24 – Familia

Haya ni maneno matakatifu ya Mungu Mwenyezi.
Hatupendi maneno ya wanadamu.
Kwa mtu yeyote anayempenda Mungu... hivi ndivyo Mungu anasema kuhusu: Familia.

Mistari 3 Muhimu Zaidi

Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo.

“Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe na hawa wawili watakuwa mwili mmoja.” Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Kristo na Kanisa. Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.

Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.” Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.

Kila Mstari katika Mpangilio wa Biblia - 302 vifungu

Kwa hiyo Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe, kwa mfano wa Mungu alimuumba; mwanaume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”

BWANA Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.” Basi BWANA Mungu alikuwa amefanyiza kutoka katika ardhi wanyama wote wa porini na ndege wote wa angani. Akawaleta kwa huyu mtu aone atawaitaje, nalo jina lo lote alilokiita kila kiumbe hai, likawa ndilo jina lake. Hivyo Adamu akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, ndege wa angani, na wanyama wote wa porini. Lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi wa kumfaa.

Hivyo BWANA Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama. Kisha BWANA Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume. Huyo mwanaume akasema, “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu na nyama ya nyama yangu, ataitwa ‘mwanamke,’ kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”

Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Adamu na mkewe wote wawili walikuwa uchi, wala hawakuona aibu.

Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa sehemu ya tunda kutoka kwenye huo mti, nami nikala.” Ndipo BWANA Mungu akamwuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”

Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na wake, huo atakuponda kichwa, nawe utamgonga kisigino.” Kwa mwanamke akasema, “Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto. Tamaa yako itakuwa kwa mumeo naye atakutawala.” Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’ “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako, kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo siku zote za maisha yako.

Adamu akamwita mkewe Eva, kwa kuwa atakuwa mama wa wote walio hai.

Adamu akakutana kimwili na mkewe Eva, akapata mimba, akamzaa Kaini. Eva akasema, “Kwa msaada wa BWANA nimemzaa mwanaume.” Baadaye akamzaa Abeli ndugu yake. Basi Abeli akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima. Baada ya muda Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba kama sadaka kwa BWANA. Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka katika baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. BWANA akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake, lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni. Kisha BWANA akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? Ukifanya lililo sawa, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.” Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamwua. Kisha BWANA akamwuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Akamjibu, “Sijui, je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” BWANA akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka katika ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako.

Hii ni orodha iliyoandikwa ya vizazi vya Adamu. Wakati Mungu alipomuumba Adamu, alimfanya kwa sura ya Mungu. Aliwaumba mwanaume na mwanamke, akawabariki. Walipokwisha kuumbwa akawaita “Mwanadamu.”

Adamu alipokuwa ameishi miaka 130, alikuwa na mwana aliyekuwa na sura yake, mwenye kufanana naye. Akamwita Sethi. Baada ya Sethi kuzaliwa, Adamu aliishi miaka 800, akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. Adamu aliishi jumla ya miaka 930, ndipo akafa.

Watu walipoanza kuongezeka idadi katika uso wa dunia na watoto wa kike wakazaliwa kwao,

Ndipo BWANA akamwambia Noa, “Ingia katika safina wewe na jamaa yako yote, kwa sababu katika kizazi hiki nimeona ya kuwa wewe ni mwenye haki.

Ndipo Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni mkaongezeke kwa idadi na mkaijaze tena dunia.

BWANA akawa amemwambia Abramu, “Ondoka katika nchi yako, waache watu wako na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha. “Mimi nitakufanya taifa kubwa na nitakubariki, Nitalikuza jina lako, nawe utakuwa baraka. Nitawabariki wale wanaokubariki, na ye yote akulaaniye nitamlaani; na kupitia kwako mataifa yote duniani yatabarikiwa.”

“Kwa upande wangu, hili ndilo Agano langu na wewe: Wewe utakuwa baba wa mataifa mengi. Jina lako hutaitwa tena Abramu, bali jina lako litakuwa Abrahamu, kwa maana nimekufanya wewe baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, kwako yatatoka mataifa nao wafalme watatoka kwako. Nitalithibitisha Agano langu kama Agano la milele kati yangu na wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo niwe Mungu wako na Mungu wa wazao wako.

Pia BWANA akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wa Sarai mkeo, hutamwita tena Sarai bali jina lake litakuwa Sara. Nitambariki na hakika nitakupatia mwana kwake. Nitambariki na kwamba atakuwa mama wa mataifa, wafalme wa mataifa watatoka kwake.” Abrahamu akaanguka kifudifudi, akacheka na kusema moyoni mwake, “Je, mtu wa miaka mia moja aweza kuzaa mwana? Je, Sara atazaa mtoto katika umri wa miaka tisini?”

Kwa maana nimemchagua yeye, ili kwamba aongoze watoto wake na jamaa yake kumtii BWANA, wawe waadilifu na kutenda haki, ili BWANA atimize ahadi yake kwa Abrahamu.”

Wakati huu BWANA akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, naye BWANA akamtendea Sara kile alichokuwa ameahidi. Sara akapata mimba, akamzalia Abrahamu mwana katika uzee wake, majira yale ya Mungu aliomwahidi. Abrahamu akamwita Isaki yule mwana ambaye Sara alimzalia.

Ndipo Isaki akamwingiza Rebeka katika hema la Sara mama yake, Isaki akamchukua Rebeka, hivyo akawa mke wake. Isaki akampenda, akafarijika baada ya kifo cha mama yake.

Uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi na mashariki, kaskazini na kusini. Kupitia wewe na uzao wako mataifa yote ya duniani yatabarikiwa.

Yakobo akampenda Raheli, akamwambia Labani, “Nitakutumikia kwa miaka saba kwa ajili ya kumpata Raheli binti yako mdogo.” Labani akasema, “Ni bora zaidi nikupe Raheli kuliko kumpa mtu mwingine ye yote. Kaa pamoja na mimi hapa.” Kwa hiyo Yakobo akatumika miaka saba ili kumpata Raheli, lakini ilionekana kwake kama siku chache tu kwa sababu ya upendo wake kwa Raheli.

Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea ndugu yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!” Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia usizae watoto?”

Ndipo BWANA akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya baba zako na kwa watu wako, nami nitakuwa pamoja nawe.”

Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni ile iliyoko katikati yenu, jitakaseni na mkabadilishe nguo zenu.

Hapo Yosefu hakuweza kujizuia zaidi mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye, akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwepo mtu ye yote pamoja na Yosefu alipojitambulisha kwa ndugu zake. Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake.

gari kubwa zuri la Yosefu liliandaliwa, naye akaenda Gosheni kumlaki baba yake Israeli. Mara Yosefu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu.

Ndipo Yosefu akawakalisha baba yake na ndugu zake katika nchi ya Misri na kuwapa milki katika sehemu bora sana ya nchi, wilaya ya Ramesesi, kama Farao alivyoelekeza. Pia Yosefu akampa baba yake, na ndugu zake na wote wa nyumbani mwa baba yake vyakula, kwa kulingana na hesabu ya watoto wao.

Usivisujudie au kuviabudu; kwa kuwa Mimi, BWANA Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi ya baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,

Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa BWANA Mungu wako.

“Ye yote amshambuliaye baba yake au mama yake ni lazima auawe.

“Usimdhulumu mjane wala yatima.

akidumisha upendo kwa maelfu, pia akisamehe uovu, uasi na dhambi. Lakini haachi kuadhibu mwenye hatia; huwaadhibu watoto na watoto wao kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata katika kizazi cha tatu na cha nne.”

Unapowachagua baadhi ya binti zao kuwa wake wa wana wenu na binti hao wakajifanyia ukahaba kwa miungu yao, watawaongoza wana wenu kufanya vivyo hivyo.

“ ‘Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na pia ni lazima kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.

“ ‘Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Karipia jirani yako kwa uwazi ili usishiriki hatia yake.

“ ‘Ikiwa mtu ye yote atamlaani baba yake au mama yake, lazima auawe. Amemlaani baba yake au mama yake, nayo damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.

“ ‘Kamwe wasioe wanawake waliojinajisi kwa ukahaba au waliopewa talaka na waume wao, kwa sababu makuhani ni watakatifu kwa Mungu wao.

“ ‘Mwanamke atakayemwoa ni lazima awe bikira. Kamwe asimwoe mjane, au mwanamke aliyepewa talaka, wala mwanamke aliyejinajisi kwa ukahaba, bali atamwoa tu bikira kutoka miongoni mwa watu wake,

“ ‘Basi, hii ndiyo sheria ya wivu mwanamke anapopotoka na kujitia unajisi wakati akiwa ameolewa na mumewe, au hisia za wivu zinapomjia mwanaume kwa sababu ya kumshuku mkewe. Kuhani atamfanya huyo mwanamke kusimama mbele za BWANA na atatumia sheria hii yote kwa huyo mwanamke. Mume atakuwa hana hatia ya kosa lo lote, bali mwanamke atayachukua matokeo ya dhambi yake.’ ”

“Wanachosema binti za Selofehadi ni sawa, ni lazima kwa hakika uwape milki kama urithi miongoni mwa ndugu za baba yao, na kubadili urithi wa baba yao uwe wao. “Waambie Waisraeli, ‘Ikiwa mtu atakufa naye hakuacha mwana, utampa binti yake urithi wake. Ikiwa hana binti, wape ndugu zake wa kiume urithi wake. Ikiwa hana ndugu wa kiume toa urithi wake kwa ndugu za baba yake. Ikiwa baba yake hakuwa na ndugu wa kiume, toa urithi wake kwa ndugu wa karibu katika ukoo wake, ili aumiliki. Hili litakuwa dai la sheria kwa Waisraeli, kama BWANA alivyomwamuru Mose.’ ”

Hivi ndivyo BWANA anavyoamuru kwa binti za Selofehadi: Wanaweza kuolewa na mtu ye yote wampendaye, mradi tu waolewe miongoni mwa koo za kabila za baba yao. Hakuna urithi katika Israeli utakaohamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila Mwisraeli atatunza ardhi ya kabila lake aliyoirithi kutoka kwa baba zake. Kila binti atakayerithi ardhi katika kabila lo lote la Israeli ni lazima aolewe na mtu kutoka kabila na ukoo wa baba yake, ili kila Mwisraeli amiliki urithi wa baba zake. Hakuna urithi uwezao kuhamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila kabila la Israeli litatunza nchi linayorithi.”

Mwe waangalifu, na makini ili msije mkasahau mambo ambayo mliyaona kwa macho yenu, wala kuyaacha yaondoke moyoni mwenu siku zote za uhai wenu. Mwafundishe hayo watoto wenu na watoto wao baada yao. Kumbuka siku uliyosimama mbele za BWANA Mungu wako kule Horebu, wakati aliponiambia, “Wakutanishe watu mbele yangu wasikie maneno yangu ili kwamba waweze kujifunza kuniheshimu kwa muda wote watakaoishi katika nchi, nao waweze kuwafundisha watoto wao maneno hayo.”

Waheshimu baba yako na mama yako, kama BWANA Mungu wako alivyokuagiza, ili siku zako zipate kuwa nyingi na kufanikiwa katika nchi BWANA Mungu wako anayokupa.

Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo.

Usioane nao. Usimtoe binti yako kuolewa na mwanawe, au kumchukua binti yake aolewe na mwanao. Kwa maana watamgeuza mwanao aache kunifuata, ili aitumikia miungu mingine, nayo hasira ya BWANA itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza ghafula.

Huwapigania yatima na wajane, humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi.

Wafundisheni watoto wenu, yazungumzeni wakati mketipo nyumbani na wakati mtembeapo njiani, wakati mlalapo na wakati mwamkapo.

Mwe waangalifu kutii masharti haya yote ninayowapa, ili kwamba siku zote mweze kufanikiwa, ninyi pamoja na watoto wenu baada yenu, kwa sababu mtakuwa mkifanya lililo jema na sahihi mbele za macho ya BWANA Mungu wenu.

Mfurahie sikukuu yenu, ninyi, wana wenu, binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi katika miji yenu.

Kamwe asioe wake wengi, la sivyo moyo wake utapotoka. Kamwe asijilimbikizie kiasi kikubwa cha fedha na dhahabu.

Je, kuna ye yote aliyeposa mwanamke na hajamwoa? Yeye na arudi nyumbani, ama sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akamwoa.”

Kama mwanaume ana wake wawili, naye anampenda mmoja na mwingine hampendi na wote wawili wamemzalia wana wa kiume, lakini mwana mzaliwa wa kwanza ni wa yule mke asiyempenda, wakati anapotoa wosia wa mali yake kwa wanawe, kamwe asitoe haki za mzaliwa wa kwanza kwa mwana wa mke ampendaye kwa upendeleo, badala ya mzaliwa hasa wa kwanza, ambaye ni mwana wa mke ambaye hampendi. Ni lazima amkubali mwana wa mke asiyempenda kama mzaliwa wa kwanza kwa kumpa sehemu ya vile vyote alivyonavyo maradufu. Mwana huyo ni ishara ya kwanza ya nguvu za baba yake. Haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake yeye.

Kama mtu ana mwana mkaidi na mwasi ambaye hamtii baba yake na mama yake, na hasikii wazazi wanapomrudi, baba yake na mama yake watamleta kwa wazee kwenye lango la mji wake. Watawaambia wazee, “Huyu mwanetu ni mkaidi na mwasi. Hatutii sisi, yeye ni mpotovu na mlevi.” Kisha wanaume wote wa mjini mwake watampiga kwa mawe mpaka afe. Ndivyo imewapasa kuondoa maovu kati yenu. Israeli yote itasikia hili na kuogopa.

Ikiwa mtu atamwoa mke na, baada ya kufanya naye tendo la ndoa, akamchukia, akimsingizia na kumwita jina baya, akisema, “Nilimwoa mwanamke huyu, lakini nilipomkaribia sikupata uthibitisho wa ubikira wake” ndipo baba na mama wa msichana wataleta uthibitisho kwamba alikuwa bikira kwa wazee wa mji kwenye lango. Baba wa msichana atawaambia wazee, “Nilimwoza binti yangu kwa huyu mwanaume, lakini hampendi. Sasa amemsingizia na kusema, ‘Sikumkuta huyu binti akiwa bikira.’ Lakini hapa kuna uthibitisho wa ubikira wa binti yangu.” Kisha wazazi wake wataonyesha nguo zake kwa wazee wa mji, nao wazee watamchukua huyo mwanaume na kumwadhibu. Watamtoza shekeli mia moja za fedha na kupewa wazazi wa msichana, kwa sababu mwanaume huyu amempa bikira wa Kiisraeli jina baya. Ataendelea kuwa mke wake; kamwe hawezi kumpa talaka siku zote za maisha yake. Hata hivyo, kama shtaka ni la kweli na hakuna uthibitisho juu ya ubikira wa huyo msichana ulioweza kupatikana, huyo msichana ataletwa kwenye mlango wa nyumba ya baba yake, na hapo watu wa mji wake watampiga kwa mawe hadi afe. Amefanya kitu cha aibu katika Israeli kwa kutokuwa na utaratibu wakati akiwa nyumbani kwa babaye. Lazima mwondoe uovu katikati yenu. Ikiwa mwanaume atakutwa akizini na mke wa mtu mwingine, wote wawili, mwanaume na mwanamke aliyezini naye, lazima wauawe. Lazima mwondoe uovu katika Israeli.

Mtu ye yote ambaye amezaliwa kwenye ndoa isiyo halali au wazao wake wasiingie kwenye kusanyiko la BWANA, hata mpaka kizazi cha kumi.

Ikiwa mtu atamwoa mke na akamchukia kwa sababu ya kukosa adabu, akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani kwake, ikiwa baada ya kuondoka nyumbani kwake atakuwa mke wa mtu mwingine, ikiwa mume wake wa pili atachukizwa naye akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani kwake, au kama akifa, basi yule mume wake wa kwanza, ambaye alimpa talaka, haruhusiwi kumwoa tena baada ya mwanamke huyo kuwa najisi. Hayo yatakuwa machukizo machoni pa BWANA. Usilete dhambi juu ya nchi ambayo BWANA Mungu wako anakupa kama urithi.

Kama mtu ameoa karibuni, kamwe asipelekwe vitani au kupewa wajibu mwingine wo wote. Kwa mwaka mmoja atakuwa huru kubaki nyumbani ili amfurahishe mke aliyemwoa.

“Alaaniwe mtu amdharauye baba yake na mama yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”

“Alaaniwe mtu apotoshaye haki ya mgeni, yatima au mjane.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”

Mambo ya siri ni ya BWANA Mungu wetu, bali yaliyofunuliwa ni yetu na watoto wetu milele, ili tuweze kuyafanya maneno yote ya sheria hii.

Kusanya watu wote, wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili waweze kusikia na kujifunza kumcha BWANA Mungu wenu na kufuata kwa bidii maneno yote ya sheria hii. Watoto wao, ambao hawaijui sheria hii, lazima waisikie na kujifunza kumcha BWANA Mungu wenu kwa muda mtakaoishi katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”

Sasa basi, tafadhali niapieni kwa BWANA, kwamba mtaitendea hisani jamaa ya baba yangu, kwa kuwa mimi nimewatendea hisani. Nipeni ishara ya uaminifu kwamba mtayahifadhi maisha ya baba yangu na mama yangu, ndugu zangu wa kiume na wa kike, pamoja na wale wote walio wa kwao na kwamba mtatuokoa na kifo.”

“ ‘Asubuhi, mjihudhurishe kabila kwa kabila. Itakuwa kabila lile atakalolitwaa BWANA litakuja mbele ukoo kwa ukoo, ukoo ule atakaotwaa BWANA utakuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ile atakayoitwaa BWANA itakuja mbele mtu baada ya mtu.

“Lakini ikiwa mtageuka na kushikamana na mabaki ya mataifa haya yaliyosalia katikati yenu na kama mtaoana na kushirikiana nao, basi mwe na hakika kuwa BWANA Mungu wenu hatawafukuza tena mataifa hayo mbele yenu. Badala yake, watakuwa tanzi na mitego kwenu, mijeledi migongoni mwenu na miiba machoni penu, mpaka mwangamie kutoka katika nchi hii nzuri, ambayo BWANA Mungu wenu amewapa.

Lakini msipoona vyema kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo Eufrati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia BWANA.”

Wakati huo Waisraeli wakaondoka sehemu ile na kwenda nyumbani kwao, kwenye makabila yao na kwa jamaa zao, kila mmoja kwenye urithi wake mwenyewe.

Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu.

Nimemchukua pia Ruthu, Mmoabi, mjane wa Maloni, awe mke wangu, ili kuendeleza jina la marehemu pamoja na mali zake, ili jina lake marehemu lisitoweke miongoni mwa jamaa yake wala katika kumbukumbu za mji wake. Leo hivi ninyi ni mashahidi!”

Elikana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?”

Naye akaweka nadhiri, akisema, “Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwa BWANA kwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.”

Niliomba mtoto huyu, naye BWANA amenijalia kile nilichomwomba. Hivyo sasa ninamtoa kwa BWANA. Kwa maana maisha yake yote atakuwa ametolewa kwa BWANA.” Naye akamwabudu BWANA huko.

Wana wa Eli walikuwa watu wabaya kabisa, hawakumheshimu BWANA.

Lakini Samweli alikuwa akihudumu mbele za BWANA, kijana akivaa kisibau cha kitani.

Naye kijana Samweli akaendelea kukua katika kimo, akimpendeza BWANA na wanadamu.

Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Atakapokosea nitamwadhibu kwa fimbo ya wanadamu, kwa adhabu ya kupigwa na wanadamu.

Hata hivyo, Mfalme Solomoni akawapenda wanawake wengi wa kigeni zaidi, mbali na binti Farao: wanawake wa Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni na Wahiti. Wakitoka katika mataifa ambayo BWANA aliwaambia Waisraeli, “Msije mkaoana nao, kwa hakika wataigeuza mioyo yenu mgeukie miungu yao.” Hata hivyo, Solomoni akakaza kuwapenda. Alikuwa na wake 700 wa uzao wa kifalme na masuria 300, nao hao wake zake wakampotosha. Kadiri Solomoni alivyozidi kuzeeka, wake zake wakageuza moyo wake kuelekea miungu mingine, na moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA Mungu wake, kama ulivyokuwa moyo wa Daudi baba yake.

Kwa hiyo, msiwaoze binti zenu kwa wana wao wala binti zao kwa wana wenu. Msitafute mkataba wa urafiki nao kwa wakati wo wote. Ndipo mtakapofanikiwa na kula mema ya nchi na kuwaachia watoto wenu nchi hiyo kama urithi wao wa milele.’

Ndipo Kuhani Ezra aliposimama akawaambia, “Mmekosa uaminifu, mmeoa wanawake wa kigeni, mkaongezea hatia ya Israeli. Sasa tubuni kwa BWANA, Mungu wa baba zenu mkafanye mapenzi yake. Jitengeni na mataifa wanaowazunguka na wake zenu wa kigeni.” Kusanyiko lote likajibu kwa sauti kubwa: “Uko sawa kabisa! Ni lazima tufanye kama unavyosema.

Mke wake akamwambia, “Je, bado unashikamana na uadilifu wako? Mlaani Mungu nawe ukafe!” Akamjibu, “Unazungumza kama vile ambavyo mwanamke mpumbavu ye yote angelinena. Je, tupokee mema mikononi mwa Mungu, nasi tusipokee na udhia?” Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi kwa kusema kwake.

Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao umeweka sifa, kwa sababu ya watesi wako, kuwanyamazisha adui na mlipiza kisasi.

ukiwatetea yatima na walioonewa, ili kwamba mwanadamu, ambaye ni udongo, asiogopeshe tena.

Hata hivyo ulinitoa tumboni, ukanifanya nikutegemee hata nilipokuwa ninanyonya matiti ya mama yangu. Nimekabidhiwa kwako tangu kuzaliwa, toka tumboni mwa mama yangu umekuwa Mungu wangu.

Hata kama baba yangu na mama wakiniacha, BWANA atanipokea.

Nilikuwa kijana na sasa ni mzee, lakini sijaona kamwe wenye haki wameachwa au watoto wao wakiomba omba chakula. Wakati wote ni wakarimu hukopesha bila masharti, watoto wao watabarikiwa.

Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi, mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu. Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni, ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima.

Baba wa yatima, mtetezi wa wajane, ni Mungu katika makao yake matakatifu. Mungu huwaweka wapweke katika jamaa, huwaongoza wafungwa wakiimba, bali waasi huishi katika nchi kame.

Nitafumbua kinywa changu kwa mafumbo, nitazungumza mambo yaliyofichika, mambo ya kale: yale ambayo tuliyasikia na kuyajua, yale ambayo baba zetu walituambia. Hatutayaficha kwa watoto wao; tutakiambia kizazi kijacho matendo yastahiliyo sifa ya BWANA, uweza wake, na maajabu aliyoyafanya. Aliagiza amri kwa Yakobo na akaweka sheria katika Israeli, ambazo aliwaamuru baba zetu wawafundishe watoto wao, ili kizazi kijacho kizijue, pamoja na watoto ambao watazaliwa, nao pia kwa wakati wao wapate kuwaeleza watoto wao. Ndipo wangeweka tumaini lao kwa Mungu, nao wasingesahau matendo yake, bali wangalizishika amri zake. Ili kwamba wasifanane na baba zao, waliokuwa kizazi cha ukaidi na uasi, ambao roho zao hazikuwa na uaminifu kwake, ambao roho zao hazikumwamini yeye.

Teteeni wanyonge na yatima, tunzeni haki za maskini na walioonewa.

Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake, ndivyo BWANA anavyowahurumia wale wanaomcha;

Lakini kutoka milele hata milele upendo wa BWANA uko kwa wale wamchao, nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao:

Enyi wazao wa Abrahamu mtumishi wake, Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye ndiye BWANA Mungu wetu, hukumu zake zimo duniani pote. Hulikumbuka Agano lake milele, neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,

Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake, akiwa mama wa watoto mwenye furaha. Msifuni BWANA.

BWANA na awawezeshe kuongezeka, ninyi na watoto wenu.

Wana ni urithi utokao kwa BWANA, watoto ni zawadi kutoka kwake. Kama mishale mikononi mwa shujaa ndivyo walivyo wana awazaao mtu katika ujana wake. Heri mtu ambaye podo lake limejazwa nao. Hawataaibishwa wanaposhindana na adui zao langoni.

Mke wako atakuwa kama mzabibu uzaao katika nyumba yako; wana wako watakuwa kama machipukizi ya mizeituni kuizunguka meza yako.

nawe ujaliwe kuishi uone watoto wa watoto wako. Amani iwe juu ya Israeli.

(Wimbo Wa Kwenda Juu. Wa Daudi) Tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza wakati ndugu wanapoishi pamoja katika umoja!

Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani; uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu. Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa kwa namna ya ajabu na ya kutisha; kazi zako ni za ajabu, ninajua hayo kikamilifu. Umbile langu halikufichika kwako, nilipoumbwa mahali pa siri. Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi, macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika. Siku zangu zote ulizonipangia ziliandikwa katika kitabu chako kabla haijakuwapo hata moja.

wanaume vijana na wanawali, wazee na watoto. Wote na walisifu jina la BWANA, kwa maana jina lake pekee limetukuka, utukufu U juu ya nchi na mbingu.

Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako, wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

Mwanangu, usidharau marudi ya BWANA na usichukie kukaripiwa naye, kwa sababu BWANA huwarudi wale awapendao, kama vile baba afanyavyo kwa mwana apendezwaye naye.

Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba yenu, sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu. Ninawapa mafundisho ya maana, kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu. Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu, ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu, baba alinifundisha akisema, “Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote, yashike maagizo yangu na wewe utaishi.

Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia, nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Ninakuongoza katika njia ya hekima na kukuongoza katika mapito yaliyonyooka.

Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia, sikiliza kwa makini maneno yangu. Usiruhusu yaondoke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako, kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata na afya kwa mwili wote wa mwanadamu. Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo, maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.

Chemchemi yako na ibarikiwe na umfurahie mke wa ujana wako. Kulungu jike apendaye, kulungu mzuri, matiti yake na yakutosheleze siku zote, nawe utekwe daima na upendo wake.

Mwanangu, zishike amri za baba yako, wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

Mithali za Solomoni: Mwana mwenye hekima huleta furaha kwa baba yake, lakini mwana mpumbavu huleta huzuni kwa mama yake.

Yeye aletaye taabu kwa jamaa yake atarithi tu upepo, naye mpumbavu atakuwa mtumishi wa wenye hekima.

Mke mwenye tabia nzuri ni taji ya mumewe, bali aaibishaye ni kama uozo katika mifupa ya mumewe.

Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya babaye, bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.

Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi, bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa kwa ajili ya wenye haki.

Yeye aizuiaye fimbo yake hampendi mwanawe, bali yeye ampendaye huwa mwangalifu kumwadibisha.

Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake, bali mpumbavu huibomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe.

Mpumbavu hubeza maonyo ya baba yake, bali ye yote akubaliye maonyo huonyesha busara.

Mwana mwenye hekima huleta furaha kwa baba yake, bali mtu mpumbavu humdharau mama yake.

Mtumishi mwenye hekima atatawala juu ya mwana aaibishaye, naye atashirikiana katika urithi kama mmoja wa hao ndugu.

Wana wa wana ni taji la wazee, nao wazazi ni fahari ya watoto wao.

Rafiki hupenda wakati wote naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.

Mwana mpumbavu huleta huzuni kwa baba yake na uchungu kwa yeye aliyemzaa.

Apataye mke apata kitu chema naye ajipatia kibali kwa BWANA.

Mwana mpumbavu ni maangamizi ya babaye, naye mke mgomvi ni kama kutonatona kusikoisha. Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi, bali mke mwenye busara hutoka kwa BWANA.

Mrudi mwanao, wakati bado liko tumaini, wala nafsi yako isifadhaike kwa kulia kwake.

Yeye amwibiaye baba yake na kumfukuza mama yake ni mwana aletaye aibu na fedheha.

Mtu mwenye haki huishi maisha yasiyo na lawama, wamebarikiwa watoto wake baada yake.

Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake, kama tabia yake ni safi na adili.

Ikiwa mtu atamlaani baba yake au mama yake, taa yake itazimwa katika giza nene.

Urithi upatikanao haraka mwanzoni, hautabarikiwa mwishoni.

Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.

Ni afadhali kuishi jangwani kuliko kuishi na mke mgomvi na mkorofi.

Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea, naye hataiacha hata akiwa mzee.

Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto, bali fimbo ya adhabu itaufukuzilia mbali naye.

Usimnyime mtoto adhabu, kwa maana ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa. Mwadhibu kwa fimbo na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini. Mwanangu, kama moyo wako una hekima, basi moyo wangu utafurahi, utu wangu wa ndani utafurahi, wakati midomo yako itakapozungumza lililo sawa.

Msikilize baba yako, aliyekuzaa, wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee. Nunua kweli wala usiiuze, pata hekima, adabu na ufahamu. Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa, naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia. Baba yako na mama yako na wafurahi, mama aliyekuzaa na ashangilie! Mwanangu, nipe moyo wako, macho yako na yafuate njia zangu,

Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.

Mke mgomvi ni kama matone yasiyokoma ya siku ya mvua.

Yeye ashikaye sheria ni mwana mwenye hekima, bali rafiki wa walafi humwaibisha baba yake.

Yeye amwibiaye babaye au mamaye na kusema, “Si kosa,” yeye ni mwenzi wa yule aharibuye.

Fimbo ya maonyo hutia hekima, bali mtoto aliyeachiwa bila maonyo humwaibisha mama yake.

Mrudi mwanao, naye atakupa amani, atakufurahisha nafsi yako.

“Wako watu wale ambao huwalaani baba zao na wala hawawabariki mama zao; wale ambao ni safi machoni pao wenyewe kumbe hawakuoshwa uchafu wao; wale ambao daima macho yao ni ya kiburi, ambao kutazama kwao ni kwa dharau;

“Jicho lile limdhihakilo baba, lile linalodharau kumtii mama, litang'olewa na kunguru wa bondeni, litaliwa na tai.

“Kuna vitu vitatu vinavyonishangaza sana, naam, vinne nisivyovielewa: Ni mwendo wa tai katika anga, mwendo wa nyoka juu ya mwamba, mwendo wa meli katika maji makuu ya bahari, nao mwendo wa mtu pamoja na msichana.

“Ee mwanangu, Ee mwana wa tumbo langu, Ee mwana wa nadhiri zangu, Usitumie nguvu zako kwa wanawake, uhodari wako kwa wale wanaowaharibu wafalme.

Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata? Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani. Mume wake anamwamini kikamilifu wala hakosi kitu cho chote cha thamani. Humtendea mumewe mema, wala si mabaya, siku zote za maisha yake. Huchagua sufu na kitani naye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii. Yeye ni kama meli za biashara akileta chakula chake kutoka mbali. Yeye huamka kungali bado giza huwapa jamaa yake chakula na mafungu kwa watumishi wake wa kike. Huangalia shamba na kulinunua, kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu. Hufanya kazi zake kwa nguvu, mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake. Huona kwamba biashara yake ina faida, wala taa yake haizimiki usiku. Huweka mikono yake kwenye pia, navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi. Huwanyoshea maskini mikono yake na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake. Theluji ishukapo, hana hofu kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake, kwa maana wote wamevikwa nguo za kutia joto. Hutengeneza mazulia ya urembo ya kufunika kitanda chake, yeye huvaa kitani safi na urujuani. Mume wake anaheshimiwa kwenye lango la mji, aketipo miongoni mwa wazee wa nchi. Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza, naye huwauzia wafanyabiashara mishipi. Amevikwa nguvu na heshima, anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo. Huzungumza kwa hekima na mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake. Huangalia mambo ya nyumbani mwake wala hali chakula cha uvivu. Watoto wake huamka na kumwita mbarikiwa na mumewe pia, naye humsifu: “Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri, lakini wewe umewapita wote.” Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu, uzuri unapita upesi, bali mwanamke anayemcha BWANA atasifiwa. Mpe thawabu anayostahili, nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.

Wawili ni afadhali kuliko mmoja, kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao: Kama mmoja akianguka, mwenzake atamwinua. Lakini ni jambo la kuhuzunisha kwa mtu yule aangukaye naye hana wa kumwinua! Pia, kama wawili wakilala pamoja watapashana joto. Lakini ni vipi mtu aweza kujipasha joto mwenyewe? Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa, watu wawili wanaweza kumkabili adui na kumshinda. Kamba ya nyuzi tatu haikatiki kwa urahisi.

Furahia maisha na mke wako, umpendaye, siku zote za maisha ya ubatili uliyopewa na Mungu chini ya jua, siku zote za ubatili. Kwa maana hili ndilo fungu lako katika maisha na katika kazi yako ya taabu chini ya jua.

Kama vile usivyofahamu njia ya upepo, au jinsi mwili uumbwavyo ndani ya tumbo la mama, vivyo hivyo huwezi kufahamu kazi ya Mungu, Muumba wa vitu vyote.

Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku za taabu, wala haijakaribia miaka utakaposema, “Mimi sifurahii hiyo”:

Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni, mumtazame Mfalme Solomoni akiwa amevaa taji, taji ambalo mama yake alimvika siku ya arusi yake, siku ambayo moyo wake ulishangilia.

Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli.

Kwa maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, nao utawala utakuwa mabegani mwake. Naye ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.

Kama mwanamke mwenye mimba aliyekaribia kuzaa anavyogaagaa na kulia kwa ajili ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa mbele zako, Ee BWANA. Tulikuwa na mimba, tuligaagaa kwa maumivu, lakini tulizaa upepo. Hatukuleta wokovu duniani, hatujazaa watu katika ulimwengu huu.

Walio hai, walio hai, wanakusifu, kama ninavyofanya leo; baba huwaambia watoto wao habari za uaminifu wako.

Nisikilizeni, Enyi visiwa, sikieni hili, ninyi mataifa mlio mbali: Kabla sijazaliwa BWANA aliniita, tangu kuzaliwa kwangu amelitaja jina langu.

“Je, mama aweza kumsahau mtoto aliyeko matitini mwake akinyonya, wala asiwe na huruma juu ya mtoto aliyemzaa? Ingawa anaweza kusahau, mimi sitakusahau wewe!

Kwa maana Muumba wako ndiye mume wako, BWANA Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ni Mkombozi wako, yeye anaitwa Mungu wa dunia yote. BWANA atakuita urudi kana kwamba ulikuwa mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni; kama mke aliyeolewa bado angali kijana na kukataliwa,” asema Mungu wako.

Watoto wako wote watafundishwa na BWANA, nayo amani ya watoto wako itakuwa kuu.

Ninafurahia sana katika BWANA, nafsi yangu inashangilia katika Mungu wangu. Kwa maana amenivika mavazi ya wokovu na kunipamba kwa joho la haki, kama vile bwana arusi apambavyo kichwa chake kama kuhani, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vito vyake vya thamani.

Kama vile mwanaume kijana aoavyo mwanamwali, ndivyo wanao watakavyokuoa wewe; kama bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi wake, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.

Kama mama anavyomfariji mtoto wake, ndivyo nitakavyokufariji wewe, nawe utafarijiwa huko Yerusalemu.”

“Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako, nilikujua; kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalum; nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.”

“Kama mtu akimpa talaka mkewe, naye akamwacha na akaolewa na mtu mwingine, je, huyo mume aweza kumrudia tena? Je, hiyo nchi haitanajisika kabisa? Lakini umeishi kama kahaba na wapenzi wengi: je, sasa utanirudia tena?” asema BWANA.

Nilimpa Israeli asiye mwaminifu hati yake ya talaka na kumfukuza kwa ajili ya uzinzi wake wote. Hata hivyo nikaona kuwa Yuda dada yake asiyemwaminifu hakuogopa, pia alitoka na kufanya uzinzi.

“Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu,” asema BWANA. “Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka kwenye mji na wawili kutoka kwenye ukoo, nami nitawaleta Sayuni.

kama msipomwonea mgeni, yatima wala mjane na kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, nanyi kama msipofuata miungu mingine kwa madhara yenu wenyewe, ndipo nitawaacha mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa baba zenu milele na milele.

Oeni wake na mzae wana na binti, waozeni wana wenu wake nanyi watoeni binti zenu waolewe, ili nao pia wazae wana na binti. Ongezekeni idadi yenu huko, wala msipungue.

“ ‘Kwa sababu hukuzikumbuka siku za ujana wako, lakini ulinikasirisha kwa mambo haya yote, hakika nitaleta juu ya kichwa chako yale uliyotenda, asema BWANA Mwenyezi. Je hukuongeza uasherati juu ya matendo yako yote ya kuchukiza? “ ‘Kila mtu atumiaye maneno ya mithali hii, atayatumia juu yako: “Alivyo mama, ndivyo alivyo bintiye.”

Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa. Mwana hataadhibiwa kwa ajili ya makosa ya baba yake, wala baba hataadhibiwa kwa ajili ya makosa ya mwanawe. Haki ya mtu mwenye haki itahesabiwa juu yake na uovu wa mtu mwovu utalipizwa juu yake.

Niliwaambia watoto wao kule jangwani, “Msifuate amri za baba zenu wala kushika sheria zao au kujinajisi kwa sanamu zao.

Ndani yako wamewadharau baba na mama, ndani yako wamewatendea wageni udhalimu na kuwaonea yatima na wajane.

Wasioe wanawake wajane wala walioachika, inawapasa kuoa wanawake bikira wenye heshima wa Israeli au wajane wa makuhani.

Nitakuposa uwe wangu milele; nitakuposa kwa uadilifu na haki, kwa upendo na huruma. Nitakuposa kwa uaminifu, nawe utamkubali BWANA.

Waelezeni watoto wenu, na watoto wenu wawaambie watoto wao, na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata.

Omboleza kama bikira aliyevaa nguo ya gunia anayehuzunika kwa ajili ya mume wa ujana wake.

“Hata itakuwa, baada ya hayo, nitamimina Roho yangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono.

Je, watu wawili hutembea pamoja wasipokubaliana kufanya hivyo?

Kwa kuwa mwana humdharau baba yake, naye binti huinuka dhidi ya mama yake, mkwe kuwa kinyume na mama mkwe wake: adui wa mtu ni wale wa nyumbani mwake hasa.

“Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: ‘Fanyeni hukumu za haki, onyesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’

Mnauliza, “Kwa nini?” Ni kwa sababu BWANA ni shahidi kati yako na mke wa ujana wako, kwa sababu umevunja uaminifu naye, ingawa yeye ni mwenzako, mke wa agano lako la ndoa. Je, BWANA hakuwafanya wao kuwa mmoja? Katika mwili na katika roho wao ni wa Mungu. Kwa nini wawe mmoja? Kwa sababu Mungu alikuwa akitafuta mzao mwenye kumcha Mungu. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, mtu asivunje uaminifu kwa mke wa ujana wake. “Ninachukia kuachana,” asema BWANA, Mungu wa Israeli, “pia nachukia mtu anayejivika jeuri kama vazi,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, wala msije mkavunja uaminifu.

Ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, la sivyo nitakuja na kuipiga nchi kwa laana.”

Habari za ukoo wa Yesu Kristo mwana wa Daudi, mwana wa Abrahamu: Abrahamu akamzaa Isaki, Isaki akamzaa Yakobo, Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake, Yuda akamzaa Peresi na Zera, ambao mama yao alikuwa Tamari, Peresi akamzaa Hesroni, Hesroni akamzaa Aramu, Aramu akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nashoni, Nashoni akamzaa Salmoni, Salmoni akamzaa Boazi, na mama yake Boazi alikuwa Rahabu, Boazi akamzaa Obedi, ambaye mama yake alikuwa Ruthu, Obedi akamzaa Yese, Yese akamzaa Daudi ambaye alikuwa mfalme. Daudi akamzaa Solomoni, ambaye mama yake ni yule aliyekuwa mke wa Uria. Solomoni akamzaa Rehoboamu, Rehoboamu akamzaa Abiya, Abiya akamzaa Asa, Asa akamzaa Yehoshafati, Yehoshafati akamzaa Yoramu, Yoramu akamzaa Uzia, Uzia akamzaa Yothamu, Yothamu akamzaa Ahazi, Ahazi akamzaa Hezekia, Hezekia akamzaa Manase, Manase akamzaa Amoni, Amoni akamzaa Yosia, wakati wa uhamisho wa Babeli, Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake. Baada ya uhamisho wa Babeli: Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli akamzaa Zerubabeli, Zerubabeli akamzaa Abiudi, Abiudi akamzaa Eliakimu, Eliyakimu akamzaa Azori, Azori akamzaa Zadoki, Zadoki akamzaa Akimu, Akimu akamzaa Eliudi, Eliudi akamzaa Eleazari, Eleazari akamzaa Matani, Matani akamzaa Yakobo, naye Yakobo akamzaa Yosefu ambaye alikuwa mumewe Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo.

Hivyo, kulikuwapo na jumla ya vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi hadi wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli, na vizazi kumi na vinne tangu wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli hadi Kristo.

Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri. Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao.” Haya yote yametukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema: “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli,” maana yake, “Mungu pamoja nasi.” Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake. Lakini hawakukutana kimwili mpaka Maria alipojifungua mwanawe kifungua mimba akamwita Jina lake Yesu.

Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake, wakamsujudu na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane.

Lakini mimi nawaambia kwamba, ye yote atakayemkasirikia ndugu yake wa kiume au wa kike, atapaswa hukumu. Tena, ye yote atakayemwambia ndugu yake wa kiume au wa kike, ‘Raca’, yaani kumdharau na kumdhihaki, atapaswa kufanyiwa baraza. Lakini ye yote atakayesema ‘Wewe mpumbavu ulaaniwe!’ Atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu. “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, iache sadaka yako hapo, mbele ya madhabahu, uende kwanza ukapatane na ndugu yako wa kiume au wa kike, kisha urudi na ukatoe sadaka yako.

“Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu ye yote amwachaye mkewe na ampe hati ya talaka.’ Lakini mimi nawaambia, ye yote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na ye yote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa azini.

“Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka? Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua jinsi ya kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao?

“Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. Kwa maana nimekuja kumfitini “ ‘mtu na babaye, binti na mamaye, mkwe na mama mkwe wake; nao adui za mtu watakuwa ni wale watu wa nyumbani kwake.’ “Ye yote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Ye yote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda Mimi, hastahili kuwa wangu.

Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja iliyogawanyika dhidi yake yenyewe haiwezi kusimama.

Wakati alipokuwa angali anazungumza na makutano, mama yake na ndugu zake walisimama nje wakitaka kuongea naye. Ndipo mtu mmoja akamwambia, “Tazama mama Yako na ndugu Zako wamesimama nje, wanataka kuongea na wewe.” Lakini yeye akamjibu na kumwambia yule mtu, “Mama yangu ni nani, nao ndugu zangu ni nani?” Akiwanyoshea mkono wanafunzi wake, akasema, “Hawa hapa ndio mama yangu na ndugu Zangu! Kwa maana ye yote afanyaye mapenzi ya Baba yangu wa mbinguni, ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu.”

“Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Maria, nao ndugu zake si Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? Nao dada zake wote hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?” Wakachukizwa naye. Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika nchi yake na nyumbani kwake.”

Kwa maana Mungu alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako’ na ‘Ye yote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’ Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia kimewekwa wakfu kwa Mungu,’ basi hana tena sababu ya kumsaidia baba yake. Basi kwa ajili ya mafundisho yenu mnavunja amri ya Mungu.

Yesu akamwita mtoto mdogo na kumsimamisha katikati yao. Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni. Kwa hiyo mtu ye yote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni. “Ye yote amkaribishaye mtoto mdogo kama huyu kwa Jina langu, anikaribisha mimi. Lakini kama mtu ye yote anamsababisha mmojawapo wa hawa wadogo wanaoniamini atende dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake na kutoswa katika kilindi cha bahari.

“Angalia ili usimdharau mmojawapo wa hawa wadogo, kwa maana nawaambia, malaika wao mbinguni daima wanauona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [

“Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako.

Ndipo Petro akamjia Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?” Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

Baadhi ya Mafarisayo wakamjia ili kumjaribu wakamwuliza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake kwa sababu yo yote?” Akawajibu, “Je, hamkusoma kwamba hapo mwanzo Muumba aliwaumba mtu mume na mtu mke. Naye akasema, ‘Kwa sababu hii mtu atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja?’ Hivyo si wawili tena, bali ni mwili mmoja. Kwa hiyo kile alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.” Wakamwuliza, “Kwa nini basi Mose aliagiza mtu kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?” Yesu akawajibu, “Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo. Mimi nawaambia, ye yote amwachaye mkewe isipokuwa kwa sababu ya uasherati naye akaoa mke mwingine, anazini. Naye amwoaye yule mwanamke aliyeachwa pia anazini.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Kama hali ndiyo hii kati ya mume na mke, ni afadhali mtu asioe!”

Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta. Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mbinguni ni wa wale walio kama hawa.”

Kila mmoja aliyeacha nyumba au ndugu zake wa kiume au wa kike au baba au mama au watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo na ataurithi uzima wa milele.

Wakamwuliza Yesu, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?” Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma, “ ‘Kutoka katika vinywa vya watoto wachanga na wale wanaonyonya umeamuru sifa kamili?’ ”

“Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja. “Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba karamu iko tayari kwa ajili yenu, nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono. Karibuni.’

Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni ye yote mtakayemwona’ Wale watumishi wakaenda barabarani wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni. “Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi. Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema.

Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kwamba hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumwuliza swali, wakisema, “Mwalimu, Mose alisema, ‘Kama mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’ Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane. Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili na wa tatu, hadi wote saba. Hatimaye, yule mwanamke naye akafa. Sasa basi, siku ile ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?” Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui maandiko wala uweza wa Mungu. Wakati wa ufufuo watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa Mungu mbinguni. Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia kwamba, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo?’ Yeye si Mungu wa wafu bali ni Mungu wa walio hai.”

Nanyi msimwite mtu ye yote ‘Baba,’ hapa duniani kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni.

Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia kwenye safina,

“Wakati huo, Ufalme wa Mbinguni utakuwa kama wanawali kumi waliochukua taa zao na kwenda kumlaki bwana arusi.

Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo),

Nayo nyumba kama ikigawanyika yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama.

Kisha wakaja ndugu zake Yesu pamoja na mama yake. Wakiwa wamesimama nje, wakamtuma mtu kumwita. Umati wa watu ulikuwa umeketi kumzunguka wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.” Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?” Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama zangu na ndugu zangu. Mtu ye yote anayetenda mapenzi ya Mungu huyo ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu.”

Huyu si yule seremala, mwana wa Maria? Na ndugu zake si Yakobo, Yosefu, Yuda na Simoni? Dada zake wote si tuko nao hapa petu?” Nao wakachukizwa sana kwa ajili yake wakakataa kumwamini. Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika mji wake mwenyewe na miongoni mwa jamaa na ndugu zake.”

Kwa mfano, Mose alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako’ na ‘Ye yote amtukanaye baba yake au mama yake auawe.’ Lakini ninyi mwasema mtu akimwambia baba yake au mama yake kuwa, ‘Msaada ambao ningekupa ni Korbani’ (yaani, umetengwa kama sadaka kwa Mungu), basi hawajibiki tena kumsaidia baba yake au mama yake. Kwa njia hiyo ninyi mnabatilisha neno la Mungu kwa taratibu zenu mlizojiwekea. Nanyi mnafanya mambo mengi ya jinsi hiyo.”

Kisha akamchukua mtoto mdogo akamsimamisha katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, “Mtu ye yote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo, kwa Jina langu anikaribisha mimi. Naye anikaribishaye mimi, amkaribisha Baba yangu aliyenituma.”

“Kama mtu ye yote akimsababisha mmojawapo wa wadogo hawa wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa afadhali mtu huyo afungiwe shingoni mwake jiwe kubwa la kusagia na kutoswa baharini.

Baadhi ya Mafarisayo wakaja ili kumjaribu kwa kumwuliza, “Je, ni halali mtu kumwacha mke wake?” Yesu akawajibu, “Je, Mose aliwaamuru nini?” Wakajibu, “Mose aliruhusu kwamba mume anaweza kumwandikia mkewe hati ya talaka na kumwacha.” Yesu akawaambia, “Mose aliwaandikia sheria hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mume na mke. Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe na hao wawili, watakuwa mwili mmoja.’ Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena bali mwili mmoja. Basi, alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.” Walipokuwa tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza kuhusu jambo hili. Akawajibu, “Mtu ye yote anayemwacha mkewe na kuoa mke mwingine, azini naye. Naye mwanamke anayemwacha mumewe na kuolewa na mume mwingine, anazini.”

Watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse lakini wanafunzi wake wakawakemea. Yesu alipoona yaliyokuwa yakitukia akachukizwa, akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa watu kama hawa. Amin, amin nawaambia, mtu ye yote asiyeukubali Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.” Akawachukua watoto mikononi mwake, akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.

Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”

Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna mtu ye yote aliyeacha nyumba, ndugu wa kiume, au ndugu wa kike, mama, baba, watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, ambaye hatalipwa mara mia katika ulimwengu huu, nyumba, ndugu wa kiume, ndugu wa kike, mama, baba, watoto, mashamba pamoja na mateso, kisha uzima wa milele katika ulimwengu ujao.

wakasema, “Mwalimu, Mose alituandikia kuwa kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi ndugu yake atamwoa huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto. Basi walikuwapo ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa na akafa pasipo kuwa na mtoto ye yote. Wa pili akamwoa yule mjane, lakini naye akafa bila kuacha mtoto ye yote. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa tatu. Hakuna hata mmojawapo wa hao ndugu wote saba aliyeacha mtoto. Hatimaye yule mwanamke naye akafa. Kwa hiyo wakati wa ufufuo, watakapofufuka wote, huyo atakuwa mke wa nani maana aliolewa na ndugu wote saba?” Yesu akawajibu, “Je, hampotoki kwa sababu hamjui maandiko wala uweza wa Mungu? Wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa, watakuwa kama malaika wa mbinguni. Basi kuhusu ufufuo wa wafu: Je, hamjasoma katika kitabu cha Mose jinsi Mungu alivyosema na Mose kutoka katika kile kichaka akisema, ‘Mimi, ni Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Isaki na Mungu wa Yakobo?’

“Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, baba atamsaliti mwanawe. Watoto watawaasi wazazi wao na kusababisha wauawe.

Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zekaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji cho chote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake. Naye atawageuza wengi wa wana wa Israeli warudi kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki na kuliweka tayari taifa lililoandaliwa kwa ajili ya Bwana.”

Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yosefu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Maria. Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!” Maria akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni, “Salamu hii ni ya namna gani?” Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, umepata kibali kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume na utamwita jina lake Yesu. Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. BWANA Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Maria akamwuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?” Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli, kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu.

Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu, akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa. Lakini ni kwa nini mimi nimepata upendeleo kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliyeko tumboni mwangu aliruka kwa furaha.

Hivyo Yosefu akapanda kutoka mji wa Nazareti ulioko Galilaya kwenda Uyahudi, mpaka Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi. Alikwenda huko kujiandikisha pamoja na Maria, ambaye alikuwa amemposa naye alikuwa mjamzito. Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Maria wa kujifungua ukawa umetimia, naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori ya kulia ng'ombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni.

Hata zilipotimia siku nane, ulikuwa ndio wakati wa kumtahiri mtoto, akaitwa Yesu, jina alilokuwa amepewa na malaika kabla hajatungwa mimba. Ulipotimia wakati wa utakaso wake Maria, kwa mujibu wa Sheria ya Mose, Yosefu na Maria walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”),

Yosefu na Maria mama yake walipomwona walishangaa. Mama yake akamwuliza, “Mwanangu, mbona umetufanyia hivi? Tazama, mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta kwa wasiwasi mkubwa kila mahali.” Yesu akawaambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua kwamba imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” Lakini wao hawakuelewa maana ya lile alilowaambia. Ndipo akashuka pamoja nao hadi Nazareti, naye alikuwa mtii kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote.

Yesu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza huduma yake. Alikuwa akidhaniwa kuwa mwana wa Yosefu, Yosefu alikuwa mwana wa Eli, Eli alikuwa mwana wa Mathati, Mathati alikuwa mwana wa Lawi, Lawi alikuwa mwana wa Melki, Melki alikuwa mwana wa Yanai, Yanai alikuwa mwana wa Yosefu, Yosefu alikuwa mwana wa Matathia, Matathia alikuwa mwana wa Amosi, Amosi alikuwa mwana wa Nahumu, Nahumu alikuwa mwana wa Esli, Esli alikuwa mwana wa Nagai, Nagai alikuwa mwana wa Maathi, Maathi alikuwa mwana wa Matathia, Matathia alikuwa mwana Semeini, Semeini alikuwa mwana wa Yoseki, Yoseki alikuwa mwana wa Yoda, Yoda alikuwa mwana wa Yoanani, Yoanani alikuwa mwana wa Resa, Resa alikuwa mwana wa Zerubabeli, Zerubabeli alikuwa mwana wa Shealtieli, Shealtieli alikuwa mwana wa Neri, Neri alikuwa mwana wa Melki, Melki alikuwa mwana wa Adi, Adi alikuwa mwana wa Kosamu, Kosamu alikuwa mwana wa Elmadamu, Elmadamu alikuwa mwana wa Eri, Eri alikuwa mwana wa Yoshua, Yoshua alikuwa mwana wa Eliezeri, Eliezeri alikuwa mwana wa Yorimu, Yorimu alikuwa mwana wa Mathati, Mathati alikuwa mwana wa Lawi, Lawi alikuwa mwana wa Simeoni, Simeoni alikuwa mwana wa Yuda, Yuda alikuwa mwana wa Yosefu, Yosefu alikuwa mwana wa Yonamu, Yonamu alikuwa mwana wa Eliakimu, Eliyakimu alikuwa mwana wa Melea, Melea alikuwa mwana wa Mena, Mena alikuwa mwana wa Matatha, Matatha alikuwa mwana wa Nathani, Nathani alikuwa mwana wa Daudi, Daudi alikuwa mwana wa Yese, Yese alikuwa mwana wa Obedi, Obedi alikuwa mwana wa Boazi, Boazi alikuwa mwana wa Salmoni, Salmoni alikuwa mwana wa Nashoni, Nashoni alikuwa mwana wa Aminadabu, Aminadabu alikuwa mwana wa Aramu, Aramu alikuwa mwana wa Hesroni, Hesroni alikuwa mwana wa Peresi, Peresi alikuwa mwana wa Yuda, Yuda alikuwa mwana wa Yakobo, Yakobo alikuwa mwana wa Isaki, Isaki alikuwa mwana wa Abrahamu, Abrahamu alikuwa mwana wa Tera, Tera alikuwa mwana wa Nahori, Nahori alikuwa mwana wa Serugi, Serugi alikuwa mwana wa Reu, Reu alikuwa mwana wa Pelegi, Pelegi alikuwa mwana wa Eberi, Eberi alikuwa mwana wa Sala, Sala alikuwa mwana wa Kenani, Kenani alikuwa mwana wa Arfaksadi, Arfaksadi alikuwa mwana wa Shemu, Shemu alikuwa mwana wa Noa, Noa alikuwa mwana wa Lameki, Lameki alikuwa mwana wa Methusela, Methusela alikuwa mwana wa Enoki, Enoki alikuwa mwana wa Yaredi, Yaredi alikuwa mwana wa Mahalaleli, Mahalaleli alikuwa mwana wa Kenani, Kenani alikuwa mwana wa Enoshi, Enoshi alikuwa mwana wa Sethi, Sethi alikuwa mwana wa Adamu, Adamu alikuwa mwana wa Mungu.

Wakati mmoja mama yake Yesu na ndugu zake walikuja kumwona, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya msongamano wa watu. Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje wanataka kukuona.” Yesu akamjibu, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wote wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”

“Je, kuna ye yote miongoni mwenu, ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala ya samaki? Au mtoto akimwomba yai atampa nge? Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu wa mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao!”

Watafarakana baba dhidi ya mwanawe na mwana dhidi ya babaye, mama dhidi ya bintiye na binti dhidi ya mamaye, mama mkwe dhidi ya mkwewe. Naye mkwe dhidi ya mama mkwe wake.”

“Mtu ye yote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe. Ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Yesu akaendelea kusema: “Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. Yule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Hivyo akawagawia wanawe mali yake. “Baada ya muda mfupi, yule mdogo akakusanya vitu vyote alivyokuwa navyo, akaenda nchi ya mbali na huko akaitapanya mali yake kwa maisha ya anasa. Baada ya kutumia kila kitu alichokuwa nacho, kukawa na njaa kali katika nchi ile yote, naye akawa hana cho chote. Kwa hiyo akaenda akaajiriwa na mwenyeji mmoja wa nchi ile ambaye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula wale nguruwe, wala hakuna mtu aliyempa cho chote. “Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa! Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili tena kuitwa mwanao, nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’ Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake. “Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu. “Yule mtoto akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’ “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake. Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi. Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena, alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.

“Mtu ye yote ampaye mkewe talaka na kumwoa mwanamke mwingine azini, naye mwanaume amwoaye mwanamke aliyetalikiwa azini.

Kwa hiyo, jilindeni. “Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe. Kama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu’, msamehe.”

Pia, watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea. Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama hawa watoto. Amin, nawaambia, ye yote ambaye hataupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”

Yesu akajibu, “Amin nawaambia, hakuna hata mmoja aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”

Baadhi ya Masadukayo, wale wasemao kwamba hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumwuliza, “Mwalimu, Mose alituandikia kwamba kama ndugu wa mtu akifa na kuacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto. Basi walikuwepo ndugu saba, wa kwanza akaoa, akafa bila kuzaa mtoto. Kisha yule wa pili akamwoa huyo mjane, naye akafa bila mtoto. Naye wa tatu pia, vivyo hivyo ndugu wote saba wakawa wamemwoa huyo mwanamke na wote wakafa pasipo kupata mtoto. Mwishowe, huyo mwanamke mjane naye akafa. Sasa basi, siku ya ufufuo huyo mwanamke atakuwa mke wa nani? Maana aliolewa na ndugu wote saba.” Yesu akawajibu, “Katika maisha haya watu huoa na kuolewa. Lakini wale ambao wamehesabiwa kwamba wanastahili kupata nafasi katika ulimwengu ule na katika ufufuo wa wafu, hawaoi wala hawaolewi.

Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. Hawa ndio waliozaliwa si kwa damu wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.

Siku ya tatu kulikuwa na arusi katika mji wa Kana ya Galilaya, naye mama yake Yesu alikuwako huko.

Bibi arusi ni wa bwana arusi. Lakini rafiki yake bwana arusi anayesimama karibu naye na kusikiliza kutoka kwake, hufurahi sana aisikiapo sauti ya bwana arusi. Kwa sababu hii furaha yangu imekamilika. Yeye hana budi kuwa mkuu zaidi na mimi nizidi kuwa mdogo.”

Yesu akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.” Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.” Yesu akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume. Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako!”

Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati ambapo Yesu alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye, pamoja na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Yesu.

Wakasema, “Huyu si Yesu, mwana wa Yosefu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?”

Yesu alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?” Yesu akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake.

Sitawaacha ninyi yatima, naja kwenu.

Mwanamke anapokuwa na utungu wa kuzaa huwa na maumivu kwa sababu saa yake imewadia. Lakini mtoto akiisha kuzaliwa, yule mwanamke husahau maumivu hayo kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtoto ulimwenguni.

Wakati huo huo karibu na msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama: Maria mama yake, Maria dada wa mamaye, yaani, mke wa Klopa na Maria Magdalene. Yesu alipomwona mama yake mahali pale pamoja na yule mwanafunzi aliyempenda wamesimama karibu, akamwambia mama yake, “Mwanamke, huyo hapo ndiye mwanao,” Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyo hapo ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Yesu nyumbani kwake.

Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwapo wanawake kadha wa kadha na Maria mama yake Yesu pamoja na ndugu zake Yesu.

“ ‘Katika siku za mwisho, asema Bwana, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu na binti zetu watatabiri, vijana wenu wataona maono na wazee wenu wataota ndoto.

Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu na kwa wale wote walio mbali na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”

Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na wote wa nyumbani mwake. Aliwapa watu sadaka nyingi na kumwomba Mungu daima.

Yeye atakupa ujumbe ambao kwa huo wewe na wa nyumbani mwako wote mtaokoka.’

Basi alipokwisha kubatizwa yeye na watu wa nyumbani mwake, alitukaribisha nyumbani mwake akisema, “Kama mmeona kweli mimi nimemwamini Bwana, karibuni mkae nyumbani mwangu.” Naye akatushawishi.

Wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na wa nyumbani mwako.” Wakamwambia neno la Bwana yeye pamoja na wote waliokuwako nyumbani mwake. Wakati ule ule yule mkuu wa gereza akawachukua akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa. Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia meza mbele yao, yeye pamoja na wa nyumbani mwake wote wakafurahi sana kwa kuwa amemwamini Mungu.

Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka katika sheria ya ndoa. Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi.

Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu hao ndio watoto wa Mungu. Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, yaani, Baba,” Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu. Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.

Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka katika utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa uchungu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa.

Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.

Basi kuhusu mambo yale mliyoniandikia: Ni vyema mwanaume asimguse mwanamke. Lakini ili kuepuka zinaa, kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. Mume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe, naye vivyo hivyo mke kwa mumewe. Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe. Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda fulani ili mweze kujitoa kwa maombi, kisha mrudiane tena ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi. Nasema haya kama ushauri na si amri. Laiti watu wangekuwa kama mimi nilivyo. Lakini kila mtu amepewa kipawa chake kutoka kwa Mungu, mmoja ana kipawa cha namna hii na mwingine ana cha namna ile.

Kwa wale wasiooa na kwa wajane, ingekuwa vizuri wabaki kama mimi nilivyo. Lakini kama hawawezi kujizuia, basi waoe na kuolewa, kwa maana ni afadhali kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa. Kwa wale waliooana nawapa amri (si mimi ila ni Bwana): Mke asimwache mumewe. Lakini kama akimwacha, ni lazima akae bila kuolewa, ama sivyo apatane tena na mumewe. Wala mume asimpe mkewe talaka.

Lakini kwa wengine nasema (si Bwana ila ni mimi): Kama ndugu ana mke asiyeamini, naye huyo mke anakubali kuishi pamoja naye, basi asimwache. Naye mwanamke aaminiye kama ameolewa na mwanaume asiyeamini na huyo mume anakubali kuishi naye, basi huyo mwanamke asimwache. Kwa maana huyo mume asiyeamini anatakaswa kupitia mkewe, naye mke asiyeamini anatakaswa kupitia mumewe. Kama isingalikuwa hivyo watoto wenu wangalikuwa si safi, lakini ilivyo sasa wao ni watakatifu. Lakini kama yule asiyeamini akijitenga, basi afanye hivyo. Katika hali kama hiyo mwanamke au mwanaume aaminiye hafungwi, kwa sababu Mungu ametuita tuishi kwa amani. Wewe mke, unajuaje kama utamwokoa mumeo? Au wewe mume unajuaje kama utamwokoa mkeo?

Basi, kuhusu wale walio bikira, mimi sina amri kutoka kwa Bwana, lakini mimi natoa shauri kama mtu ambaye ni mwaminifu kwa rehema za Bwana. Kwa sababu ya shida iliyoko, naona ni vyema mkibaki kama mlivyo. Je, umeolewa? Basi usitake talaka. Je, hujaoa? Usitafute mke. Lakini kama ukioa, hujatenda dhambi; na kama bikira akiolewa, hajatenda dhambi. Lakini wale wanaooa watakabiliana na matatizo mengi katika maisha haya, nami nataka kuwazuilia hayo. Lakini ndugu zangu, nina maana kwamba muda uliobaki ni mfupi. Tangu sasa wale waliooa waishi kama wasio na wake;

Ningetaka msiwe na masumbufu. Mwanaume ambaye hajaoa anajishughulisha na mambo ya Bwana, yaani, jinsi ya kumpendeza Bwana. Lakini mwanaume aliyeoa anajishughulisha na mambo ya dunia, yaani, jinsi ya kumfurahisha mkewe, pia kuna tofauti kati ya mwanamke aliyeolewa na msichana bikira. Mwanamke asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana ili awe mtakatifu kimwili na kiroho, lakini yule aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia, jinsi atakavyoweza kumfurahisha mumewe. Ninasema haya kwa faida yenu, sio ili kuwawekea kizuizi cho chote, bali mpate kuishi kwa jinsi ilivyo vyema bila kuvutwa pengine katika kujitoa kwenu kwa Bwana.

Kama mtu ye yote anadhani kwamba hamtendei ilivyo sawa mwanamwali ambaye amemposa, naye akiwa umri wake unazidi kuendelea na mtu huyo anajisikia kwamba inampasa kuoa, afanye kama atakavyo. Yeye hatendi dhambi. Yawapasa waoane. Lakini kama mwanaume ambaye ameshaamua moyoni mwake kutokuoa bila kulazimishwa na mtu ye yote, kama anaweza kujitawala kabisa; basi anafanya vyema kutokumwoa huyo mwanamwali. Hivyo basi, yeye mwanaume amwoaye huyo mwanamwali afanya vyema, lakini yeye asiyemwoa afanya vyema zaidi. Mwanamke aliyeolewa amefungwa na sheria maadamu mumewe yu hai. Lakini kama mumewe akifa, basi mwanamke huyo yuko huru kuolewa na mume mwingine ampendaye, lakini lazima tu awe katika Bwana. Lakini kwa uamuzi wangu, naona kuwa angekuwa na furaha zaidi akibaki alivyo. Nami nadhani pia nina Roho wa Mungu.

Lakini napenda mfahamu kwamba kichwa cha kila mwanaume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, nacho kichwa cha Kristo ni Mungu. Kila mwanaume anayeomba au kutoa unabii akiwa amefunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake. Lakini kila mwanamke anayeomba au kutoa unabii pasipo kufunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake, kwani ni sawa na yeye aliyenyoa nywele. Kama mwanamke hatajifunika kichwa chake, basi inampasa kunyoa nywele zake. Lakini kama ni aibu kwa mwanamke kunyoa nywele zake, basi afunike kichwa chake. Haimpasi mwanaume kufunika kichwa chake kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na utukufu wa Mungu, lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume. Kwa maana mwanaume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke alitoka kwa mwanaume. Wala mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume. Kwa sababu hii na kwa sababu ya malaika, inampasa mwanamke awe na ishara ya mamlaka iliyo juu yake. Lakini katika Bwana, mwanamke hajitegemei pasipo mwanaume na mwanaume hajitegemei pasipo mwanamke. Kama vile mwanamke alivyoumbwa kutoka kwa mwanaume, vivyo hivyo mwanaume huzaliwa na mwanamke. Lakini vitu vyote vyatoka kwa Mungu. Hukumuni ninyi wenyewe: Je, inafaa kwa mwanamke kumwomba Mungu bila kufunika kichwa chake? Je, maumbile ya asili hayatufundishi kuwa ni aibu kwa mwanaume kuwa na nywele ndefu? Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni utukufu kwake. Kwa maana mwanamke amepewa nywele ndefu ili kumfunika. Kama mtu anataka kubishana juu ya jambo hili, sisi wala makanisa ya Mungu hatutambui desturi nyingine.

Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno. Upendo hauna kiburi. Haukosi kuwa na adabu. Upendo hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.

Nilipokuwa mtoto, nilisema kama mtoto, niliwaza kama mtoto, nilifikiri kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima niliacha mambo ya kitoto.

wanawake wanapaswa kuwa kimya kanisani. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama sheria isemavyo. Kama wakitaka kuuliza kuhusu jambo lo lote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza kanisani. Je, neno la Mungu lilianzia kwenu? Au ni ninyi tu ambao neno la Mungu limewafikia? Kama mtu ye yote akidhani kwamba yeye ni nabii, au ana karama za rohoni, basi na akubali kwamba haya ninayoandika ni maagizo kutoka kwa Bwana. Kama mtu akipuuza jambo hili yeye mwenyewe atapuuzwa.

Msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa, kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu? Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza? Kuna mapatano gani kati ya Kristo na Beliari? Yeye aaminiye ana sehemu gani na yeye asiyeamini? Kuna mapatano gani kati ya Hekalu la Mungu na sanamu? Kwa kuwa sisi tu Hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu alivyosema: “Nitakaa pamoja nao na kutembea katikati yao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.” “Kwa hiyo tokeni miongoni mwao, mkatengwe nao, asema Bwana. Msiguse kitu cho chote kilicho najisi, nami nitawakaribisha.” “Mimi nitakuwa Baba kwenu, nanyi mtakuwa wanangu na binti zangu, asema Bwana Mwenyezi.”

Ninawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi.

Lile nisemalo ni kwamba wakati wote mrithi akiwa bado ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ndiye mmiliki wa mali yote. Yeye huwa yuko chini ya uangalizi wa walezi na wadhamini mpaka ufike wakati uliowekwa na baba yake.

Kwa sababu ninyi ni watoto wa Mungu, Mungu amemtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, anayelia, “Abba, Baba.” Kwa hiyo, wewe si mtumwa tena, bali ni mtoto, kwa kuwa wewe ni mtoto, Mungu amekufanya wewe pia kuwa mrithi kwa kupitia Kristo.

Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu.

Ninyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Kristo alivyo kichwa cha Kanisa, ambalo ni mwili wake, naye Kristo ni Mwokozi wake. Basi, kama vile Kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo. Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake, apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lo lote, bali takatifu lisilo na hatia. Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza Kanisa lake. Sisi tu viungo vya mwili wake. “Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe na hawa wawili watakuwa mwili mmoja.” Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Kristo na Kanisa. Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.

Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.” Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.

Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe na uchungu dhidi yao. Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hivi ndivyo inavyompendeza Bwana. Ninyi akina baba msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

lakini tulikuwa wapole katikati yenu kama mama anayewatunza watoto wake wadogo.

Maana mnajua kwamba tuliwatendea kila mmoja wenu kama vile baba awatendeavyo watoto wake mwenyewe.

Vivyo hivyo nataka wanawake wajipambe kwa adabu na kwa heshima katika mavazi yanayostahili, si kwa kusuka nywele, kuvalia dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa, bali kwa matendo mazuri kama iwapasavyo wanawake wanaokiri kuwa wanamcha Mungu. Mwanamke na ajifunze kwa utulivu na kwa utii wote. Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume. Mwanamke inampasa kukaa kimya. Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza, kisha Eva. Wala si Adamu aliyedanganywa, bali ni mwanamke aliyedanganywa akawa mkosaji. Lakini mwanamke ataokolewa kwa kuzaa kwake kama wakiendelea kudumu katika imani, upendo na utakatifu, pamoja na kuwa na kiasi.

Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?)

Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasiozungumza maneno ya kuwadhuru wengine, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo. Shemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema.

Usimkemee mzee kwa ukali bali umuonye kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako, wanawake wazee uwatendee kama mama zako na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote. Waheshimu wanawake wajane ambao ni wajane kweli kweli. Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo, kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe ili wawarudishie wema ule wazazi wao waliowatendea, kwa kuwa hivi ndivyo impendezavyo Mungu.

Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.

Mjane ye yote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na ambaye alikuwa mke wa mume mmoja, awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna. Lakini kwa habari za wajane vijana usiwaweke kwenye orodha hiyo, maana tamaa zao za kimaumbile zikizidi kule kujitoa kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena. Nao kwa njia hiyo watajiletea hukumu kwa kukiuka ahadi yao ya kwanza. Zaidi ya hayo, wajane kama hao huwa na tabia ya uvivu wakizurura nyumba kwa nyumba, wala hawawi wavivu tu, bali pia huwa wasengenyaji, wajiingizao katika mambo yasiyowahusu na kusema mambo yasiyowapasa kusema. Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu. Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani. Lakini kama mwanamke ye yote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kanisa, ili kanisa liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.

Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.

Mzee wa kanisa asiwe na lawama, awe mume wa mke mmoja, mtu ambaye watoto wake ni waaminio na wala hawashtakiwi kwa ufisadi.

ili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao, wawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu ye yote asije akalikufuru neno la Mungu.

Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza utii kutokana na mateso aliyoyapata,

Kwa imani, Noa alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.

Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema: “Mwanangu, usidharau kuadibishwa na Bwana, wala usikate tamaa akikukemea, kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao, na humwadhibu kila mmoja anayemkubali kuwa mtoto wake.” Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake? Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali. Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi?

Ndoa na iheshimiwe na watu wote, nayo malazi yawe safi, kwa kuwa Mungu atawahukumu wazinzi na waasherati wote.

Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu Baba yetu, ndiyo hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.

Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, mmoja wenu akamwambia, “Enenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? Vivyo hivyo, imani peke yake kama haikuambatana na matendo, imekufa.

Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama wako wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno, kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu. Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi. Badala yake kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa ndani, kwa uzuri usioharibika, wa roho ya upole na utulivu, ambako ni kwa thamani sana machoni pa Mungu. Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao, kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara kama mkitenda yaliyo mema na bila kuogopa jambo lo lote. Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha thamani cha uzima, ili kusiwepo na cho chote cha kuzuia maombi yenu. Hatimaye, ninyi nyote iweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, wasikitivu na wanyenyekevu.

Vivyo hivyo ninyi mlio vijana hamna budi kuwatii wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu katika kuhudumiana, kila mtu na mwenzake, kwa kuwa, “Mungu huwapinga wenye kiburi bali huwapa wanyenyekevu neema.”

Sisi tunajua ya kwamba tumepita kutoka mautini kuingia uzimani, kwa sababu tunawapenda ndugu. Kila asiyempenda ndugu yake akaa mautini. Ye yote amchukiaye ndugu yake ni mwuaji, nanyi mwajua ya kwamba mwuaji hana uzima wa milele ndani yake. Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo?

Imenipa furaha kuu kuona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile Baba alivyotuagiza.

Sina furaha kubwa kuliko hii, kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.

Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua na mwezi ukiwa chini ya miguu yake na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa kichwani mwake. Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa. Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi na taji saba katika vichwa vyake. Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa. Yule mwanamke akazaa mtoto mwanamume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi. Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku 1,260.

Tufurahi, tushangilie na kumpa utukufu! Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia na bibi arusi wake amejiweka tayari. Akapewa kitani safi, nyeupe inayong'aa, ili avae.” (Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.) Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.”

Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe.

Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba ya hayo mapigo saba ya mwisho akaja akaniambia, “Njoo, nami nitakuonyesha bibi arusi, yaani, mke wa Mwana-Kondoo.”

Roho na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Naye asikiaye na aseme, “Njoo!” Ye yote mwenye kiu na aje na kila anayetaka na anywe maji ya uzima bure.

Swahili - Kiswahili - SW

NEN'2014 - Neno Bibilia Takatifu Kiswahili Contemporary Version - 2014

This Bible text is from Biblica Open Kiswahili Contemporary Version Neno 2015
https://open.bible/bibles/swahili-biblica-text-bible/
provided by: Biblica Inc, available by Creative Commons CC-BY-SA-4.0,
and this new compilation is shared as www.creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0.
Languages are made available to you by www.ipedge.net