko kuwa na miguu miwili ukaingia jehanamu mahali ambako moto hauzimiki. [Mahali ambako funza wake hawafi wala moto hauzimiki.] Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, ling'oe. Ni afadhali kuwa chongo ukaingia katika Ufalme wa Mungu kuliko kuwa na macho mawili na ukatupwa jehanamu, mahali ambako “ ‘funza wake hawafi, wala moto wake hauzimiki.’

Ye yote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini ye yote asiyeamini atahukumiwa.

Pepeto lake liko mkononi, tayari kusafisha sakafu yake ya kupuria na kuikusanya ngano ghalani, lakini makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”

Yesu akamwuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Legioni,” kwa kuwa alikuwa ameingiwa na pepo wachafu wengi mno. Wale pepo wachafu wakamsihi sana asiwaamuru kwenda Shimoni.

Je, itamfaidia nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake?

Nawe, Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu.” “Yeye awasikilizaye ninyi, anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi, amenikataa mimi. Lakini yeye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”

Lakini nitawaambia nani wa kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua mwili, ana mamlaka ya kuwatupa motoni. Naam, nawaambia mwogopeni huyo!

La hasha! Ninyi nanyi msipotubu, mtaangamia vivyo hivyo.

Mtu mmoja akamwuliza, “Bwana, ni watu wachache tu watakaookolewa?” Yesu akawaambia, “Jitahidini kuingia kwa kupitia mlango mwembamba, kwa maana, nawaambia, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza. Wakati mwenye nyumba atakapoondoka na kufunga mlango, mtasimama nje mkigonga mlango na kusema, ‘Bwana, utufungulie mlango.’ “Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi wala mtokako.’ “Ndipo mtamjibu, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe, tena ulifundisha katika mitaa yetu.’ “Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi wala mtokako. Ondokeni kwangu ninyi watenda maovu!’ “Ndipo kutakuwako kilio na kusaga meno, mtakapomwona Abrahamu, Isaki na Yakobo na manabii wote wakiwa katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi mkiwa mmetupwa nje.

“Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa, kila siku. Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima. Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kulamba vidonda vyake. “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake. Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’ “Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. Zaidi ya hayo kati yetu na ninyi huko, kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu ye yote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’ “Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu, maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso. “Abrahamu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Mose na Manabii, wawasikilize hao.’ “Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Abrahamu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’ “Abrahamu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Mose na manabii, hawataweza kushawishiwa hata kama atafufuka mtu kutoka kwa wafu.’ ”

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kwa yeye ulimwengu upate kuokolewa. Ye yote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakumwamini Mwana pekee wa Mungu. Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe.

Ye yote anayemwamini Mwana ana uzima wa milele, lakini yeye asiyemwamini Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yake.”

“Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka nje, wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima na wale waliotenda maovu, watafufuka wahukumiwe.

Mtu ye yote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea.

Kwa maana hutaniacha kaburini, wala hutamwacha aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.

Daudi akiona mambo yaliyoko mbele, akanena juu ya kufufuka kwa Kristo, kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu.

Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameliweka wazi kwao. Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, umeonekana waziwazi ukitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru. Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. Ingawa wakijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga

Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa. Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu.

Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti.

Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa, asema Bwana.”

Kwa kuwa imeandikwa: “ ‘Kama niishivyo,’ asema Bwana, ‘kila goti litapigwa mbele zangu, na kila ulimi utamkiri Mungu.’ ” Hivyo basi kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe kwa Mungu.

Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya. Basi, kwa kuwa tunajua kumcha Bwana, tunajitahidi kuwavuta wengine, lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia.

Ye yote atendaye mabaya atalipwa kwa ajili ya mabaya yake, wala hakuna upendeleo.

Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu. Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa uweza wake,

Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu,

Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao utakaowaangamiza adui za Mungu.

Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Kulipiza kisasi ni juu yangu; mimi nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.” Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.

Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki, ili awalete ninyi kwa Mungu. Mwili wake ukauawa, lakini akafanywa hai katika Roho, ambayo kwa hiyo alikwenda na kuzihubiria roho zilizokuwa kifungoni.

Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama vile watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu, ambao kwa siri, wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli hata kumkana Bwana wa pekee aliyewanunua na kujiletea juu yao maangamizi ya haraka. Hata hivyo, wengi watafuata njia zao za ufisadi ambao kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa. Nao katika tamaa zao mbaya, watajipatia faida kwenu kwa maneno ya madanganyo waliyotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, ambayo haikawii wala uangamivu wao haujalala usingizi.

Kwa maana kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa kuzimu, katika vifungo vya giza wakae humo mpaka ije hukumu; kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, akamhifadhi Noa, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba; kama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu na kama alimwokoa Loti, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu (kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku), ikiwa hivyo ndivyo, basi Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa wacha Mungu kutoka katika majaribu na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu. Hii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka. Kwa ushupavu na kwa kiburi watu hawa hawaogopi kunena mabaya dhidi ya viumbe vya mbinguni, lakini hata malaika, ingawa wana nguvu na uwezo zaidi, hawaleti mashtaka dhidi ya viumbe kama hao mbele za Bwana.

Watu hawa ni chemchemi zisizo na maji na ukungu upeperushwao na tufani, ambao giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao.

Lakini kwa neno lilo hilo mbingu za sasa na dunia, zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.

Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake kama watu wengine wanavyodhani kukawia. Yeye anawavumilia, maana hataki mtu ye yote aangamie, bali kila mmoja afikilie toba.

Ye yote amchukiaye ndugu yake ni mwuaji, nanyi mwajua ya kwamba mwuaji hana uzima wa milele ndani yake.

Huu ndio ushuhuda: kwamba Mungu ametupa uzima wa milele, nao huo uzima umo katika Mwanawe. Aliye naye Mwana wa Mungu anao uzima, yeye asiye na Mwana wa Mungu hana uzima.

Kwa kuwa kuna watu waliojipenyeza kwa siri katikati yenu, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, waovu, wapotoshao neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi wakimkana yeye aliye Bwana wetu wa pekee, Bwana Yesu Kristo.

Nao malaika ambao hawakulinda nafasi zao, lakini wakayaacha makao yaliyokuwa yao hasa, hawa amewaweka katika giza, wakiwa wamefungwa kwa minyororo ya milele kwa ajili ya hukumu siku ile kuu. Vivyo hivyo, Sodoma na Gomora na pia ile miji iliyokuwa kandokando, ambayo kwa jinsi moja na hao, walijifurahisha kwa uasherati na kufuata tamaa za mwili zisizo za asili, waliwekwa wawe mfano kwa kuadhibiwa katika moto wa milele.

Watu hawa ni dosari katika karamu zenu za upendo, wakila pamoja nanyi bila hofu, wakijilisha pasipo hofu. Wao ni mawingu yasiyokuwa na maji, yakichukuliwa na upepo, miti isiyo na matunda wakati wa mapukutiko, ambayo hunyauka, iliyokufa mara mbili na kung'olewa kabisa. Wao ni mawimbi makali ya bahari, yakitoa povu la aibu yao wenyewe, ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele.

wengine waokoeni kwa kuwanyakua kutoka kwenye moto; nao wengine wahurumieni mkiwa na hofu, mkichukia hata vazi lenye mawaa na kutiwa unajisi na mwili.

Mimi ni yeye aliye hai, niliyekuwa nimekufa na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na kuzimu.

“Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatadhuriwa na mauti ya pili.

Malaika wa tano akaipiga tarumbeta yake, nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka toka angani hadi ardhini. Nyota hiyo ilipewa ufunguo wa lile Shimo lisilo na mwisho. Alipolifungua hilo Shimo lisilo na mwisho, moshi ukapanda kutoka humo kama moshi wa tanuru kubwa sana. Jua na anga vikatiwa giza na ule moshi uliotoka katika hilo shimo lisilokuwa na mwisho.

Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu ye yote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye kipaji chake cha uso au kwenye mkono wake, yeye naye, atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo. Nao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa ye yote anayepokea chapa ya jina lake.”

Yule mnyama aliyekuwepo wakati fulani na ambaye sasa hayupo, yeye ni mfalme wa nane. Ni miongoni mwa wale saba, naye anakwenda kwenye maangamizi yake.

Naye akalia kwa nguvu kwa sauti kubwa, akisema: “Umeanguka! Umeanguka Babeli uliye Mkuu! Umekuwa makao ya mashetani na makazi ya kila pepo mchafu, makazi ya kila ndege na kila mnyama achukizaye. Kwa maana mataifa yote yamekunywa mvinyo wa uasherati wake. Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye, nao wafanya biashara wa dunia wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.”

Mwanga wa taa hautaangaza ndani yako tena. Sauti ya bwana arusi na bibi arusi kamwe haitasikiwa ndani yako tena. Wafanyabiashara wako walikuwa watu maarufu wa dunia. Mataifa yote yalipotoshwa kwa uchawi wako. Ndani yake ilionekana damu ya manabii na ya watakatifu na wote waliouawa duniani.”

kwa maana hukumu zake ni za kweli na za haki. Amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake. Mungu amemlipiza kisasi kwa ajili ya damu ya watumishi wake.” Wakasema tena kwa nguvu: “Haleluya! Moshi wake huyo kahaba unapanda juu milele na milele.”

Alikuwa amevaa joho lililochovywa kwenye damu na Jina lake ni “Neno la Mungu.” Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani nzuri, nyeupe safi. Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Atalikanyaga shinikizo la mvinyo wa ghadhabu ya Mungu Mwenyezi.

Nami nikamwona malaika amesimama ndani kwenye jua, akaita ndege wote warukao angani kwa sauti kuu, “Njoni, kusanyikeni kwa ajili ya karamu kubwa ya Mungu, ili mpate kula nyama ya wafalme na ya majemadari, ya mashujaa, ya farasi na ya wapanda farasi, nyama ya wanadamu, wote walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”

Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo ambaye alikuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti. Wale waliosalia waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule aliyekuwa amempanda huyo farasi mweupe, nao ndege wote wakajishibisha kwa nyama yao.

Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa ameshika ufunguo wa lile Shimo lisilo na mwisho na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ndiye ibilisi na Shetani, naye akamfunga kwa muda wa miaka 1,000. Akamtupa katika lile Shimo lisilo na mwisho, akamfunga humo na kulitia lakiri, ili kumzuia asiendelee kudanganya mataifa mpaka hiyo miaka 1,000 itimie. Baada ya hayo lazima afunguliwe kwa muda mfupi.

Hiyo miaka 1,000 itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka kifungoni mwake, naye atatoka ili kuyadanganya mataifa yaliyopo katika pembe nne za dunia, yaani, Gogu na Magogu apate kuwakusanya tayari kwa vita. Idadi yao ni kama mchanga ulioko Pwani. Nao walitembea katika eneo lote la dunia, wakaizunguka kambi ya watakatifu na ule mji unaopendwa. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza. Naye ibilisi aliyewadanganya akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti walikokuwa wametupwa yule mnyama na yule nabii wa uongo. Watateswa humo mchana na usiku, milele na milele.

Kisha nikaona kiti kikubwa cheupe cha enzi pamoja na yeye aliyeketi juu yake. Dunia na mbingu zikaukimbia uso wake wala mahali pao hapakuonekana. Nami nikawaona wafu wakubwa na wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao kama yalivyoandikwa ndani ya hivyo vitabu. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake, nayo mauti na kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Kila mtu akahukumiwa kulingana na yale aliyotenda. Kisha Mauti na Kuzimu zikatupwa katika ziwa la moto. Hii ndio Mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto.

Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

Atendaye mabaya na aendelee kutenda mabaya, aliye mchafu na aendelee kuwa mchafu, yeye atendaye haki na aendelee kutenda haki na yeye aliye mtakatifu na aendelee kuwa mtakatifu.”

Namwonya kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Mtu ye yote akiongeza humo cho chote, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Kama mtu ye yote akipunguza humo cho chote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.

Swahili - Kiswahili - SW

NEN'2014 - Neno Bibilia Takatifu Kiswahili Contemporary Version - 2014

This Bible text is from Biblica Open Kiswahili Contemporary Version Neno 2015
https://open.bible/bibles/swahili-biblica-text-bible/
provided by: Biblica Inc, available by Creative Commons CC-BY-SA-4.0,
and this new compilation is shared as www.creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0.
Languages are made available to you by www.ipedge.net