04 – Uumbaji

Haya ni maneno matakatifu ya Mungu Mwenyezi.
Hatupendi maneno ya wanadamu.
Kwa mtu yeyote anayempenda Mungu... hivi ndivyo Mungu anasema kuhusu: Uumbaji.

Mistari 3 Muhimu Zaidi

Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.

Lakini Mungu huipa hiyo mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake. Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti.

Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, umeonekana waziwazi ukitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

Kila Mstari katika Mpangilio wa Biblia - 104 vifungu

Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. Wakati huu Dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu, giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametanda juu ya maji. Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.

Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi na akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili.

Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema. Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu.

Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe mchana na usiku, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka, nayo iwe ndiyo mianga kwenye nafasi ya anga itoe nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, itawale mchana na usiku, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.

Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini, kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mkaongezeke mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.

Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wafugwao kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.

Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.” Kwa hiyo Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe, kwa mfano wa Mungu alimuumba; mwanaume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.” Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa kwa ajili ya chakula chenu, cha wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi. Kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo. Mungu akatazama vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.

Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo. Katika siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya, hivyo siku ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote. Mungu akaibariki siku ya saba akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya.

Haya ndiyo maelezo ya mbingu na dunia wakati zilipoumbwa. BWANA Mungu alipoziumba mbingu na dunia, hapakuwepo na mche wa shambani uliokuwa umejitokeza ardhini, wala hapakuwepo na mmea wa shamba uliokuwa umeota, kwa kuwa BWANA Mungu alikuwa hajanyeshea mvua juu ya nchi, na hapakuwepo mtu wa kuilima ardhi, lakini umande ulitokeza kutoka ardhini na kunyesha uso wote wa nchi: BWANA Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, mtu akawa kiumbe hai. Basi BWANA Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, huko akamweka huyo mtu aliyemuumba.

Hii ni orodha iliyoandikwa ya vizazi vya Adamu. Wakati Mungu alipomuumba Adamu, alimfanya kwa sura ya Mungu. Aliwaumba mwanaume na mwanamke, akawabariki. Walipokwisha kuumbwa akawaita “Mwanadamu.” Adamu alipokuwa ameishi miaka 130, alikuwa na mwana aliyekuwa na sura yake, mwenye kufanana naye. Akamwita Sethi.

Kwa kuwa kwa siku sita, BWANA aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo ndani yake, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo BWANA akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.

Itakuwa ishara kati yangu na Waisraeli milele, kwa kuwa kwa muda wa siku sita BWANA aliumba mbingu na dunia, na siku ya saba akaacha kufanya kazi, akapumzika.’ ”

Hata hivyo, kwa hakika kama niishivyo, na kwa hakika kama utukufu wa BWANA uijazavyo dunia yote,

Sasa uliza kuhusu siku za zamani, zamani kabla ya wakati wako, tangu siku ile Mungu alipomwumba mtu juu ya nchi, uliza kutoka mwisho mmoja wa mbingu mpaka mwisho mwingine wa mbingu. Je, kumepata kutokea jambo jingine lililo kubwa kama hili, au kuna jambo jingine kama hilo limepata kusikiwa?

Mbingu, hata mbingu za juu sana, dunia na kila kitu kilichomo ndani yake, ni mali ya BWANA Mungu wako.

Humwinua maskini kutoka mavumbini na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu; huwaketisha pamoja na wakuu na kuwafanya warithi kiti cha enzi cha heshima. “Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya BWANA; juu yake ameuweka ulimwengu.

Mabonde ya bahari yalifunuliwa na misingi ya dunia ikawa wazi kwa kukaripia kwake BWANA, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwake.

Naye Hezekia akamwomba BWANA akisema: “Ee BWANA, Mungu wa Israeli, uliyeketi kwenye kiti chako cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako, ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe ndiye uliyeumba mbingu na dunia.

Ukuu na uweza, ni vyako, Ee BWANA, na utukufu na enzi na uzuri, kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani ni chako wewe. Ee BWANA, ufalme ni wako, umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.

Wewe peke yako ndiwe BWANA. Uliumba mbingu, hata mbingu za mbingu, nalo jeshi lote la angani, dunia na vyote vilivyo ndani yake, bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.

Aitikisa dunia kutoka mahali pake na kuzifanya nguzo zake zitetemeke. Husema na jua nalo likaacha kuangaza, naye huizima mianga ya nyota. Yeye peke yake huzitandaza mbingu na kuyakanyaga mawimbi ya bahari. Yeye ndiye Muumba wa nyota za Dubu na Orioni, Kilimia na kundi la nyota za kusini. Hutenda maajabu yasiyopimika, miujiza isiyoweza kuhesabiwa.

“Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha, au ndege wa angani, nao watawaambia, au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha, au acheni samaki wa baharini wawape taarifa. Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua kwamba mkono wa BWANA ndio uliofanya hili? Mkononi mwake uko uhai wa kila kiumbe na pumzi ya wanadamu wote.

Hutandaza anga la kaskazini mahali patupu, naye huining'iniza dunia mahali pasipo na kitu. Huyafungia maji kwenye mawingu yake, hata hivyo mawingu hayapasuki kwa uzito wake. Huufunika uso wa mwezi mpevu, akitandaza mawingu juu yake. Amechora mstari wa upeo juu ya uso wa maji, ameweka mpaka wa nuru na giza. Nguzo za mbingu nazo zatetemeka, zinatishika anapozikemea.

Roho wa Mungu ameniumba, pumzi ya Mwenyezi hunipa uhai.

Kisha BWANA akamjibu Ayubu kutoka katika upepo wa kisulisuli. Akasema: “Nani huyu atiaye mashauri yangu giza kwa maneno yasiyo na maarifa? Jikaze kama mwanaume, nami nitakuuliza swali, nawe unijibu. “Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia? Niambie, kama unafahamu. Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake? Hakika wewe unajua! Ni nani aliyenyosha kamba ya kupimia juu yake? Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini, au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni, wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha? “Ni nani aliyeifungia bahari milango ilipopasuka kutoka katika tumbo, nilipoyafanya mawingu kuwa vazi lake na kuyafungia katika giza nene, Nilipoamuru mipaka yake na kuiweka milango yake na makomeo mahali pake, niliposema, ‘Unaweza kufika mpaka hapa wala si zaidi, hapa ndipo mawimbi yako yenye kiburi yatakapokomea’?

“Mwangalie kiboko, niliyemwumba kama nilivyokuumba wewe, ambaye anajilisha kwa majani kama ng'ombe. Tazama basi, nguvu alizo nazo kwenye viuno vyake, uwezo alio nao kwenye misuli ya tumbo lake! Mkia wake hutikisika kama mwerezi, mishipa ya mapaja yake imesukwa pamoja.

Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota, ulizoziratibisha,

Ee BWANA, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako, sakafu ya bahari ikaonekana, misingi ya dunia ikawa wazi.

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi) Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu, anga zahubiri kazi ya mikono yake.

Sauti yao imeenea duniani pote, maneno yao yameenea mpaka miisho ya dunia. Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua,

(Zaburi Ya Daudi) Dunia ni mali ya BWANA, pamoja na vyote vilivyomo ndani yake, ulimwengu na wote waishio ndani yake, maana aliiwekea misingi yake baharini na kuifanya imara juu ya maji.

Kwa neno la BWANA mbingu ziliumbwa, jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake.

Mbingu ni zako, nayo nchi pia ni yako, uliuwekea ulimwengu msingi pamoja na vyote vilivyomo. Uliumba kaskazini na kusini; Tabori na Hermoni wanaliimbia jina lako kwa furaha.

Kabla ya kuzaliwa milima au hujaumba dunia na ulimwengu, wewe ni Mungu tangu milele hata milele.

Bahari ni yake, kwani ndiye aliyeifanya, na mikono yake iliumba nchi kavu. Njoni, tusujudu tumwabudu, tupige magoti mbele za BWANA Muumba wetu,

Hapo mwanzo uliweka misingi ya dunia, na mbingu ni kazi ya mikono yako. Hivi vitatoweka, lakini wewe utadumu, vyote vitachakaa kama vazi. Utavibadilisha kama nguo navyo vitaondoshwa.

Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA. Ee BWANA Mungu wangu, wewe ni mkuu sana, umejivika utukufu na enzi. Amejifunika katika nuru kama vile kwa vazi, amezitandaza mbingu kama hema na kuziweka nguzo za orofa yake juu ya maji. Huyafanya mawingu kuwa gari lake kubwa zuri, na hupanda kwenye mbawa za upepo. Hufanya pepo kuwa wajumbe wake, miali ya moto watumishi wake. Ameiweka dunia kwenye misingi yake, hawezi kamwe kuondoshwa.

Ee BWANA, jinsi gani zilivyo nyingi kazi zako! Kwa hekima ulizifanya zote, dunia imejaa viumbe vyako. Pale iko bahari, kubwa na yenye nafasi tele, imejaa viumbe visivyo na idadi, vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo.

Kazi za BWANA ni kuu, wote wanaopendezwa nazo huzitafakari.

Mbarikiwe na BWANA Muumba wa mbingu na dunia. Mbingu zilizo juu sana ni mali ya BWANA, lakini dunia amempa mwanadamu.

Hii ndiyo siku BWANA aliyoifanya, tushangilie na kufurahi ndani yake.

Msaada wangu hutoka kwa BWANA, Muumba wa mbingu na dunia.

Msaada wetu ni katika jina la BWANA, Muumba wa mbingu na dunia.

BWANA hufanya lo lote apendalo, mbinguni na duniani, katika bahari na vilindi vyake vyote.

Ambaye kwa ufahamu wake aliziumba mbingu, Fadhili zake zadumu milele. Ambaye aliitandaza dunia juu ya maji, Fadhili zake zadumu milele. Ambaye aliumba mianga mikubwa, Fadhili zake zadumu milele. Jua litawale mchana, Fadhili zake zadumu milele. Mwezi na nyota vitawale usiku, Fadhili zake zadumu milele.

Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani; uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu. Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa kwa namna ya ajabu na ya kutisha; kazi zako ni za ajabu, ninajua hayo kikamilifu.

Muumba wa mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo ndani yake: BWANA anayedumu kuwa mwaminifu milele na milele.

Huzihesabu nyota na huipa kila moja jina lake.

Kwa hekima BWANA aliiweka misingi ya dunia, kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake;

“BWANA aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, kabla ya matendo yake ya zamani; niliteuliwa tangu milele, tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa. Wakati hazijakuwapo bahari, nilikwishazaliwa, wakati hazijakuwapo chemchemi zilizojaa maji, kabla milima haijawekwa mahali pake, kabla vilima havijakuwapo, nilikwishazaliwa, kabla hajaumba dunia wala mashamba yake au vumbi lo lote la dunia. Nilikuwapo alipoziweka mbingu mahali pake, wakati alipochora mstari wa upeo wa macho juu ya uso wa kilindi, wakati alipoweka mawingu juu na kuziweka imara chemchemi za bahari, wakati alipoiwekea bahari mpaka wake ili maji yasivunje agizo lake, na wakati alipoweka misingi ya dunia. Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake. Nilijazwa na furaha siku baada ya siku, nikifurahi daima mbele zake, nikifurahi katika dunia yake yote nami nikiwafurahia wanadamu.

Masikio yasikiayo na macho yaonayo, BWANA ndiye aliyevifanya vyote viwili.

Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ni BWANA Mwenye Nguvu Zote; dunia yote imejaa utukufu wake.”

Hawatadhuru wala kuharibu juu ya mlima wangu mtakatifu wote, kwa kuwa dunia itajawa na kumjua BWANA kama maji yajazavyo bahari.

Mnapindua mambo juu chini, kana kwamba mfinyanzi aweza kufikiriwa kuwa kama udongo wa mfinyanzi! Je, kile kilichofinyangwa chaweza kumwambia yule aliyekifinyanga, “Wewe hukunifinyanga mimi?” Je, chungu kinaweza kumwambia mfinyanzi, “Wewe hujui cho chote?”

“Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Umeumba mbingu na nchi.

Ni nani aliyepima maji ya bahari kwenye konzi ya mkono wake, au kuzipima mbingu kwa shibiri yake? Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu, au kupima milima kwenye kipimio na vilima kwenye mizani?

Je, hujui? Je, hujasikia? Je, hujaambiwa tangu mwanzo? Je, hujafahamu tangu kuumbwa kwa dunia? Anakaa kwenye kiti cha enzi juu ya duara ya dunia, nao watu wakaao ndani yake ni kama panzi. Huzitandaza mbingu kama chandarua na kuzitandaza kama hema la kuishi.

Inueni macho yenu mtazame mbinguni: Ni nani aliyeumba hivi vyote? Yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine na kuziita kila moja kwa jina lake? Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu, hakuna hata mojawapo inayokosekana.

Je wewe, hufahamu? Je wewe, hujasikia? BWANA ni Mungu wa milele, Muumba wa miisho ya dunia. Hatachoka wala kulegea, wala hakuna hata mmoja awezaye kuupima ufahamu wake.

Hili ndilo asemalo Mungu, BWANA, yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda, aliyeitandaza dunia na vyote vitokavyo humo, awapaye watu wake pumzi na uzima kwa wale waendao humo:

kila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu, niliyemwumba kwa utukufu wangu, niliyemhuluku na kumfanya.”

“Hili ndilo asemalo BWANA, Mkombozi wako, aliyekuumba tumboni: “Mimi ni BWANA, yeye aliyeumba vitu vyote, yeye peke yake aliyezitanda mbingu, yeye aliyeitandaza nchi mwenyewe,

“Hili ndilo asemalo BWANA, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake: Kuhusu mambo yatakayokuja, je, unaniuliza habari za watoto wangu, au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu? Mimi ndiye niliyeumba dunia na kumwumba mwanadamu juu yake. Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu, nikayapanga majeshi yake yote ya angani.

Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA, yeye aliyeumba mbingu, ndiye Mungu; yeye aliyeifanya dunia na kuiumba, yeye ndiye aliyeiwekea misingi imara, hakuiumba ili iwe tupu, bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake, anasema: “Mimi ndimi BWANA, wala hakuna mwingine.

“Ee Yakobo, nisikilize mimi, Israeli, ambaye nimekuita: Mimi ndiye; mimi ndimi mwanzo na mwisho. Mkono wangu mwenyewe uliweka misingi ya dunia, nao mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu; niziitapo, zote husimama pamoja.

kwamba mnamsahau BWANA Muumba wenu, aliyezitanda mbingu na kuiweka misingi ya dunia, kwamba mnaishi katika hofu siku zote kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu, ambaye nia yake ni kuangamiza? Iko wapi basi ghadhabu ya mdhalimu?

Lakini, Ee BWANA, wewe ndiwe Baba yetu. Sisi ni udongo wa mfinyanzi wewe ndiye mfinyanzi; sisi sote tu kazi ya mkono wako.

Hili ndilo asemalo BWANA, “Mbingu ni kiti changu cha enzi, nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu. Iko wapi nyumba mtakayojenga kwa ajili yangu? Mahali pangu pa kupumzika patakuwa wapi? Je, mkono wangu haukufanya vitu hivi vyote, hivyo vikapata kuwepo?” asema BWANA. “Mtu huyu ndiye ninayemthamini: yeye ambaye ni mnyenyekevu na mwenye roho yenye toba, atetemekaye asikiapo neno langu.

Lakini BWANA ni Mungu wa kweli, yeye ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele. Akiwa amekasirika, dunia hutetemeka, mataifa hayawezi kustahimili hasira yake. “Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka duniani na kutoka chini ya mbingu.’ ” Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake, akaufanya ulimwengu kwa hekima yake na kwa ufahamu wake akazitandaza mbingu.

Kwa uwezo wangu mkuu na kwa mkono wangu ulionyooshwa nimeumba dunia na watu wake na wanyama walioko ndani yake, nami humpa ye yote inipendezavyo.

“Ee BWANA Mwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza.

“Aliifanya dunia kwa uweza wake; ameweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake na kuzitandaza mbingu kwa ufahamu wake.

(yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni, ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko na mchana kuwa usiku, ambaye huyaita maji ya bahari na kuyamwaga juu ya uso wa nchi: BWANA ndilo jina lake;

yeye ambaye hujenga jumba lake la kifalme katika mbingu na kuisimika misingi yake juu ya dunia, yeye aitaye maji ya bahari na kuyamwaga juu ya uso wa nchi: BWANA ndilo jina lake.

Akajibu, “Mimi ni Mwebrania, nami namwabudu BWANA, Mungu wa Mbinguni, aliyeumba bahari na nchi kavu.”

Kwa kuwa dunia itajazwa na maarifa ya utukufu wa BWANA, kama maji yaifunikavyo bahari.

Hili ni neno la BWANA kuhusu Israeli. BWANA, yeye azitandaye mbingu, awekaye misingi ya dunia na aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake, asema:

Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mume na mke.

Kenani alikuwa mwana wa Enoshi, Enoshi alikuwa mwana wa Sethi, Sethi alikuwa mwana wa Adamu, Adamu alikuwa mwana wa Mungu.

Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu. Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna cho chote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa.

Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kwa yeye, haukumtambua.

Yule mkuu wa meza akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilika kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji wao walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando akamwambia, “Watu wote hutoa kwanza divai nzuri, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa vya kutosha, lakini wewe umeiweka ile nzuri kupita zote mpaka sasa.”

“ ‘Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu. Mtanijengea nyumba ya namna gani? asema Bwana. Au mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?

“Enyi watu, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi ni wanadamu tu kama ninyi! Tunawaletea habari njema, tukiwaambia kwamba mgeuke mtoke katika mambo haya yasiyofaa mmwelekee Mungu aliye hai, aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na kila kitu kilicho ndani yake.

“Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji cho chote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’

Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, umeonekana waziwazi ukitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu ambaye alimwamini, Mungu awapaye ahadi waliokufa na kuvitaja vile vitu ambavyo haviko kana kwamba vimekwisha kuwako.

Kwa hiyo kama vile dhambi ilivyoingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja na kupitia dhambi hii, mauti ikawafikia watu wote, kwa sababu wote wamefanya dhambi.

Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka katika utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa uchungu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa.

Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake. Utukufu ni wake milele! Amen.

Lakini kwetu sisi yuko Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vyatoka kwake na kwa ajili yake sisi twaishi na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa yeye vitu vyote vimekuwepo na kwa yeye sisi tunaishi.

Lakini Mungu huipa hiyo mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake. Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti.

Kwa hiyo imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika kiumbe hai”; Adamu wa mwisho, yeye ni roho iletayo uzima. Lakini si ule wa kiroho uliotangulia, bali ni ule wa asili, kisha ule wa kiroho. Mtu wa kwanza aliumbwa kwa mavumbi ya ardhini, mtu wa pili alitoka mbinguni. Kama vile alivyokuwa yule wa ardhini, ndivyo walivyo wale walio wa ardhini; na kwa vile alivyo mtu yule aliyetoka mbinguni, ndivyo walivyo wale walio wa mbinguni.

Kwa kuwa Mungu, yeye aliyesema, “Nuru na ing'ae gizani,” ameifanya nuru yake ing'ae mioyoni mwetu ili kutupatia nuru ya maarifa ya utukufu wa Mungu katika uso wa Kristo.

kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa kwa nyakati zote katika Mungu aliyeumba vitu vyote.

Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa, vile vitu vinavyoonekana na vile visivyoonekana, kama ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala, vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. Yeye alikuwapo kabla ya vitu vyote na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja.

lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kwa yeye aliuumba ulimwengu. Mwana ni mng'ao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko mbinguni.

Pia asema, “Hapo mwanzo, Ee Bwana, uliweka misingi ya dunia, nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.

Kwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu.

Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana viliumbwa kwa vitu visivyoonekana.

Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu ya kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbaya, wakisema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipokufa, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.” Wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo tangu zamani nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa hayo maji, ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa na kuangamia. Lakini kwa neno lilo hilo mbingu za sasa na dunia, zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu. Lakini wapenzi, msisahau neno hili, kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu na miaka elfu ni kama siku moja.

“Bwana wetu na Mungu wetu, wewe umestahili kupokea utukufu na heshima na uweza, kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa mapenzi yako viliumbwa na vimekuwako.”

Naye akaapa kwa Jina la Mungu aishiye milele na milele, aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, dunia na vyote viijazavyo, pamoja na bahari na vyote vilivyomo ndani yake, akasema, “Hakuna kungoja tena!

Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale waishio duniani, yaani, kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa. Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”

Swahili - Kiswahili - SW

NEN'2014 - Neno Bibilia Takatifu Kiswahili Contemporary Version - 2014

This Bible text is from Biblica Open Kiswahili Contemporary Version Neno 2015
https://open.bible/bibles/swahili-biblica-text-bible/
provided by: Biblica Inc, available by Creative Commons CC-BY-SA-4.0,
and this new compilation is shared as www.creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0.
Languages are made available to you by www.ipedge.net