22 – Miujiza

Haya ni maneno matakatifu ya Mungu Mwenyezi.
Hatupendi maneno ya wanadamu.
Kwa mtu yeyote anayempenda Mungu... hivi ndivyo Mungu anasema kuhusu: Miujiza.

Mistari 3 Muhimu Zaidi

Ndipo Yesu akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa mamlaka juu ya pepo wachafu kuwatoa na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila aina.

Yesu akawajibu akawaambia, “Mwaminini Mungu. Amin, amin nawaambia, mtu ye yote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng'oka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea nayo yatakuwa yenu.

Mitume wakafanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Nao wale wote walioamini walikuwa wakikusanyika katika ukumbi wa Solomoni kwa nia moja. Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. Lakini wengi walioamini idadi kubwa ya wanaume na wanawake wakaongezeka kwa Bwana. Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. Pia watu wakakusanyika kutoka katika miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu, hao wote wakaponywa.

Kila Mstari katika Mpangilio wa Biblia - 266 vifungu

Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. Wakati huu Dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu, giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametanda juu ya maji. Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo.

BWANA Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, mtu akawa kiumbe hai.

Farao akamwambia Yosefu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia ikisemwa kwa habari yako kwamba unapoelezwa ndoto waweza kuifasiri.” Yosefu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.”

Huko malaika wa BWANA akamtokea Mose katika mwali wa moto kutoka katika kichaka. Mose akaona hilo, ingawa kile kichaka kilikuwa kinawaka moto, kilikuwa hakiteketei. Ndipo Mose akawaza, “Nitageuka sasa nione kitu hiki cha ajabu, nami nione ni kwa nini kichaka hiki hakiteketei.” BWANA alipoona kuwa amegeuka ili aone, Mungu akamwita kutoka ndani ya kile kichaka, “Mose! Mose!” Naye Mose akajibu, “Mimi hapa.” Mungu akamwambia, “Usikaribie zaidi. Vua viatu vyako, kwa maana mahali unaposimama ni ardhi takatifu.”

Ndipo BWANA akamwambia, “Ni nini hicho kilicho mkononi mwako?” Akajibu, “Fimbo.” BWANA akasema, “Itupe chini.” Mose akaitupa chini hiyo fimbo nayo ikawa nyoka, naye akaikimbia. Kisha BWANA akamwambia, “Nyosha mkono wako uikamate mkiani.” Basi Mose akanyosha mkono akamkamata yule nyoka, nayo ikabadilika tena kuwa fimbo mkononi mwake. BWANA akasema, “Hivi ndivyo Waisraeli watakavyoamini kuwa BWANA, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo, amekutokea wewe.”

Kisha BWANA akamwambia, “Weka mkono wako ndani ya joho lako.” Basi Mose akaweka mkono wake ndani ya joho lake, naye alipoutoa, ulikuwa na ukoma, mweupe kama theluji. Mungu akamwambia, “Sasa urudishe tena huo mkono ndani ya joho lako.” Basi Mose akaurudisha mkono wake ndani ya joho lake na alipoutoa, ulikuwa mzima, kama sehemu zingine za mwili wake. Ndipo BWANA akamwambia, “Kama hawatakuamini wewe, au kutojali ishara ya kwanza, wataamini ishara ya pili. Lakini kama hawataamini ishara hizi mbili au hawatawasikiliza ninyi, chukua kiasi cha maji kutoka Mto Nile uyamimine juu ya ardhi kavu. Maji mtakayotoa mtoni yatakuwa damu juu ya ardhi.”

naye Aroni akawaambia kila kitu BWANA alichokuwa amemwambia Mose. Pia akafanya ishara mbele ya watu, nao wakaamini. Nao waliposikia kuwa BWANA anajishughulisha nao na kwamba ameona mateso yao, walisujudu na kuabudu.

Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, hata ingawa nitazidisha ishara na maajabu katika Misri,

“Farao atakapowaambia, ‘Fanyeni mwujiza,’ basi mwambie Aroni, ‘Chukua fimbo yako na uitupe chini mbele ya Farao,’ nayo fimbo itakuwa nyoka.” Ndipo Mose na Aroni wakaenda kwa Farao wakafanya sawasawa kama vile BWANA alivyoagiza. Aroni akaitupa ile fimbo yake chini mbele ya Farao na maafisa wake, nayo ikawa nyoka. Farao naye akawaita watu wenye maarifa na wachawi na waganga wa Kimisri, nao wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao. Kila mmoja alitupa fimbo yake chini, nayo ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza zile fimbo zao.

Mose na Aroni wakafanya kama vile BWANA alivyokuwa amewaagiza. Akainua fimbo yake machoni pa Farao na maafisa wake na kuyapiga maji ya Mto Nile, na maji yote yakabadilika kuwa damu. Samaki katika Mto Nile wakafa, nao mto ukanuka vibaya sana kiasi kwamba Wamisri hawakuweza kunywa maji yake. Damu ilikuwa kila mahali katika nchi ya Misri. Lakini waganga wa Misri kwa kutumia siri ya uganga wao wakafanya vivyo hivyo, nao moyo wa Farao ukawa mgumu, hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile BWANA alivyokuwa amesema. Badala yake, akageuka akaenda kwenye jumba lake la kifalme, wala hakulitia hili moyoni.

Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu. Kama ukikataa kuwaruhusu kuondoka, basi nitaipiga nchi yako yote kwa kuwaletea vyura. Mto Nile utafurika vyura. Watakuja kwenye jumba lako la kifalme na katika chumba chako cha kulala na kitandani mwako, katika nyumba za maafisa wako na kwa watu wako, vyura hao wataingia katika meko yenu na kwenye vyombo vya kukandia unga. Vyura watapanda juu yako, juu ya watu wako na maafisa wako wote.’ ” Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyosha mkono wako ukiwa na ile fimbo yako juu ya vijito, mifereji na madimbwi, fanya vyura waje juu ya nchi ya Misri.’ ” Ndipo Aroni akaunyosha mkono wake juu ya maji ya Misri, nao vyura wakatokea na kuifunika nchi. Lakini waganga wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao, nao pia wakafanya vyura kuja juu ya nchi ya Misri.

Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyosha fimbo yako uyapige mavumbi ya ardhi,’ nayo nchi yote ya Misri mavumbi yatakuwa viroboto.” Wakafanya hivyo, Aroni aliponyosha mkono wake wenye fimbo na kuyapiga mavumbi ya nchi, viroboto wakawajia watu na wanyama. Mavumbi yote katika nchi ya Misri yakawa viroboto. Lakini waganga walipojaribu kutengeneza viroboto kwa siri ya uganga wao, hawakuweza. Nao viroboto walikuwa juu ya watu na wanyama. Waganga wale wakamwambia Farao, “Hiki ni kidole cha Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukawa mgumu naye hakuwasikiliza, kama vile BWANA alivyosema.

Kisha BWANA akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi na usimame mbele ya Farao wakati anapokwenda mtoni nawe umwambie, ‘Hili ndilo BWANA asemalo: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu. Kama hutawaachia watu wangu waondoke nitakupelekea makundi ya mainzi juu yako, kwa maafisa wako, kwa watu wako na kwenye nyumba zenu. Nyumba za Wamisri zitajazwa mainzi, hata na ardhi yote ya Misri. “ ‘Lakini siku ile nitafanya kitu tofauti katika nchi ya Gosheni, ambapo watu wangu wanaishi, hapatakuwepo na makundi ya mainzi, ili mpate kujua kwamba Mimi, BWANA, niko katika nchi hii. Nitaweka tofauti kati ya watu wangu na watu wenu. Ishara hii ya ajabu itatokea kesho.’ ” Naye BWANA akafanya hivyo. Makundi makubwa ya mainzi yalimiminika katika jumba la kifalme la Farao na katika nyumba za maafisa wake, pia nchi yote ya Misri ikaharibiwa na mainzi.

Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo BWANA, Mungu wa Waebrania asemalo: “Waachie watu wangu waende ili wapate kuniabudu.” Kama ukikataa kuwaachia waende, nawe ukiendelea kuwashikilia, mkono wa BWANA utaleta pigo baya kwa mifugo yako, juu ya farasi wako, punda, ngamia, ng'ombe wako, kondoo na mbuzi. Lakini BWANA ataweka tofauti kati ya mifugo ya Israeli na ile ya Misri, kwamba hakuna mnyama wa Mwisraeli atakayekufa.’ ” BWANA akaweka wakati na kusema, “Kesho BWANA atalitenda hili katika nchi.” Siku iliyofuata BWANA akalitenda: Mifugo yote ya Wamisri ikafa, lakini hakuna hata mnyama mmoja wa wana wa Israeli iliyekufa. Farao akatuma watu kuchunguza, nao wakakuta kuwa hakuna hata mnyama mmoja wa Waisraeli aliyekufa. Lakini moyo wa Farao haukukubali kuwaachia watu waende.

Kisha BWANA akamwambia Mose na Aroni, “Chukueni majivu ya tanuru, naye Mose ayarushe angani mbele ya Farao. Yatakuwa vumbi jepesi juu ya nchi yote ya Misri, pia yatatokea majipu yenye kufura juu ya watu na wanyama katika nchi yote.” Basi wakachukua majivu kwenye tanuru na kusimama mbele ya Farao. Mose akayarusha hewani, nayo majipu yenye kufura yakatokea miilini mwa watu na wanyama. Waganga hawakuweza kusimama mbele ya Mose kwa sababu ya majipu yale yaliyokuwa miilini mwao na juu ya miili ya Wamisri wote. Lakini BWANA akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni, sawasawa kama vile BWANA alivyokuwa amemwambia Mose.

Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako kuelekea angani ili kwamba mvua ya mawe inyeshe juu ya Misri yote, juu ya watu, wanyama na juu ya kila kitu kiotacho katika mashamba ya Misri.” Mose alipoinyosha fimbo yake kuelekea angani, BWANA akatuma ngurumo na mvua ya mawe, umeme wa radi ulimulika hadi nchi. Kwa hiyo BWANA akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi ya Misri, mvua ya mawe ikanyesha na radi ikamulika pote. Ikawa dhoruba ya kutisha ambayo haijakuwako katika nchi ya Misri, tangu nchi hiyo iwe taifa. Mvua ya mawe ikaharibu kila kitu katika nchi ya Misri kilichokuwa katika mashamba, watu na wanyama, ikaharibu kila kitu kinachoota mashambani na kuvunja kila mti. Mahali pekee ambapo mvua ya mawe haikunyesha ni nchi ya Gosheni, ambako Waisraeli waliishi. Ndipo Farao akawaita Mose na Aroni akawaambia, “Wakati huu nimetenda dhambi. BWANA ni mwenye haki, mimi na watu wangu ni wakosaji.

Basi BWANA akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya Misri ili kundi la nzige liweze kuingia juu ya nchi na kutafuna kila kitu kiotacho katika mashamba na kila kitu kilichosazwa na ile mvua ya mawe.” Kwa hiyo Mose akanyosha fimbo yake juu ya Misri, BWANA akauleta upepo wa mashariki ukavuma katika nchi yote mchana wote na usiku kucha, kufikia asubuhi upepo ukawa umeleta nzige. Wakaivamia Misri yote na kukaa kila eneo la nchi kwa wingi. Kamwe hapajapata kuwepo pigo la nzige kama hilo, wala halitakuwepo tena. Wakafunika ardhi yote mpaka ardhi ikawa nyeusi. Wakatafuna kile chote kilichokuwa kimebakizwa na ile mvua ya mawe, kila kitu kiotacho mashambani pamoja na matunda kwenye miti. Hakuna kitu cho chote cha kijani kilichosalia katika miti au mmea katika nchi yote ya Misri. Farao akawaita Mose na Aroni kwa haraka na kuwaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya BWANA Mungu wenu na dhidi yenu pia.

Kisha BWANA akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako kuelekea angani ili giza litande katika nchi ya Misri, giza ambalo watu wanaweza kulipapasa na kulihisi.” Kwa hiyo Mose akaunyosha mkono wake kuelekea angani, na giza nene likafunika pote katika nchi ya Misri kwa muda wa siku tatu. Hakuna mtu ye yote aliyeweza kumwona mwenzake, wala kuondoka mahali alipokuwa kwa muda wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga katika maeneo yao waliyokuwa wanaishi.

Ilipofika usiku wa manane, BWANA akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika Misri, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa, aliyekuwa gerezani, na wazaliwa wa kwanza wa mifugo yote pia. Farao, na maafisa wake wote, na Wamisri wote wakaamka usiku, na kulikuwa na kilio kikubwa katika nchi ya Misri, kwa kuwa haikuwepo nyumba ambayo hakufa mtu. Wakati huo Farao akawaita Mose na Aroni na kuwaambia, “Ondokeni! Tokeni katika watu wangu, ninyi pamoja na Waisraeli! Nendeni mkamwabudu BWANA kama mlivyoomba. Chukueni makundi yenu ya kondoo na mbuzi pamoja na ng'ombe, kama mlivyosema, nanyi mwende zenu. Nanyi pia mnibariki.” Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke kwa haraka na kuacha nchi yao. Kwa kuwa walisema, “La sivyo, tutakufa wote!”

Ndipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma, ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha. Ndipo Mose akanyosha mkono wake juu ya bahari, naye BWANA akayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika, nao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto. Wamisri wakawafuatia ndani ya bahari, pamoja na farasi wote wa Farao, magari ya vita na wapanda farasi. Karibia mapambazuko, BWANA akaliangalia jeshi la Wamisri kutoka katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha. Mungu akayaondoa magurudumu ya magari yao, kwa hivyo wakayaendesha kwa shida. Nao Wamisri wakasema, “Tuachane na Waisraeli! BWANA anawapigania dhidi ya Misri.” Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya bahari ili maji yarudiane yawafunike Wamisri, magari yao ya vita na wapanda farasi wao.” Mose akanyosha mkono wake juu ya bahari, wakati wa mapambazuko bahari ikarudiana na kuwa kama kawaida. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji, lakini BWANA akawasukumia ndani ya bahari. Maji yakarudiana na kuyafunika magari ya vita na wapanda farasi pamoja na jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuata Waisraeli ndani ya bahari. Hakuna hata mmoja wao aliyenusurika. Lakini Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, ukiwepo ukuta wa maji upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.

Mungu akasema, “Kama mkisikiliza kwa bidii sauti ya BWANA Mungu wenu na kuyafanya yaliyo sawa machoni pake, kama mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wo wote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi BWANA, niwaponyaye.”

BWANA akasema, “Sikilizeni maneno yangu: “Akiwapo nabii wa BWANA miongoni mwenu, nitajifunua kwake kwa maono, nitanena naye katika ndoto.

hakuna hata mmoja wa watu hawa ambao waliuona utukufu wangu na ishara za miujiza niliyotenda huko Misri na huko jangwani, lakini ambaye hakunitii na akanijaribu mara hizi kumi,

Mlisogea karibu na mkasimama chini ya mlima wakati ulipowaka moto mpaka mbinguni juu, pamoja na mawingu meusi na giza nene. Ndipo BWANA alipozungumza nanyi kutoka katika moto. Mkasikia sauti ya maneno lakini hamkuona umbo, kulikuwa na sauti tu. Aliwatangazia Agano lake na Amri Kumi, ambazo aliwaamuru mzifuate, kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe.

Je, kuna watu wengine wo wote waliosikia sauti ya Mungu ikizungumza kwenye moto, kama mlivyosikia, nao wakaishi? Je, kuna mungu ye yote amepata kujaribu mwenyewe kuchukua taifa moja kutoka taifa lingine, kwa mapigo, kwa ishara za miujiza na maajabu, kwa vita, kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyooshwa au kwa matendo makuu yakutisha, kama yale ambayo BWANA Mungu wenu aliyofanya kwa ajili yenu huko Misri mbele ya macho yenu?

BWANA akapeleka mbele yetu ishara za miujiza na maajabu makubwa na ya kutisha mno juu ya Misri na Farao pamoja na nyumba yake yote.

BWANA atawakinga na kila ugonjwa. Mungu hatatia juu yenu ugonjwa wo wote mbaya mlioufahamu huko Misri, lakini atatia ugonjwa juu ya wale wote wanaokuchukia.

Mliona kwa macho yenu wenyewe majaribu makubwa, ishara za miujiza na maajabu, mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, ambao kwa huo BWANA Mungu wenu aliwatoa mtoke Misri. BWANA Mungu wenu atawafanyia hivyo watu wote ambao mnawaogopa sasa.

Alikudhili na kukufanya uone njaa kisha akulishe kwa mana, ambayo wewe wala baba zako hamkuijua, awafundishe kuwa mwanadamu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha BWANA. Nguo zenu hazikuchakaa wala miguu yenu haikuvimba kwa miaka hii arobaini.

Tangu wakati huo, katika Israeli hajainuka nabii mwingine kama Mose, ambaye BWANA alimjua uso kwa uso, aliyetenda ishara zote zile za miujiza na maajabu ambayo BWANA alimtuma kuyatenda huko Misri, yaani kwa Farao na maafisa wake wote na nchi yake yote. Kwa kuwa hakuna mtu ye yote aliyewahi kuonyesha nguvu nyingi ama kutenda matendo ya kutisha ambayo Mose aliwahi kuyafanya mbele ya Israeli yote.

Basi, watu walipovunja kambi ili kuvuka Yordani, makuhani wakiwa wamebeba Sanduku la Agano waliwatangulia. Wakati huu ulikuwa wakati wa mavuno, nao Mto Yordani ulikuwa umefurika hadi kwenye kingo zake. Ilikuwa kawaida ya Yordani kufurika nyakati zote za mavuno. Mara tu makuhani wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Agano walipofika mtoni na nyayo zao kuzama ndani ya yale maji, maji hayo yaliyotiririka kutoka upande wa juu yalitindika yakasimama kama chuguu mbali nao, kwenye mji ulioitwa Adamu karibu na Sarethani, wakati yale maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), yalikauka kabisa. Hivyo watu wakavuka kukabili Yeriko. Wale makuhani waliobeba Sanduku la Agano la BWANA, wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Mto Yordani, wakati Waisraeli wote wakiwa wanapita hadi taifa lile lote likaisha kuvuka mahali pakavu.

Siku ya saba, wakaamka asubuhi na mapema wakazunguka mji kama walivyokuwa wakifanya, isipokuwa siku ile waliuzunguka mji mara saba. Walipouzunguka mara ya saba, makuhani walipopiga baragumu kwa sauti kubwa, Yoshua akawaamuru watu akisema, “Pigeni kelele! Kwa maana BWANA amewapa mji huu! Mji huu pamoja na vyote vilivyomo ndani yake utawekwa wakfu kwa BWANA kwa kuangamizwa kabisa. Ila Rahabu tu, yaani yule kahaba na wote ambao wako pamoja naye nyumbani mwake ndio watakaosalimishwa, kwa sababu aliwaficha wale wapelelezi tuliowatuma. Lakini mjiepushe na vitu vilivyowekwa wakfu, msije mkachukua cho chote katika hivyo, msije mkajiletea maangamizi katika maskani ya Israeli na kuiletea taabu. Fedha yote na dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa BWANA, lazima viletwe katika hazina.” Wakati baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele, kwa sauti ya baragumu, na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akasonga mbele moja kwa moja kutokea pale alipokuwa kutokea kila upande na kuuteka mji.

Katika siku ile ambayo BWANA aliwatia Waamori mikononi mwa Israeli, Yoshua akasema na BWANA mbele ya Waisraeli: “Wewe jua, simama kimya juu ya Gibeoni, wewe mwezi, simama katika Bonde la Aiyaloni.” Hivyo jua likasimama kimya, nao mwezi ukatulia, hadi Waisraeli walipokwisha kujipatilizia kwa adui zao, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yashari. Jua likasimama katikati ya mbingu kimya, likachelewa kuzama muda wa siku moja nzima.

Samsoni akatelemkia Timna pamoja na baba yake na mama yake. Walipofika kwenye mashamba ya mizabibu huko Timna, ghafula mwana simba akamjia akimngurumia. Roho wa BWANA akaja juu yake kwa nguvu, naye akampasua yule simba kwa mikono yake bila silaha yo yote kama vile mtu ampasuavyo mwana-mbuzi, wala hakumwambia baba yake wala mama yake aliyoyafanya.

Ndipo Samsoni akazikaribia zile nguzo mbili za katikati ambazo lile jengo lilikuwa linazitegemea. Akazishika moja kwa mkono wa kuume na nyingine mkono wa kushoto. Samsoni akasema, “Nife pamoja na Wafilisti!” Ndipo akazisukuma zile nguzo kwa nguvu zake zote, lile jengo likaanguka juu ya viongozi na watu wote waliokuwamo mle ndani yake. Hivyo akawaua watu wengi wakati wa kufa kwake kuliko siku za uhai wake.

Kisha wakaliingiza lile Sanduku ndani ya hekalu la Dagoni na kuliweka kando ya huyo Dagoni. Watu wa Ashdodi walipoamka asubuhi na mapema kesho yake kumbe, wakamkuta Dagoni ameanguka chini kifudifudi mbele ya Sanduku la BWANA! Wakamwinua Dagoni na kumrudisha mahali pake. Lakini asubuhi iliyofuata, walipoamka kumbe, walimkuta huyo Dagoni ameanguka chini kifudifudi mbele ya Sanduku la BWANA! Kichwa chake na mikono vilikuwa vimevunjwa navyo vimelala kizingitini, ni kiwiliwili chake tu kilichokuwa kimebaki.

Mkono wa BWANA ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi na vijiji vya jirani akaleta uharibifu juu yao na kuwatesa kwa majipu. Watu wa Ashdodi walipoona kile kilichokuwa kikitokea, wakasema, “Sanduku la Mungu wa Israeli kamwe lisikae hapa pamoja na sisi, kwa sababu mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya Dagoni mungu wetu.” Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kuwauliza, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Mungu wa Israeli?” Wakajibu, “Sanduku la Mungu wa Israeli na liende Gathi.” Basi wakalihamisha Sanduku la Mungu wa Israeli. Lakini baada ya kulihamisha, mkono wa BWANA ulikuwa dhidi ya huo mji wa Gathi, akiuweka katika fadhaa kuu. Mungu akawatesa watu wa huo mji, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu. Basi wakapeleka Sanduku la Mungu Ekroni. Wakati Sanduku la Mungu lilipokuwa linaingia Ekroni, watu wa Ekroni walilia wakisema “Wamelileta Sanduku la Mungu wa Israeli kwetu ili kutuua sisi na watu wetu.” Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kusema, “Liondoeni Sanduku la Mungu wa Israeli na lirudishwe mahali pake, la sivyo litatuua sisi na watu wetu.” Kwa kuwa kifo kilikuwa kimeujaza mji hofu, kwani mkono wa Mungu, ulikuwa mzito sana juu yake. Wale ambao hawakufa walipatwa na majipu, na kilio cha mji kilikwenda juu hadi mbinguni.

Lakini Mungu aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-Shemeshi, akiwaua watu sabini miongoni mwao kwa sababu walichungulia ndani ya Sanduku la BWANA. Watu wakaomboleza kwa sababu ya pigo zito kutoka kwa BWANA, nao watu wa Beth-Shemeshi wakauliza, “Ni nani awezaye kusimama mbele za BWANA, huyu Mungu aliye mtakatifu? Sanduku litapanda kwenda kwa nani kutoka hapa?”

Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mtumishi wako amekuwa akichunga kondoo za baba yake. Wakati simba au dubu alipokuja na kuchukua kondoo kutoka katika kundi, nilifuatia, nikampiga na nikampokonya kondoo kwenye kinywa chake. Aliponigeukia, nilimkamata nywele zake, nikampiga na kumwua. Mtumishi wako ameshaua simba na dubu pia; huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wa hao, kwa sababu ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai. BWANA ambaye aliniokoa toka katika makucha ya simba na makucha ya dubu ataniokoa kutoka katika mikono ya huyu Mfilisti,.” Sauli akamwambia Daudi, “Nenda, naye BWANA na awe pamoja nawe.”

Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana. Siku hii leo BWANA atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli. Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya BWANA, naye atawatia wote mikononi mwetu.” Yule Mfilisti aliposogea karibu ili kumshambulia, Daudi akaenda mbio kuelekea safu ya vita kukutana naye. Akatia mkono wake mfukoni na kuchukua jiwe, akalirusha kwa kombeo, nalo likampiga yule Mfilisti kwenye paji la uso. Lile jiwe likaingia kipajini mwa uso, akaanguka chini kifudifudi. Basi Daudi akamshinda huyo Mfilisti kwa kombeo na jiwe; bila kuwa na upanga mikononi mwake akampiga huyo Mfilisti na kumwua. Daudi akakimbia na kusimama juu yake. Akaushika upanga wa huyo Mfilisti na kuuvuta toka kwenye ala yake. Baada ya kumwua, akakata kichwa chake kwa ule upanga. Wafilisti walipoona kuwa shujaa wao amekufa, wakageuka na kukimbia.

Walipofika kwenye sakafu ya kupuria ya Nakoni, Uza akanyoosha mkono na kulishika Sanduku la Mungu kwa sababu maksai walijikwaa. Hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Uza kwa sababu ya kitendo chake cha kukosa heshima, kwa hiyo Mungu akampiga akafia papo hapo kando ya Sanduku la Mungu.

Basi Eliya, Mtishbi kutoka Tishbi katika Gileadi, akamwambia Ahabu, “Kama Mungu wa Israeli aishivyo, ambaye ninamtumikia, hapatakuwa na umande wala mvua katika miaka hii isipokuwa kwa neno langu.”

Akamjibu, “Hakika kama BWANA Mungu wako aishivyo, sina mkate wo wote, isipokuwa konzi ya unga kwenye gudulia na mafuta kidogo kwenye chupa. Ninakusanya kuni chache nipeleke nyumbani na nikapike chakula kwa ajili yangu na mwanangu, ili kwamba tule, kiishe, tukafe.” Eliya akamwambia, “Usiogope. Nenda nyumbani ukafanye kama ulivyosema. Lakini kwanza unitengenezee mimi mkate mdogo kutoka vile ulivyonavyo kisha uniletee na ndipo utayarishe cho chote kwa ajili yako na mwanao. Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli: ‘Lile gudulia la unga halitakwisha wala ile chupa ya mafuta haitakauka hadi siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi.’ ” Akaondoka na kufanya kama Eliya alivyomwambia. Kwa hiyo kukawa na chakula kila siku kwa ajili ya Eliya, yule mwanamke na jamaa yake. Kwa kuwa lile gudulia la unga halikwisha na ile chupa ya mafuta haikukauka, sawasawa na lile neno la BWANA alilosema Eliya.

Baada ya muda, mwana wa yule mwanamke mwenye nyumba akaugua. Hali yake ikaendelea kuwa mbaya sana, na hatimaye akaacha kupumua. Akamwambia Eliya, “Una nini dhidi yangu, ewe mtu wa Mungu? Umekuja ili kukumbushia dhambi yangu na kusababisha kifo cha mwanangu?” Eliya akamjibu, “Nipe mwanao.” Eliya akampokea kutoka kifuani mwake, akambeba mpaka chumba cha juu alipokuwa anaishi, akamlaza kitandani mwake. Kisha akamlilia BWANA, akasema “Ee BWANA Mungu wangu, je, pia umeleta msiba juu ya mjane huyu ninayeishi pamoja naye, kwa kusababisha mwanawe kufa?” Kisha akajinyoosha juu ya kijana mara tatu na kumlilia BWANA, akisema, “Ee BWANA Mungu wangu, nakuomba roho ya huyu kijana imrudie!” BWANA akasikia kilio cha Eliya, na roho ya kijana ikamrudia, naye akafufuka. Eliya akamtwaa kijana na kumbeba kutoka chumbani mwake akamshusha kumpeleka kwenye nyumba. Akampa mama yake na kusema, “Tazama, mwanao yu hai!” Ndipo yule mwanamke akamwambia Eliya, “Sasa ninajua kwamba wewe ni mtu wa Mungu, na kwamba neno la BWANA kutoka kinywani mwako ni kweli.”

Kwa mawe hayo, akajenga madhabahu katika jina la BWANA, na akachimba handaki kuizunguka, ukubwa wa kutosha vipimo viwili vya mbegu. Akapanga kuni, akamkata yule fahali vipande vipande na kuvipanga juu ya kuni. Kisha akawaambia, “Jazeni mapipa manne maji na kuyamwaga juu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya kuni.” Akawaambia, “Fanyeni hivyo tena.” Nao wakafanya hivyo tena. Akaagiza, “Fanyeni kwa mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo kwa mara ya tatu. Maji yakatiririka kuizunguka madhabahu na hata kujaza lile handaki. Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee BWANA, Mungu wa Abrahamu, na Isaki na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu katika Israeli na ya kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unijibu mimi, Ee BWANA, nijibu mimi, ili watu hawa wajue kwamba wewe, Ee BWANA, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.” Kisha moto wa BWANA ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki. Wakati watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “BWANA: yeye ndiye Mungu! BWANA: yeye ndiye Mungu!”

Eliya akachukua vazi lake, akalisokota na kupiga nalo maji. Maji yakagawanyika upande wa kuume na upande wa kushoto, nao wawili wakavuka pakavu.

Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Eliya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli. Elisha aliona hili akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Elisha hakumwona tena. Kisha akazishika nguo zake mwenyewe na kuzichana. Akaliokota lile vazi lililoanguka kutoka kwa Eliya, kisha akarudi na kusimama ukingoni mwa Yordani. Ndipo akalichukua lile vazi ambalo lilikuwa limeanguka kutoka kwa Eliya naye akayapiga nalo yale maji. Akauliza, “Yuko wapi sasa BWANA, Mungu wa Eliya?” Alipoyapiga maji, yakagawanyika kulia na kushoto, naye akavuka.

Kutoka huko Elisha akakwea kwenda Betheli. Ikawa alipokuwa akitembea barabarani, baadhi ya vijana wakatoka mjini na kumfanyia mzaha. Wakisema, “Paa, wewe mwenye upaa! Paa, wewe mwenye upaa!” Akageuka, akawatazama na kuwalaani kwa Jina la BWANA. Kisha dubu wawili wa kike wakatokea mwituni na kuwararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao.

Elisha akamjibu, “Nitawezaje kukusaidia? Niambie, una nini ndani ya nyumba yako?” Akasema, “Mtumishi wako hana kitu cho chote kabisa isipokuwa mafuta kidogo.” Elisha akasema, “Zunguka kwa majirani zako wote ukaombe vyombo vitupu. Usiombe vichache. Kisha ingia ndani na ujifungie mlango wewe na wanao. Mimina mafuta kwenye vyombo vyote, kila kimoja kinapojaa, kiweke kando.” Yule mjane akaondoka na kujifungia ndani, yeye na wanawe. Wao wakamletea vyombo naye akaendelea kumimina mafuta. Vyombo vyote vilipojaa, akamwambia mwanawe, “Niletee chombo kingine.” Lakini mwanawe akajibu, “Hakuna chombo kingine kilichobaki.” Basi mafuta yakakoma kutiririka. Yule mwanamke akamwendea yule mtu wa Mungu, naye mtu wa Mungu akasema, “Nenda ukayauze hayo mafuta ulipe madeni yako. Wewe na wanao mnaweza kuishi kwa kile kinachosalia.”

Elisha alipofika kwenye ile nyumba, mtoto alikuwa amelala juu ya kitanda chake angali amekufa. Akaingia ndani, akajifungia yeye na yule mtoto, akamwomba BWANA. Kisha akapanda kitandani, akalala juu ya yule mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, macho yake juu ya macho ya mtoto, mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Naye alipojinyosha juu yake, mwili wa mtoto ukapata joto. Elisha akajiondoa juu yake na kuanza kutembeatembea ndani ya chumba na kisha akarudi tena kitandani na kujinyosha tena juu ya mtoto mara nyingine. Mtoto akapiga chafya mara saba na akafungua macho yake.

Mchuzi ukagawiwa watu, lakini walipoanza kula, wakalia, “Ee mtu wa Mungu, kuna mauti ndani ya chungu.” Nao hawakuweza kula. Elisha akasema, “Leteni unga.” Akauweka ndani ya chungu na kusema, “Wagawie watu ili wale.” Wala hapakuwa na kitu cho chote chenye madhara ndani ya chungu. Akaja mtu kutoka Baal-Shalisha, akimletea mtu wa Mungu mikate ishirini ya shayiri iliyookwa kutokana na nafaka ya kwanza, pamoja na masuke ya nafaka mpya. Elisha akasema, “Wape watu ili wale.” Mtumishi wake akamwuliza, “Nitawezaje kuandaa hii mbele ya watu mia?” Lakini Elisha akajibu, “Wape watu ili wale. Kwa maana hivi ndivyo asemavyo BWANA: ‘Watakula na kusaza.’ ” Basi akaiandaa mbele yao ile mikate, wakala na baadhi yake wakasaza, sawasawa na neno la BWANA.

Elisha akamtuma mjumbe kumwambia, “Nenda ukaoge katika Mto Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itapona nawe utatakasika.” Lakini Naamani akaondoka akiwa amekasirika na kusema, “Hakika nilidhani kwamba angetoka nje asimame na kuliitia jina la BWANA Mungu wake na kuweka mkono wake juu ya mahali pagonjwa aniponye ukoma wangu. Je, Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora zaidi kuliko mito yo yote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga ndani ya hiyo mito na kutakasika?” Basi akageuka na kuondoka kwa hasira kuu. Watumishi wa Naamani wakamwendea na kumwambia, “Baba yangu, kama huyo nabii angekuambia kufanya jambo lililo kubwa, je, usingefanya? Je, si zaidi sana basi, anapokuambia, ‘Oga na utakasike!’ ” Hivyo akashuka na kujizamisha ndani ya Mto Yordani mara saba, kama vile huyo mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia, nayo nyama ya mwili wake ikapona na kutakasika kama ya mwili wa mvulana mdogo.

Mmoja wao alipokuwa anakata mti, shoka lilitumbukia kwenye maji. Akapiga kelele akasema, “Ee bwana wangu, shoka lilikuwa la kuazima!” Mtu wa Mungu akauliza, “Je, liliangukia wapi?” Alipomwonyesha mahali penyewe, Elisha akakata kijiti na kukitupa mahali pale, nalo shoka likaelea. Akasema, “Lichukue.” Kisha yule mtu akanyosha mkono wake akalichukua.

Wakati huo mfalme wa Aramu alikuwa akipigana vita na Israeli. Baada ya kukubaliana na maafisa wake, akasema, “Nitapiga kambi yangu mahali fulani na fulani.” Mtu wa Mungu akatuma ujumbe kwa mfalme wa Israeli: “Jihadhari usije ukapita mahali pale, kwa sababu Waaramu wanashuka huko.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akatuma neno la tahadhari mahali pale alikokuwa ameelekezwa na mtu wa Mungu. Mara kwa mara Elisha alimwonya mfalme kwamba watu wawe macho kwenye maeneo kama hayo. Hili lilimfadhaisha sana mfalme wa Aramu. Akawaita maafisa wake naye akawauliza, “Je, hamtaniambia ni nani miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?” Mmoja wa maafisa wake akasema, “Mfalme bwana wangu, hakuna hata mmoja wetu; lakini Elisha, yule ambaye ni nabii katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli hata yale maneno unayozungumza ukiwa katika chumba chako cha kulala.”

Kesho yake asubuhi na mapema mtumishi wa mtu wa Mungu alipoamka na kutoka nje, jeshi pamoja na farasi na magari ya vita likawa limeuzunguka mji. Mtumishi wake akasema, “Ole wetu bwana wangu! Tutafanya nini?” Nabii akajibu, “Usiogope. Wale walio pamoja nasi ni wengi zaidi kuliko wale walio pamoja nao.” Kisha Elisha akaomba, “Ee BWANA, mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo BWANA akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya moto yote yamemzunguka Elisha pote. Wakati adui waliposhuka kumwelekea Elisha, Elisha akamwomba BWANA akasema: “Wapige watu hawa kwa upofu.” Basi Mungu akawapiga kwa upofu, kama Elisha alivyoomba. Elisha akawaambia, “Hii sio njia yenyewe na huu sio huo mji. Nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa huyo mtu mnayemtafuta.” Naye akawapeleka Samaria. Baada ya kuingia mjini, Elisha akasema, “BWANA, yafungue macho ya watu hawa ili wapate kuona.” Ndipo BWANA akayafungua macho yao na walipotazama, kumbe hapo ndipo walipojikuta, ndani ya Samaria.

Ikawa Waisraeli fulani walipokuwa wanamzika mtu, ghafula wakaona kikosi cha washambuliaji, basi wakaitupa ile maiti ya yule mtu ndani ya kaburi la Elisha. Wakati ile maiti ilipogusa mifupa ya Elisha, yule mtu akafufuka na kusimama kwa miguu yake.

Isaya akajibu, “Hii ndiyo ishara ya BWANA kwako kwamba BWANA atafanya kile alichoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele, au kivuli kirudi nyuma hatua kumi?” Hezekia akasema, “Ni jambo rahisi kwa kivuli kutangulia mbele hatua kumi, kuliko kukifanya kirudi nyuma hatua kumi.” Ndipo nabii Isaya akamwita BWANA, naye BWANA akakifanya kivuli kurudi nyuma hatua kumi ambazo kilikuwa kimeshuka kwenye ngazi ya Ahazi.

Katika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wake, Asa alipatwa na ugonjwa kwenye miguu yake. Ingawa ugonjwa wake ulimzidia sana, hata katika kuugua kwake hakutafuta msaada kutoka kwa BWANA bali kwa matabibu tu.

Lakini baada ya Uzia kuwa na nguvu sana, majivuno yake yakamsababishia kuanguka. Alikosa uaminifu kwa BWANA Mungu wake, naye akaingia hekaluni mwa BWANA ili afukize uvumba kwenye madhabahu ya kufukizia uvumba. Azaria kuhani akiwa pamoja na makuhani wengine themanini wa BWANA wenye ujasiri wakamfuata huko ndani. Wakamkabili na kumwambia, “Siyo sawa kwako, Uzia, kumfukizia BWANA uvumba. Hiyo ni kazi ya makuhani, wazao wa Aroni, ambao wamewekwa wakfu ili kufukiza uvumba. Ondoka mahali patakatifu, kwa kuwa umekosa uaminifu nawe hutaheshimiwa na BWANA.” Uzia, ambaye alikuwa na chetezo mkononi mwake tayari kufukiza uvumba, akakasirika. Alipokuwa anawaghadhibikia makuhani mbele ya madhabahu ya kufukizia uvumba katika Hekalu la BWANA, ukoma ukamtokea penye kipaji chake cha uso. Azaria Kuhani Mkuu pamoja na makuhani wengine wote walipomtazama wakaona kwamba alikuwa na ukoma penye kipaji chake cha uso wakaharakisha kumtoa nje. Naam, hata yeye mwenyewe alikuwa anatamani kuondoka kwa sababu BWANA alikuwa amempiga.

Ulituma ishara za miujiza na maajabu dhidi ya Farao, dhidi ya maafisa wake wote na watu wote wa nchi yake, kwa kuwa ulifahamu jinsi Wamisri walivyowafanyia ufidhuli. Ukajifanyia jina linalodumu hadi leo.

“Lakini ingekuwa ni mimi, ningemlalamikia Mungu, ningeliweka shauri langu mbele zake. Yeye hutenda maajabu yasiyoweza kutambuliwa, miujiza isiyoweza kuhesabika.

Ninyi, hata hivyo, hunipakaza uongo, ninyi ni matabibu wasiofaa kitu, ninyi nyote!

Ee BWANA, Mungu wangu, nilikuita unisaidie na wewe umeniponya.

BWANA atamtegemeza awapo mgonjwa kitandani, atamwinua kutoka kitandani mwake. Nilisema, “Ee BWANA nihurumie, niponye, maana nimekutenda dhambi wewe.”

Wewe ndiwe Mungu utendaye miujiza, umeonyesha uwezo wako katikati ya mataifa.

akusamehe dhambi zako zote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi, akuvika taji ya upendo na huruma, atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema, ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.

Anawaponya waliovunjika mioyo na kuvifunga vidonda vyao.

Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli.

Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu, alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu; adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake, na kwa majeraha yake sisi tumepona.

Lakini nitakurudishia afya yako na kuyaponya majeraha yako,’ asema BWANA, ‘kwa sababu umeitwa mwenye kutupwa, Sayuni ambaye hakuna ye yote anayekujali.’

Ulitenda ishara za miujiza na maajabu huko Misri na umeyaendeleza mpaka leo, katika Israeli na miongoni mwa wanadamu wote, nawe umejulikana na kufahamika hivyo mpaka leo. Uliwatoa watu wako Israeli kutoka Misri kwa ishara na maajabu, kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa na kwa matisho makuu.

Mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu, naye akanitoa nje kwa Roho wa BWANA na kuniweka katikati ya bonde lililokuwa limejaa mifupa tele. Akanipitisha pande zote kwenye hiyo mifupa, nami nikaona mifupa mingi sana ndani ya lile bonde, mifupa iliyokuwa imekauka sana. Akaniuliza, “Mwanadamu, mifupa hii yaweza kuishi?” Nikajibu, “Ee BWANA Mwenyezi, wewe peke yako wajua.” Ndipo akaniambia, “Itabirie mifupa hii na uiambie, ‘Enyi mifupa mikavu, sikieni neno la BWANA! Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo kwa hii mifupa: Nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi. Nitawawekea mishipa, nami nitaifanya nyama ije juu yenu na kuwafunika kwa ngozi. Nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtakuwa hai. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ ” Basi nikatabiri kama nilivyoamriwa. Wakati nilipokuwa ninatabiri, kukawa na sauti, sauti ya kugongana, nayo mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe. Nikatazama, mishipa na nyama vikatokea juu ya mifupa na ngozi ikaifunika, lakini hapakuwepo pumzi ndani yake. Ndipo aliponiambia, “Utabirie upepo, tabiri, mwanadamu na uuambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Njoo kutoka pande nne, Ee pumzi, nawe upulizie pumzi ndani ya hawa waliouawa, ili wapate kuishi.’ ” Hivyo nikatabiri kama alivyoniamuru, nayo pumzi ikawaingia, wakawa hai na wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.

Mfalme akamwuliza Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza), “Je, unaweza kuniambia nilichoona katika ndoto yangu na kuifasiri?” Danieli akajibu, “Hakuna mwenye hekima, msihiri, mganga au mwaguzi anayeweza kumweleza mfalme siri aliyouliza, lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri. Amemwonyesha Mfalme Nebukadneza kitakachotokea siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyopita akilini mwako ulipokuwa umelala kitandani mwako ni haya: “Ee mfalme, ulipokuwa umelala kitandani, yalikujia mawazo kuhusu mambo yatakayotokea baadaye, naye mfunuaji wa siri akakuonyesha ni kitu gani kitakachotokea. Kwangu mimi, siri hii imefunuliwa kwangu, si kwa sababu nina hekima kubwa kuliko watu wengine wanaoishi, bali ni ili wewe, Ee mfalme, upate kujua tafsiri na ili uweze kuelewa kile kilichopita akilini mwako.

Ndipo Nebukadneza akawa na ghadhabu kali sana kwa Shadraki, Meshaki na Abednego, nayo nia yake ikabadilika juu yao. Akaagiza tanuru ichochewe moto mara saba kuliko kawaida yake na kuwaamuru baadhi ya askari wake wenye nguvu kuliko wengine wote katika jeshi lake kuwafunga Shadraki, Meshaki na Abednego na kuwatupa ndani ya tanuru iwakayo moto. Hivyo watu hawa, walifungwa na kutupwa ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamevaa majoho yao, suruali, vilemba na nguo zao nyingine. Amri ya mfalme ilikuwa ya haraka sana na tanuru ilikuwa na moto mkali kiasi kwamba miali ya moto iliwaua wale askari waliowachukuwa Shadraki, Meshaki na Abednego. Watu hawa watatu, wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana, walianguka ndani ya tanuru iwakayo moto. Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?” Washauri wakajibu, “Hakika, Ee mfalme.” Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembea-tembea ndani ya moto, hawakufungwa na hawakudhurika, naye mtu yule wanne anaonekana kama mwana wa miungu.” Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iwakayo moto na kupaza sauti, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njoni huku!” Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto. Nao maliwali, wasimamizi, watawala na washauri wa kifalme wakakusanyika kuwazunguka. Waliona kwamba moto haukudhuru miili yao, wala unywele wa vichwa vyao haukuungua, majoho yao hayakuungua, wala hapakuwepo na harufu ya moto kwenye miili yao. Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Waliomtumaini na kutoogopa amri ya mfalme nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine ye yote isipokuwa Mungu wao. Kwa hiyo ninaamuru kwamba watu wa taifa lo lote au lugha yo yote watakaosema kitu cho chote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego wakatwe vipande vipande na nyumba zao zifanywe kuwa malundo ya kokoto, kwa maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.” Kisha mfalme akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika jimbo la Babeli.

Mfalme Nebukadneza, Kwa kabila za watu, mataifa na watu wa kila lugha, wanaoishi katika ulimwengu wote: Amani na mafanikio yawe kwenu! Ni furaha yangu kuwaambia kuhusu ishara ya miujiza na maajabu ambayo Mungu Aliye Juu Sana amenifanyia. Tazama jinsi ishara zake zilivyo kuu, jinsi maajabu yake yalivyo na nguvu! Ufalme wake ni ufalme wa milele; enzi yake hudumu kutoka kizazi hadi kizazi.

Ghafula vidole vya kitanga cha mwanadamu vilitokea na kuandika juu ya ukuta, karibu na kinara cha taa ndani ya jumba la mfalme. Mfalme akatazama kitanga kilivyokuwa kikiandika. Uso wa mfalme ukageuka rangi naye aliogopa sana kiasi kwamba magoti yake yaligongana na miguu yake ikalegea.

Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli wakamtupa ndani ya tundu la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako unayemtumikia daima na akuokoe!” Jiwe likaletwa na kuwekwa kwenye mdomo wa tundu, naye mfalme akalitia muhuri kwa pete yake mwenyewe pamoja na kwa pete za wakuu wake, ili kwamba hali ya Danieli isiweze kubadilishwa. Kisha mfalme akarudi kwenye jumba lake la kifalme na usiku kucha hakula chakula wala kutumia viburudisho alivyoletewa. Wala hakuweza kulala. Mapema alfajiri mfalme akaondoka na kuharakisha kwenda kwenye tundu la simba. Wakati alipokaribia lile tundu, alimwita Danieli kwa sauti ya uchungu, “Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je, Mungu wako unayemtumikia daima, ameweza kukuokoa na simba hawa?” Danieli akajibu, “Ee mfalme, uishi milele! Mungu wangu alimtuma malaika wake, naye akafunga vinywa vya hawa simba. Hawajanidhuru, kwa sababu nilionekana sina hatia mbele zake. Wala kamwe sijafanya jambo lo lote baya mbele yako, Ee mfalme.” Mfalme akafurahi mno naye akatoa amri Danieli atolewe kwenye lile tundu. Danieli alipotolewa katika lile tundu, hakukutwa na jeraha lo lote, kwa sababu alikuwa amemtumaini Mungu wake. Kwa amri ya mfalme wale watu waliokuwa wamemshtaki Danieli kwa uongo waliletwa na kutupwa ndani ya lile tundu la simba, pamoja na wake zao na watoto wao. Nao kabla hawajafika chini kwenye sakafu ya lile tundu, simba wakawakamata na kusaga mifupa yao yote.

Kisha Mfalme Dario akawaandikia kabila zote za watu, mataifa na watu wa kila lugha katika nchi yote: “Ninyi na mstawi sana! “Natoa amri hii kwamba katika kila sehemu ya ufalme wangu lazima watu wamwogope na kumheshimu Mungu wa Danieli. “Kwa maana yeye ni Mungu aliye hai naye hudumu milele, ufalme wake hautaangamizwa, nao utawala wake kamwe hauna mwisho. Huponya na kuokoa: hufanya ishara na maajabu mbinguni na duniani. Amemponya Danieli kutoka katika nguvu za simba.”

“Hata itakuwa, baada ya hayo, nitamimina Roho yangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono. Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho yangu. Nami nitaonyesha maajabu katika mbingu na juu ya nchi, damu, moto na wimbi la moshi. Jua litageuzwa kuwa giza na mwezi kuwa damu kabla ya kuja siku ya BWANA iliyo kuu na ya kutisha.

Yesu akapita katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu, akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu. Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Shamu, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya.

Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake akasema, “Bwana, kama ukitaka, unaweza kunitakasa.” Yesu akanyosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka, takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake.

Yesu alipoingia nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wake Petro amelala kitandani akiwa ana homa. Akamgusa mkono wake na homa ikamtoka, naye akainuka na kuanza kumhudumia.

Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuponya wagonjwa wote. Haya yalifanyika ili litimie lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba: “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu na alichukua magonjwa yetu.”

Ghafula kukainuka dhoruba kali baharini hata chombo kikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Yesu alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!” Naye Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nako kukawa shwari kuu. Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”

Walipofika ng'ambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili waliopagawa na pepo wachafu wakitoka makaburini walikutana naye. Watu hawa walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kupita njia ile. Wakapiga kelele, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati ulioamriwa?” Mbali kidogo kutoka pale walipokuwa, kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha. Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu, “Ukitutoa humu, turuhusu tuende kwenye lile kundi la nguruwe.” Akawaambia, “Nendeni!” Hivyo wakatoka na kuwaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likatelemka mbio gengeni, likaingia baharini na kufa ndani ya maji. Wale waliokuwa wakiwachunga hao nguruwe wakakimbia wakaingia mjini, wakaeleza yote kuhusu yale yaliyowatokea wale waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu. Kisha watu wote wa mji huo wakatoka kwenda kukutana na Yesu. Nao walipomwona wakamsihi aondoke kwenye nchi yao.

Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye kitanda. Yesu alipoona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu, dhambi zako zimesamehewa.” Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa sheria wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!” Lakini Yesu akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu? Kwa kuwa ni lipi lililo rahisi: kusema, ‘Dhambi zako zimesamehewa,’ au kusema, ‘Simama, utembee’? Lakini, ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Simama, chukua kitanda chako na uende nyumbani kwako.” Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani kwake. Makutano walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu ambaye alikuwa ametoa mamlaka kama hii kwa wanadamu.

Wakati huo huo mwanamke mmoja ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaja nyuma ya Yesu akagusa upindo wa vazi lake, kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.” Yesu akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo mkuu, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa ile ile.

Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele, akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka. Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka. Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.

Yesu alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata, wakipiga kelele kwa nguvu na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!” Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?” Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.” Ndipo Yesu akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na mnavyoamini.” Macho yao yakafunguka. Yesu akawaonya vikali, akisema, “Angalieni mtu ye yote asijue kuhusu jambo hili.” Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote.

Walipokuwa wanatoka, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu na ambaye hakuweza kuongea aliletwa kwa Yesu. Yule pepo mchafu alipotolewa, yule mtu aliyekuwa bubu akaongea. Ule umati wa watu ukastaajabu na kusema, “Jambo kama hili kamwe halijapata kuonekana katika Israeli.”

Yesu akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme na kuponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu.

Ndipo Yesu akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa mamlaka juu ya pepo wachafu kuwatoa na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila aina.

Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure.

Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema.

huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, wakamwuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?” Yesu akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa? Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.” Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine.

Lakini Yesu alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi wakamfuata, naye akawaponya wote,

Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye ni kipofu na bubu, Yesu akamponya, hata akaweza kusema na kuona. Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?”

Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.

Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Yesu alipofika kando ya bahari aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao.

Ilipofika jioni, wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha, waage makutano ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.” Yesu akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.” Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.” Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.” Akaagiza makutano wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate, kisha akawapa wanafunzi wake hiyo mikate na hao samaki, wanafunzi wakawagawia makutano. Wote wakala, wakatosheka, nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili. Idadi ya wale watu waliokula walikuwa wanaume 5,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.

Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji. Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa. Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni Mimi. Msiogope.”

Petro akamjibu, “Bwana, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.” Yesu akamwambia, “Njoo.” Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Yesu. Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, huku akipiga kelele, “Bwana, niokoe!” Mara Yesu akanyosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?” Nao walipoingia ndani ya chombo, upepo ukakoma. Ndipo wote waliokuwamo ndani ya kile chombo wakamwabudu Yesu wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”

Watu wa eneo lile walipomtambua Yesu, walipeleka habari sehemu zote za jirani. Watu wakawaleta wagonjwa wao wote wakamsihi awaruhusu wagonjwa waguse tu pindo la vazi lake, nao wote waliomgusa, wakaponywa.

Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi jirani na sehemu hizo akaja kwake, akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi, binti yangu amepagawa na pepo mchafu na anateseka sana.” Lakini Yesu hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.” Yesu akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.” Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Yesu, akasema, “Bwana, nisaidie!” Yesu akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza za bwana zao.” Ndipo Yesu akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile.

Umati mkubwa wa watu ukamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake, naye akawaponya. Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli.

Kisha Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia, “Ninahurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula cho chote, nami sipendi kuwaaga wakiwa na njaa wasije wakazimia njiani.” Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha umati huu wa watu mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.” Yesu akawaambia ule umati wa watu waketi chini. Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akiisha kumshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa ule umati wa watu. Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. Idadi ya watu walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.

Wakiwa huko, Yesu alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukang'aa kama jua na nguo zake zikawa na weupe wa kuumiza macho.

Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Yesu na kupiga magoti mbele yake, akasema, “Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji. Nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumponya.” Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka, nitakaa nanyi hata lini, nami nitawavumilia hadi lini? Mleteni kijana hapa kwangu.” Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona saa ile ile.

Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu wakati ambapo hakuna watu, wakamwuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?” Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani kama punje ndogo ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu.”

Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua, fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”

“Amin, nawaambia, lo lote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni na lo lote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni. “Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lo lote watakaloomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”

Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote yanawezekana.”

Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapita, wakapiga kelele wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, uturehemu!” Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, uturehemu.” Yesu akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.” Yesu akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.

Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya.

Akauona mtini kando ya barabara, akaukaribia lakini hakupata tunda lo lote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe na usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka. Wanafunzi wake walipoona jambo hili wakashangaa, wakamwuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?” Yesu akawajibu, “Amin, amin nawaambia, kama mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ng'oka, ukatupwe baharini,’ nalo litafanyika. Lo lote mtakaloomba katika kusali, mkiamini, mtapokea.”

Ghafula pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni akaenda penye kaburi akalivingirisha lile jiwe na kulikalia.

Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama vile alivyosema. Njoni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa. Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye awatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtakakomwona. Sasa nimekwisha kuwaambia.’ ”

Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.

Wakati huo huo, palikuwa na mtu kwenye sinagogi lao aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye alikuwa akipiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Nakujua wewe ni nani, wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu!” Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” Yule pepo mchafu akamtikisatikisa sana huyo mtu kwa nguvu akipiga kelele kwa sauti kubwa, kisha akamtoka. Watu wote wakashangaa, hata kuulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu nao wanamtii!” Sifa zake zikaanza kuenea kwa upesi katika eneo lote la karibu na Galilaya.

Mara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake. Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.

Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme kwa sababu walimjua kuwa yeye ni nani.

Kwa hiyo akazunguka Galilaya kote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.

Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.” Yesu akiwa amejawa na huruma, akanyosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka takasika!” Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika. Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake akimwambia, “Hakikisha humwambii mtu ye yote habari hizi, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani na ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwa ushuhuda kwao.” Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi isipokuwa alikaa sehemu zisizo na watu. Lakini bado watu wakamfuata huko kutoka kila upande.

Ndipo baadhi ya watu wakaja wakamletea Yesu mtu aliyepooza, akiwa amebebwa na watu wanne. Kwa kuwa walikuwa hawawezi kumfikisha kwa Yesu kwa ajili ya umati wa watu, walitoboa tundu kwenye paa mahali pale alipokuwa Yesu, wakamshusha yule aliyepooza kwa kitanda alichokuwa amelalia. Yesu alipoona imani yao, alimwambia yule aliyepooza, “Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.” Basi baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wameketi huko wakawaza mioyoni mwao, “Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?” Mara moja Yesu akatambua kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu? Ni jambo gani lililo rahisi, kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue kitanda chako uende’? Lakini ili mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anao uwezo duniani wa kusamehe dhambi…” Yesu akamwambia yule aliyepooza, “Nakuambia, inuka, chukua kitanda chako uende nyumbani kwako.” Yule mtu aliyekuwa amepooza akainuka, akachukua kitanda chake akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!”

Yesu akaingia tena ndani ya sinagogi na huko palikuwa na mtu mwenye mkono uliopooza. Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki. Yesu akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele.” Kisha Yesu akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato, kufanya jema au baya, kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza kimya. Yesu akawatazama pande zote kwa hasira, akahuzunika sana kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukapona kabisa!

Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa. Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.” Lakini aliwaonya wasimseme yeye ni nani.

Akawachagua kumi na wawili ambao pia aliwaita mitume, ili wapate kuwa pamoja naye na kuwatuma kwenda kuhubiri na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu.

Kukawa na dhoruba kali, nayo mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikawa karibu kujaa maji. Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?” Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?” Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”

Yesu alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini akakutana naye. Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo, kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa kwa minyororo mikononi na miguuni, akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu ye yote aliyekuwa na nguvu za kumzuia. Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe. Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia akapiga magoti mbele yake. Akapiga kelele kwa nguvu akisema, “Una nini nami, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!” Kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!” Yesu akamwuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tuko wengi.” Akamwomba sana Yesu asiwapeleke nje ya nchi ile. Kundi kubwa la nguruwe lilikuwa karibu likilisha kando ya kilima. Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu wakisema, “Tuamuru twende kwenye wale nguruwe, turuhusu tuwaingie.” Basi Yesu akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao 2,000, likatelemkia gengeni kwa kasi nalo likazama baharini. Wale waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakatoka kwenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia. Walipofika kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu Legioni, akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na pia akiwa na akili zake timamu. Wakaogopa. Wale walioyaona mambo haya wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule aliyekuwa na pepo wachafu na lile kundi la nguruwe. Basi watu wakaanza kumwomba Yesu aondoke katika nchi yao.

Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi na kutumia kila kitu alichokuwa nacho lakini badala ya kupona hali yake ilizidi kuwa mbaya. Alikuwa amesikia habari za Yesu naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake, kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikiweza kuligusa vazi lake tu, nitapona.” Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa. Ghafula Yesu akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akaugeukia ule umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyenigusa?” Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi umati wa watu unavyokusonga, wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’ ” Lakini Yesu akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa. Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”

Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?” Kwa kusikia hayo waliyosema, Yesu akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.” Hakumruhusu mtu mwingine ye yote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana nduguye Yakobo. Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa. Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa bali amelala tu.” Wale watu wakamcheka kwa dharau. Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao. Wakaingia ndani mpaka pale alipokuwa yule mtoto. Akamshika mtoto mkono akamwambia, “Talitha koum!” (Maana yake, “Msichana, ninakuambia, amka!”) Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili). Walipoona haya, wakastaajabu sana.

Ilipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi na wengi waliomsikia wakashangaa. Wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake!

Hakufanya miujiza yo yote huko isipokuwa kuweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya.

Akawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu.

Wakatoa pepo wachafu wengi, wakawapaka wagonjwa wengi mafuta na kuwaponya.

Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Mahali hapa ni mbali na pasipo na watu, nazo saa zimekwenda sana. Waage watu ili waweze kwenda sehemu za mashambani na vijiji vya jirani, wakajinunulie chakula.” Lakini Yesu akawajibu, “Wapeni ninyi chakula.” Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari 200 ili tuwape watu hawa wale?” Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.” Walipokwisha kuona wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.” Kisha Yesu akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani, nao wakaketi kwenye makundi ya watu mia mia na wengine hamsini hamsini. Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili akatazama mbinguni, akashukuru, kisha akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili. Watu wote wakala, wakashiba. Wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. Idadi ya wanaume waliokula walikuwa 5,000.

Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Karibu na mapambazuko, Yesu akawaendea wanafunzi wake, akitembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita, lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu, wakapiga yowe, kwa sababu wote walipomwona waliogopa. Mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni Mimi, msiogope!” Akapanda kwenye mashua yao na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa.

Mara waliposhuka kutoka katika mashua yao, watu wakamtambua Yesu, wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali po pote waliposikia kuwa Yesu yupo. Kila mahali Yesu alipokwenda, iwe vijijini, mijini na mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni, wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa, waliponywa.

Ndipo Yesu akaondoka hapo akaenda sehemu za Tiro. Akaingia katika nyumba moja, naye hakutaka mtu ye yote ajue kwamba yuko humo. Lakini hakuweza kujificha. Lakini mwanamke mmoja ambaye binti yake mdogo alikuwa na pepo mchafu, akaja na kumpigia magoti miguuni pake. Basi huyo mwanamke alikuwa Myunani, aliyezaliwa Foinike ya Siria. Akamsihi Yesu amtoe binti yake huyo pepo mchafu. Yesu akamwambia, “Waache watoto washibe kwanza, kwa maana si vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Lakini yule mwanamke akamjibu, “Bwana, hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya chakula cha watoto.” Ndipo Yesu akamjibu, “Kwa sababu ya jibu lako, enenda zako nyumbani, yule pepo mchafu amemtoka binti yako.” Akaenda zake nyumbani akamkuta binti yake amelala kitandani, yule pepo mchafu akiwa amemtoka.

Huko, watu wakamletea Yesu mtu mmoja kiziwi, ambaye pia alikuwa na kigugumizi, wakamwomba aweke mkono wake juu ya huyo mtu na amponye. Baadaye Yesu akampeleka yule kiziwi kando mbali na watu, Yesu akatia vidole vyake masikioni mwa yule mtu. Kisha akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. Ndipo Yesu akatazama mbinguni, akavuta hewa ndani kwa nguvu akamwambia, “Efatha!” Yaani, “Funguka!” Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukaachiwa akaanza kuongea sawasawa. Yesu akawaamuru wasimwambie mtu ye yote habari hizi. Lakini kadiri alivyowazuia, ndivyo walivyozidi kutangaza kwa bidii. Walistaajabu mno. Wakasema, “Amefanya mambo yote vizuri mno! Amewawezesha viziwi wasikie na bubu waseme!”

Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia, “Ninauhurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula. Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.” Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?” Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?” Wakajibu, “Tuna mikate saba.” Akawaambia watu waketi chini. Akiisha kuichukua mikate saba na kushukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo. Walikuwa pia na visamaki vichache, Yesu akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu. Wale watu walikula na kutosheka, baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia wakajaza vikapu saba. Watu waliokula walikuwa wapata 4,000. Akiisha kuwaaga,

Wakafika Bethsaida na baadhi ya watu wakamleta mtu mmoja kipofu wakamsihi Yesu amguse. Yesu akamshika mkono huyo kipofu akampeleka nje ya kijiji. Baada ya kuyatemea mate macho ya yule kipofu na kumwekea mikono, Yesu akamwuliza, “Unaona cho chote?” Yule kipofu akaangalia, akasema, “Ninaona watu, wanaonekana kama miti inayotembea.” Yesu akamwekea tena mikono machoni. Kisha macho yake yakafunguka, kuona kwake kukarejea naye akaona kila kitu dhahiri.

Baada ya siku sita, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana akawapeleka juu ya mlima mrefu, mahali walipokuwa faraghani. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao. Mavazi yake yakawa na weupe wa kuzima macho, meupe kuliko ambavyo mtu ye yote duniani angaliweza kuyang'arisha.

Mtu mmoja miongoni mwa ule umati wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anamfanya asiweze kuongea. Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.” Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakuwa pamoja nanyi mpaka lini? Nitachukuliana nanyi mpaka lini? Mleteni huyo mvulana kwangu.” Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Yesu, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani. Yesu akamwuliza baba yake, “Mwanao amekuwa akitokewa na hali hii tangu lini?” Akamjibu, “Tangu utoto wake. Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lo lote, tafadhali tuhurumie utusaidie.” Yesu akamwambia, “Kama ukiweza kuamini, yote yawezekana kwake yeye aaminiye.” Mara baba yake yule mvulana akapiga kelele akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!” Yesu alipoona kwamba umati wa watu unakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, “Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke wala usimwingie tena!” Yule pepo mchafu akiisha kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, “Amekufa.” Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua, naye akasimama.

Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu hili haliwezekani, lakini kwa Mungu sivyo. Yote kwa Mungu yanawezekana.”

Kisha wakafika Yeriko. Wakati Yesu alipokuwa akiondoka mjini na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu mmoja, jina lake Bartimayo, mwana wa Timayo, alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada. Aliposikia kuwa ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita, akaanza kupaza sauti akisema, “Yesu, Mwana wa Daudi, unihurumie!” Watu wengi wakamkemea, wakamwambia akae kimya, lakini yeye akazidi kupaza sauti akisema, “Mwana wa Daudi, unihurumie!” Yesu akasimama na kusema, “Mwiteni.” Hivyo wakamwita yule mtu kipofu wakamwambia, “Jipe moyo! Inuka, anakuita.” Akiwa analivua lile joho lake, alisimama na kumwendea Yesu. Yesu akamwuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Yule kipofu akajibu, “Mwalimu, nataka kuona.” Yesu akamwambia, “Nenda zako, imani yako imekuponya.” Mara akapata kuona, akamfuata Yesu njiani.

Yesu akawajibu akawaambia, “Mwaminini Mungu. Amin, amin nawaambia, mtu ye yote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng'oka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea nayo yatakuwa yenu.

Yule malaika akawaambia, “Msistaajabu. Mnamtafuta Yesu, Mnazareti, aliyesulibiwa. Amefufuka! Hayuko hapa. Tazameni mahali walipomlaza.

Nazo ishara hizi zitafuatana na wale waaminio: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu, watasema kwa lugha mpya, watashika nyoka kwa mikono yao na hata wakinywa kitu cho chote cha kuua, hakitawadhuru kamwe, wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”

Baada ya Bwana Yesu kusema nao, alichukuliwa juu mbinguni na kuketi mkono wa kuume wa Mungu.

Kisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.

Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”

Ndani ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, akapiga kelele kwa nguvu akisema, “Tuache! Tuna nini nawe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.” Basi Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akisema, “Nyamaza na umtoke!” Yule pepo mchafu akamwangusha chini yule mtu mbele yao wote, akatoka pasipo kumdhuru. Watu wote wakashangaa wakaambiana, “Mafundisho haya ni ya namna gani? Kwa mamlaka na nguvu, anawaamuru pepo wachafu, nao wanatoka!” Habari zake zikaanza kuenea kila mahali katika sehemu ile.

Yesu akatoka kwenye sinagogi akaenda nyumbani kwa Simoni. Basi huko alimkuta mkwewe Simoni ana homa kali, nao wakamwomba Yesu amsaidie. Hivyo Yesu akamwinamia na kukemea ile homa, nayo ikamwacha. Akaamka saa ile ile akaanza kuwahudumia.

Jua lilipokuwa linatua, watu wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbalimbali wakawaleta kwa Yesu, naye akaweka mikono yake juu ya kila mgonjwa, akawaponya. Pepo wachafu pia wakawatoka watu wengi, nao walipokuwa wakitoka wakapiga kelele wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea na kuwazuia wasiseme, kwa maana walimjua kuwa yeye ni Kristo.

Alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.” Simoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua cho chote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.” Nao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika. Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama. Simoni Petro alipoona haya yaliyotukia alianguka miguuni mwa Yesu na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu, mimi ni mtu mwenye dhambi!” Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata,

Ikawa siku moja Yesu alipokuwa katika mji fulani, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamjia. Alipomwona Yesu, alianguka chini mpaka uso wake ukagusa ardhi na kumsihi akisema, “Bwana, ukitaka waweza kunitakasa.” Yesu akanyosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka, takasika!” Naye mara ukoma ukapona. Yesu akamwagiza akisema, “Usimwambie mtu ye yote, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani na ukatoe dhabihu alizoagiza Mose ili kuwa ushuhuda kwao.” Lakini habari zake Yesu zikazidi sana kuenea kotekote kuliko wakati mwingine wo wote, makutano makubwa ya watu yalikuwa yakikusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao.

Siku moja Yesu alipokuwa akifundisha, Mafarisayo na walimu wa sheria, waliokuwa wametoka kila kijiji cha Galilaya na kutoka Uyahudi na Yerusalemu, walikuwa wameketi huko. Nao uweza wa Bwana ulikuwa juu yake kuponya wagonjwa. Wakaja watu wamembeba mgonjwa aliyepooza kwenye mkeka. Wakajaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Yesu. Walipokuwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu ya umati wa watu, wakapanda juu ya paa, wakaondoa baadhi ya vigae, wakapata nafasi ya kumtelemsha yule mgonjwa kwa mkeka wake katikati ya ule umati pale pale mbele ya Yesu. Yesu alipoiona imani yao, akamwambia yule mgonjwa, “Rafiki, dhambi zako zimesamehewa.” Mafarisayo na wale walimu wa sheria wakaanza kuuliza, “Ni nani mtu huyu anayesema maneno ya makufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?” Yesu akijua mawazo yao akawauliza, “Kwa nini mnawaza haya mioyoni mwenu? Je, ni lipi lililo rahisi zaidi, kumwambia huyu, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Simama, uende?’ Lakini ili mpate kujua ya kuwa Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani ya kusamehe dhambi,” Akamwambia yule aliyepooza, “Nakuambia, Simama, chukua mkeka wako uende nyumbani kwako.” Mara yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama mbele yao wote, akachukua mkeka wake akaenda zake nyumbani, huku akimtukuza Mungu. Kila mmoja akashangaa na kumtukuza Mungu. Wakajawa na hofu ya Mungu, wakasema, “Leo tumeona mambo ya ajabu.”

Ikawa siku nyingine ya Sabato Yesu aliingia ndani ya sinagogi akawa anafundisha, huko palikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza. Mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, hivyo wakawa wanamwangalia kwa karibu ili waone kama ataponya katika siku ya Sabato. Lakini Yesu alijua mawazo yao, hivyo akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka.” Hivyo yule mtu akainuka, akasimama mbele yao wote. Ndipo Yesu akawaambia wale walimu wa sheria na Mafarisayo, akisema, “Nawauliza ninyi, ni lipi lililo halali siku ya Sabato, kutenda mema au kutenda mabaya? Kuokoa maisha au kuyaangamiza?” Akawatazama watu wote waliokuwepo, kisha akamwambia yule aliyepooza mkono, “Nyosha mkono wako!” Akaunyosha na mkono wake ukawa tena mzima kabisa.

Akashuka pamoja nao akasimama mahali penye uwanja tambarare. Hapo palikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu kutoka sehemu zote za Uyahudi, Yerusalemu na kutoka pwani ya Tiro na Sidoni, waliokuwa wamekuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Wale waliokuwa wakiteswa na pepo wachafu akawaponya. Watu wote walikuwa wanajitahidi kumgusa kwa sababu nguvu zilikuwa zikimtoka na kuwaponya wote.

Mtumishi wa jemadari mmoja wa Kirumi, ambaye bwana wake alimthamini sana, alikuwa mgonjwa sana karibu ya kufa. Jemadari huyo aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee wa Kiyahudi kwake, wakamwomba aje kumponya mtumishi wa huyo jemadari. Wale wazee walipofika kwa Yesu, wakamsihi sana amsaidie yule jemadari wakisema, “Mtu huyu anastahili wewe umfanyie jambo hili, kwa sababu analipenda taifa letu tena ametujengea sinagogi.” Hivyo Yesu akaongozana nao, lakini alipokuwa hayuko mbali na nyumbani, yule jemadari akatuma rafiki zake kumwambia Yesu, “Bwana, usijisumbue kwani mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. Ndiyo maana sikujiona ninastahili hata kuja kwako. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na huyu, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hili,’ yeye hufanya.” Yesu aliposikia maneno haya alimshangaa sana, akaugeukia ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akawaambia, “Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.” Nao wale watu waliokuwa wametumwa kwa Yesu waliporudi nyumbani walimkuta yule mtumishi amepona.

Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule ulikuwa pamoja na huyo mwanamke. Bwana Yesu alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.” Kisha akasogea mbele akaligusa lile jeneza na wale waliokuwa wamelibeba wakasimama kimya. Akasema, “Kijana, nakuambia inuka.” Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Yesu akamkabidhi kwa mama yake. Watu wote wakajawa na hofu ya Mungu, nao wakamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea miongoni mwetu, Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.” Habari hizi za mambo aliyofanya Yesu zikaenea Uyahudi wote na sehemu zote za jirani.

Wakati huo huo, Yesu aliwaponya wengi waliokuwa na magonjwa, maradhi na pepo wachafu, pia akawafungua vipofu wengi macho wakaona. Hivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yohana yote mliyoyaona na kuyasikia. Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wahubiriwa Habari Njema.

pia baadhi ya wanawake waliokuwa wametolewa pepo wachafu na kuponywa magonjwa miongoni mwao alikuwepo Maria Magdalene, aliyetolewa pepo wachafu saba,

Siku moja Yesu alipanda ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Twendeni tuvuke mpaka ng'ambo ya ziwa.” Hivyo walipokuwa wakienda, akalala usingizi. Dhoruba kali ikatokea mle ziwani, hata mashua ikawa inajaa maji, nao walikuwa katika hatari kubwa. Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakipiga kelele, wakisema, “Bwana, Bwana, tunaangamia!” Yeye akaamka akaukemea ule upepo na yale mawimbi, vikakoma, pakawa shwari. Akawauliza wanafunzi wake, “Imani yenu iko wapi?” Kwa woga na mshangao wakaulizana, “Huyu ni mtu wa namna gani ambaye anaamuru hata upepo na maji navyo vikamtii?”

Yesu aliposhuka katika mashua na kukanyaga pwani, alikutana na mtu mmoja wa mji ule aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye kwa muda mrefu alikuwa havai nguo wala kuishi nyumbani, bali makaburini. Alipomwona Yesu alipiga kelele, akajitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kuu, “Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Nakuomba, usinitese!” Wakati huo Yesu alikuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke huyo mtu. Mara nyingi huyo pepo mchafu alimpagaa na hata alipofungwa kwa minyororo mikono na miguu na kuwekwa chini ya ulinzi alikata hiyo minyororo na kupelekwa na huyo pepo mchafu kwenda nyikani. Yesu akamwuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Legioni,” kwa kuwa alikuwa ameingiwa na pepo wachafu wengi mno. Wale pepo wachafu wakamsihi sana asiwaamuru kwenda Shimoni. Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe hapo karibu wakilisha kandokando ya kilima. Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie hao nguruwe, naye akawaruhusu. Wale pepo wachafu walipomtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likatelemkia gengeni likatumbukia ziwani na kuzama. Wale watu waliokuwa wakichunga lile kundi la nguruwe walipoona yaliyotukia, wakakimbia, wakaeneza habari hizi mjini na mashambani. Nao watu wakatoka kwenda kujionea wenyewe yaliyotukia. Walipofika hapo alipokuwa Yesu wakamkuta yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu amekaa karibu na Yesu, akiwa amevaa nguo na mwenye akili timamu! Wakaogopa sana. Wale walioona mambo hayo wakawaeleza wenzao jinsi yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu alivyoponywa. Ndipo watu wote wa nchi ile ya Wagerasi wakamwomba Yesu aondoke kwao, kwa sababu walikuwa wamejawa na hofu. Basi akaingia katika mashua akaondoka zake.

Katika umati huo alikuwepo mwanamke mmoja aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, tena alikuwa amegharimia yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya matibabu, wala hakuna ye yote aliyeweza kumponya. Huyo mwanamke akaja kwa nyuma na kugusa upindo wa vazi la Yesu, mara kutokwa damu kwake kukakoma. Yesu akauliza, “Ni nani aliyenigusa?” Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, huu umati wa watu unakusonga na kukusukuma kila upande.” Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.” Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Yesu, akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara. Basi Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”

Yesu alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani kwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.” Yesu aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope, amini tu, naye binti yako atapona.” Walipofika nyumbani kwa Yairo, hakumruhusu mtu ye yote aingie ndani pamoja naye isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, baba na mama wa yule binti. Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Yesu akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa ila amelala.” Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa. Yesu akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!” Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara. Akaamuru apewe kitu cho chote cha kula. Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Yesu akawakataza wasimwambie mtu ye yote juu ya yale yaliyotukia.

Yesu akiisha kuwaita wale kumi na wawili pamoja, aliwapa mamlaka na uwezo wa kutoa pepo wachafu wote na kuponya magonjwa yote, kisha akawatuma waende wakahubiri Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa.

Hivyo wale wanafunzi wakaondoka wakaenda kutoka kijiji hadi kijiji, wakihubiri habari njema na kuponya wagonjwa kila mahali.

Lakini umati wa watu ulipofahamu alikokwenda, ukamfuata. Akawakaribisha na kunena nao kuhusu Ufalme wa Mungu na kuwaponya wale wote waliokuwa wanahitaji uponyaji.

Ilipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakamjia Yesu na kumwambia, “Uage umati huu wa watu uondoke ili uweze kwenda kwenye vijiji vya karibu na sehemu za jirani, ili kupata chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani.” Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.” Wao wakasema, “Hatuna zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, labda tuende tukanunue chakula cha kuwatosha watu wote hawa.” Kwa kuwa walikuwako wanaume wapatao 5,000. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “waketisheni katika makundi ya watu hamsini hamsini.” Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega, kisha akawapa wanafunzi wake waugawie ule umati wa watu. Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyobaki, vikajaa vikapu kumi na viwili.

Alipokuwa akiomba, mwonekano wa sura yake ukabadilika, mavazi yake yakametameta kama mwanga wa umeme wa radi.

Mtu mmoja katika ule umati wa watu akapiga kelele, akasema, “Mwalimu, naomba umwangalie mwanangu, ndiye mtoto wangu wa pekee. Mara kwa mara pepo mchafu humpagaa na kumfanya apige kelele, kisha humwangusha na kumtia kifafa akatokwa na povu kinywani. Huyo pepo mchafu anamtesa sana na hamwachi ila mara chache. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.” Yesu akajibu akawaambia, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka, nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini? Mlete mwanao hapa.” Hata yule mtoto alipokuwa akija, yule pepo mchafu akamwangusha, akamtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu amtoke, akamponya yule mtoto, akamrudisha kwa baba yake. Watu wote wakastaajabia uweza mkuu wa Mungu. Wakati bado watu wanastaajabia hayo yote aliyokuwa akiyafanya Yesu, yeye akawaambia wanafunzi wake:

“Mkienda katika mji na watu wake wakawakaribisha, kuleni cho chote kiwekwacho mbele yenu, waponyeni wagonjwa waliomo na waambieni: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’

Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui, wala hakuna kitu cho chote kitakachowadhuru kwa namna yo yote. Basi msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Basi Yesu alikuwa anamtoa pepo mchafu kutoka kwa mtu aliyekuwa bubu. Yule pepo mchafu alipomtoka yule mtu aliyekuwa bubu, akaanza kuongea, nao umati wa watu ukashangaa.

Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato. Wakati uo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na minane, wala alikuwa hawezi kunyoka wima. Yesu alipomwona, akamwita akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.” Yesu alipomwekea mikono yake, mara akasimama wima akaanza kumtukuza Mungu. Lakini mkuu wa sinagogi, akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Kwa hiyo mkuu wa sinagogi akaendelea kuuambia ule umati wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi, katika siku hizo, njoni mponywe, lakini si kuja kuponywa siku ya Sabato.” Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ng'ombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato? Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti wa Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na minane, hakustahili kufunguliwa kutoka katika kifungo hicho siku ya Sabato?” Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.

Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie yule mbweha, ‘Ninafukuza pepo wachafu na kuponya wagonjwa leo na kesho, nami siku ya tatu nitaikamilisha kazi yangu.’

Papo hapo mbele yake palikuwa na mtu mmoja mwenye ugonjwa wa kuvimba mwili. Yesu akawauliza wale Mafarisayo na walimu wa sheria, “Je, ni halali kuponya watu siku ya Sabato au la?” Wakakaa kimya. Hivyo Yesu akamshika yule mgonjwa mkono na kumponya, akamruhusu aende zake.

Wanafunzi wake wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.” Yesu akawajibu, “Kama mngekuwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu, ‘Ng'oka ukaote baharini,’ Nao ungewatii.

Alipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali, wakapaza sauti, wakasema, “Yesu, Bwana, tuhurumie!” Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika. Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Yesu, akimsifu Mungu kwa sauti kuu. Akajitupa miguuni mwa Yesu akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria. Yesu akauliza, “Je, hawakuponywa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa? Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?” Yesu akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”

Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu kwa Mungu yawezekana.”

Yesu alipokuwa anakaribia Yeriko, kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada. Kipofu huyo aliposikia umati wa watu ukipita, akauliza, “Kuna nini?” Wakamwambia, “Yesu wa Nazareti anapita.” Akapaza sauti, akasema, “Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu!” Wale waliokuwa wametangulia mbele wakamkemea wakamwambia akae kimya. Lakini yeye akapaza sauti zaidi, “Mwana wa Daudi, unirehemu!” Yesu akasimama, akawaamuru huyo mtu aletwe kwake. Alipokaribia, Yesu akamwuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Akajibu, “Bwana, nataka kuona.” Yesu akamwambia, “Basi upate kuona, imani yako imekuponya.” Akapata kuona saa ile ile, akamfuata Yesu, huku akimsifu Mungu. Watu wote walipoona mambo hayo, nao wakamsifu Mungu.

Mmoja wao akampiga mtumishi wa Kuhani Mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume. Lakini Yesu akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya.

Hayuko hapa, amefufuka! Kumbukeni alivyowaambia alipokuwa bado yuko pamoja nanyi huko Galilaya kwamba:

Divai ilipokwisha, mama yake Yesu akamwambia, “Wameishiwa na divai.” Yesu akamwambia, “Mwanamke, nina nini nawe? Saa yangu haijawadia.” Mama yake akawaambia wale watumishi, “Lo lote atakalowaambia, fanyeni.” Basi ilikuwapo huko mitungi sita ya kuhifadhia maji iliyotengenezwa kwa mawe kwa ajili ya kujitakasa kwa desturi ya Kiyahudi, kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu. Yesu akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi mpaka juu. Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo, mpelekeeni mkuu wa meza.” Hivyo wakachota, wakampelekea. Yule mkuu wa meza akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilika kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji wao walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando akamwambia, “Watu wote hutoa kwanza divai nzuri, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa vya kutosha, lakini wewe umeiweka ile nzuri kupita zote mpaka sasa.” Huu, ndio uliokuwa mwujiza wa kwanza Yesu aliofanya huko Kana ya Galilaya. Hivyo Yesu alidhihirisha utukufu wake na wanafunzi wake wakamwamini.

Ikawa Yesu alipokuwa Yerusalemu kwenye Sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliona ishara na miujiza aliyokuwa akifanya, wakamwamini.

Huyu alimjia Yesu usiku akamwambia, “Rabi, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kufanya miujiza hii uifanyayo wewe, kama Mungu hayuko pamoja naye.”

Hivyo Yesu akaja tena mpaka Kana ya Galilaya, kule alikokuwa amebadili maji kuwa divai. Huko kulikuwako na mtu mmoja afisa wa kifalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. Huyo mtu aliposikia kwamba Yesu alikuwa amewasili Galilaya kutoka Uyahudi, alimwendea na kumwomba ili aje kumponya mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa. Yesu akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.” Yule afisa wa kifalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.” Yesu akamjibu, “Enenda zako, mwanao yu hai.” Yule afisa akaamini yale maneno Yesu aliyomwambia, akaondoka akaenda zake. Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima. Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana yapata saa saba, homa ilimwacha.” Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati ambapo Yesu alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye, pamoja na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Yesu.

Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, palikuwa na bwawa moja lililoitwa kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa limezungukwa na kumbi tano. Hapa palikuwa na idadi kubwa ya wasiojiweza, yaani, vipofu, viwete, na waliopooza, wakingojea maji yatibuliwe [kwa maana malaika alikuwa akishuka wakati fulani, akayatibua maji na yule aliyekuwa wa kwanza kuingia ndani baada ya maji kutibuliwa alipona ugonjwa wo wote aliokuwa nao]. Mtu mmoja alikuwako huko ambaye alikuwa ameugua kwa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona akiwa amelala hapo, naye akijua kuwa amekuwako hapo kwa muda mrefu, akamwambia, “Je, wataka kuponywa?” Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kuniingiza bwawani maji yanapotibuliwa. Nami ninapotaka kutumbukia bwawani, mtu mwingine huingia kabla yangu.” Yesu akamwambia, “Simama, chukua mkeka wako na uende.” Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea. Basi siku hiyo ilikuwa siku ya Sabato.

Umati mkubwa wa watu uliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa.

Yesu alipotazama na kuuona ule umati mkubwa wa watu ukimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya. Filipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili, hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa kila mtu apate kidogo.” Mmoja wa wanafunzi wake, aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia, “Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa umati wote huu?” Yesu akasema, “waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi, palikuwa na wanaume 5,000. Ndipo Yesu akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wamekaa kwa kiasi walichohitaji. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka. Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee cho chote.” Hivyo wakavikusanya wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vilivyobaki vya ile mikate mitano na samaki wale wawili wadogo. Baada ya watu kuona mwujiza ule Yesu aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!”

Wanafunzi walipokuwa wamekwenda mwendo wa karibu maili tatu au nne, walimwona Yesu akitembea juu ya maji akikaribia mashua, wakaogopa sana. Lakini Yesu akawaambia, “Ni mimi, msiogope.” Ndipo kwa furaha wakamkaribisha kwenye mashua, na mara wakafika walikokuwa wanakwenda.

Ndipo wakaokota mawe ili kumpiga, lakini Yesu akajificha, naye akatoka Hekaluni.

Yesu alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?” Yesu akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake. Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi. Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.” Baada ya kusema haya, akatema mate ardhini, akatengeneza tope kwa mate na kumpaka yule mtu kipofu machoni. Kisha akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Siloamu, maana yake ni aliyetumwa.) Ndipo yule kipofu akaenda, akanawa, naye akarudi akiwa anaona. Majirani zake na wale wote waliokuwa wamemwona hapo awali akiombaomba wakaanza kuuliza, “Je, huyu si yule aliyekuwa akiketi akiombaomba?”

Tangu kuumbwa kwa ulimwengu hatujasikia kwamba mtu amemponya ye yote aliyekuwa kipofu. Kama huyu mtu hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya lo lote.”

Yesu akasema, “Liondoeni hilo jiwe.” Martha ndugu yake yule aliyekuwa amekufa akasema, “Lakini Bwana, wakati huu atakuwa ananuka kwani amekwisha kuwako kaburini siku nne.” Yesu akamwambia, “Sikukuambia kwamba kama ukiamini utauona utukufu wa Mungu?” Kwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka penye kaburi. Yesu akainua macho yake juu akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia. Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya umati huu uliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.” Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti yake akaita, “Lazaro, njoo huku!” Yule aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono yake na miguu yake ikiwa imeviringishiwa vitambaa vya kitani na leso usoni pake. Yesu akawaambia, “Mfungueni, mwacheni aende zake.”

Kwa hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaita mkutano wa baraza, wakaulizana, “Tufanyeje? Huyu mtu anafanya ishara nyingi.

Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini.

Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo. Amin, amin nawaambia, ye yote aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo yeye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizi atazifanya, kwa sababu mimi ninakwenda kwa Baba.

Nanyi mkiomba lo lote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana. Kama mkiniomba lo lote kwa Jina langu nitalifanya.

Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lo lote mtakalo, nanyi mtatendewa.

Ikawa jioni ya ile siku ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walipokuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa Wayahudi, Yesu aliwatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi.” Baada ya kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana.

Hivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.” Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.” Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomasi alikuwa pamoja nao. Ndipo Yesu akaja milango ikiwa imefungwa na kusimama katikati yao akasema, “Amani iwe nanyi.” Kisha akamwambia Tomasi, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.” Tomasi akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”

Yesu alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki.

Simoni Petro akawaambia wenzake, “Mimi nakwenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Tutakwenda pamoja nawe.” Wakatoka, wakaingia ndani ya mashua, lakini usiku ule hawakupata cho chote. Mara baada ya kupambazuka, Yesu akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Yesu. Yesu akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wo wote?” Wakamjibu, “La.” Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu na tazama wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua. Yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia haya, akajifunga nguo yake kwa kuwa alikuwa uchi, naye akajitosa baharini. Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliyojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa 200. Walipofika pwani, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake na mikate. Yesu akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.” Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu pwani. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa 153. Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika.

Petro akageuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akiwafuata. (Huyu ndiye yule mwanafunzi aliyeegama kifuani mwa Yesu walipokula naye chakula cha mwisho na kuuliza, “Bwana, ni nani atakayekusaliti?”) Petro alipomwona huyo mwanafunzi, akamwuliza Yesu, “Bwana na huyu je?” Yesu akamjibu, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini? Wewe inakupasa unifuate!” Kwa sababu ya maneno haya ya Yesu, uvumi ukaenea miongoni mwa ndugu kwamba huyu mwanafunzi hangekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa hangekufa. Yeye alisema tu kwamba, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini?”

Lakini kuna mambo mengine mengi ambayo Yesu alifanya. Kama yote yangeliandikwa, nadhani hata ulimwengu wote usingekuwa na nafasi ya kutosha kuweka vitabu vyote ambavyo vingeandikwa. Amen.

Baada ya mateso yake, alijionyesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu Ufalme wa Mungu.

Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.” Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.

Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo uliotoka mbinguni, ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia. Basi walikuwepo Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu. Waliposikia sauti hii, umati wa watu ulikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

“ ‘Katika siku za mwisho, asema Bwana, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu na binti zetu watatabiri, vijana wenu wataona maono na wazee wenu wataota ndoto. Hata juu ya watumishi wangu nitamwaga Roho wangu, nao watatabiri. Nami nitaonyesha maajabu mbinguni juu na ishara duniani chini, damu, moto na mvuke wa moshi mnene. Jua litakuwa giza na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana iliyo tukufu.

“Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kwa kupitia yeye, kama ninyi wenyewe mjuavyo.

Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume.

Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni. Huyu mtu akiwaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, aliwaomba wampe sadaka. Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.” Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini kile nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu wa Nazareti simama, uende.” Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu. Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu. Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu, wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu juu ya yale yaliyomtukia. Yule mtu kiwete aliyeponywa alipokuwa akiambatana na Petro na Yohana, watu wote walishangaa mno, wakaja wanawakimbilia mpaka kwenye ukumbi wa Solomoni.

Petro alipoona watu wamekusanyika akawaambia, “Enyi waume wa Israeli, kwa nini mnastaajabu kuhusu jambo hili? Mbona mnatukazia macho kwa mshangao kana kwamba ni kwa uwezo wetu au utakatifu wetu tumefanya mtu huyu kutembea?

Kwa imani katika jina la Yesu, huyu mtu mnayemwona na kumfahamu ametiwa nguvu. Ni kwa jina la Yesu na imani ile itokayo kwake ambayo imemponya kabisa huyu mtu, kama ninyi wote mnavyoona.

Wale viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana na kujua ya kuwa walikuwa watu wa kawaida, wasio na elimu, walishangaa sana, wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Yesu. Lakini kwa kuwa walikuwa wanamwona yule kiwete aliyeponywa amesimama pale pamoja nao, hawakuweza kusema lo lote kuwapinga. Wakawaamuru watoke nje ya baraza wakati wakisemezana jambo hilo wao kwa wao. Wakaulizana, “Tuwafanyie nini watu hawa? Hatuwezi kukanusha mwujiza huu mkubwa walioufanya ambao ni dhahiri kwa kila mtu Yerusalemu.

Sasa, Bwana angalia vitisho vyao na utuwezeshe sisi watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri mkuu. Nyosha mkono wako ili kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miujiza kwa jina la Mwanao mtakatifu Yesu.” Walipokwisha kuomba, mahali pale walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.

Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. Mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume. Petro akamwuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.” Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakamchukua nje kumzika. Saa tatu baadaye mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. Petro akamwuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.” Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho Mtakatifu wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakuchukua nje.” Saa ile ile akaanguka chini miguuni mwake na kufa, wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe. Hofu kuu ikalipata kanisa lote pamoja na watu wote waliosikia juu ya matukio haya.

Mitume wakafanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Nao wale wote walioamini walikuwa wakikusanyika katika ukumbi wa Solomoni kwa nia moja. Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. Lakini wengi walioamini idadi kubwa ya wanaume na wanawake wakaongezeka kwa Bwana. Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. Pia watu wakakusanyika kutoka katika miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu, hao wote wakaponywa.

Lakini wakati wa usiku malaika wa Bwana akaja akafungua milango ya gereza akawatoa nje akawaambia, “Nendeni, mkasimame Hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uzima huu mpya.” Waliposikia haya wakaenda Hekaluni alfajiri wakaendelea kufundisha watu. Kuhani Mkuu na wale waliokuwa pamoja nao walipowasili, alikusanya baraza na wazee wote wa Israeli wakatuma wale mitume waletwe kutoka gerezani. Lakini wale walinzi wa Hekalu walipokwenda gerezani hawakuwakuta wale mitume mle. Kwa hiyo wakarudi na kutoa habari. Wakasema, “Tumekuta milango ya gereza imefungwa sawasawa na maaskari wa gereza wamesimama nje ya mlango, lakini tulipofungua milango hakuwepo mtu ye yote ndani.” Basi mkuu wa walinzi wa Hekalu, viongozi na makuhani waliposikia haya, wakafadhaika na kushangaa sana kwa ajili yao kwamba jambo hili litakuwaje. Ndipo mtu mmoja akaja akawaambia, “Tazameni watu wale mliowatia gerezani wako Hekaluni wakiwafundisha watu.”

Stefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu.

Watu wote waliokuwa wameketi katika baraza wakimkazia macho Stefano, wakaona uso wake unang'aa kama uso wa malaika.

“Basi baada ya miaka arobaini kupita, malaika wa Mungu akamtokea Mose jangwani karibu na Mlima Sinai katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto.

Aliwaongoza wana wa Israeli kutoka Misri, baada ya kufanya ishara na maajabu mengi huko Misri, katika Bahari ya Shamu na katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini.

Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza aliyofanya, wakasikiliza kwa bidii yale aliyosema. Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.

Simoni naye akaamini na akabatizwa. Akamfuata Filipo kila mahali, akistaajabishwa na ishara kuu na miujiza aliyoiona.

Nao walipopanda kutoka kwenye maji, ghafula Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, naye towashi hakumwona tena, lakini akaenda zake akifurahi. Filipo akajikuta yuko Azoto, akasafiri akihubiri injili katika miji yote mpaka alipofika Kaisaria.

Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?” Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?” Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu unayemtesa.” “Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.” Watu wale waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila kuwa na la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza. Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu cho chote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza mpaka Dameski. Naye kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu naye hakula wala kunywa cho chote.

Kisha Anania akaenda kwenye ile nyumba, akaingia ndani. Akaweka mikono yake juu ya Sauli akasema, “Ndugu Sauli, Bwana Yesu aliyekutokea njiani amenituma kwako ili upate kuona tena na ujazwe Roho Mtakatifu.” Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa.

Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea, ambaye alikuwa amepooza na kwa muda wa miaka minane alikuwa hajaondoka kitandani. Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya, inuka utandike kitanda chako.” Mara Ainea akainuka. Watu wote wa Lida na Sharoni walipomwona Ainea akitembea wakamgeukia Bwana.

Wakati huo akaugua, akafa na wakiisha kuuosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani. Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.” Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao, naye alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonyesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi. Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai. Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana.

Jinsi Mungu alivyomtia Yesu wa Nazareti mafuta katika Roho Mtakatifu na jinsi alivyokwenda huku na huko akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za Shetani, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.

Baada ya kumkamata alimtia gerezani, chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari, vyenye askari wanne kila kimoja. Herode alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka mbele ya watu baada ya Pasaka. Kwa hiyo Petro akawekwa gerezani, lakini kanisa lilikuwa likimwombea kwa Mungu kwa bidii. Usiku ule kabla ya siku ambayo Herode Agripa alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili, akiwa amefungwa kwa minyororo miwili. Nao walinzi wa zamu walikuwa wakilinda penye lango la gereza. Ghafula malaika wa Bwana akatokea na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro. Yule malaika akamwambia, “Vaa nguo zako na viatu vyako.” Petro akafanya hivyo. Kisha akamwambia, “Jifunge vazi lako na unifuate.” Petro alitoka mle gerezani akiwa amefuatana na yule malaika. Hakujua wakati huo kuwa yaliyokuwa yakitukia yalikuwa kweli. Alidhani kuwa anaona maono. Wakapita lindo la kwanza na la pili, ndipo wakafika kwenye lango la chuma linaloelekea mjini. Lango likawafungukia lenyewe, nao wakapita hapo wakatoka nje. Baada ya kutembea umbali wa mtaa mmoja, ghafula yule malaika akamwacha Petro. Ndipo Petro akarudiwa na fahamu, akasema, “Sasa ninajua bila shaka yo yote kuwa Bwana amemtuma malaika wake na kuniokoa kutoka katika makucha ya Herode Agripa na kutoka katika matazamio yote ya Wayahudi.”

Lakini Elima yule mchawi (hii ndiyo maana ya jina lake), aliwapinga Barnaba na Sauli na kujaribu kumpotosha yule mkuu wa kile kisiwa aiache imani. Ndipo Sauli, ambaye pia aliitwa Paulo, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akamkazia macho yule Elima mchawi, kamwambia, “Ewe mwana wa ibilisi, wewe ni adui wa kila kilicho haki! Umejaa kila aina ya udanganyifu na ulaghai. Je, hutaacha kuzipotosha njia za Bwana zilizonyooka? Nawe sasa sikiliza, mkono wa Bwana u dhidi yako. Utakuwa kipofu, wala hutaona jua kwa muda.” Mara ukungu na giza vikamfunika, naye akaenda huko na huko akitafuta mtu wa kumshika mkono ili amwonyeshe njia. Yule mkuu wa kile kisiwa alipoona yaliyotukia, akaamini kwa sababu alistaajabishwa na mafundisho kuhusu Bwana.

Hivyo Paulo na Barnaba wakakaa huko kwa muda wa kutosha wakihubiri kwa ujasiri juu ya Bwana, ambaye alithibitisha ujumbe wa neema yake kwa kuwawezesha kufanya ishara na miujiza.

Katika mji wa Listra, alikuweko kiwete, ambaye alikuwa amelemaa tangu kuzaliwa na hakuwa ametembea kamwe. Alimsikiliza Paulo alipokuwa akihubiri. Paulo alipomtazama akaona ana imani ya kuponywa. Paulo akapaza sauti, “Simama kwa miguu yako!” Mara yule mtu akasimama upesi akaanza kutembea!

Kusanyiko lote likakaa kimya, wakawasikiliza Paulo na Barnaba wakieleza jinsi Mungu alivyowatumia kutenda ishara na maajabu kwa watu Mataifa.

Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka. Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka.

Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kwa mkono wa Paulo, kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao na pepo wachafu wakawatoka.

Kijana mmoja jina lake Eutiko, aliyekuwa amekaa dirishani, wakati Paulo alipokuwa akiendelea kuhubiri kwa muda mrefu, alipatwa na usingizi mzito, akaanguka kutoka ghorofa ya tatu, wakamwinua akiwa amekufa. Paulo akashuka chini, akajitupa juu ya yule kijana na kumkumbatia, akasema, “Msishtuke, uzima wake bado umo ndani yake.” Kisha Paulo akapanda tena ghorofani, akamega mkate na kula. Baada ya kuongea mpaka mapambazuko, akaondoka. Watu wakamrudisha yule kijana nyumbani akiwa hai nao wakafarijika sana.

Paulo alikuwa amekusanya mzigo wa kuni na alipokuwa anaweka kwenye moto kwa ajili ya joto, nyoka mwenye sumu akatoka humo na kujisokotea mkononi mwake. Wale wenyeji wa kile kisiwa walipomwona yule nyoka akining'inia mkononi mwa Paulo, wakaambiana, “Huyu mtu lazima awe ni mwuaji, ingawa ameokoka kutoka baharini, haki haijamwacha aishi.” Lakini Paulo akamkung'utia yule nyoka ndani ya moto wala yeye hakupata madhara yo yote. Watu walikuwa wanangoja avimbe au aanguke ghafula na kufa. Lakini baada ya kungoja kwa muda mrefu na kuona hakuna cho chote kisicho cha kawaida kilichomtokea, wakabadili mawazo yao na kuanza kusema kwamba yeye ni mungu.

Basi karibu na sehemu ile, palikuwa na shamba kubwa la mtu mmoja kiongozi wa kile kisiwa, aliyeitwa Publio, ambaye alitupokea akatuhudumia kwa ukarimu mkubwa kwa muda wa siku tatu. Baba yake Publio alikuwa mgonjwa kitandani, akiwa anaumwa homa na kuhara damu. Paulo akaingia ndani ili kumwona na baada ya maombi, akaweka mikono juu yake na kumponya. Jambo hili lilipotukia, watu wote wa kisiwa kile waliokuwa wagonjwa wakaja, nao wakaponywa.

Basi, imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo.

kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake mpaka Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu.

Wayahudi wanataka miujiza na Wayunani wanatafuta hekima, lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulibiwa, ambaye kwa Wayahudi ni kitu cha kukwaza na kwa Wayunani ni upuzi. Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi pia Wayunani, Kristo ni nguvu na hekima ya Mungu.

Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu. Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu cho chote wakati nikiwa nanyi isipokuwa Yesu Kristo, naye amesulibiwa msalabani. Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana. Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya kuwashawishi watu, bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho Mtakatifu ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.

Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya. Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, kwa mwingine tafsiri za lugha. Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo mwenyewe.

Mungu ameweka katika kanisa, kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu, kisha watenda miujiza, pia karama za kuponya, karama za masaidiano, karama za maongozi, aina mbalimbali za lugha. Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote wanafanya miujiza? Je, wote wana karama ya kuponya? Je, wote hunena kwa lugha mpya? Je, wote wanatafsiri? Basi tamanini sana karama zilizo kuu. Nami nitawaonyesha njia iliyo bora zaidi.

Hata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo. Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu.

Fuateni upendo na kutaka sana karama za roho, hasa karama ya unabii. Kwa maana mtu ye yote anayesema kwa lugha, hasemi na wanadamu bali anasema na Mungu. Kwa kuwa hakuna mtu ye yote anayemwelewa, kwani anasema mambo ya siri kwa Roho. Lakini anayetoa unabii anasema na watu akiwajenga, kuwatia moyo na kuwafariji. Anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, bali atoaye unabii hulijenga kanisa. Ningependa kila mmoja wenu anene kwa lugha mpya, lakini ningependa zaidi nyote mtoe unabii. Kwa kuwa yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko anenaye kwa lugha, isipokuwa kama kuna mtu wa kutafsiri, ili kanisa zima lipate kujengwa. Sasa ndugu zangu, kama nikija kwenu nikasema kwa lugha mpya nitawafaidia nini kama sikuwaletea ufunuo au neno la maarifa au unabii au mafundisho?

Basi kunena kwa lugha mpya ni ishara, si kwa watu waaminio, bali kwa ajili ya wasioamini, wakati unabii si kwa ajili ya wasioamini, bali kwa ajili ya waaminio. Kwa hiyo kama kanisa lote likikutana na kila mmoja akanena kwa lugha, kisha wakaingia wageni wasioamini, je, hawatasema kwamba wote mna wazimu? Lakini kama mtu asiyeamini au asiyeelewa akiingia wakati kila mtu anatoa unabii, ataaminishwa na watu wote kuwa yeye ni mwenye dhambi na kuhukumiwa na wote, nazo siri za moyo wake zitawekwa wazi. Kwa hiyo ataanguka chini na kumwabudu Mungu akikiri, “Kweli Mungu yuko katikati yenu!”

Kwa hiyo ndugu zangu, takeni sana kutoa unabii na msikataze watu kusema kwa lugha.

Mambo yanayomtambulisha mtume wa kweli, yaani, ishara, miujiza na maajabu, yalifanywa miongoni mwenu kwa saburi nyingi.

Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu,

Pia Mungu aliushuhudia kwa ishara, maajabu na kwa miujiza mbalimbali, na karama za Roho Mtakatifu alizozigawa kulingana na mapenzi yake.

Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni udhahiri wa mambo yasiyoonekana.

Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana ye yote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.

Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku.

Je, kuna ye yote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana. Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua na kama ametenda dhambi, atasamehewa. Kwa hiyo ungamianeni makosa yenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.

Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi. Akaomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. Kisha akaomba tena, mbingu zikatoa mvua nayo ardhi ikatoa mazao yake.

Ndipo nikageuka ili nione ni sauti ya nani iliyokuwa ikisema nami. Nami nilipogeuka, nikaona vinara saba vya taa vya dhahabu, katikati ya vile vinara vya taa, nikaona mtu kama Mwana wa Adamu, amevaa joho refu na mkanda wa dhahabu umefungwa kifuani mwake. Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji, nayo macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. Nyayo zake zilikuwa kama shaba iliyosuguliwa sana, kama vile imesafishwa katika tanuru ya moto, nayo sauti yake ilikuwa kama sauti ya maji mengi. Katika mkono wake wa kuume alishikilia nyota saba na kinywani mwake ulitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake kama jua kali linalong'aa kwa nguvu zake zote.

Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwepo na bahari tena. Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe.

Swahili - Kiswahili - SW

NEN'2014 - Neno Bibilia Takatifu Kiswahili Contemporary Version - 2014

This Bible text is from Biblica Open Kiswahili Contemporary Version Neno 2015
https://open.bible/bibles/swahili-biblica-text-bible/
provided by: Biblica Inc, available by Creative Commons CC-BY-SA-4.0,
and this new compilation is shared as www.creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0.
Languages are made available to you by www.ipedge.net