18 – Walimu wa Uongo

Haya ni maneno matakatifu ya Mungu Mwenyezi.
Hatupendi maneno ya wanadamu.
Kwa mtu yeyote anayempenda Mungu... hivi ndivyo Mungu anasema kuhusu: Walimu wa Uongo.

Mistari 3 Muhimu Zaidi

Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama vile watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu, ambao kwa siri, wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli hata kumkana Bwana wa pekee aliyewanunua na kujiletea juu yao maangamizi ya haraka. Hata hivyo, wengi watafuata njia zao za ufisadi ambao kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa. Nao katika tamaa zao mbaya, watajipatia faida kwenu kwa maneno ya madanganyo waliyotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, ambayo haikawii wala uangamivu wao haujalala usingizi.

Huandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha kwa maangamizi yao wenyewe, kama wapotoshavyo pia Maandiko mengine.

Lakini nabii ambaye atathubutu kusema kwa Jina langu kitu cho chote ambacho sikumwamuru akiseme, au nabii ambaye husema kwa jina la miungu mingine ni lazima auawe.”

Kila Mstari katika Mpangilio wa Biblia - 328 vifungu

Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao BWANA Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wo wote wa bustanini’?” Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala msiguse kabisa, la sivyo mtakufa.’ ” Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

Ndipo BWANA Mungu akamwuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.” Hivyo BWANA Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili, “Umelaaniwa kuliko wanyama wote wa kufugwa na wa porini! Utatambaa kwa tumbo lako na kula mavumbi siku zote za maisha yako. Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na wake, huo atakuponda kichwa, nawe utamgonga kisigino.”

Usivisujudie au kuviabudu; kwa kuwa Mimi, BWANA Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi ya baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, lakini ninaonyesha upendo kwa vizazi elfu vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.

“Usieneze habari za uongo. Usimsaidie mtu mwovu kwa kuwa shahidi mwenye nia ya kudhuru wengine. “Usifuate umati wa watu katika kutenda mabaya. Unapotoa ushahidi kwenye mashtaka, usipotoshe haki ukijumuika na umati wa watu,

“ ‘Usiibe. “ ‘Usiseme uongo. “ ‘Msidanganyane.

“ ‘Usiende huko na huko ukieneza uchochezi miongoni mwa watu wako. “ ‘Usifanye kitu cho chote kile kinachohatarisha maisha ya jirani yako. Mimi ndimi BWANA. “ ‘Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Karipia jirani yako kwa uwazi ili usishiriki hatia yake.

Mungu si mtu, hata aseme uongo, wala yeye si mwanadamu, hata ajute. Je, anasema, kisha asitende? Je, anaahidi, asitimize?

Mliona kwa macho yenu wenyewe kile BWANA alichokifanya kule Baal-Peori. BWANA Mungu wenu aliwaangamiza kutoka miongoni mwenu kila mmoja aliyemfuata Baali wa Peori,

Hivyo iweni waangalifu kuyafanya yale BWANA Mungu wenu aliyowaagiza; msigeuke upande wa kuume wala wa kushoto.

Kumbuka jinsi BWANA Mungu wenu alivyowaongoza katika njia yote katika jangwa kwa miaka hii arobaini, kukunyenyekeza na kukujaribu ili ajue lililoko moyoni mwako, kwamba utayashika maagizo yake au la. Alikudhili na kukufanya uone njaa kisha akulishe kwa mana, ambayo wewe wala baba zako hamkuijua, awafundishe kuwa mwanadamu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha BWANA.

Mjue basi ndani ya mioyo yenu kama mtu anavyomwadibisha mwanawe, ndivyo BWANA Mungu wako atawaadibisha ninyi. Shikeni maagizo ya BWANA Mungu wenu mtembee katika njia zake na kumheshimu.

Jihadharini, la sivyo mtashawishika kugeuka na kuabudu miungu mingine na kuisujudia.

Angalieni kwamba mnafanya yote niliyowaamuru; msiongeze kitu wala msipunguze kitu.

Kama nabii, au yule anayetabiri kwa njia ya ndoto, akijitokeza miongoni mwenu na akawatangazia ishara ya miujiza na ajabu, ikiwa ishara au ajabu ya aliyozungumza ikatokea, naye akasema, “Na tufuate miungu mingine” (miungu ambayo hamjaifahamu) “na tuiabudu,” kamwe msiyasikilize maneno ya nabii wala mwota ndoto huyo. BWANA Mungu wenu anawajaribu kuangalia kama mnampenda kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote.

Lakini nabii ambaye atathubutu kusema kwa Jina langu kitu cho chote ambacho sikumwamuru akiseme, au nabii ambaye husema kwa jina la miungu mingine ni lazima auawe.”

Mnaweza kuulizana wenyewe, “Tutawezaje kujua wakati ujumbe haukusemwa na BWANA?” Ikiwa kile nabii anachotangaza kwa jina la BWANA hakikutokea au kutimia, huo ni ujumbe ambao BWANA hakusema. Nabii huyo amesema kwa ujuaji. Msimwogope huyo.

Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi, nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu. Kwa sababu umelikataa neno la BWANA, naye amekukataa wewe kuendelea kuwa mfalme.”

Mwishoni, pepo mchafu akajitokeza, akasimama mbele za BWANA na kusema, ‘Nitamshawishi.’ “BWANA akauliza, ‘Kwa njia gani?’ “Akasema, ‘Nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’ “BWANA akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’ “Kwa hiyo sasa BWANA ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. BWANA ameamuru maafa kwa ajili yako.”

Mwishoni, roho akajitokeza, akasimama mbele za BWANA na kusema, ‘Nitamshawishi.’ “BWANA akauliza, ‘Kwa njia gani?’ “Akasema, ‘Nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’ “BWANA akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’ “Kwa hiyo sasa BWANA ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. BWANA ameamuru maafa kwa ajili yako.”

BWANA, Mungu wa baba zao, akawapelekea neno kupitia wajumbe wake tena na tena, kwa sababu alikuwa anawahurumia watu wake pamoja na mahali pa maskani yake. Lakini waliwadhihaki wajumbe wa BWANA wakayadharau maneno yake na kuwacheka manabii wake mpaka ghadhabu ya BWANA ikawa kubwa dhidi ya watu wake na hakukuwa na namna ya kuituliza.

Ninyi, hata hivyo, hunipakaza uongo, ninyi ni matabibu wasiofaa kitu, ninyi nyote!

Kwa nini mataifa wanashauriana kufanya mabaya, na mataifa kula njama bure? Wafalme wa dunia wanajipanga na watawala wanajikusanya pamoja dhidi ya BWANA na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake. Wanasema, “Tuvunje minyororo yao na kuvitupilia mbali vifungo vyao.” Yeye atawalaye mbinguni hucheka, Bwana huwadharau.

Unawaangamiza wasemao uongo, wamwagao damu na wadanganyifu BWANA huwachukia.

Hakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika, mioyo yao imejaa maangamizi. Koo zao ni kaburi lililo wazi, kwa ndimi zao hunena udanganyifu.

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Mahalathi. Zaburi Ya Daudi) Mpumbavu anasema moyoni mwake, “Hakuna Mungu.” Wameharibika, matendo yao ni maovu kabisa; hakuna atendaye mema. Toka mbinguni BWANA anawachungulia wanadamu chini aone kama wako wenye akili, wo wote wanaomtafuta Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja; hakuna atendaye mema, naam! Hata mmoja.

Midomo yao isemayo uongo na inyamazishwe, kwa maana kwa kiburi na dharau husema kwa majivuno dhidi ya wenye haki.

auzuie ulimi wake na mabaya na midomo yake kutokana na kusema uongo.

Lakini kwake mtu mwovu, Mungu asema: “Una haki gani kunena sheria zangu au kuchukua Agano langu midomoni mwako? Unachukia mafundisho yangu na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi, ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila. Unapenda mabaya kuliko mema, uongo kuliko kusema kweli. Unapenda kila neno lenye kudhuru, ewe ulimi wenye hila! Hakika Mungu atakushusha chini kwa maangamizi ya milele: atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu kutoka katika hema yako, atakung'oa kutoka nchi ya walio hai.

Mazungumzo yake ni laini kama siagi, hata hivyo vita vimo moyoni mwake, maneno yake mororo kuliko mafuta, hata hivyo ni upanga mkali uliofutwa.

Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao, kwa ajili ya maneno ya midomo yao, waache wanaswe katika kiburi chao. Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka,

Mdanganyifu hatakaa nyumbani mwangu, yeye asemaye kwa uongo hatasimama mbele yangu.

Unawakataa wote wanaoyaasi maagizo yako, kwa maana udanganyifu wao ni bure.

Ninachukia na kuchukizwa sana na uongo, lakini napenda sheria yako.

Kumcha BWANA ndiyo chanzo cha maarifa, lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.

“Enyi wajinga, mtang'ang'ania ujinga wenu hadi lini? Mpaka lini wenye mizaha watafurahia mizaha na wapumbavu kuchukia maarifa? Kama mngekuwa mmeitikia karipio langu, ningekuwa nimemimina roho yangu kwenu na kuwafahamisha maneno yangu.

Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote wala usizitegemee akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe, mche BWANA ukajiepushe na uovu.

Epusha kinywa chako na ukaidi, weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako.

Macho yako na yatazame mbele, kaza macho yako moja kwa moja mbele yako. Sawazisha mapito ya miguu yako na njia zako zote ziwe zimethibitika. Usigeuke kulia wala kushoto, epusha mguu wako na ubaya.

Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA, naam, viko saba vilivyo chukizo kwake: macho ya kiburi, ulimi udanganyao, mikono imwagayo damu isiyo na hatia, moyo ule uwazao mipango miovu, miguu ile iliyo myepesi kukimbilia uovu, shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.

“Ye yote anayemkosoa mwenye mzaha hukaribisha matukano, ye yote anayekemea mtu mwovu hupatwa na matusi. Usimkemee mwenye mzaha la sivyo atakuchukia; mkemee mwenye hekima naye atakupenda. Mfundishe mtu mwenye hekima naye atakuwa na hekima zaidi, mfundishe mtu mwadilifu naye atazidi kufundishika.

“Kumcha BWANA ni mwanzo wa hekima na kumjua Mtakatifu ni ufahamu.

Midomo isemayo kweli hudumu milele, bali ulimi wa uongo hudumu kwa muda mfupi tu.

BWANA anachukia sana midomo idanganyayo, bali hufurahia watu ambao ni wa kweli.

Shahidi wa kweli hadanganyi, bali shahidi wa uongo humimina uongo. Mwenye mzaha huitafuta hekima na haipati, bali maarifa huja kwa urahisi kwa anayepambanua. Kaa mbali na mtu mpumbavu, kwa maana hutapata maarifa katika midomo yake.

Shahidi wa kweli huokoa maisha, bali shahidi wa uongo ni mdanganyifu.

Mwenye mzaha huchukia maonyo, hatataka shauri kwa mwenye hekima.

Mtu mwovu husikiliza midomo mibaya, mwongo husikiliza kwa makini ulimi wa madhara.

Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa, naye amwagaye uongo hataachwa huru.

Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa, naye amwagaye uongo ataangamia.

Mfukuze mwenye dhihaka, nayo mashindano yatatoweka; ugomvi na matukano vitakoma.

Usishuhudie dhidi ya jirani yako bila sababu, au kutumia midomo yako kudanganya.

Afadhali karipio la wazi kuliko upendo uliofichika. Majeraha kutoka kwa rafiki yaonyesha uaminifu, bali busu la adui ni udanganyifu.

Kama mtawala akisikiliza uongo, maafisa wake wote huwa waovu.

“Kila neno la Mungu ni kamilifu; yeye ni ngao kwa wale wanaomkimbilia. Usiongeze kwenye maneno yake, ama atakukemea na kukuthibitisha kuwa mwongo.

Afadhali sifa nzuri kuliko manukato safi, nayo siku ya kufa kuliko ya kuzaliwa.

Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia! Kwa maana BWANA amesema: “Nimewalisha watoto na kuwalea, lakini wameniasi mimi. Ng'ombe anamjua bwana wake, naye punda anajua hori la mmiliki wake, lakini Israeli hajui, watu wangu hawaelewi.” Lo! Taifa lenye dhambi, watu waliolemewa na uovu, uzao wa watenda mabaya, watoto waliozoelea upotovu! Wamemwacha BWANA, Wamemkataa kwa dharau yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na kumgeuzia kisogo. Kwa nini mzidi kupigwa? Kwa nini kudumu katika uasi? Kichwa chako chote kimejeruhiwa, moyo wako wote ni mgonjwa.

Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa, nao wanaomwacha BWANA wataangamia.

Ole wao wanaoita ubaya ni wema na wema ni ubaya, wawekao giza badala ya nuru na nuru badala ya giza, wawekao uchungu badala ya utamu na utamu badala ya uchungu. Ole wao walio na hekima machoni pao wenyewe na kujiona wenye akili machoni pao wenyewe.

BWANA Mwenye Nguvu Zote ndiye peke yake ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu, ndiye peke yake utakayemwogopa, ndiye peke yake utakayemhofu, naye atakuwa mahali patakatifu; lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa na mwamba wa kuwaangusha. Kwa watu wa Yerusalemu atakuwa mtego na tanzi.

Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko.

Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko! Umetupwa chini duniani, wewe uliyepata kuangusha mataifa! Ulisema moyoni mwako, “Nitapanda juu hadi mbinguni, nitakiinua kiti changu cha enzi juu ya nyota za Mungu, nitaketi nimetawazwa juu ya mlima wa kusanyiko, kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu. Nitapaa juu kupita mawingu, nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.” Lakini umeshushwa chini hadi kuzimu, hadi kwenye vina vya shimo. Wale wanaokuona wanakukazia macho, wanatafakari hatima yako: “Je, huyu ndiye yule aliyetikisa dunia na kufanya falme zitetemeke,

Wamisri watakufa moyo, na nitaifanya mipango yao kuwa batili, watatafuta ushauri kwa sanamu na kwa roho za waliokufa, kwa wapiga ramli na kwa wale waongeao na mizimu.

Hawa pia wanapepesuka kwa sababu ya mvinyo, wanayumbayumba kwa sababu ya kileo: Makuhani na manabii wanapepesuka kwa sababu ya kileo, wanachanganyikiwa kwa sababu ya mvinyo; wanapepesuka wanapoona maono, wanajikwaa wanapotoa maamuzi.

Bwana anasema: “Watu hawa hunikaribia kwa vinywa vyao na kuniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami. Huniabudu bure, mafundisho yao ni sheria tu walizofundishwa na wanadamu.

Mnapindua mambo juu chini, kana kwamba mfinyanzi aweza kufikiriwa kuwa kama udongo wa mfinyanzi! Je, kile kilichofinyangwa chaweza kumwambia yule aliyekifinyanga, “Wewe hukunifinyanga mimi?” Je, chungu kinaweza kumwambia mfinyanzi, “Wewe hujui cho chote?”

Wale wanaopotoka rohoni watapata ufahamu, wale wanaolalamika watayakubali mafundisho.”

Hawa ni watu waasi, watoto wadanganyifu, watoto ambao hawataki kusikiliza mafundisho ya BWANA.

Wanawaambia waonaji, “Msione maono tena!” Nako kwa manabii wanasema, “Msiendelee kutupatia maono ambayo ni ya kweli! Tuambieni mambo ya kupendeza, tabirini mambo ya uongo. Acheni njia hii, ondokeni katika mapito haya, nanyi acheni kutukabili pamoja na yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!” Kwa hiyo, hili ndilo asemalo yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa sababu mmekataa ujumbe huu, mkategemea uonevu na kutumainia udanganyifu, dhambi hii itakuwa kwenu kama ukuta mrefu, wenye ufa na wenye kubetuka, ambao unaanguka ghafula, kwa mara moja.

“yeye huzipinga ishara za manabii wa uongo, na kuwatia upumbavu waaguzi, ayapinduaye maarifa ya wenye hekima, na kuyafanya kuwa upuzi,

Walinzi wa Israeli ni vipofu, wote wamepungukiwa na maarifa; wote ni mbwa walio bubu hawawezi kubweka; hulala na kuota ndoto, hupenda kulala. Ni mbwa wenye tamaa kubwa, kamwe hawatosheki. Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu; wote wamegeukia njia yao wenyewe, kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe.

Mnamdhihaki nani? Ni nani mnayemcheka kwa dharau na kumtolea ndimi zenu? Je, ninyi si watoto wa waasi, Uzao wa waongo?

Nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda wamekuwa si waaminifu kwangu kamwe,” asema BWANA. Wamedanganya kuhusu BWANA, wamesema, “Yeye hatafanya jambo lo lote! Hakuna dhara litakalotupata; kamwe hatutaona upanga wala njaa. Manabii ni upepo tu, wala neno halimo ndani yao, kwa hiyo hayo wayasemayo na yatendeke kwao.”

“Jambo la kutisha na kushtusha limetokea katika nchi hii: Manabii wanatabiri uongo, makuhani wanatawala kwa mamlaka yao wenyewe, nao watu wangu wanapenda hivyo. Lakini mtafanya nini mwisho wake?

“Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi mkubwa kabisa, wote wanatamani kupata faida isiyo halali; makuhani na manabii wanafanana, wote wanafanya udanganyifu. Hufunga majeraha ya watu wangu kama vile hawakuumia sana. Husema, ‘Amani, amani,’ wakati hakuna amani.

Rafiki humdanganya rafiki, hakuna ye yote asemaye kweli. Wamefundisha ndimi zao kudanganya, wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi. Unakaa katikati ya udanganyifu; katika udanganyifu wao wanakataa kunitambua mimi,” asema BWANA.

Ndimi zao ni mshale wenye sumu, hunena kwa udanganyifu. Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake, lakini moyoni mwake humtegea mtego.

Ndipo BWANA akaniambia, “Manabii wanatabiri uongo kwa Jina langu. Sikuwatuma wala sikuwaweka wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, maaguzi, maono ya sanamu zisizofaa kitu na madanganyo ya mawazo yao wenyewe. Kwa hiyo, hili ndilo BWANA asemalo kuhusu manabii wanaotabiri kwa Jina langu: Mimi sikuwatuma, lakini wanasema, ‘Hakuna upanga wala njaa itakayoigusa nchi hii.’ Manabii hao hao watakufa kwa upanga na kwa njaa.

Hili ndilo asemalo BWANA: “Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu, ategemeaye mwenye mwili kwa ajili ya nguvu zake, ambaye moyo wake umemwacha BWANA.

Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote, ni mwovu kupita kiasi. Ni nani awezaye kuujua? “Mimi BWANA huchunguza moyo na kuzijaribu nia, kumlipa mtu kwa kadiri ya mwenendo wake, kwa kadiri ya matendo yake yanavyostahili.”

Kuhusu manabii: Moyo wangu umevunjika ndani yangu; mifupa yangu yote inatetemeka. Nimekuwa kama mtu aliyelewa, kama mtu aliyelemewa na divai, kwa sababu ya BWANA na maneno yake matakatifu.

“Nabii na kuhani wote si wacha Mungu; hata hekaluni mwangu ninaona uovu wao,” asema BWANA. “Kwa hiyo mapito yao yatakuwa utelezi, watafukuziwa mbali gizani na huko wataanguka. Nitaleta maafa juu yao katika mwaka wa kuadhibiwa kwao,” asema BWANA.

Nako miongoni mwa manabii wa Yerusalemu nimeona jambo baya sana: Wanafanya uzinzi na kuenenda katika uongo. Wanatia nguvu mikono ya watenda mabaya, kwa ajili hiyo hakuna ye yote anayeachana na uovu wake. Wote wako kama Sodoma kwangu; watu na Yerusalemu wako kama Gomora.” Kwa hiyo, hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote asemalo kuhusu manabii: “Nitawafanya wale chakula kichungu na kunywa maji yaliyotiwa sumu, kwa sababu kutokana na manabii wa Yerusalemu kutokumcha Mungu kumeenea katika nchi yote.”

Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote asemalo: “Msisikilize wanachowatabiria manabii, wanawajaza matumaini ya uongo. Wanasema maono kutoka katika akili zao wenyewe, hayatoki katika kinywa cha BWANA. Huendelea kuwaambia wale wanaonidharau mimi kwamba, BWANA asema: ‘Mtakuwa na amani.’ Kwa wale wote wafuatao ugumu wa mioyo yao husema, ‘Hakuna dhara litakalowapata.’

Hasira ya BWANA haitageuka mpaka amelitimiza kusudi la moyo wake. Siku zijazo mtalifahamu kwa wazi. Mimi sikuwatuma manabii hawa, lakini bado wamekimbia wakitangaza ujumbe wao. Mimi sikusema nao, lakini wametabiri.

“Nimesikia wanayoyasema manabii, hao wanaotabiri uongo kwa Jina langu. Wanasema, ‘Nimeota ndoto! Nimeota ndoto!’ Mambo haya yataendelea mpaka lini ndani ya mioyo ya hawa manabii wa uongo, ambao hutabiri maono ya uongo ya akili zao wenyewe? Wanadhani ndoto wanazoambiana wao kwa wao zitawafanya watu wangu walisahau Jina langu, kama baba zao walivyolisahau Jina langu kwa kumwabudu Baali. Mwache nabii aliye na ndoto aseme ndoto yake, lakini yule aliye na neno langu na aliseme kwa uaminifu. Kwa maana jani kavu lina uhusiano gani na ngano?” asema BWANA. “Je, neno langu si kama moto,” asema BWANA, “na kama nyundo ivunjayo mwamba vipande vipande?

“Naam, mimi niko kinyume na manabii wanaotikisa ndimi zao wenyewe na kusema, ‘BWANA asema.’ Kweli, niko kinyume na hao wanaotabiri ndoto za uongo,” asema BWANA. “Wanazisimulia na kuwapotosha watu wangu kwa uongo wao bila kujali, lakini sikuwatuma wala sikuwaweka. Hawawafaidii watu hawa hata kidogo,” asema BWANA.

Kwa habari ya nabii, kuhani, au wale watu wasemao, ‘Mzigo wa BWANA,’ nitawaadhibu wao na nyumba zao. Hivyo mtaambiana kila mmoja na mwenzake, miongoni mwenu: ‘BWANA amejibu nini?’ au ‘BWANA amesema nini?’ Lakini kamwe msiseme tena, ‘Nina mzigo wa BWANA,’ kwa sababu kila neno la mtu binafsi linakuwa mzigo wake mwenyewe na hivyo kupotosha maneno ya Mungu aliye hai, BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wetu.

Ingawa unadai, ‘Huu ni mzigo wa BWANA,’ hili ndilo BWANA asemalo: Ulitumia maneno, ‘Huu ndio mzigo wa BWANA,’ hata ingawa nilikuambia kuwa kamwe usiseme, ‘Huu ni mzigo wa BWANA.’ Kwa hiyo, hakika nitakusahau na kukutupa mbali na uso wangu pamoja na mji niliowapa ninyi na baba zenu. Nitaleta juu yako fedheha ya kudumu na aibu ya kudumu ambayo haitasahaulika.”

Kwa hiyo msiwasikilize manabii wenu, waaguzi wenu, waota ndoto wenu, watabiri na wachawi wanaowaambia ninyi, ‘Hamtamtumikia mfalme wa Babeli.’ Wanawatabiria ninyi uongo ambako kutawafanya ninyi mhamishwe mbali kutoka kwenye nchi yenu, nitawafukuzia mbali nanyi mtaangamia.

Msiyasikilize maneno ya manabii wanaowaambia kwamba, ‘Hamtamtumikia mfalme wa Babeli,’ kwa sababu wanawatabiria uongo. ‘Sikuwatuma hao,’ asema BWANA. ‘Wanatabiri uongo kwa Jina langu. Kwa hiyo, nitawafukuzia mbali nanyi mtaangamia, ninyi pamoja na manabii wanaowatabiria.’ ” Kisha nikawaambia makuhani na watu wote hawa, “Hili ndilo asemalo BWANA: Msiwasikilize manabii wanaosema, ‘Hivi karibuni sana vyombo vya nyumba ya BWANA vitarudishwa kutoka Babeli.’ Wanawatabiria ninyi uongo.

Naam, hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Msikubali manabii na wabashiri walioko miongoni mwenu wawadanganye. Msisikilize ndoto ambazo mmewatia moyo kuota. Wanawatabiria ninyi uongo kwa Jina langu. Sikuwatuma,” asema BWANA.

“Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea; wachungaji wao wamewapotosha na kuwasababisha kuzungukazunguka juu ya milima. Walitangatanga juu ya mlima na kilima na kusahau mahali pao wenyewe pa kupumzikia.

Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ na wewe usipomwonya mtu huyo au kumshauri aache njia zake mbaya ili kuokoa maisha yake, huyo mtu mwovu atakufa katika dhambi yake na damu yake nitaidai mkononi mwako. Lakini ukimwonya mtu mwovu naye akakataa kuacha uovu wake na njia zake mbaya, atakufa katika dhambi yake, lakini wewe utakuwa umejiokoa nafsi yako. “Tena, mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda maovu, nami nikaweka kikwazo mbele yake mtu huyo atakufa. Kwa kuwa hukumwonya, atakufa katika dhambi yake. Mambo ya haki aliyotenda, hayatakumbukwa, damu yake nitaidai mkononi mwako. Lakini ukimwonya mwenye haki asitende dhambi na akaacha kutenda dhambi, hakika ataishi kwa sababu alipokea maonyo na utakuwa umejiokoa nafsi yako.”

Kwa maana hapatakuwepo tena na maono ya uongo wala ubashiri wa udanganyifu miongoni mwa watu wa Israeli.

Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, tabiri dhidi ya manabii wa Israeli wanaotabiri sasa. Waambie hao ambao hutabiri kutokana na mawazo yao wenyewe: ‘Sikia neno la BWANA! Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ole wao manabii wapumbavu wafuatao roho yao wenyewe na wala hawajaona cho chote!

Manabii wako, Ee Israeli ni kama mbweha katikati ya magofu. Hamjakwea kwenda kuziba mahali palipobomoka katika ukuta ili kuukarabati kwa ajili ya nyumba ya Israeli, ili kwamba isimame imara kwenye vita katika siku ya BWANA. Maono yao ni ya uongo na ubashiri wao ni wa udanganyifu. Wao husema, “BWANA amesema,” wakati BWANA hakuwatuma, bado wakitarajia maneno yao kutimizwa. Je, hamjaona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu hapo msemapo, “BWANA asema,” lakini Mimi sijasema?

“ ‘Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ya uongo wa maneno yenu na kwa madanganyo ya maono yenu, Mimi ni kinyume na ninyi, asema BWANA Mwenyezi.

Mkono wangu utakuwa dhidi ya manabii ambao huona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu. Hawatakuwa katika baraza la watu wangu au kuandikwa katika kumbukumbu ya nyumba ya Israeli wala hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA Mwenyezi. “ ‘Kwa sababu ni kweli wanapotosha watu wangu, wakisema, “Amani,” wakati ambapo hakuna amani, pia kwa sababu, wakati ukuta dhaifu unapojengwa, wanaufunika kwa kupaka chokaa, kwa hiyo waambie hao wanaoupaka chokaa isiyokorogwa vyema kwamba ukuta huo utaanguka. Mvua kubwa ya mafuriko itanyesha, nami nitaleta mvua ya mawe inyeshe kwa nguvu, nao upepo wa dhoruba utavuma juu yake. Wakati ukuta utakapoanguka, je, watu hawatawauliza, “Iko wapi chokaa mliyopaka ukuta?” “ ‘Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Katika ghadhabu yangu nitauachia upepo wa dhoruba, pia katika hasira yangu mvua ya mawe na mvua ya mafuriko itanyesha ikiwa na ghadhabu ya kuangamiza. Nitaubomoa ukuta mlioupaka chokaa na kuuangusha chini ili msingi wake uachwe wazi. Utakapoanguka, mtaangamizwa ndani yake, nanyi mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA. Hivyo ndivyo nitakavyoitimiza ghadhabu yangu dhidi ya huo ukuta na dhidi yao walioupaka chokaa. Nitawaambia ninyi, “Ukuta umebomoka na vivyo hivyo wale walioupaka chokaa, wale manabii wa Israeli waliotabiri juu ya Yerusalemu na kuona maono ya amani kwa ajili yake wakati kulipokuwa hakuna amani, asema BWANA Mwenyezi.” ’

“Sasa, mwanadamu, kaza uso wako dhidi ya binti za watu wako wanaotabiri mambo kutoka katika mawazo yao wenyewe. Tabiri dhidi yao

Kwa sababu mliwavunja moyo wenye haki kwa uongo wenu, wakati mimi sikuwaletea huzuni na kwa kuwa mliwatia moyo waovu ili wasiziache njia zao mbaya na hivyo kuokoa maisha yao, kwa hiyo hamtaona tena maono ya uongo wala kufanya ubashiri. Nitawaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu. Nanyi ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ ”

Manabii wake wanapaka chokaa matendo haya kwa maono ya uongo na utabiri wa udanganyifu. Wanasema, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo,’ wakati BWANA hajasema.

“ ‘Kwa hiyo, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Kwa sababu unafikiri una hekima, mwenye hekima kama mungu, mimi nitawaleta wageni dhidi yako, taifa katili kuliko yote; watafuta panga zao dhidi ya uzuri wa hekima yako, na kuchafua fahari yako inayong'aa.

naye auonapo upanga unakuja dhidi ya nchi na kupiga tarumbeta kuonya watu, kama mtu ye yote asikiapo sauti ya tarumbeta hakukubali kuonywa, basi upanga ujapo na kuutoa uhai wake, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisikia sauti ya tarumbeta lakini hakukubali maonyo, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. Kama angekubali maonyo, angelijiokoa mwenyewe. Lakini kama mlinzi akiona upanga unakuja na asipige tarumbeta kuonya watu na upanga ukija na kutoa uhai wa mmoja wao, yule mtu ataondolewa kwa sababu ya dhambi yake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwa mlinzi huyo.’

“Mwanadamu, nimekufanya wewe kuwa mlinzi kwa ajili ya nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo na uwape maonyo kutoka kwangu. Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Ewe mtu mwovu, hakika utakufa,’ nawe hukusema neno la kumwonya ili atoke katika njia zake, yule mtu mwovu atakufa kwa ajili ya dhambi yake, mimi nitaitaka damu yake mkononi mwako. Lakini kama utamwonya huyo mtu mwovu aache njia zake mbaya naye hafanyi hivyo, atakufa kwa ajili ya dhambi yake, lakini utakuwa umejiokoa mwenyewe.

Nami kama nikimwambia mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ kisha akageuka kutoka katika dhambi yake na kufanya lile lililo haki na sawa, kama akirudisha kile alichochukuwa rehani kwa ajili ya deni, akarudisha alichoiba na kufuata amri zile ziletazo uzima, wala hafanyi uovu, hakika ataishi, hatakufa.

“Lakini watu wako wanasema, ‘Njia ya Bwana si sawa.’ Lakini ni njia zao ambazo si sawa. Kama mtu mwenye haki akigeuka kutoka katika uadilifu wake na kufanya uovu, atakufa kwa ajili ya huo uovu. Naye mtu mwovu kama akigeuka kutoka katika uovu wake na kufanya lile lililo haki na sawa, kwa kufanya hivyo ataishi. Lakini, Ee nyumba ya Israeli, unasema, ‘Njia ya Bwana si sawa.’ Lakini nitamhukumu kila mmoja wenu sawasawa na njia zake mwenyewe.”

“Mwanadamu, tabiri juu ya wachungaji wa Israeli, tabiri na uwaambie: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ole wa wachungaji wa Israeli ambao hujitunza wenyewe tu! Je, haiwapasi wachungaji kutunza kundi la kondoo? Mnakula mafuta ya wanyama, mnavaa mavazi ya sufu na kuchinja kondoo walionona, lakini hamlitunzi kundi. Hamkuwatia nguvu walio dhaifu wala hamkuwaganga wenye maradhi wala kuwafunga waliojeruhiwa. Hamkuwarudisha waliotangatanga wala kuwatafuta wale waliopotea. Badala yake mmewatawala kwa ukali na kwa ukatili. Hivyo walitawanyika kwa sababu hapakuwepo mchungaji, nao walipotawanyika, wakawa chakula cha wanyama wa mwitu wote. Kondoo wangu walitawanyika, wakatangatanga kwenye milima yote na kwenye kila kilima kirefu. Kondoo wangu walitawanyika juu ya uso wa dunia yote bila kuwa na ye yote wa kuwaulizia wala wa kuwatafuta.

Kwa hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, kwa sababu kondoo zangu wamekosa mchungaji na hivyo wametekwa nyara na kuwa chakula cha wanyama wote wa mwituni na kwa sababu wachungaji wangu, hawakuwatafuta kondoo zangu, bali wachungaji wamejitunza wenyewe, nao hawakuwalisha kondoo zangu, kwa hiyo enyi wachungaji, sikieni neno la BWANA: Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mimi ni kinyume na wachungaji nami nitawadai kondoo zangu mikononi mwao. Nitawafukuza kutoka kwenye kuchunga kundi langu, ili wachungaji wasiendelee kujitunza wenyewe. Nitaokoa kondoo zangu kutoka kwenye vinywa vyao, nao kondoo hawatakuwa tena chakula chao.

“ ‘Kwa habari yenu, enyi kundi langu, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo, kati ya kondoo waume na mbuzi.

“ ‘Kwa hiyo, hili ndilo BWANA Mwenyezi awaambialo: Tazama, mimi mwenyewe nitahukumu kati ya kondoo wanono na waliokonda. Kwa sababu mmewapiga kikumbo na kuwapiga kwa pembe zenu kondoo wote walio dhaifu mpaka wakawafukuza, nitaliokoa kundi langu na hawatatekwa nyara tena. Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo.

Ulijigamba dhidi yangu na kusema maneno dhidi yangu bila kujizuia, nami nikayasikia.

watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa, “Kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeacha kuijali sheria ya Mungu wako mimi nami sitawajali watoto wako.

wa watu wangu. Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti nao hujibiwa na fimbo ya mti. Roho ya ukahaba imewapotosha, hawana uaminifu kwa Mungu wao.

Hili ndilo asemalo BWANA: “Kuhusu manabii wanaowapotosha watu wangu, mtu akiwalisha, wanatangaza ‘amani’; kama hakufanya hivyo, wanaandaa kupigana vita dhidi yake. Kwa hiyo usiku utawajieni, msiweze kuwa na maono, na giza, msiweze kubashiri. Jua litawachwea manabii hao, nao mchana utakuwa giza kwao. Waonaji wataaibika na waaguzi watafedheheka. Wote watafunika nyuso zao kwa sababu hakuna jibu litokalo kwa Mungu.”

Viongozi wake wanahukumu kwa rushwa, na makuhani wake wanafundisha kwa malipo, nao manabii wake wanatabiri kwa fedha. Hata hivyo wanamwegemea BWANA na kusema, “Je, BWANA si yumo miongoni mwetu? Hakuna maafa yatakayotupata.”

Haya ndiyo mtakayoyafanya: Semeni kweli kila mtu kwa mwenzake, mtoe hukumu ya kweli na haki kwenye mahakama zenu, usipange mabaya dhidi ya jirani yako, msipende kuapa kwa uongo, nayachukia yote haya,” asema BWANA.

Sanamu huzungumza udanganyifu, waaguzi huona maono ya uongo; husimulia ndoto ambazo si za kweli, wanatoa faraja batili. Kwa hiyo watu wanatangatanga kama kondoo walioonewa kwa kukosa mchungaji.

“Ole wa mchungaji asiyefaa, anayeliacha kundi! Upanga na uupige mkono wake na jicho lake la kuume! Mkono wake na unyauke kabisa, jicho lake la kuume lipofuke kabisa!”

“Katika siku hiyo, nitayakatilia mbali majina ya sanamu kutoka nchi, nayo hayatakumbukwa tena,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. “Nitaondoa manabii wao pamoja na roho ya uchafu katika nchi. Ikiwa yupo ye yote atakayeendelea kutabiri, baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Ni lazima ufe, kwa sababu umesema uongo kwa jina la BWANA.’ Atakapotabiri, wazazi wake mwenyewe watampasua tumbo. “Katika siku hiyo, kila nabii ataaibika kwa maono ya unabii wake. Hatavaa vazi la kinabii la nywele ili apate kudanganya watu. Atasema, ‘Mimi sio nabii. Mimi ni mkulima; ardhi imekuwa kazi yangu tangu ujana wangu.’

“Kwa maana yapasa midomo ya kuhani kuhifadhi maarifa. Tena kutoka kinywani mwake watu wangepaswa kutafuta mafundisho, kwa sababu yeye ni mjumbe wa BWANA Mwenye Nguvu Zote. Lakini mmegeuka mkaiacha njia na kwa mafundisho yenu mmesababisha wengi kujikwaa, mmevunja agano na Lawi,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. “Kwa hiyo nimewasababisha ninyi kudharauliwa na kufedheheshwa mbele ya watu wote, kwa sababu hamkufuata njia zangu, bali mmeonyesha upendeleo katika mambo ya sheria.”

Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki, maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao. “Heri ninyi watu watakapowashutumu na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kuu.

“Msidhani kwamba nimekuja kufuta Torati au Manabii, sikuja kuondoa bali kutimiza. Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yo yote kutoka kwenye Torati mpaka kila kitu kiwe kimetimia. Kwa hiyo, ye yote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini ye yote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni.

“Kwa nini unatazama kibanzi kidogo kilichomo kwenye jicho la ndugu yako na wala huoni boriti iliyoko kwenye jicho lako? Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe kibanzi kwenye jicho lako wakati kuna boriti kwenye jicho lako mwenyewe?’ Ewe mnafiki, toa kwanza boriti kwenye jicho lako mwenyewe, nawe ndipo utakapoona wazi ili kuondoa kibanzi kilichoko kwenye jicho la ndugu yako. “Msiwape mbwa vitu vilivyo vitakatifu, wala msitupie nguruwe lulu zenu. Kama mkifanya hivyo, watazikanyaga-kanyaga na kisha watawageukia na kuwararua vipande vipande.

“Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo. Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.

“Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa mwitu wakali.

Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Hivyo kwa matunda yao mtawatambua.

“Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

Mtu ye yote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini ye yote anenaye neno dhidi ya Roho Mtakatifu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao.

Hii ndiyo sababu nasema nao kwa mifano: “Ingawa wanatazama, hawaoni, wanasikiliza, lakini hawasikii wala hawaelewi. Kwao unatimia ule unabii wa Isaya aliposema: “ ‘Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa, na pia mtatazama lakini hamtaona.

“Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi: Mtu ye yote anaposikia neno la Ufalme, naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake, hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia. Ile mbegu iliyopandwa kwenye sehemu yenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na mara hulipokea kwa furaha. Lakini kwa kuwa hana mizizi yenye kina ndani yake, lile neno hukaa kwa muda mfupi. Inapotokea dhiki au mateso kwa ajili ya hilo neno, yeye mara huchukizwa. Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno, lakini masumbufu ya dunia na ushawishi wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda. Lakini ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika hutoa matunda, akizaa mara mia, au mara sitini, au mara thelathini ya mbegu iliyopandwa.”

Yesu akawajibu, “Mbona ninyi mnavunja amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu?

“ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami. Kuniabudu kwao ni bure, nayo mafundisho yao ni maagizo ya wanadamu tu.’ ”

Akawajibu, “Kila pando ambalo Baba yangu wa mbinguni hakulipanda, litang'olewa. Waacheni, wao ni viongozi vipofu, wanaoongoza vipofu. Kama kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, wote wawili watatumbukia shimoni.”

Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” Ndipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi juu ya chachu ya kutengeneza mikate, bali juu ya mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.

Lakini Yesu akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

“Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako. Lakini kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno lithibitishwe na ushahidi wa mashahidi wawili au watatu. Kama akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa, naye kama akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi mtendeeni mtu huyo kama vile ambavyo mngemtendea asiyeamini.

Lakini Yesu akijua makusudi yao mabaya akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega?

Kisha Yesu akauambia ule umati wa watu pamoja na wanafunzi wake: “Walimu wa sheria na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Mose, hivyo inawapasa kuwatii na kufanya kila kitu wanachowaambia. Lakini msifuate yale wanayotenda, kwa sababu hawatendi yale wanayohubiri. Wao hufunga mizigo mikubwa na kuiweka mabegani mwa watu, lakini wao wenyewe hawako radhi hata kuinua kidole ili kuisogeza. “Wao hutenda mambo yao yote ili waonekane na watu. Hufanya vikasha vya ngozi vyenye maandiko ya sheria na kurefusha matamvua ya mavazi yao,

wanapenda kukaa viti vya sehemu za heshima karamuni na vile viti maalum sana katika masinagogi, hupenda kusalimiwa masokoni na kutaka watu wawaite ‘Rabi.’ “Lakini ninyi msiitwe ‘Rabi’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu. Nanyi msimwite mtu ye yote ‘Baba,’ hapa duniani kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni. Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Kristo. Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu. Kwa kuwa ye yote anayejikweza atashushwa na ye yote anayejinyenyekeza atakwezwa.

“Lakini ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Kwa maana mnawafungia watu milango ya Ufalme wa Mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii humo, nao wale wanaotaka kuingia mnawazuia. [ Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Mnakula katika nyumba za wajane, nanyi kwa kujifanya kuwa wema, mnasali sala ndefu. Kwa hiyo adhabu yenu itakuwa kubwa zaidi.] “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Ninyi mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja ageuke na kuwafuata ninyi, lakini baada ya kumpata, mnamfanya mwana wa jehanamu mara mbili kuliko ninyi!

“Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani, haki, huruma na uaminifu. Haya imewapasa kuyafanya bila kusahau hayo mengine. Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia! “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha nje ya kikombe na kisahani, lakini ndani mmejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. Enyi Mafarisayo vipofu! Safisheni kwanza ndani ya kikombe na kisahani, ndipo nje patakuwa safi. “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo yanapendeza kwa nje lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. Vivyo hivyo, kwa nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.

“Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya wenye haki. Nanyi mwasema, ‘Kama tungaliishi wakati wa baba zetu, tusingalikuwa tumeshiriki katika kumwaga damu ya manabii!’ Hivyo mnajishuhudia wenyewe kwamba ninyi ni wana wa wale waliowaua manabii. Haya basi, kijazeni kipimo cha dhambi ya baba zenu! “Ninyi nyoka, ninyi uzao wa nyoka wenye sumu! Mtaiepukaje hukumu ya jehanamu? Kwa sababu hii tazama nawapelekea manabii na wenye hekima na walimu. Baadhi yao mtawaua na kuwasulibisha, wengine mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na wengine mtawafuatia kutoka mji mmoja hadi mji mwingine. Hivyo ile damu ya wenye haki wote iliyomwagwa hapa duniani, tangu damu ya Abeli, ambaye alikuwa hana hatia, hadi damu ya Zekaria mwana wa Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu, itawajia juu yenu.

Yesu akawajibu, “Angalieni, mtu asiwadanganye. Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’ nao watawadanganya wengi.

Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa,

Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo na kufanya ishara kubwa na miujiza mingi ili kuwapotosha, hata ikiwezekana wale wateule hasa. Angalieni, nimetangulia kuwaambia mapema.

Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Kwa sababu hii, enendeni ulimwenguni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.” Amen.

Yule mpanzi hupanda neno. Hawa ndio wale walio kando ya njia, ambako neno lilipandwa. Walisikiapo neno, Shetani huja mara na kulichukua lile neno lililopandwa ndani yao. Nazo hizi ni zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye miamba, wanapolisikia neno, mara hulipokea kwa furaha. Basi kwa kuwa hawana mizizi, hudumu kwa muda mfupi tu, kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, wao mara huiacha imani. Lakini wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye miiba, hulisikia lile neno, lakini masumbufu ya maisha haya, udanganyifu wa mali na tamaa ya mambo mengine huja na kulisonga lile neno na kulifanya lisizae. Wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri, hulisikia lile neno, wakalipokea na kutoa mazao: Wengine thelathini, wengine sitini na wengine mara mia moja ya ile iliyopandwa.”

Yesu akawajibu, “Nabii Isaya alisema ukweli alipotabiri juu yenu, ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa: “ ‘Watu hawa wananiheshimu kwa midomo yao, lakini mioyoni mwao wako mbali nami. Huniabudu bure, wakifundisha mapokeo ya wanadamu.’

Ninyi mmeziacha amri za Mungu na kushika desturi za watu.” Naye akawaambia, “Ninyi mnayo njia nzuri ya kukataa amri za Mungu ili mpate kuzishika desturi zenu!

Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara na maajabu ili kuwapotosha, ikiwezekana hata wale wateule. Hivyo jihadharini, nimekwisha kuwaambia mambo haya yote mapema kabla hayajatukia.

Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

Yesu akajibu akamwambia, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno la Mungu.’ ”

Ole wenu watu watakapowasifu, kwani ndivyo baba zao walivyowasifu manabii wa uongo.

Pia akawapa mfano akasema, “Je, kipofu aweza kumwongoza kipofu? Je, wote wawili hawatatumbukia shimoni? Mwanafunzi hamzidi mwalimu wake, ila yule aliyehitimu aweza kuwa kama mwalimu wake.

“Maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu. Zile zilizoanguka kando ya njia, ni wale ambao husikia neno na ibilisi huja na kuliondoa kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka. Zile za kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa kitambo kidogo, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani. Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui. Lakini zile mbegu kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu na wa utii, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.

Kwa maana hakuna jambo lo lote lililofichika ambalo halitafichuliwa, wala lo lote lililositirika ambalo halitajulikana na kuwekwa wazi. Kwa hiyo, iweni waangalifu mnavyosikia. Kwa maana ye yote aliye na kitu atazidishiwa na ye yote asiye nacho, hata kile anachodhani anacho atanyang'anywa.”

Lakini ni rahisi zaidi mbingu na nchi kupita kuliko hata herufi moja kuondoka katika Sheria.

Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa. Maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai kwamba, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati umekaribia.’ Msiwafuate.

Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.”

Lakini Yesu hakujiaminisha kwao kwa sababu aliwajua wanadamu wote. Hakuhitaji ushuhuda wa mtu ye yote kuhusu mtu, kwa kuwa alijua yote yaliyokuwa moyoni mwa mtu.

Ye yote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakumwamini Mwana pekee wa Mungu. Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe.

Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Watu wanaoabudu namna hii, ndio Baba anawatafuta. Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

Ndipo Yesu akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma. Mtu ye yote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe.

Je, Mose hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?” Ule umati wa watu ukamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?”

Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”

Kisha Yesu akasema nao tena akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu ye yote akinifuata hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”

Kisha Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli. Ndipo mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru.”

Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho. Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo.

Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.”

Yesu akasema, “Nimekuja ulimwenguni humu kwa ajili ya kuhukumu, ili wale walio vipofu wapate kuona, nao wale wanaoona, wawe vipofu.” Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa karibu naye wakamsikia na kumwambia, “Je, kweli sisi ni vipofu?” Yesu akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu kweli, msingekuwa na hatia ya dhambi, lakini kwa kuwa mnasema, ‘Tunaona,’ basi mna hatia.

“Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, ni mwivi na mnyang'anyi. Yeye anayeingia kwa kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo. Mlinzi humfungulia lango na kondoo huisikia sauti yake. Huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi. Akiisha kuwatoa wote nje, hutangulia mbele yao na kondoo humfuata kwa kuwa wanaijua sauti yake. Lakini kondoo hawatamfuata mgeni bali watamkimbia, kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.”

Mtu wa kuajiriwa ambaye kondoo si mali yake, amwonapo mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo na mbwa mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya. Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo.

Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini. Hii ilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema: “Bwana, ni nani aliyesadiki ujumbe wetu na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?” Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine: “Amewafanya vipofu na kuifanya mioyo yao kuwa migumu, ili wasiweze kuona kwa macho yao, wala kuelewa kwa mioyo yao, wasije wakageuka, nami nikawaponya.”

Yuko amhukumuye yeye anikataaye mimi na kutokuyapokea maneno yangu, yaani, yale maneno niliyosema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho.

Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu.

“Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu.

Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu.

Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.

“Lakini atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, yaani, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi.

Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo.

Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndilo kweli.

Petro akamwuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.”

“Ninyi watu wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, daima hamwachi kumpinga Roho Mtakatifu, kama walivyofanya baba zetu.

Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.

Najua kwamba baada mimi kuondoka, mbwa mwitu wakali watakuja katikati yenu ambao hawatalihurumia kundi. Hata kutoka miongoni mwenu wenyewe watainuka watu na kuupotosha ukweli ili wawavute wanafunzi wawafuate. Hivyo jilindeni! Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuacha kamwe kuwaonya, kila mmoja kwa machozi usiku na mchana.

uyafumbue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni na kutoka kwenye nguvu za Shetani, wamgeukie Mungu ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini mimi.’

Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao,

Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, umeonekana waziwazi ukitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru. Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza.

Ingawa wakijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga

Kwa sababu waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen.

Kwa maana si wale wanaoisikia sheria ambao ni wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale wanaoitii sheria ndio watakaohesabiwa haki.

La hasha! Mungu na aonekane mwenye haki na kila mwanadamu kuwa mwongo, kama ilivyoandikwa: “Ili uweze kujulikana kuwa na haki katika maneno yako, nawe ukashinde katika hukumu.”

Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu, hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu. Wote wamegeukia mbali, wote kwa pamoja hawafai; hakuna atendaye mema, naam, hata mmoja.” “Makoo yao ni makaburi wazi; kwa ndimi zao hufanya udanganyifu.” “Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.”

Hivyo basi, sheria yenyewe ni takatifu na amri ni takatifu na ya haki, tena ni njema.

Ninasema kweli katika Kristo, wala sisemi uongo, dhamiri yangu inanishuhudia katika Roho Mtakatifu.

Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wanajuhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa. Kwa kuwa hawakuijua haki itokayo kwa Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu. Kwa maana Kristo ni ukomo wa sheria ili kuwe na haki kwa kila mtu aaminiye.

Basi, imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo.

kama ilivyoandikwa: “Mungu aliwapa bumbuazi la mioyo, macho ili wasiweze kuona na masikio ili wasiweze kusikia, hadi leo.”

Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake.

Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza. Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana Kristo, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga.

Kwa kuwa katika hekima ya Mungu, ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa wale waaminio kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. Wayahudi wanataka miujiza na Wayunani wanatafuta hekima, lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulibiwa, ambaye kwa Wayahudi ni kitu cha kukwaza na kwa Wayunani ni upuzi. Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi pia Wayunani, Kristo ni nguvu na hekima ya Mungu. Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.

Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu. Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu cho chote wakati nikiwa nanyi isipokuwa Yesu Kristo, naye amesulibiwa msalabani. Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana. Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya kuwashawishi watu, bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho Mtakatifu ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.

Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika. Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika kwa wanadamu, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu. Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati zetu aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangelielewa, wasingemsulibisha Bwana wa utukufu.

Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho yule atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure. Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa wale watu wa kiroho.

Mtu ambaye hana Roho wa Mungu hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa jinsi ya rohoni. Mtu wa kiroho hutambua mambo yote, lakini yeye mwenyewe hatambuliwi na mtu ye yote. “Kwa maana ni nani aliyejua nia ya Bwana ili apate kumfundisha?” Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.

Kwa maana hakuna mtu ye yote awezaye kuweka msingi mwingine wo wote isipokuwa ule uliokwisha kuwekwa, ambao ni Yesu Kristo.

Msijidanganye. Kama mtu ye yote miongoni mwenu akidhani kuwa ana hekima kwa viwango vya dunia hii, inampasa awe mjinga ili apate kuwa na hekima. Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuzi mbele za Mungu. Kama ilivyoandikwa: “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao,” Tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni ubatili.”

Basi je, thawabu yangu ni nini? Thawabu yangu ni hii: Ni kwamba katika kuhubiri Injili niitoe bila gharama, nisije nikatumia vibaya ule uwezo wangu nilio nao katika Injili.

Wala tusimjaribu Bwana, kama baadhi yao walivyofanya, wakafa kwa kuumwa na nyoka.

Kama mtu anataka kubishana juu ya jambo hili, sisi wala makanisa ya Mungu hatutambui desturi nyingine.

Kwanza, mnapokutana kama kanisa, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo. Bila shaka lazima pawe na tofauti miongoni mwenu ili kuonyesha ni nani anayekubaliwa na Mungu.

Kwa hiyo, mtu ye yote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana. Inampasa mtu ajichunguze mwenyewe, kabla ya kula mkate na kukinywea kikombe. Kwa maana mtu ye yote alaye na kunywa pasipo kuutambua mwili wa Bwana, anajiletea hukumu juu yake mwenyewe. Hii ndiyo sababu wengi miongoni mwenu ni wagonjwa na dhaifu na wengine wenu hata wamekufa. Lakini kama tungejipambanua wenyewe tusingehukumiwa. Tunapohukumiwa na Bwana, tunaadabishwa ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.

Lakini ndani ya kanisa ni afadhali niseme maneno matano ya kueleweka kwa akili ili niwafundishe wengine kuliko kusema maneno 10,000 kwa lugha. Ndugu zangu, msiwe kama watoto katika kufikiri kwenu, afadhali kuhusu uovu mwe kama watoto wachanga, lakini katika kufikiri kwenu, mwe watu wazima. Katika sheria imeandikwa kwamba: “Kwa kupitia watu wenye lugha ngeni na kupitia midomo ya watu wageni, nitasema na watu hawa, lakini hata hivyo hawatanisikiliza,” asema Bwana.

Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani. Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu, wanawake wanapaswa kuwa kimya kanisani. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama sheria isemavyo. Kama wakitaka kuuliza kuhusu jambo lo lote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza kanisani. Je, neno la Mungu lilianzia kwenu? Au ni ninyi tu ambao neno la Mungu limewafikia? Kama mtu ye yote akidhani kwamba yeye ni nabii, au ana karama za rohoni, basi na akubali kwamba haya ninayoandika ni maagizo kutoka kwa Bwana. Kama mtu akipuuza jambo hili yeye mwenyewe atapuuzwa.

Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama. Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili.

Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.” Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.

ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatuachi kuzijua hila zake.

Lakini Mungu ashukuriwe, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Kristo. Naye kwa kupitia sisi hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye. Kwa maana sisi kwa Mungu ni harufu nzuri ya manukato ya Kristo miongoni mwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea, sisi kwa wale wanaopotea ni harufu ya mauti iletayo mauti, lakini kwa wale wanaookolewa sisi ni harufu nzuri iletayo uzima. Ni nani awezaye mambo hayo? Tofauti na watu wengine wengi, sisi hatufanyi biashara na Neno la Mungu kwa ajili ya kupata faida. Kinyume chake, katika Kristo tunalisema Neno la Mungu kwa unyofu, kama watu tuliotumwa kutoka kwa Mungu.

Yeye ndiye aliyetuwezesha sisi kuwa wahudumu wa Agano Jipya: si wa andiko, bali wa Roho; kwa kuwa andiko huua bali Roho hutia uzima.

Lakini akili zao zilipumbazwa, kwa maana mpaka leo utaji ule ule hufunika wakati Agano la Kale lisomwapo. Huo utaji haujaondolewa kwa maana ni katika Kristo peke yake unaondolewa. Hata leo, Torati ya Mose isomwapo, utaji hufunika mioyo yao. Lakini wakati wo wote mtu anapomgeukia Bwana, “utaji unaondolewa.”

Tumekataa mambo ya siri na ya aibu, wala hatufuati njia za udanganyifu, tukichanganya Neno la Mungu na uongo. Kinyume cha hayo, tunadhihirisha kweli waziwazi na kujitambulisha wenyewe kwenye dhamiri ya kila mtu mbele za Mungu. Hata nayo Injili yetu kama imetiwa utaji, ni kwa wale tu wanaopotea. Kwa habari yao, mungu wa dunia hii amepofusha akili za wasioamini, ili wasione nuru ya Injili ya utukufu wa Kristo, aliye sura ya Mungu.

Silaha za vita vyetu si za mwili, Bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome. Tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo, tena tukiwa tayari kuadhibu kila tendo la kutokutii, kutii kwenu kutakapokamilika.

Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo. Kwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi.

Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo. Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.

Jichunguzeni wenyewe mwone kama mnaishi katika imani. Jipimeni wenyewe. Je, hamtambui ya kuwa Yesu Kristo yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi, mmeshindwa kufikia kipimo hicho!

Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo yeye aliyewaita kwa neema ya Kristo na kuifuata injili nyingine, ambayo kwa kweli si injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo.

Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele! Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu ye yote atawahubiria injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele!

Je, sasa mimi ninatafuta kukubaliwa na wanadamu au kukubaliwa na Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa bado najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumishi wa Kristo. Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu. Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo.

Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, wapate kututia utumwani, hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili kwamba ukweli wa Injili ubaki nanyi.

Lakini Petro alipofika Antiokia, mimi nilimpinga ana kwa ana kwa sababu alikuwa amekosea kwa wazi. Kabla baadhi ya watu waliotoka kwa Yakobo hawajafika, alikuwa akila pamoja na watu Mataifa. Lakini hao watu walipofika alianza kujiondoa na kujitenga na watu Mataifa kwa sababu aliwaogopa wale wa kundi la tohara. Pia Wayahudi wengine waliungana naye katika unafiki huu, hata Barnaba naye akapotoshwa na unafiki wao. Nilipoona kwamba hawatendi sawasawa na kweli ya Injili, nilimwambia Petro mbele ya wote, “Wewe ni Myahudi, nawe unaishi kama mtu Mataifa na wala si kama Myahudi. Imekuwaje basi, mnawalazimisha watu Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi?

Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaloga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulibiwa.

Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejezeni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo. Kama mtu ye yote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe.

Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote. Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. Apandaye kwa mwili, katika mwili wake, atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo.

Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao. Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao.

Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja.

Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao.

Mtu ye yote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama haya juu ya wale wasiomtii.

Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, lakini sasa ninyi ni nuru katika Bwana. Enendeni kama watoto wa nuru (kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli), nanyi tafuteni yale yanayompendeza Bwana.

Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni.

Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani. Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu.

Haya ndiyo maombi yangu kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote, ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Kristo,

Nawaambia mambo haya ili mtu ye yote asiwadanganye kwa maneno ya kuwashawishi.

Angalieni mtu ye yote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu ambayo siyo ya Kristo.

Mtu ye yote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kumnyenyekea yeye na kuabudu malaika, akidumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu,

Kwa kuwa mlikufa pamoja na Kristo, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kama vile ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri: “Msishike! Msionje! Msiguse!”? Haya yote mwisho wake ni kuharibika yanapotumiwa, kwa sababu huo msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu. Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hayafai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.

Msiambiane uongo kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, nanyi mmevaa utu mpya unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake.

Jaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema.

Mtu ye yote na asiwadanganye kwa namna yo yote kwa maana siku ile haitakuja mpaka uasi utokee kwanza na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa.

Kuja kwa yule mwasi kutaonekana kana kwamba ni kutenda kazi kwake Shetani ambaye hutumia nguvu zote, ishara, maajabu ya uongo na kila aina ya udanganyifu kwa wale wanaoangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli wapate kuokolewa. Kwa sababu hii, Mungu ameruhusu watawaliwe na nguvu ya udanganyifu, ili waendelee kuamini uongo na hivyo wote wahukumiwe ambao hawakuamini ule ukweli bali wamefurahia uovu.

Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua.

Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa.

Kama nilivyokusihi kuendelea kubaki Efeso, wakati nilipokwenda Makedonia, ili kwamba upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha zisizo na mwisho za majina ya vizazi ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Kimungu utokanao na imani. Kusudi la maagizo haya ni upendo, utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli. Watu wengine wamepotoka kutoka katika haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa, wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.

anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli. Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani, mwanadamu Kristo Yesu, aliyejitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake. Nami kwa kusudi hili nimewekwa niwe mhubiri na mtume (nasema kweli katika Kristo wala sisemi uongo), mwalimu wa watu Mataifa katika imani na kweli.

Mwanamke na ajifunze kwa utulivu na kwa utii wote. Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume. Mwanamke inampasa kukaa kimya. Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza, kisha Eva. Wala si Adamu aliyedanganywa, bali ni mwanamke aliyedanganywa akawa mkosaji.

Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani. Mafundisho kama hayo huja kwa kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto.

Kama ukiwakumbusha ndugu mambo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, uliyelelewa katika kweli ya imani na yale mafundisho mazuri uliyoyafuata. Usijishughulishe kamwe na hadithi za kipagani na masimulizi ya uongo ya wanawake wazee, badala yake, jizoeze kuwa mtauwa.

Mambo haya yaagize na kuyafundisha. Mtu ye yote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waaminio katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi. Fanya bidii kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. Usiache kutumia kipawa kilicho ndani yako, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee walipokuwekea mikono. Uwe na bidii katika mambo haya, jitolee kwa ajili ya mambo hayo kikamilifu, ili kila mtu aone kuendelea kwako. Jilinde sana nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika hayo, kwa maana kwa kufanya hivyo utajiokoa wewe mwenyewe pamoja na wale wanaokusikia.

Wazee wa kanisa wanaoongoza shughuli za kanisa vizuri wanastahili heshima mara mbili, hasa wale ambao kazi yao ni kuhubiri na kufundisha. Kwa maana Maandiko husema, “Usimfunge ng'ombe kinywa apurapo nafaka,” tena, “Mfanyakazi anastahili mshahara wake.”

Usiendekeze mashtaka dhidi ya mzee isipokuwa yawe yameletwa na mashahidi wawili au watatu. Wale wanaodumu katika dhambi uwakemee hadharani, ili wengine wapate kuogopa. Ninakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu na mbele za malaika wateule, shika maagizo haya pasipo ubaguzi wala upendeleo. Usiwe na haraka kumwekea mtu mikono wala usishiriki dhambi za watu wengine. Jilinde nafsi yako uwe safi.

Ikiwa mtu ye yote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa, huyo amejivuna wala hajui kitu cho chote. Yeye ni mgonjwa aliyejaa tamaa ya mabishano na ugomvi ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.

Timotheo, linda kile kilichowekwa amana kwako. Epuka majadiliano yasiyo ya utauwa na mabishano ambayo kwa uongo huitwa elimu, ambayo wengine kwa kujidai kuwa nayo wameiacha imani. Neema iwe nanyi. Amen.

Endelea kuwakumbusha mambo haya ukiwaonya mbele za Bwana waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yo yote bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia.

Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtenda kazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli. Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu.

Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kuwako na kupotosha baadhi ya watu. Lakini msingi wa Mungu ulio madhubuti umesimama ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Bwana anawajua walio wake” tena, “Kila alitajaye jina la Bwana auache uovu.”

Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.

Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wapendao anasa zaidi kuliko kumpenda Mungu. Wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu wa namna hiyo.

Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya. Wakijifunza siku zote lakini kamwe wasiweze kufikia ujuzi wa kweli.

Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Mose, vivyo hivyo watu hawa hupingana na ile kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani. Lakini hawataendelea sana, kwa sababu upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama ulivyokuwa dhahiri upumbavu wa hao watu wawili.

Naam, ye yote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Kristo Yesu atateswa. Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.

Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kuwaongoza na kuwafundisha katika haki ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, ili apate kutenda kila kazi njema.

Uhubiri Neno, uwe tayari wakati ufaao na wakati usiofaa, karipia, kemea na kuonya kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri. Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima, badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia. Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo.

Inampasa alishike kwa uthabiti lile neno la imani kama lilivyofundishwa, kusudi aweze kuwafundisha wengine kwa mafundisho manyofu na kuwakanusha wale wanaopingana nayo. Kwa maana wako wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, hasa wale wa kikundi cha tohara. Hao ni lazima wanyamazishwe, kwa sababu wanaharibu watu wa nyumba nzima wakifundisha mambo yasiyowapasa kufundisha. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia mapato ya udanganyifu. Hata mmojawapo wa manabii wao mwenyewe amesema “Wakrete ni waongo siku zote, wanyama wabaya, walafi, wavivu.” Ushuhuda huu ni kweli. Kwa hiyo, uwakemee kwa ukali wapate kuwa wazima katika imani, ili wasiendelee kuangalia hadithi za Kiyahudi au maagizo ya wale watu wanaoikataa kweli. Kwa wale walio safi, kila kitu ni safi kwao. Lakini kwa wale waliopotoka na wasioamini, hakuna cho chote kilicho safi. Kwa kweli nia zao na dhamiri zao zimepotoka. Wanadai kumjua Mungu, lakini kwa matendo yao wanamkana. Hao watu ni chukizo, wasiotii, wasiofaa kwa jambo lo lote jema.

Lakini kwa habari yako wewe, inakupasa kufundisha kulingana na mafundisho yenye uzima. Wafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi.

Vivyo hivyo wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa unyenyekevu unaostahili utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema, ili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao, wawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu ye yote asije akalikufuru neno la Mungu.

Vivyo hivyo, sisitiza vijana wawe na kiasi. Katika kila jambo wewe mwenyewe uwe kielelezo cha matendo mema na katika mafundisho yako uonyeshe unyofu, utaratibu, ukweli na maneno yenye uzima, yale ambayo hayawezi kulaumiwa, hata wale wenye kukupinga watahayari, wakose neno lo lote baya la kusema juu yetu.

Wafundishe watumwa kuwatii mabwana zao katika kila jambo, wakijitahidi kuwapendeza wala wasijibizane nao, wala wasiwaibie, bali watumwa waonyeshe kuwa wanaweza kuaminika kabisa, ili kwamba kwa kila namna wayafanye mafundisho ya Mungu Mwokozi wetu kuwa ya kupendeza.

Lakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu haya hayana faida tena ni ubatili. Mtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena. Kwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe.

Kwa hiyo, imetupasa kuwa waangalifu sana kuhusu kile tulichosikia, ili tusije tukakiacha. Kwa kuwa ujumbe ulionenwa na malaika ulikuwa imara na kila uasi na kutokutii kulipata adhabu ya haki, je, sisi tutapaje kupona kama tusipojali wokovu mkuu namna hii? Wokovu huu, ambao mwanzo ulitangazwa na Bwana, kisha ulithibitishwa kwetu na wale waliomsikia.

Ndugu zangu, angalieni, asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai.

Ni nani hao ambao Mungu aliapa kuwa kamwe hawataingia rahani mwake isipokuwa ni wale waliokataa kutii? Hivyo tunaona kwamba hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu tena lina makali kuliko upanga uwao wote wenye makali kuwili, tena linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe cho chote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye kwake ni lazima tutatoa hesabu.

Kwa kuwa ni vigumu kuwarejeza tena katika toba wale ambao wakati fulani walishapata nuru, ambao walishaonja kipawa cha mbinguni, ambao wamekwisha kushiriki katika Roho Mtakatifu, wale ambao wameonja uzuri wa Neno la Mungu na nguvu za wakati ujao, kisha wakaanguka, kwa kuwa kwa nafsi zao wanamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili na kumdhalilisha hadharani.

Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao utakaowaangamiza adui za Mungu. Ye yote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema?

Angalieni sana mtu ye yote asiikose neema ya Mungu na kwamba shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo. Angalieni miongoni mwenu asiwepo mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, ambaye kwa ajili ya mlo mmoja aliuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza. Mnajua kwamba baadaye kama mnavyofahamu, alipotaka kurithi ile baraka, alikataliwa, maana hakupata nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.

Msichukuliwe na kila aina ya mafundisho ya kigeni. Ni vyema mioyo yenu iimarishwe kwa neema, wala si kwa sheria kuhusu utaratibu wa vyakula, ambavyo havina faida kwa wale wanaozishika hizo sheria.

kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu cho chote. Kama mtu ye yote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa.

Basi iweni watendaji wa Neno wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu. Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na mara husahau jinsi alivyo.

Ndugu zangu, msiwe walimu wengi, kwa maana mnafahamu kwamba sisi tufundishao tutahukumiwa vikali zaidi. Sisi sote tunajikwaa katika mambo mengi. Ikiwa mtu ye yote hakosei kamwe katika yale anayosema, yeye ni mkamilifu, naye anaweza kuuzuia pia na mwili wake wote.

Vivyo hivyo ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini hujivuna majivuno makuu. Fikirini jinsi moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa! Ulimi pia ni moto, ndio ulimwengu wa uovu kati ya viungo vya mwili. Ulimi huutia mwili wote wa mtu unajisi na kuuwasha moto mfumo mzima wa maisha yake, nao wenyewe huchomwa moto wa jehanamu.

Kwenu ninyi mnaoamini, yeye ni wa thamani. Lakini kwao wasioamini, “Jiwe lile walilolikataa waashi limekuwa Jiwe Kuu la pembeni,” tena, “Jiwe lenye kuwafanya watu wajikwae, mwamba wa kuwafanya waanguke.” Wanajikwaa kwa sababu hawakulitii lile neno: kama walivyowekewa tangu zamani.

Kwa maana, “Ye yote apendaye uzima na kuona siku njema, basi auzuie ulimi wake usinene mabaya na midomo yake isiseme hila.

Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu ye yote atakayewauliza kuhusu tumaini lililomo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima, mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo, waaibike kwa ajili ya masingizio yao.

Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi, kama simba angurumaye huzungukazunguka akitafuta mtu ili apate kummeza. Mpingeni huyo mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso yayo hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

Awali ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe. Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama vile watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu, ambao kwa siri, wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli hata kumkana Bwana wa pekee aliyewanunua na kujiletea juu yao maangamizi ya haraka. Hata hivyo, wengi watafuata njia zao za ufisadi ambao kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa. Nao katika tamaa zao mbaya, watajipatia faida kwenu kwa maneno ya madanganyo waliyotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, ambayo haikawii wala uangamivu wao haujalala usingizi.

Kwa kuwa kama wameukimbia upotovu wa dunia kwa kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo, kisha wakanaswa tena humo na kushindwa, hali yao ya mwisho ni mbaya zaidi kuliko ile ya kwanza. Ingelikuwa afadhali kwao kama wasingeliijua kamwe njia ya haki, kuliko kuijua kisha wakaiacha ile amri takatifu waliyokabidhiwa.

Huandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha kwa maangamizi yao wenyewe, kama wapotoshavyo pia Maandiko mengine.

Basi, ninyi wapenzi, kwa kuwa mmekwisha kujua mambo haya, jilindeni msije mkachukuliwa na kosa la watu hao waasi na kuanguka kutoka kwenye uthabiti wenu. Bali kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na milele! Amen.

Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lo lote. Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli.

Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua kama tunazishika amri zake. Mtu ye yote asemaye kuwa, “Ninamjua” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli. Lakini kama mtu ye yote analitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake. Ye yote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.

Ninawaandikia mambo haya kuhusu wale watu ambao wanajaribu kuwapotosha. Kwa habari yenu ninyi, upako ule mlioupata kutoka kwake unakaa ndani yenu, wala ninyi hamna haja ya mtu ye yote kuwafundisha. Lakini kama vile upako wake unavyowafundisha kuhusu mambo yote nayo ni kweli wala si uongo, basi kama ulivyowafundisha kaeni ndani yake.

Wapenzi, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho mwone kama zimetoka kwa Mungu, kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea ulimwenguni. Hivi ndivyo mnavyoweza kutambua Roho wa Mungu: Kila roho inayokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatoka kwa Mungu. Lakini kila roho ambayo haimkubali Yesu haitoki kwa Mungu. Hii ndiyo roho ya mpinga Kristo, ambayo mmesikia kwamba inakuja na sasa tayari iko ulimwenguni.

Wao wanatokana na ulimwengu na kwa hiyo hunena yaliyo ya ulimwengu, hivyo ulimwengu huwasikiliza. Sisi twatokana na Mungu na ye yote anayemjua Mungu hutusikiliza, lakini asiyetokana na Mungu hatusikilizi. Hivi ndivyo tunavyoweza kutambua Roho wa Kweli na roho ya upotovu.

Hili ndilo pendo, kwamba tuenende sawasawa na amri zake. Hii ndiyo amri yake kama vile mlivyosikia tangu mwanzo, kwamba mwenende katika upendo.

Wadanganyifu wengi, wasiokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili, wametokea ulimwenguni. Mtu wa namna hiyo ni mdanganyifu na mpinga Kristo. Jihadharini msije mkapoteza kile mlichokitenda, bali mpate kupewa thawabu kamilifu.

Mtu ye yote asiyedumu katika mafundisho ya Kristo, bali akayaacha, yeye hana Mungu. Ye yote anayedumu katika mafundisho ana Baba na Mwana pia. Msimpokee mtu ye yote anayewajia ambaye hawaletei mafundisho haya, wala msimkaribishe nyumbani mwenu. Ye yote amkaribishaye mtu wa namna hiyo anashiriki katika matendo maovu ya mtu huyo.

Nililiandikia kanisa, lakini Deotrefe, yeye apendaye kujifanya wa kwanza, hakubali mamlaka yetu. Hivyo kama nikija, nitakumbuka matendo yake atendayo, akitusingizia kwa maneno ya hila. Wala hatosheki na hayo anayotusingizia, bali pia hukataa kuwakaribisha ndugu na hata huwazuia wale walio tayari kufanya hivyo na kuwafukuza watoke kanisani.

Wapenzi, ingawa nilikuwa ninatamani sana kuwaandikia kuhusu wokovu ambao tunaushiriki sisi sote, niliona imenipasa kuwaandikia na kuwasihi kwamba mwishindanie imani iliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. Kwa kuwa kuna watu waliojipenyeza kwa siri katikati yenu, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, waovu, wapotoshao neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi wakimkana yeye aliye Bwana wetu wa pekee, Bwana Yesu Kristo.

Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo.

Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, wao ni sinagogi la Shetani.

“Hata hivyo, nina mambo machache dhidi yako: Unao watu wafuatao mafundisho ya Balaamu, yule aliyemfundisha Balaki kuwashawishi Waisraeli watende dhambi kwa kula vitu vilivyotolewa kafara kwa sanamu na kufanya uasherati. Vivyo hivyo unao wale wayashikao mafundisho ya Wanikolai. Basi tubuni! Ama sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga wa kinywa changu.

“Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu.

Nayajua matendo yako, ya kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungelikuwa baridi au moto. Hivyo kwa kuwa u uvuguvugu, kwamba wewe si baridi wala si moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu. Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu cho chote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi.

“Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu.

Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwenguni wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake. Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema: “Sasa Wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja na mamlaka ya Kristo wake. Kwa kuwa ametupwa chini mshtaki wa ndugu zetu, anayewashtaki mbele za Mungu usiku na mchana. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo na kwa neno la ushuhuda wao. Wala wao hawakuyapenda maisha yao hata kufa.

Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema: “Tokeni katikati yake, enyi watu wangu, ili msije mkashiriki dhambi zake, ili msije mkapatwa na pigo lake lo lote;

Mwanga wa taa hautaangaza ndani yako tena. Sauti ya bwana arusi na bibi arusi kamwe haitasikiwa ndani yako tena. Wafanyabiashara wako walikuwa watu maarufu wa dunia. Mataifa yote yalipotoshwa kwa uchawi wako.

Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo ambaye alikuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.

Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ndiye ibilisi na Shetani, naye akamfunga kwa muda wa miaka 1,000. Akamtupa katika lile Shimo lisilo na mwisho, akamfunga humo na kulitia lakiri, ili kumzuia asiendelee kudanganya mataifa mpaka hiyo miaka 1,000 itimie. Baada ya hayo lazima afunguliwe kwa muda mfupi.

Naye ibilisi aliyewadanganya akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti walikokuwa wametupwa yule mnyama na yule nabii wa uongo. Watateswa humo mchana na usiku, milele na milele.

Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

Lakini kitu kichafu hakitaingia humo kamwe, wala mtu ye yote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali watakaoingia humo ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.

Huko nje wako mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabuduo sanamu na kila mtu apendaye udanganyifu na kuufanya.

Namwonya kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Mtu ye yote akiongeza humo cho chote, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Kama mtu ye yote akipunguza humo cho chote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.

Swahili - Kiswahili - SW

NEN'2014 - Neno Bibilia Takatifu Kiswahili Contemporary Version - 2014

This Bible text is from Biblica Open Kiswahili Contemporary Version Neno 2015
https://open.bible/bibles/swahili-biblica-text-bible/
provided by: Biblica Inc, available by Creative Commons CC-BY-SA-4.0,
and this new compilation is shared as www.creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0.
Languages are made available to you by www.ipedge.net