23 – Upendo

Haya ni maneno matakatifu ya Mungu Mwenyezi.
Hatupendi maneno ya wanadamu.
Kwa mtu yeyote anayempenda Mungu... hivi ndivyo Mungu anasema kuhusu: Upendo.

Mistari 3 Muhimu Zaidi

“Lakini nawaambia wale wanaonisikia, wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. Kama mtu akikupiga shavu moja mgeuzie na la pili. Mtu akikunyang'anya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia.

Wapenzi na tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu. Kila apendaye amezaliwa na Mungu naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa hamjui Mungu, kwa sababu Mungu ni pendo. Hivi ndivyo Mungu alivyoonyesha pendo lake kwetu, kwa sababu Mungu alimtuma Mwanawe wa pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba tulimpenda Mungu, bali yeye alitupenda, akamtuma Mwanawe, ili yeye awe dhabihu ya kipatanisho kwa ajili ya dhambi zetu. Wapenzi, kama Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana.

“Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake, hata kama akiacha uchaji wa Mwenyezi.

Kila Mstari katika Mpangilio wa Biblia - 326 vifungu

Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.

Kwa hiyo Yakobo akatumika miaka saba ili kumpata Raheli, lakini ilionekana kwake kama siku chache tu kwa sababu ya upendo wake kwa Raheli.

Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa BWANA Mungu wako.

Usiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wake au punda wake, wala cho chote kile alicho nacho jirani yako.”

“Kama ukikutana na maksai au punda wa adui yako anapotea, hakikisha umemrudisha kwake. Ukiona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, usimwache hapo alipoangukia; hakikisha kuwa umemsaidia.

BWANA akapita mbele ya Mose, akitangaza, “BWANA, BWANA, Mungu mwenye huruma na neema, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa upendo na uaminifu,

“ ‘Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Karipia jirani yako kwa uwazi ili usishiriki hatia yake. “ ‘Usijilipizie kisasi wala kuwa na kinyongo dhidi ya mmoja wa jamaa yako, lakini mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi BWANA.

Mgeni anayeishi pamoja nawe ni lazima umtendee kama mmoja wa wazawa wa nchi yako. Mpende kama unavyojipenda mwenyewe, kwa maana ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi BWANA Mungu wako.

“ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini naye akashindwa kujitegemeza mwenyewe katikati yako, msaidie kama vile ambavyo ungelimsaidia mgeni au kama mkazi wa muda, ili aweze kuendelea kuishi katikati yako. Usichukue riba wala faida yo yote kutoka kwake, bali utamwogopa Mungu wako, ili kwamba mzawa wa nchi yako aweze kuendelea kuishi katikati yako. Usimkopeshe fedha ili alipe na riba, wala usimwuzie chakula kwa faida.

(Basi Mose alikuwa mtu mnyenyekevu sana, mnyenyekevu kuliko mtu mwingine ye yote katika uso wa dunia.)

Mpende BWANA Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa nguvu zako zote.

Basi ujue kwamba BWANA Mungu wako ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayetunza Agano la upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaompenda na kuzishika amri zake. Lakini kwa wale wanaomchukia atawalipiza kwenye nyuso zao kwa maangamizi; hatachelewa kuwalipiza kwenye nyuso zao wale wamchukiao.

Huwapigania yatima na wajane, humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi. Nanyi wapendeni wageni, kwa kuwa ninyi wenyewe mlikuwa wageni huko Misri.

Mpende BWANA Mungu wako na kushika masharti yake, amri zake, sheria zake na maagizo yake siku zote.

Hivyo kama mkiyatii maagizo yangu ninayowapa leo kwa uaminifu, yaani kwa kumpenda BWANA Mungu wenu, na kumtumikia kwa moyo wako wote na kwa roho yenu yote,

kamwe msiyasikilize maneno ya nabii wala mwota ndoto huyo. BWANA Mungu wenu anawajaribu kuangalia kama mnampenda kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote.

Mpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili BWANA Mungu wenu atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako. Siku zote watakuwepo watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe na mikono iliyokunjuliwa kuwaelekea ndugu zenu, kuwaelekea maskini na wahitaji katika nchi yenu.

Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi ambavyo BWANA Mungu wenu alivyowabariki.

BWANA Mungu wako ataitairi mioyo yenu na mioyo ya wazao wenu ili mweze kumpenda kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote ukaishi.

na ili upate kumpenda BWANA Mungu wako, uisikilize sauti yake na kuambatana naye. Kwa kuwa BWANA ndiye uzima wako, na atakupa wingi wa siku ili upate kuishi katika nchi aliyoapa kuwapa baba zako Abrahamu, Isaki na Yakobo.

Lakini mwe waangalifu sana kushika amri na sheria zile Mose mtumishi wa BWANA alizowapa: yaani kumpenda BWANA Mungu wenu na kuenenda katika njia zake zote, kutii amri zake, kushikamana naye kwa uthabiti na kumtumikia kwa moyo wenu wote na roho yenu yote.”

“Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi, kwa kuwa BWANA ndiye Mungu ajuaye, na kwa yeye matendo hupimwa.

Baada ya Daudi kumaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi, naye akampenda kama nafsi yake mwenyewe. Kuanzia siku ile Sauli akamchukua Daudi naye hakumruhusu kurudi nyumbani kwa baba yake. Yonathani akafanya agano na Daudi kwa sababu alimpenda kama nafsi yake mwenyewe. Yonathani akavua joho alilokuwa amevaa na kumpa Daudi, pamoja na koti lake, silaha zake, hata pamoja na upanga wake, upinde wake na mshipi wake.

Baada ya mvulana kwenda, Daudi akainuka kutoka upande wa kusini wa lile jiwe, naye akasujudu uso wake mpaka nchi mara tatu mbele ya Yonathani. Kisha kila mmoja akambusu mwenzake, wakalia pamoja. Lakini Daudi akalia zaidi sana. Yonathani akamwambia Daudi, “Nenda kwa amani, kwa kuwa tumeapiana kiapo cha urafiki kati yetu kwa jina la BWANA, tukisema, ‘BWANA ndiye shahidi kati yako na mimi, na kati ya wazao wako na wazao wangu milele.’ ” Kisha Daudi akaondoka, naye Yonathani akarudi mjini.

“Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake, hata kama akiacha uchaji wa Mwenyezi.

Kumbuka, Ee BWANA, rehema zako kuu na upendo, kwa maana zimekuwapo tangu zamani. Usizikumbuke dhambi za ujana wangu wala njia zangu za uasi, sawasawa na upendo wako unikumbuke, kwa maana wewe ni mwema, Ee BWANA.

Huwaongoza wanyenyekevu katika haki, naye huwafundisha njia yake.

Njia zote za BWANA ni za upendo na aminifu kwa wale wanaoshika Agano na shuhuda zake.

Mpendeni BWANA ninyi watakatifu wake wote! BWANA huwahifadhi waaminifu, lakini wenye kiburi huwalipiza kikamilifu.

Upendo wako, Ee BWANA, unafika hadi katika mbingu, uaminifu wako hadi kwenye anga. Haki yako ni kama milima mikubwa, hukumu zako ni kama kilindi kirefu sana. Ee BWANA, wewe huwahifadhi mwanadamu na mnyama. Upendo wako usiokoma ni wa thamani mno! Wale wa daraja ya juu na ya chini miongoni mwa wanadamu hupata kimbilio katika uvuli wa mbawa zako.

Ee BWANA, usizuilie huruma zako, upendo wako na kweli yako daima vinilinde.

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi) Heri mtu yule anayemjali mnyonge, BWANA atamwokoa wakati wa shida. BWANA atamlinda na kuyahifadhi maisha yake, atambariki katika nchi na hatamwacha katika tamaa ya adui zake. BWANA atamtegemeza awapo mgonjwa kitandani, atamwinua kutoka kitandani mwake.

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi Baada Ya Kukemewa Na Nabii Nathani Kwa Kuzini Na Bathsheba) Ee Mungu, unihurumie, kwa kadiri ya upendo wako usiokoma, kwa kadiri ya huruma yako kuu uyafute makosa yangu.

Ee BWANA, unijibu, kwa wema wa upendo wako; kwa huruma zako nyingi unigeukie.

Ee BWANA, wewe ni mwema na mwenye kusamehe, umejaa upendo kwa wote wakuitao.

Lakini wewe, Ee BWANA, ni Mungu wa huruma na neema, si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo na uaminifu.

Kila amsingiziaye jirani yake kwa siri, huyo nitamnyamazisha; mwenye macho ya dharau na moyo wa kiburi sitamvumilia.

BWANA ni mwenye huruma na rehema, si mwepesi wa hasira, amejaa upendo. Yeye hatalaumu siku zote, wala haweki hasira yake milele, yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu. Kama vile mbingu zilivyo juu sana juu ya dunia, ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha; kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi.

Lakini kutoka milele hata milele upendo wa BWANA uko kwa wale wamchao, nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao:

Mshukuruni BWANA, kwa kuwa yeye ni mwema, upendo wake wadumu milele.

Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu, kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema.

Kwa kuwa upendo wake kwetu ni mkuu, uaminifu wa BWANA unadumu milele. Msifuni BWANA.

(Wimbo Wa Kwenda Juu. Wa Daudi) Tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza wakati ndugu wanapoishi pamoja katika umoja!

Mshukuruni Mungu wa mbinguni, Fadhili zake zadumu milele.

BWANA ni mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo. BWANA ni mwema kwa wote, ana huruma kwa vyote alivyovifanya.

BWANA huwahifadhi wanyenyekevu lakini huwashusha waovu mpaka mavumbini.

Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe; vifunge shingoni mwako, viandike katika ubao wa moyo wako.

Kunywa maji kutoka kwenye kisima chako mwenyewe, maji yanayotiririka kutoka kwenye kisima chako mwenyewe. Je, chemchemi zako zifurike katika barabara za mji na vijito vyako vya maji viwanjani? Na viwe vyako mwenyewe, kamwe visishirikishwe wageni. Chemchemi yako na ibarikiwe na umfurahie mke wa ujana wako. Kulungu jike apendaye, kulungu mzuri, matiti yake na yakutosheleze siku zote, nawe utekwe daima na upendo wake. Kwa nini mwanangu, utekwe na mwanamke kahaba? Kwa nini ukumbatie kifua cha mke wa mwanaume mwingine?

Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA, naam, viko saba vilivyo chukizo kwake: macho ya kiburi, ulimi udanganyao, mikono imwagayo damu isiyo na hatia, moyo ule uwazao mipango miovu, miguu ile iliyo myepesi kukimbilia uovu, shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.

Kumcha BWANA ni kuchukia uovu, ninachukia kiburi na majivuno, tabia mbaya na mazungumzo potovu.

Nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.

Chuki huchochea faraka, lakini upendo husitiri mabaya yote.

Kiburi kinapokuja, ndipo huja aibu, bali unyenyekevu huja na hekima.

Mwanaume mwenye huruma hujinufaisha mwenyewe, bali mwanaume katili hujiletea taabu mwenyewe.

Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi, mwingine huzuia, lakini huwa maskini. Mtu mkarimu atastawi; yeye awaburudishaye wengine ataburudishwa mwenyewe.

Yeye aizuiaye fimbo yake hampendi mwanawe, bali yeye ampendaye huwa mwangalifu kumwadibisha.

Yeye anayemdharau jirani yake hutenda dhambi, bali amebarikiwa yeye aliye na huruma kwa mhitaji.

Yeye amwoneaye maskini huonyesha dharau kwa Muumba wao, bali ye yote anayemhurumia mhitaji humheshimu Mungu.

Jawabu la upole hugeuza ghadhabu, bali neno liumizalo huchochea hasira.

BWANA hubomoa nyumba ya mtu mwenye kiburi, bali huilinda mipaka ya mjane isiguswe.

BWANA huwachukia sana wote wenye kiburi cha moyo. Uwe na hakika kwa hili: Hawataepuka kuadhibiwa. Kwa upendo na uaminifu uovu huondolewa, kwa kumcha BWANA mtu hujiepusha na ubaya.

Kiburi hutangulia maangamizi, roho ya majivuno hutangulia maanguko. Ni afadhali kuwa mnyenyekevu katika roho miongoni mwa walioonewa kuliko kugawana nyara pamoja na wenye kiburi.

Maneno ya kupendeza ni kama sega la asali, ni matamu kwa nafsi na uponyaji kwenye mifupa.

Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo, bali ye yote arudiaye jambo hutenganisha marafiki wa karibu.

Rafiki hupenda wakati wote naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.

Mauti na uzima viko katika uwezo wa ulimi, nao waupendao watakula matunda yake.

Mtu mwenye marafiki wengi wanaweza kumharibu, bali yuko rafiki aambatanaye na mtu kwa karibu kuliko ndugu.

Yeye amhurumiaye maskini humkopesha BWANA, naye atamtuza kwa aliyotenda.

Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho, afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo.

Kufanya yaliyo sawa na haki inakubalika zaidi kwa BWANA kuliko dhabihu. Macho ya kudharau na moyo wa kiburi, ambavyo ni taa ya waovu, vyote ni dhambi!

Kama mtu akizibia masikio kilio cha maskini, yeye pia atalia wala hatajibiwa.

Yeye afuatiaye haki na upendo hupata uzima, mafanikio na heshima.

Yeye alindaye kinywa chake na ulimi wake hujilinda na maafa. Mtu mwenye kiburi na majivuno, “Mdhihaki” ndilo jina lake; hutenda mambo kwa kiburi kilichozidi.

Mtu mkarimu yeye mwenyewe atabarikiwa kwa kuwa hushiriki chakula chake na maskini.

Mfukuze mwenye dhihaka, nayo mashindano yatatoweka; ugomvi na matukano vitakoma. Yeye apendaye moyo safi na yeye ambaye maneno yake ni ya neema, mfalme atakuwa rafiki yake.

Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale, kama ana kiu, mpe maji anywe. Kwa kufanya hivi, unampalia makaa ya moto kichwani pake, naye BWANA atakupa thawabu.

Yeye ampaye maskini hatapungukiwa na kitu cho chote, bali yeye awafumbiaye maskini macho hupata laana nyingi.

Mtu mwenye hasira huchochea ugomvi, naye mtu mwenye hasira ya haraka hutenda dhambi nyingi.

Kiburi cha mtu humshusha, bali mtu mwenye roho ya unyenyekevu hupata heshima.

“Kuna vitu vitatu vinavyonishangaza sana, naam, vinne nisivyovielewa: Ni mwendo wa tai katika anga, mwendo wa nyoka juu ya mwamba, mwendo wa meli katika maji makuu ya bahari, nao mwendo wa mtu pamoja na msichana.

“Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea, kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa. Sema na uamue kwa haki, tetea haki za maskini na wahitaji.”

Usiwe mwepesi kukasirika rohoni mwako, kwa kuwa hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.

Wimbo ulio Bora wa Solomoni. Unibusu kwa busu la kinywa chako, kwa maana upendo wako unafurahisha kuliko divai. Manukato yako yananukia vizuri, jina lako ni kama manukato yaliyomiminwa. Ndiyo sababu wanawali wanakupenda! Nichukue twende nawe, na tufanye haraka! Mfalme na anilete ndani ya vyumba vyake. Tunakushangilia na kukufurahia, tutasifu upendo wako zaidi kuliko divai. Tazama ni jinsi gani ilivyo haki wakupende!

Mpenzi wangu, ninakufananisha na farasi jike aliyefungwa katika mojawapo ya magari ya vita ya Farao. Mashavu yako yanapendeza yakiwa na vipuli, shingo yako ikiwa na mikufu ya vito. Tutakufanyia vipuli vya dhahabu, vyenye kupambwa kwa fedha. Wakati mfalme alipokuwa mezani pake, manukato yangu yasambaza harufu yake nzuri. Mpenzi wangu kwangu mimi ni kifuko cha manemane kati ya matiti yangu. Mpenzi wangu kwangu mimi ni kama kishada cha maua ya mhina yaliyochanua kutoka mashamba ya mizabibu ya En-Gedi. Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu! Tazama jinsi ulivyo mzuri! Macho yako ni kama ya hua. Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu! O, tazama ni jinsi gani unavyopendeza! Na kitanda chetu ni cha majani mabichi mazuri.

Mimi ni ua la waridi la Sharoni, yungiyungi ya bondeni. Mpenzi Kama yungiyungi katikati ya miiba ndivyo alivyo mpenzi wangu katikati ya wanawali. Kama mti wa mtofaa miongoni mwa miti ya msituni ndivyo alivyo mpenzi wangu miongoni mwa wanaume vijana. Ninafurahia kuketi kivulini mwa mwanaume huyu, na tunda lake ni tamu kwangu. Amenichukua mpaka kwenye ukumbi wa karamu, na bendera ya huyu mwanaume juu yangu ni upendo. Nitie nguvu kwa zabibu kavu, niburudishe kwa matofaa, kwa maana ninazimia kwa mapenzi. Mkono wa kushoto uko chini ya kichwa changu, na mkono wake wa kuume unanikumbatia. Binti za Yerusalemu, ninawaagiza kwa paa na kwa ayala wa shambani: Msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe. Sikiliza! Mpenzi wangu! Tazama! Huyu hapa anakuja, akirukaruka juu milimani akizunguka juu ya vilima. Mpenzi wangu ni kama paa au swala kijana. Tazama! Anasimama nyuma ya ukuta wetu, akitazama kupitia madirishani, akichungulia kimiani.

Mpenzi wangu alizungumza na kuniambia, “Inuka, mpenzi wangu, mrembo wangu, tufuatane. Tazama! Wakati wa masika umepita, mvua imekwisha imekwenda zake. Maua yanatokea juu ya nchi; majira ya kuimba yamewadia, sauti za njiwa zinasikika katika nchi yetu. Mtini unatunga matunda yake ya mwanzoni, zabibu zinazochanua zaeneza harufu yake nzuri. Inuka, njoo, mpenzi wangu, mrembo wangu, tufuatane.” Hua wangu penye nyufa za majabali, mafichoni pembezoni mwa mlima, nionyeshe uso wako, na niisikie sauti yako, kwa maana sauti yako ni tamu, na uso wako unapendeza. Tukamatie mbweha, mbweha wadogo wale wanaoharibu mashamba ya mizabibu, mashamba yetu ya mizabibu yaliyochanua. Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake, hujilisha katikati ya yungiyungi. Mpaka jua linapochomoza, na vivuli vikimbie, rudi, mpenzi wangu, na uwe kama paa, au kama ayala kijana juu ya vilima vya Betheri.

Binti za Yerusalemu, ninawaagiza kwa paa na kwa ayala wa shambani: Msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe. Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani kama nguzo ya moshi, anayenukia manemane na uvumba iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote vya mfanyabiashara?

Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu! O, jinsi ulivyo mzuri! Macho yako nyuma ya shela yako ni kama ya hua. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi zikishuka kutoka Mlima Gileadi. Meno yako ni kama kundi la kondoo waliokatwa manyoya sasa hivi, watokao kuogeshwa. Kila mmoja ana pacha lake, hakuna hata mmoja aliye peke yake. Midomo yako ni kama uzi mwekundu, kinywa chako kinapendeza. Mashavu yako nyuma ya shela yako ni kama vipande viwili vya komamanga. Shingo yako ni kama mnara wa Daudi, uliojengwa kwa madaha, juu yake zimetundikwa ngao elfu, zote ni ngao za mashujaa. Matiti yako mawili ni kama wana paa wawili, kama mapacha ya wana paa wale wajilishao katikati ya yungiyungi. Hata papambazuke na vivuli vikimbie, nitakwenda kwenye mlima wa manemane na kwenye kilima cha uvumba. Wewe ni mzuri kote, mpenzi wangu, hakuna hitilafu ndani yako.

Umeiba moyo wangu, dada yangu, bibi arusi wangu; umeiba moyo wangu kwa mtupo mmoja wa macho yako, kwa kito kimoja cha thamani cha mkufu wako. Tazama jinsi pendo lako linavyofurahisha, dada yangu, bibi arusi wangu! Ni mara ngapi zaidi pendo lako linafurahisha kuliko divai, na harufu ya manukato yako zaidi kuliko kikolezo cho chote! Midomo yako inadondosha utamu kama sega la asali, bibi arusi wangu; maziwa na asali viko chini ya ulimi wako. Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ile ya Lebanoni. Wewe ni bustani iliyofungwa, dada yangu, bibi arusi wangu; wewe ni chanzo cha maji kilichozungushiwa kabisa, chemchemi yangu peke yangu. Mimea yako ni bustani ya komamanga yenye matunda mazuri sana, yenye hina na nardo, nardo na zafarani, mchai na mdalasini, pamoja na kila aina ya mti wa uvumba, manemane na udi, na aina zote za vikolezo bora kuliko vyote. Wewe ni chemchemi ya bustani, kisima cha maji yatiririkayo, yatiririkayo kutoka Lebanoni. Amka, upepo wa kaskazini, na uje, upepo wa kusini! Vuma juu ya bustani yangu, ili harufu yake nzuri iweze kuenea mpaka ng'ambo. Mpendwa wangu na aje bustanini mwake na kuonja matunda mazuri sana.

Nimekuja kwenye bustani yangu, dada yangu, bibi arusi wangu; nimekusanya manemane yangu pamoja na kikolezo changu. Nimekula sega langu la asali na asali yangu; nimekunywa divai yangu na maziwa yangu. Kuleni, enyi marafiki, mnywe; kunyweni ya kutosha, Ee wapenzi. Nililala lakini moyo wangu ulikuwa macho. Sikiliza! Mpenzi wangu anabisha: “Nifungulie, dada yangu, mpenzi wangu, hua wangu, asiye na hitilafu. Kichwa changu kimeloa umande, na nywele zangu manyunyu ya usiku.” Nimevua joho langu: je, ni lazima nivae tena? Nimenawa miguu yangu: je, ni lazima niichafue tena? Mpenzi wangu aliweka mkono wake kwenye tundu la komeo; moyo wangu ulianza kugonga kwa ajili yake.

Enyi binti za Yerusalemu, ninawaagiza: kama mkimpata mpenzi wangu, mtamwambia nini? Mwambieni ninazimia kwa mapenzi. Je, mpendwa wako ni bora kuliko wengine namna gani, ni mzuri sana kupita wanawake wote? Je, mpendwa wako ni mzuri kuliko wengine, kwa namna gani, hata unatuagiza hivyo?

Mpenzi wangu anang'aa tena mwekundu kwa afya, wakuvutia miongoni mwa wanaume kumi elfu. Kichwa chake ni dhahabu safi kuliko zote, nywele zake ni za mawimbi na ni nyeusi kama kunguru. Macho yake ni kama ya hua kandokando ya vijito vya maji, aliyeogeshwa kwenye maziwa, yamepangwa kama vito vya thamani. Mashavu yake ni kama matuta ya vikolezo yakitoa manukato. Midomo yake ni kama yungiyungi inayodondosha manemane. Mikono yake ni fimbo za dhahabu iliyopambwa kwa Krisolitho. Mwili wake ni kama pembe ya ndovu iliyong'arishwa iliyopambwa na yakuti samawi. Miguu yake ni nguzo za marmar zilizosimikwa katika vitako vya dhahabu safi. Sura yake ni kama Lebanoni, mzuri kama miti yake ya mierezi. Kinywa chake chenyewe ni utamu, kwa ujumla yeye ni wa kupendeza. Huyu ndiye mpenzi wangu, huyu ndiye rafiki yangu, Ee binti za Yerusalemu.

Mimi ni wake mpenzi wangu, na mpenzi wangu ni wangu mimi; huyu mwanaume hulisha katikati ya yungiyungi.

Uyageuze macho yako mbali nami, yananigharikisha. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi wanaotelemka kutoka Gileadi.

Ee binti wa mwana wa mfalme, tazama jinsi inavyopendeza miguu yako katika viatu! Miguu yako yenye madaha ni kama vito vya thamani, kazi ya mikono ya fundi stadi. Kitovu chako ni kama bilauri ya mviringo ambayo kamwe haikosi divai iliyochanganywa. Kiuno chako ni kichuguu cha ngano kilichozungukwa kwa yungiyungi. Matiti yako ni kama wana paa wawili, mapacha wa swala. Shingo yako ni kama mnara wa pembe ya ndovu. Macho yako ni vidimbwi vya Heshboni karibu na lango la Beth-Rabi. Pua yako ni kama mnara wa Lebanoni ukitazama kuelekea Dameski. Kichwa chako kinakuvika taji kama mlima Karmeli. Nywele zako ni kama zulia nene la kutundika ukutani; mfalme ametekwa na mashungi yake. Tazama jinsi ulivyo mzuri na unavyopendeza, Ee pendo, kwa uzuri wako! Umbo lako ni kama la mtende, nayo matiti yako kama vishada vya matunda. Nilisema, “Nitakwea mtende, nami nitayashika matunda yake.” Matiti yako na yawe kama vishada vya mzabibu, harufu nzuri ya pumzi yako kama matofaa, na kinywa chako kama divai bora kuliko zote. Divai na iende moja kwa moja kwa mpenzi wangu, ikitiririka pole pole juu ya midomo na meno.

Mimi ni mali ya mpenzi wangu, nayo shauku yake ni juu yangu. Njoo, mpenzi wangu, twende mashambani, twende tukalale huko vijijini. Hebu na twende mapema katika mashamba ya mizabibu tuone kama mizabibu imechipua, kama maua yake yamefunguka, pia kama mikomamanga imetoa maua: huko nitakupa penzi langu. Mitunguja hutoa harufu zake nzuri, kwenye milango yetu kuna matunda mazuri, mapya na ya zamani, ambayo nimekuhifadhia wewe, mpenzi wangu.

Mkono wa kushoto wa huyo mwanaume uko chini ya kichwa changu, na mkono wake wa kuume unanikumbatia.

Binti za Yerusalemu, ninawaagiza: msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe. Ni nani huyu anayekuja kutoka nyikani akimwegemea mpenzi wake? Nilikuamsha chini ya mtofaa, huko mama yako alipotunga mimba yako, huko yeye alipata utungu akakuzaa.

Nitie kama muhuri moyoni mwako, kama muhuri kwenye mkono wako; kwa maana upendo una nguvu kama mauti, wivu wake ni mkatili kama kuzimu. Unachoma kama mwali wa moto, kama mwali mkubwa wa moto wa BWANA hasa. Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, mito haiwezi kuugharikisha. Kama mtu angelitoa mali yote ya nyumbani mwake kwa ajili ya upendo, angelidharauliwa kabisa.

Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa na kiburi cha wanadamu kitashushwa, BWANA peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo. BWANA Mwenye Nguvu Zote anayo siku aliyoiweka akiba kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi, kwa wote wanaojikweza (nao watanyenyekezwa),

Lakini mtu mwungwana hufanya mipango ya kiungwana na kwa matendo ya kiungwana yeye hufanikiwa.

Niliwapa mgongo wangu wale wanipigao, mashavu yangu wale wang'oao ndevu zangu; sikuuficha uso wangu kutokana na fedheha na kutemewa mate.

Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso. Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika alichukua udhaifu wetu na akajitwika huzuni zetu, hata hivyo tulifikiri amepigwa na Mungu, amepigwa sana naye na kuteswa. Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu, alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu; adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake, na kwa majeraha yake sisi tumepona. Sisi sote, kama kondoo, tumepotea, kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe, naye BWANA aliweka juu yake maovu yetu sisi sote. Alionewa na kuteswa, hata hivyo hakufungua kinywa chake; aliongozwa kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, kama vile kondoo anyamazavyo mbele yake yeye amkataye manyoya, hivyo hakufungua kinywa chake.

Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi, unapomwona aliye uchi, umvike, wala si kumkimbia mtu wa nyama na damu yako mwenyewe?

nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu na kutosheleza mahitaji ya walioonewa, ndipo nuru yenu itakapong'aa gizani, nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.

Nitasimulia juu ya wema wa BWANA, kwa ajili ya matendo ambayo kwayo apaswa kusifiwa, sawasawa na yote ambayo BWANA ametenda kwa ajili yetu: naam, mambo mengi mema aliyoyatenda kwa ajili ya nyumba ya Israeli, sawasawa na huruma zake na wema wake mwingi.

BWANA alitutokea wakati uliopita akisema: “Nimekupenda kwa upendo wa milele, nimekuvuta kwa wema.

Kwa sababu ya upendo mkuu wa BWANA hatuangamii, kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe. Ni mpya kila asubuhi, uaminifu wako ni mkuu.

Nikamwomba BWANA Mungu wangu na kutubu: “Ee Bwana, Mungu mkuu na unayetisha, anayeshika Agano lake la upendo kwao wanaompenda na kutii maagizo yake,

Nitakuposa uwe wangu milele; nitakuposa kwa uadilifu na haki, kwa upendo na huruma. Nitakuposa kwa uaminifu, nawe utamkubali BWANA.

Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu. BWANA anataka nini kwako? Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.

Mtafuteni BWANA, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi, ninyi ambao hufanya lile analoamuru. Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu; labda mtahifadhiwa siku ya hasira ya BWANA.

BWANA Mungu wako yu pamoja nawe, yeye ni mwenye nguvu kuokoa. Atakufurahia kwa furaha kubwa, atakutuliza kwa pendo lake, atakufurahia kwa kuimba.”

“Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: ‘Fanyeni hukumu za haki, onyesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’

“Heri walio maskini wa roho, maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao. Heri wale wanaohuzunika, maana hao watafarijiwa. Heri walio wapole, maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watatoshelezwa. Heri wenye huruma, maana hao watapata rehema. Heri walio na moyo safi, maana hao watamwona Mungu. Heri walio wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki, maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao. “Heri ninyi watu watakapowashutumu na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kuu.

Lakini mimi nawaambia kwamba, ye yote atakayemkasirikia ndugu yake wa kiume au wa kike, atapaswa hukumu. Tena, ye yote atakayemwambia ndugu yake wa kiume au wa kike, ‘Raca’, yaani kumdharau na kumdhihaki, atapaswa kufanyiwa baraza. Lakini ye yote atakayesema ‘Wewe mpumbavu ulaaniwe!’ Atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu. “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, iache sadaka yako hapo, mbele ya madhabahu, uende kwanza ukapatane na ndugu yako wa kiume au wa kike, kisha urudi na ukatoe sadaka yako.

“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia, Kama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua shati lako, mwachie achukue na koti pia. Kama mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.

“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ Lakini mimi ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Kama mkiwapenda wale wanaowapenda tu, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? Kwa hiyo iweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

“Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni. “Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.

Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe na ninyi pia. Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

“Hakuna mtu ye yote awezaye kuwatumikia mabwana wawili, kwa kuwa ama atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau huyu mwingine. Ninyi hamwezi kumtumikia Mungu na Mali.

“Usihukumu ili usije ukahukumiwa. Kwa maana kwa jinsi ile unavyowahukumu wengine, ndivyo utakavyohukumiwa na kwa kipimo kile utakachotoa ndicho utakachopokea. “Kwa nini unatazama kibanzi kidogo kilichomo kwenye jicho la ndugu yako na wala huoni boriti iliyoko kwenye jicho lako? Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe kibanzi kwenye jicho lako wakati kuna boriti kwenye jicho lako mwenyewe?’ Ewe mnafiki, toa kwanza boriti kwenye jicho lako mwenyewe, nawe ndipo utakapoona wazi ili kuondoa kibanzi kilichoko kwenye jicho la ndugu yako.

Kwa hiyo cho chote ambacho mnataka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Torati na Manabii.

“Njoni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni. Kwa hiyo mtu ye yote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni.

“Mwaonaje? Ikiwa mtu anao kondoo mia moja na mmoja wao akapotea, hatawaacha wale tisini na tisa vilimani na kwenda kumtafuta huyo mmoja aliyepotea? Naye akisha mpata, amin, nawaambia, hufurahi zaidi kwa ajili ya huyo kondoo mmoja kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea. Vivyo hivyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmojawapo wa hawa wadogo apotee.

“Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako.

Ndipo Petro akamjia Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?” Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

waheshimu baba yako na mama yako na umpende jirani yako kama nafsi yako.”

Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

“Vivyo hivyo, wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”

Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, ye yote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, Naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu ni lazima awe mtumwa wenu, kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’

Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu. Kwa kuwa ye yote anayejikweza atashushwa na ye yote anayejinyenyekeza atakwezwa.

“Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njoni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu, urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’ “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu wakisema, ‘Bwana, ni lini tulikuona una njaa tukakulisha au ukiwa na kiu tukakunywesha? Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha au ukiwa uchi tukakuvika? Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’ “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin, amin ninawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’

“Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’ “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’ “Naye atawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’

mwanamke mmoja alimjia akiwa na chupa ya marumaru yenye manukato ya thamani kubwa, akayamimina kichwani mwa Yesu alipokuwa ameketi mezani kula chakula.

Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi akaomba, akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniepuke, lakini si kama nitakavyo mimi bali kama utakavyo wewe.”

Akaketi, akawaita wote kumi na wawili akawaambia: “Kama mtu ye yote akitaka kuwa wa kwanza hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”

Lakini sivyo kwenu. Badala yake ye yote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu na ye yote anayetaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa mtumwa wa wote. Kwa kuwa hata Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake kuwa ukombozi kwa ajili ya wengi.”

Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni, mkiwa na neno na mtu ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.”

Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote na kwa nguvu zako zote.’ Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Yule mwalimu wa sheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja wala hakuna mwingine ila yeye. Kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa akili zote na kwa nguvu zote na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora zaidi kuliko kutoa sadaka ya kuteketezwa na dhabihu.”

Yesu alipokuwa huko Bethania nyumbani kwa Simoni aliyekuwa na ukoma, wakati alipokuwa ameketi mezani akila chakula cha jioni, mwanamke mmoja aliingia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa. Akaivunja hiyo chupa, akamiminia hayo manukato kichwani mwa Yesu.

Yohana akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.”

“Lakini nawaambia wale wanaonisikia, wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. Kama mtu akikupiga shavu moja mgeuzie na la pili. Mtu akikunyang'anya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia. Mpe kila akuombaye na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie. Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.

“Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao. Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ hufanya vivyo hivyo. Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha wenye dhambi wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote.

Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na waovu. Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”

Naye mwanamke mmoja kwenye ule mji, ambaye alikuwa mwenye dhambi, alipojua kwamba Yesu alikuwa akila chakula nyumbani kwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marmar yenye manukato. Yule mwanamke akiwa amesimama nyuma ya miguu ya Yesu akilia. Akailowanisha miguu yake kwa machozi yake, kisha akaifuta kwa nywele zake akaibusu na kuimiminia manukato.

“Palikuwa na mtu mmoja aliyewakopesha watu wawili fedha: Mmoja alidaiwa dinari 500 na mwingine dinari hamsini. Wote wawili walipokuwa hawawezi kulipa, aliyafuta madeni yao wote wawili. Sasa ni yupi kati yao atakayempenda yule aliyewasamehe zaidi?” Simoni akajibu, “Nadhani ni yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi.” Naye Yesu akamwambia, “Umehukumu kwa usahihi.” Kisha akamgeukia yule mwanamke akamwambia Simoni, “Je, unamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu yangu, lakini huyu ameninawisha miguu kwa machozi yake na kunifuta kwa nywele zake. Hukunisalimu kwa busu, lakini huyu mwanamke hajaacha kuibusu miguu yangu tangu nilipoingia. Hukunipaka mafuta kichwani mwangu, lakini yeye ameipaka miguu yangu manukato. Kwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonyesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.”

Akajibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote, tena mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ ”

Yesu akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akitelemka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyang'anyi, wakampiga, wakaondoka, wakamwacha karibu ya kufa. Kwa bahati nzuri kuhani mmoja alikuwa anapitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. Vivyo hivyo Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri kupitia njia hiyo alipomwona, alimhurumia, akamwendea, akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake akamleta mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza. Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yo yote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’ “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu, wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang'anyi?” Yule mtaalamu wa sheria akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.” Ndipo Yesu akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”

“Mtu akikualika arusini, usikae mahali pa mgeni wa heshima kwa kuwa inawezekana amealikwa mtu mheshimiwa kuliko wewe. Kama mkifanya hivyo yule aliyewaalika ninyi wawili atakuja na kukuambia, ‘Mpishe huyu mtu kiti chako.’ Ndipo kwa aibu utalazimika kukaa katika nafasi ya chini kabisa. Badala yake, unapoalikwa, chagua nafasi ya chini, ili yule mwenyeji wako atakapokuona atakuja na kukuambia, ‘Rafiki yangu, nenda kwenye nafasi iliyo bora zaidi.’ Kwa jinsi hii utakuwa umepewa heshima mbele ya wageni wenzako wote. Kwa maana kila mtu ajikwezaye atashushwa, naye ajishushaye atakwezwa.”

Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu, ukifanya hivyo, wao nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umelipwa kile ulichofanya na kupata thawabu yako. Bali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu, nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”

Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake. “Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu. “Yule mtoto akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’ “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake. Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi. Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena, alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.

“Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Ama atamchukia mmoja na kumpenda mwingine au atamheshimu mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.”

Kama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu’, msamehe.”

“Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana ye yote ajikwezaye atashushwa na ye yote ajishushaye atakwezwa.”

Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu ye yote kitu cho chote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.”

Yesu akasema, “Amin, amin nawaambia, huyu mjane maskini ameweka humo sadaka kubwa zaidi kuliko wengine wote. Hawa watu wengine wote wametoa sadaka kwa Mungu kutokana na wingi wa mali zao, lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake vyote alivyokuwa navyo kwa ajili ya maisha yake.”

Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye atawalaye na awe kama yeye ahudumuye. Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule aketiye mezani au ni yule ahudumiaye? Si ni yule aliyekaa mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule ahudumiaye.

Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata kifoni.”

Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kwa yeye ulimwengu upate kuokolewa.

Yeye hana budi kuwa mkuu zaidi na mimi nizidi kuwa mdogo.”

Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena.

Yesu akalia machozi. Ndipo Wayahudi wakasema, “Tazama jinsi alivyompenda Lazaro!”

Kisha Maria akachukua chupa ya painti moja yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa akayamimina miguuni mwa Yesu na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato.

Ilikuwa mara tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua ya kuwa wakati wake wa kuondoka ulimwenguni ili kurudi kwa Baba umewadia. Alikuwa amewapenda watu wake waliokuwa ulimwenguni, naam, aliwapenda hadi kipimo cha mwisho.

Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni.

Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala anayetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri yenu ninyi kama mkiyatenda.

Mmoja wa wanafunzi wake, ambaye Yesu alimpenda sana alikuwa ameegama kifuani mwa Yesu.

“Amri mpya nawapa: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi, vivyo hivyo nanyi mpendane. Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.”

“Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu.

Ye yote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”

Yesu akamjibu, “Mtu ye yote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. Mtu ye yote asiyenipenda hayashiki maneno yangu na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.

“Kama vile Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu iwe kamili. Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu.

Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.

kwa maana Baba mwenyewe anawapenda, kwa sababu mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu.

Mimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.

Nimefanya jina lako lijulikane kwao nami nitaendelea kufanya lijulikane, ili kwamba upendo ule unaonipenda mimi uwe ndani yao na mimi mwenyewe nipate kuwa ndani yao.”

Walipokwisha kula, Yesu akamwuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?” Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.” Yesu akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.” Yesu akamwambia tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?” Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.” Yesu akamwambia, “Chunga kondoo zangu.” Kwa mara ya tatu Yesu akamwuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?” Petro akahuzunika sana kwa kuwa Yesu alimwuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.” Yesu akamwambia, “Lisha kondoo zangu.

Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, wakamgawia kila mtu kwa kadiri alivyokuwa anahitaji. Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe,

Wala hapakuwepo mtu ye yote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa wale mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu” Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.

Huyu towashi alikuwa anasoma fungu hili la maandiko: “Aliongozwa kama kondoo aendaye machinjoni, kama mwana-kondoo anyamazavyo mbele yake yeye amkataye manyoya, hivyo hakukifungua kinywa chake. Katika kufedheheshwa kwake alinyimwa haki yake. Nani awezaye kueleza juu ya kizazi chake? Kwa maana maisha yake yameondolewa kutoka duniani.”

Katika kila jambo nililofanya, nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni baraka zaidi kutoa kuliko kupokea.’ ”

wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia. Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. Hakika, ni vigumu mtu ye yote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu. Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka katika ghadhabu ya Mungu kwa yeye! Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake.

Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? Kama ilivyoandikwa: “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.” Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.

Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine cho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.

Upendo lazima usiwe wa unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa kindugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana. Iweni na furaha katika tumaini, katika dhiki iweni na saburi, dumuni katika maombi. Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.

Wabarikini wale wanaowatesa, barikini wala msilaani. Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao. Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu. Msimlipe mtu ye yote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote.

Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa, asema Bwana.” Badala yake: “Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mnyweshe. Maana ukifanya hivyo, utampalia makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.” Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

Msidaiwe kitu na mtu ye yote, isipokuwa kupendana, kwa maana yeye ampendaye mwenzake, ameitimiza Sheria. Kwa kuwa amri hizi zisemazo, “Usizini,” “Usiue,” “Usiibe,” “Usitamani,” na amri nyingine zote, zinajumlishwa katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Upendo haumfanyii jirani jambo baya. Kwa hiyo upendo ndio utimilifu wa Sheria.

Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake.

Basi kwa nini wewe wamhukumu ndugu yako? Au kwa nini wewe unamdharau ndugu yako? Kwa kuwa sote tutasimama mbele ya kiti cha Mungu cha hukumu. Kwa kuwa imeandikwa: “ ‘Kama niishivyo,’ asema Bwana, ‘kila goti litapigwa mbele zangu, na kila ulimi utamkiri Mungu.’ ” Hivyo basi kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe kwa Mungu.

Kwa hiyo tusiendelee kuhukumiana: Badala yake mtu asiweke kamwe kikwazo au kizuizi katika njia ya mwingine. Ninajua tena nimehakikishiwa sana katika Bwana Yesu kwamba hakuna kitu cho chote ambacho ni najisi kwa asili yake. Lakini kama mtu anakiona kitu kuwa ni najisi, basi kwake huyo kitu hicho ni najisi. Kama ndugu yako anahuzunishwa kwa sababu ya kile unachokula, basi huenendi tena katika upendo. Usiruhusu kile unachokula kiwe sababu ya kumwangamiza ndugu yako ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.

Kwa hiyo na tufanye bidii kutafuta yale yaletayo amani na kujengana sisi kwa sisi.

Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe. Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani. Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.” Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini. Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu, ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Kristo alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu.

Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo yanawasalimu.

Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza. Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana Kristo, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga.

Lakini ni kama ilivyoandikwa: “Lile jambo ambalo jicho halijapata kuona, sikio halijapata kusikia, wala halikuingia moyoni, lile ambalo Mungu aliwaandalia wale wampendao”:

Ukweli ni kwamba huko kuwa na mashtaka dhidi ya mwingine miongoni mwenu tayari ni kushindwa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyang'anywa?

Basi kuhusu mambo yale mliyoniandikia: Ni vyema mwanaume asimguse mwanamke. Lakini ili kuepuka zinaa, kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. Mume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe, naye vivyo hivyo mke kwa mumewe. Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe. Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda fulani ili mweze kujitoa kwa maombi, kisha mrudiane tena ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi.

Ingawa mimi ni huru, wala si mtumwa wa mtu ye yote, nimejifanya kuwa mtumwa wa kila mtu, ili niweze kuwavuta wengi zaidi.

Mtu ye yote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine.

Msiwe kikwazo kwa mtu ye yote, kwa Wayahudi au kwa Wayunani, au kwa Kanisa la Mungu, kama mimi ninavyojaribu kumpendeza kila mtu kwa kila namna. Kwa maana sitafuti mema kwa ajili yangu mwenyewe bali mema kwa ajili ya faida ya wengi, ili waweze kuokolewa.

ili pasiwe na mafarakano katika mwili, bali viungo vyote vihudumiane kwa usawa kila kimoja na mwenzake. Kama kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia pamoja nacho, kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.

Hata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo. Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno. Upendo hauna kiburi. Haukosi kuwa na adabu. Upendo hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote. Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita.

Basi sasa, yanadumu mambo haya matatu: Imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu miongoni mwa haya matatu ni upendo.

Fuateni upendo na kutaka sana karama za roho, hasa karama ya unabii.

Fanyeni kila kitu katika upendo.

Kwa kuwa upendo wa Kristo unatutia nguvu, kwa sababu tunasadiki kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote, kwa hiyo wote walikufa. Naye alikufa kwa ajili ya watu wote, ili kwamba wote wanaoishi wasiishi tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuka tena kwa ajili yao.

bali kama watumishi wa Mungu tuonyeshe kwa kila njia saburi nyingi katika dhiki, katika misiba, katika shida, katika kupigwa, katika kufungwa gerezani na katika ghasia, katika kazi ngumu, katika kukesha na katika njaa, katika utakatifu, katika ufahamu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika Roho Mtakatifu na upendo wa kweli, katika maneno ya kweli na katika nguvu za Mungu, kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto, katika utukufu na katika kudharauliwa, katika sifa mbaya na katika sifa nzuri, kama wadanganyaji lakini tukiwa wakweli tukiwa maarufu lakini tukihesabiwa kama tusiojulikana, tukiwa kama wanaokufa lakini tunaishi, tukipigwa lakini hatuuawi, kama wenye huzuni lakini siku zote tukifurahi, tukionekana maskini lakini tukitajirisha wengi, tukiwa kama wasio na kitu lakini tuna vitu vyote.

Pamoja na majaribu makali na taabu walizopata, furaha waliyokuwa nayo ilikuwa kubwa, ingawa walikuwa maskini kupindukia, kwa upande wao walifurika kwa wingi wa ukarimu. Kwa maana nashuhudia kwamba wao walitoa kwa kadiri wawezavyo, hata na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe, wakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu. Wala hawakufanya tulivyotazamia, bali walijitoa wao wenyewe kwa Bwana kwanza na ndipo wakajitoa kwa ajili yetu, kufuatana na mapenzi ya Mungu.

Lakini kama vile mlivyo mbele sana katika yote: Katika imani, katika usemi, katika maarifa, katika uaminifu wote na katika upendo wenu kwetu sisi, vivyo hivyo tunataka pia mzidi katika neema hii ya kutoa. Siwaamrishi, lakini nataka kujaribu unyofu wa upendo wenu kwa kuulinganisha na bidii ya wengine. Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.

Kwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kulingana na kile mtu alicho nacho, wala si kwa kile ambacho hana.

Kwa hiyo waonyesheni wazi hawa ndugu uthibitisho wa upendo wenu na sababu inayotufanya tujivune kwa ajili yenu, mbele ya makanisa, ili yapate kuona.

Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu.

Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi!

Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

Hatimaye, ndugu zangu, kwaherini. Iweni wakamilifu, mkafarijike, nieni pamoja, kaeni kwa amani, naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu.

Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote. Amen.

Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu.

Kwa maana ndani ya Kristo, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kwa njia ya upendo.

Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.

Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.

Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejezeni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.

Kama mtu ye yote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe. Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine.

Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake.

Kwa sababu hii, tangu niliposikia juu ya imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watakatifu wote, sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu.

Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema.

Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo na kujua upendo huu kwamba unapita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.

Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa. Iweni wanyenyekevu kabisa na wapole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji. Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao. Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwa huyo mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. Iweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wapendwao, Mkiishi maisha ya upendo, kama vile Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu.

Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kwa heshima kwa ajili ya Kristo.

Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake

Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza Kanisa lake. Sisi tu viungo vya mwili wake.

“Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe na hawa wawili watakuwa mwili mmoja.” Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Kristo na Kanisa. Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.

Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.” Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana. Ninyi watumwa, watiini hao walio mabwana zenu hapa duniani kwa heshima na kwa kutetemeka na kwa moyo mmoja, kama vile mnavyomtii Kristo.

Amani iwe kwa ndugu, na pendo pamoja na imani kutoka kwa Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo. Neema iwe na wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo kwa upendo wa dhati. Amen.

Mungu ni shahidi yangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Kristo Yesu. Haya ndiyo maombi yangu kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote, ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Kristo,

Kama kukiwa na jambo lo lote la kutia moyo, kukiwako faraja yo yote katika upendo, kukiwa na ushirika wo wote katika Roho, kukiwa na wema wo wote na huruma, basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia kama hiyo, mkiwa na upendo huo huo, wenye roho moja na kusudi moja. Msitende jambo lo lote kwa nia ya kujitukuza, bali kwa unyenyekevu, kila mtu akimhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. Kila mmoja wenu asiangalie mambo yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

Iweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu: Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa, hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikilia, bali alijifanya si kitu, akajifanya sawa hasa na mtumwa, akazaliwa katika umbo la mwanadamu. Naye akiwa na umbo la mwanadamu, alijinyenyekeza, akatii hata mauti: naam, mauti ya msalaba!

Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji yangu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana, ninyi wapenzi wangu.

Siku zote tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, tunapowaombea ninyi, kwa sababu tumesikia juu ya imani yenu katika Kristo Yesu na juu ya upendo wenu mlio nao kwa watakatifu wote,

Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni Kanisa.

Kusudi langu ni kuwa watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu kikamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani, Kristo mwenyewe,

Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote, yaani: Hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu. Msiambiane uongo kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, nanyi mmevaa utu mpya unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote na ndani ya wote.

Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu, wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. Vumilianeni na kusameheana. Mtu akiwa na lalamiko lo lote dhidi ya mwenzake, sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu. Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. Lo lote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika Jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe na uchungu dhidi yao. Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hivi ndivyo inavyompendeza Bwana. Ninyi akina baba msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu wa hapa duniani katika mambo yote. Fanyeni hivyo si wakiwepo tu, bali mkimwogopa Mungu, wala si kwa kutafuta upendeleo wao wakati wanapowaona. Lo lote mfanyalo, fanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana na si wanadamu.

Iweni na hekima jinsi mnavyoenenda mbele yao wale walio nje, mkiutumia vizuri wakati wenu. Maneno yenu yawe yamejaa neema siku zote, yanayofaa, ili mjue jinsi iwapasavyo na inavyofaa kumjibu kila mtu.

Bwana na auongeze upendo wenu na kuuzidisha kati ya ninyi kwa ninyi na kwa wengine wote, kama vile tulivyo na upendo mwingi kwenu. Tunamwomba Mungu awaimarishe mioyo yenu katika utakatifu ili msiwe na lawama mbele za Mungu wetu aliye Baba yetu wakati wa kuja kwake Bwana Yesu pamoja na watakatifu wote.

Sasa kuhusu upendano wa ndugu hamna haja mtu ye yote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda.

Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa. Sasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana na ambao wanawaonya. Mkawajali sana katika upendo kwa ajili ya kazi yao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi. Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni wale wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na iweni na uvumilivu na kila mtu. Angalieni kuwa mtu asilipe ovu kwa ovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.

Ndugu, imetubidi kumshukuru Mungu kwa ajili yenu siku zote, kama ulivyo wajibu wetu, kwa sababu imani yenu inakua zaidi na zaidi na upendo wa kila mmoja wenu alio nao kwa mwenzake unazidi kuongezeka. Ndiyo sababu miongoni mwa makanisa ya Mungu, tunajivuna kuhusu saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili. Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili Ufalme wa Mungu, ambao ninyi mnateswa kwa ajili yake.

Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Kristo.

Kusudi la maagizo haya ni upendo, utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli.

Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.

Mtu ye yote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waaminio katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi.

Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.

Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole.

Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi, kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu. Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha.

Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi. Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu,

Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli,

Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wapendao anasa zaidi kuliko kumpenda Mungu. Wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu wa namna hiyo.

Lakini wewe umeyajua mafundisho yangu, mwenendo, makusudi, imani, uvumilivu, upendo, ustahimilivu,

Lakini kwa habari yako wewe, inakupasa kufundisha kulingana na mafundisho yenye uzima. Wafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi. Vivyo hivyo wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa unyenyekevu unaostahili utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema, ili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao, wawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu ye yote asije akalikufuru neno la Mungu. Vivyo hivyo, sisitiza vijana wawe na kiasi. Katika kila jambo wewe mwenyewe uwe kielelezo cha matendo mema na katika mafundisho yako uonyeshe unyofu, utaratibu, ukweli na maneno yenye uzima, yale ambayo hayawezi kulaumiwa, hata wale wenye kukupinga watahayari, wakose neno lo lote baya la kusema juu yetu.

Wakumbushe watu kuwanyenyekea watawala na kuwatii wenye mamlaka, wawe tayari kutenda kila lililo jema. Wasimnenee mtu ye yote mabaya, wasiwe wagomvi, bali wawe wapole, wakionyesha unyenyekevu kwa watu wote. Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi. Lakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa, alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kwa njia ya Roho Mtakatifu,

Siku zote ninamshukuru Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu, kwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote.

Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu. Hata hivyo, ingawa katika Kristo ningeweza kuwa na ujasiri na kukuagiza yale yakupasayo kutenda, lakini ninakuomba kwa upendo, mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Kristo Yesu,

Mungu si dhalimu, hataisahau kazi yenu na upendo ule mlioonyesha kwa ajili yake katika kuwahudumia watakatifu na kama vile mnavyoendelea kuwahudumia.

Kwa kuwa nitasamehe uovu wao, wala sitazikumbuka dhambi zao tena!”

Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi ya kukutana, tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.

kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao, na humwadhibu kila mmoja anayemkubali kuwa mtoto wake.” Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake? Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali. Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi?

Upendo wa kidugu na udumu. Msisahau kuwakaribisha wageni, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengine waliwakaribisha malaika pasipo kujua. Wakumbukeni wale waliofungwa gerezani kama vile nanyi mmefungwa pamoja nao, pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kama vile ni ninyi wenyewe mnateswa.

Msiache kutenda mema na kushirikiana vile mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.

Ndugu asiye na cheo kikubwa yampasa ajivunie hali hiyo maana ametukuzwa.

Ndugu zangu wapendwa, fahamuni jambo hili: Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza, lakini asiwe mwepesi wa kusema wala wa kukasirika. Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu. Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu.

Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake mtu huyo haifai kitu.

Kwa maana kama akija mtu katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, pia akaingia mtu maskini mwenye mavazi yaliyochakaa, nanyi mkampa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,” je, hamjawabagua na kuwa mahakimu mioyoni mwenu mkihukumu kwa mawazo yenu maovu? Ndugu zangu, sikilizeni: Je, Mungu hakuwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi Ufalme aliowaahidi wale wampendao? Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani?

Kama kweli mnaitimiza ile sheria ya kifalme inayopatikana katika Maandiko isemayo, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako,” mnafanya vyema. Lakini kama mnakuwa na upendeleo kwa watu, mnatenda dhambi na sheria inawahukumu kuwa ninyi ni wakosaji.

Kwa kuwa hukumu bila huruma itatolewa kwa mtu ye yote asiyekuwa na huruma. Huruma huishinda hukumu.

Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, mmoja wenu akamwambia, “Enenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? Vivyo hivyo, imani peke yake kama haikuambatana na matendo, imekufa.

Vivyo hivyo ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini hujivuna majivuno makuu. Fikirini jinsi moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa! Ulimi pia ni moto, ndio ulimwengu wa uovu kati ya viungo vya mwili. Ulimi huutia mwili wote wa mtu unajisi na kuuwasha moto mfumo mzima wa maisha yake, nao wenyewe huchomwa moto wa jehanamu.

Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima. Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli.

Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna. Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, ya upole, iliyo tayari kusikiliza maneno ya watu wengine, yenye unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki. Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.

Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu? Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hamumwombi Mungu. Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.

Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema: “Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.” Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, ninyi wenye dhambi na kuisafisha mioyo yenu, ninyi wenye nia mbili. Huzunikeni, ombolezeni na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza na furaha yenu kuwa huzuni. Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua. Ndugu, msineneane mabaya ninyi kwa ninyi. Mtu ye yote anayesema mabaya dhidi ya ndugu yake au kumhukumu anasema dhidi ya sheria na kuihukumu. Unapoihukumu sheria, basi huishiki sheria bali umekuwa hakimu wa kuihukumu hiyo sheria.

Basi mtu ye yote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.

Ninyi nanyi vumilieni tena simameni imara, kwa sababu kuja kwa Bwana kumekaribia. Ndugu zangu, msinung'unikiane msije mkahukumiwa. Hakimu amesimama mlangoni! Ndugu zangu, waangalieni manabii walionena kwa Jina la Bwana, ili kuwa mfano wa uvumilivu katika kukabiliana na mateso.

Kwa hiyo ungamianeni makosa yenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.

Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli kwa njia ya Roho kwa kuwapenda ndugu zenu kwa upendo wa kweli, pendaneni kwa dhati kutoka moyoni.

Kwa hiyo, wekeni mbali nanyi uovu wote na udanganyifu wote, unafiki, wivu na masingizio ya kila namna. Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine cho chote, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu,

Mheshimuni kila mtu. Wapendeni jamaa ya waaminio. Mcheni Mungu. Mpeni heshima mfalme. Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu kwa heshima yote, si wale mabwana walio wema na wapole peke yao, bali pia wale walio wakali.

Kwa kuwa ninyi mliitwa kwa ajili ya hayo, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mzifuate nyayo zake. “Yeye hakutenda dhambi, wala udanganyifu haukuonekana kinywani mwake.” Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano, alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki.

Hatimaye, ninyi nyote iweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, wasikitivu na wanyenyekevu. Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka.

Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. Iweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manung'uniko. Kila mmoja na atumie kipawa cho chote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu.

Vivyo hivyo ninyi mlio vijana hamna budi kuwatii wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu katika kuhudumiana, kila mtu na mwenzake, kwa kuwa, “Mungu huwapinga wenye kiburi bali huwapa wanyenyekevu neema.” Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote kwa maana hujishughulisha sana na mambo yenu.

Salimianeni kwa busu la upendo. Amani iwe nanyi nyote mlio katika Kristo. Amen.

Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema na katika wema wenu maarifa, katika maarifa yenu kiasi, katika kiasi, saburi, katika saburi yenu, utauwa, katika utauwa wenu upendano wa kidugu, katika upendano wa kidugu, upendo.

Lakini kama mtu ye yote analitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake.

Ye yote anayesema yumo nuruni lakini anamchukia ndugu yake bado yuko gizani. Yeye ampendaye ndugu yake anakaa nuruni, wala hakuna kitu cho chote ndani yake cha kumkwaza. Lakini ye yote amchukiaye ndugu yake, yuko gizani na anaenenda gizani, wala hajui anakokwenda, kwa sababu giza limempofusha macho.

Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyoko ulimwenguni. Kama mtu ye yote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake.

Oneni ni pendo kuu namna gani alilotupa Baba, kwamba sisi tuitwe watoto wa Mungu! Nasi ndivyo tulivyo. Sababu kwa nini ulimwengu haututambui, ni kwa kuwa haukumtambua yeye.

Hili ndilo neno mlilolisikia tangu mwanzo: Kwamba imetupasa tupendane sisi kwa sisi.

Sisi tunajua ya kwamba tumepita kutoka mautini kuingia uzimani, kwa sababu tunawapenda ndugu. Kila asiyempenda ndugu yake akaa mautini. Ye yote amchukiaye ndugu yake ni mwuaji, nanyi mwajua ya kwamba mwuaji hana uzima wa milele ndani yake. Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? Watoto wangu wadogo, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na katika kweli.

Hii ndiyo amri yake: kwamba tuliamini Jina la Mwanawe, Yesu Kristo na kupendana sisi kwa sisi kama yeye alivyotuamuru.

Wapenzi na tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu. Kila apendaye amezaliwa na Mungu naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa hamjui Mungu, kwa sababu Mungu ni pendo. Hivi ndivyo Mungu alivyoonyesha pendo lake kwetu, kwa sababu Mungu alimtuma Mwanawe wa pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba tulimpenda Mungu, bali yeye alitupenda, akamtuma Mwanawe, ili yeye awe dhabihu ya kipatanisho kwa ajili ya dhambi zetu. Wapenzi, kama Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna mtu ye yote aliyemwona Mungu wakati wo wote. Kama tukipendana, Mungu anakaa ndani yetu na pendo lake limekamilika ndani yetu.

Hivyo nasi twajua na kulitumainia pendo la Mungu alilo nalo kwa ajili yetu. Mungu ni Upendo. Kila akaaye katika upendo hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake. Kwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu. Katika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo. Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza. Ikiwa mtu atasema, “Nampenda Mungu”, lakini anamchukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa maana kila mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, atampendaje Mungu ambaye hamwoni? Naye ametupa amri hii: Ye yote anayempenda Mungu lazima pia ampende ndugu yake.

Kila mtu anayeamini kwamba Yesu ndiye Kristo amezaliwa na Mungu na ye yote ampendaye Baba humpenda pia mtoto aliyezaliwa naye. Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu, kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake. Huku ndiko kumpenda Mungu, yaani, kuzitii amri zake. Nazo amri zake si nzito.

Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwanawe Baba, itakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.

Sasa, bibi mpendwa, nakuomba, si kwamba ninakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. Sisi na tupendane kila mmoja na mwenzake. Hili ndilo pendo, kwamba tuenende sawasawa na amri zake. Hii ndiyo amri yake kama vile mlivyosikia tangu mwanzo, kwamba mwenende katika upendo.

Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele. Wahurumieni wengine wale wenye shaka; wengine waokoeni kwa kuwanyakua kutoka kwenye moto; nao wengine wahurumieni mkiwa na hofu, mkichukia hata vazi lenye mawaa na kutiwa unajisi na mwili.

na kutoka kwa Yesu Kristo ambaye ni shahidi mwaminifu, aliye mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ambaye yeye ndiye mtawala wa wafalme wa dunia. Kwake yeye anayetupenda na ambaye ametuweka huru kutoka katika dhambi zetu kwa damu yake,

“Lakini nina neno juu yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza.

Nayajua matendo yako, upendo wako, imani yako, huduma na saburi yako na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza.

“Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu.

Kamwe hawataona njaa wala kiu tena. Jua halitawapiga wala joto lo lote liunguzalo. Kwa maana Mwana-Kondoo aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi atakuwa Mchungaji wao; naye atawaongoza kwenda kwenye chemchemi za maji yaliyo hai. Naye Mungu atafuta kila chozi kutoka katika macho yao.”

Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe.

Atafuta kila chozi, kutoka katika macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.” Naye yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nayafanya mambo yote kuwa mapya!” Kisha akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika tena ni kweli.” Akaniambia, “Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Yeye aonaye kiu nitampa kunywa kutoka katika chemchemi ya maji ya uzima bila gharama yo yote. Yeye atakayeshinda atayarithi haya yote, Nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

Swahili - Kiswahili - SW

NEN'2014 - Neno Bibilia Takatifu Kiswahili Contemporary Version - 2014

This Bible text is from Biblica Open Kiswahili Contemporary Version Neno 2015
https://open.bible/bibles/swahili-biblica-text-bible/
provided by: Biblica Inc, available by Creative Commons CC-BY-SA-4.0,
and this new compilation is shared as www.creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0.
Languages are made available to you by www.ipedge.net